Waridi wa BBC: Nimebadili maisha ya wanawake elfu 10 kwa taulo za bure

Mvumbuzi wa sodo za kufua za muda mrefu
Maelezo ya picha, Dkt.Idda Mhindi, mbunifu wa sodo za hedhi salama
    • Author, Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC News Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

‘Mimi binafsi ni binti ambaye nimekulia vijijini, mbali na kusoma shuleni lakini katika hatua zote za ukuaji wangu, tangu naanza kuingia hedhi na kujua hedhi ni nini na kujua nini cha kutumia wakati wa hedhi, ilikuwa changamoto kubwa, sana’. Huyo ni Idda Mhindi, ambaye ni daktari wa binadamu na mbunifu katika sekta ya afya anasimulia jinsi makuzi yake yalivyochochea kutafuta suluhisho la hedhi kwa mabinti wa mazingira ya vijijini.

Katika jamii yake ilikuwa ni mwiko kuzungumzia kuhusu masuala ya usafi wa hedhi au afya ya uzazi miongoni mwa jamii kuanzia ngazi ya familia.

Tangu nimalize chuo, nilikuwa na fikra ya jinsi mabinti kama mimi wanavyopitia changamoto kama nilizopitia.

"Hakuna mtu yeyote aliyekuwa anaweza kupata taulo za kike, na kwa wasichana waliovunja ungo, hali hii ilizidisha ugumu wa maisha."

Jambo lilisababisha kufanya utafiti wa njia mbadala wa tatizo hilo kwa kuanzisha kiwanda kinachozalisha taulo za kike mbadala yaani (SODO) zinazoweza kutumika tena ambazo ni rafiki wa mazingira (FURSA Pads). Alikuwa na shabaha ya kushughulikia usafi wa hedhi huku akiwawezesha mabinti wa maeneo ya vijijini.

Dkt.Idda

Chanzo cha picha, Dkt.Idda

Kazi yake inatoa suluhisho endelevu wa usafi wa hedhi na inatoa fursa kwa wanawake na vijana.

Kupitia ubunifu wake, Idda anachangia kufikia lengo la kupunguza changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya hedhi barani Afrika na kwingineko duniani.

Anaeleza: Nimeshuhudia wasichana wengi wakitumia mbadala wa taulo za kike kama nguo za zamani yaani (matambala), bidhaa za wanyama, au majani, huku wengine wakilazimika kushiriki ngono ili kupata fedha za kununulia taulo za kike!

"Kwa upande wangu binafsi, nina shauku ya kufanya kazi za kijamii, hivyo nilipojiunga na chuo kikuu nilianza kushiriki katika shughuli za hisani kama vile kuhudumia Watoto wahitaji (yatima) na kuendesha programu za shule na kuwaelimisha wasichana kuhusu hedhi kupitia taaluma yangu.

Nilipokuwa nikitembelea kwenye shule mbalimbali, wasichana walianza kushirikishana changamoto zao, na mojawapo ya changamoto hizo ilikuwa ni ukosefu wa taulo za kike.

Sodo za kufuliwa

Chanzo cha picha, Dkt.Idda

Maelezo ya picha, Wanafunzi waliofaidika na sodo za fursa

Hawakuwa na fedha za kununua taulo za kike, hivyo nikaanza kuchangisha fedha ili kununua taulo zinazotumika mara moja. Hata hivyo, kugawa hizi taulo haikuwa suluhisho, kwani zinadumu kwa mwezi mmoja tu.

Ndipo nilipokutana na rafiki yangu aliyeniambia kuhusu taulo za kike zinazotengenezwa na kudumu kwa muda mrefu hata mwaka mzima na kwa Afrika kiwanda hicho kipo Uganda.

"Nikamuomba aniunganishe nao'

kisha nikaanza kutafuta rasilimali ili kujua zaidi kuhusu taulo za kike zinazoweza kutumika tena, nikiangalia jinsi wanavyofanya huko India, mahitaji ya malighafi zinazotumika wakati wa uzalishaji, majina ya malighafi hizo, na sifa zinazohitajika. Ndipo nilipoanza kutumia malighafi zinazofanana na zilizopo kwenye mazingira yetu, zenye uwezo wa kufyonza na kuzuia maji kupenyeza".

mm

Chanzo cha picha, Dkt.Idda

Maelezo ya picha, Sodo zinazosambazwa kwa mabinti maeneo ya vijijini katika shule mbalimbali
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anasema baadaye walipata sampuli ya kwanza, ambapo waliendelea kujaribu kupata maoni kutoka kwa watumiaji wo. Hatimaye, wakapeleka katika mamlaka ya udhibiti wa dawa na vifaa toba, (TMDA), hatua ambayo iliwachukua takriban miaka miwili kukamilisha mchakato wote hadi kufikia hatua ambayo wangeweza kugawa bure shuleni.

Anafafanua: Baada ya hapo nikaanza kutafuta watu mbalimbali ili kuendelea na michango ya hisani. Hata hivyo, kwa kuwa ni kiwanda na ili kuhakikisha uendelevu, tulianza sehemu ya biashara ndani ya shirika letu ili tuweze kuuza bidhaa kwa watumiaji wengine, maduka, NGOs (mashirika yasiyoya kiserikali), na kampuni.

"Kupitia programu zetu kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, zaidi ya wasichana 10,000 wa shule wamepata taulo za kike bure.

Lengo letu kuu ni kwamba hedhi isiwazuie wasichana kupata elimu au wanawake kupata fursa. Makundi yaliyo hatarini zaidi ni wanawake wa vijijini na familia zenye kipato cha chini, ambao nchini Tanzania ni zaidi ya asilimia 60, anaeleza

Sodo

Chanzo cha picha, Dkt.Idda

Siwezi kusema ninachokifanya ni jambo jipya kwani ni la kawaida katika nchi nyingine na baadhi ya bidhaa huingizwa kutoka nje, lakini uzalishaji wa ndani ndiyo unaleta upekee na kuwa sehemu ya kubadilisha mazingira yangu.

Mpaka sasa, ubunifu wa Dkt.Idda umewawezesha akina mama wadogo katika mchakato wa uzalishaji. Kundi hili la akina mama vijana, wale waliopata mimba wakiwa na umri wa miaka 15 hadi 20 na hivyo wakatolewa katika mfumo rasmi wa shule.

Tumewafundisha jinsi ya kufanya hatua zote za uzalishaji, na sasa wao ndiyo wanaendesha mchakato mzima wa uzalishaji ikiwa ni Sehemu ya uwezeshaji wanawake, anaweka bayana huku akionesha kuifurahia kazi yake.

.

Chanzo cha picha, Dkt.Idda

Maelezo ya picha, Dkt.Idda akipokea tuzo ya ubunifu wa masuala ya afya

Imehaririwa na Florian Kaijage