Waridi wa BBC:‘Mimi na wadogo zangu 7 wote hatuoni'

mama
Maelezo ya picha, Leila Nassoro, mjasiliamali kutoka ‘familia ya wasioona’ asimulia tamu na chungu ya maisha
    • Author, Eagan salla
    • Nafasi, Mwandishi
    • Akiripoti kutoka, BBC News, Dar es Salaam
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Leila Nassoro Likame, alizaliwa akiwa na shida ya kutoona. Wazazi wake hawakubaini tatizo hilo hadi aliponza kutembea kutokana na kujikwaa kila alipokuwa anatembea ndipo walibaini ana shida ya kuona na kuamua kuanza kutafuta matibabu kwa njia za jadi na baadaye kwenda katika hospitali mbalimbali nchini Tanzania.

“Bibi yangu alimwambia mama watafute chanzo ni nini wakatafuta lakini hawakuona, tumehangaika hospitali sijui Tumbi, Msasani, na kwingineko lakini sikubahatika kuona” walizunguka hospitali mbalimbali kwa nyakati tafauti tangu mwaka 1987 hadi mwaka 2004 walipokata tamaa”.

ulemavu
Maelezo ya picha, Leila akiwa na familia yake, ambayo wote hawaoni

Watoto wangu wote wana tatizo la uoni hafifu

mm
Maelezo ya picha, Mama yao ndiye anayeona vizuri peke yake katika familia ila anatuhumiwa kuwa yeye ndiyo chanzo cha watoto wake kuwa vipofu sababu ya 'ushirikina'

Leila ni mzaliwa kwanza katika familia ya watu nane ambao wote hawaoni isipokuwa mama yao pekee, ambaye kwa kiasi kikubwa ndiye msaidizi wao wa karibu licha ya jamii kumnyooshea vidole kuwa yeye ndiye chanzo cha tatizo la watoto wake kutoona, wengi wakimtuhumu kuwa ni mshirikina.

Kwa sasa Leila ana miaka 46 na ni mama wa watoto watano kwa baba wawili tofauti na kati ya watoto hao watano, watatu ni wa kike na wawili ni wa kiume ambao nao pia wana uoni hafifu, inapofika wakati wa jioni huwa hawaoni kabisa.

Bibi alitufundisha kusuka mikeka ili iwe nguzo ya maisha yetu

Kutokana na changamoto hizo za kutokuona, Leila na wadogo zake ambao nao hawaoni hawakubahatika kupata elimu kwa ngazi hata ya msingi. Walikulia nyumbani wakiwasaidia wazazi kazi ndogondogo kama vile kulima kuchoma mkaa na nyinginezo ili kujipatia kipato ambacho kiliwasaidia kujikimu.

“Mama alikuwa anaenda ‘kukata ngwe’ (kufanya vibarua) tunamsaidia kulima ili tupate chakula na mahitaji mengine ya nyumbani”

Kadiri umri wao ulivyozidi kuongezeka bibi yao alianza kumfundisha Leila ususi wa mikeke akimsistiza kwamba ameshakuwa mtu mzima anahitaji kuwa na ujuzi utakaomuwezesha kujitegemea. Leila anasema bibi yao alikuwa masaidizi wao wa karibu tangu walipokuwa wadogo hata baada ya kuwa watu wazima kabla ya kufariki dunia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

“Bibi alikuwa anatushikisha ukili anakuambia weka hapa mjukuu wangu mpaka tukajua ijapokuwa ilikuwa ngumu hatuoni lakini Mungu katupa akili tulikuwa tunapima kwa kutumia mikono tu”

Baada ya kujifunza kwa muda mrefu Leila alifanikiwa kusuka mkeka wake wa kwanza ambao aliulalia mwenyewe. Kutokana na furaha aliyoipata baada ya kuumaliza, wakati huo anasema mkeka wa ukindu ulikuwa ukiuzwa shilingi 1500 za Tanzania ambazo ni chini ya dola moja ya Marekani kwa sasa.

Mteja wake wa kwanza alikuwa ni mjomba wake, ambaye alivutiwa na mkeka wake wa kwanza hivyo akampa kazi ya kumsukia wa kwake. Kwa sasa mkeka mmoja wa ukindu unauzwa shilingi elfu 25000 za Tanzania ambazo ni pungufu kidogo ya dola kumi za Marekani.

Licha ya ujuzi huu, Leila pia anajishughulisha na kilimo kwenye vipande vya ardhi vya kuazima na wakati mwingine hushirikiana na ndugu zake na mama yao kwenda msituni kuchoma mkaa, lakini wamekuwa wakifukuzwa mara kadhaa kutokana na sheria kali zilizopo za uhifadhi wa mazingira.

Tunaibiwa, kunyapaliwa kwa kuwa hatuoni

mm

Leila na wadogo zake hutumia muda mwingi kusuka ukili wakiamini kuombaomba ni tabia tu ya mtu, ndiyo maana wao licha ya ulemavu walionao wanajishughulisha kutafuta riziki kwa kufanya kazi licha ya changamoto wanakutana nazo, ikiwa ni pamoja na kudhulumiwa na kuibiwa na wateja wasio waaminifu.

“Inatuvunja moyo sana mfano tulikuwa tunauza machungwa tumefilisika, tumeuza matikiti tumefilisika, sasa hivi tunajaribu tena korosho biashara ndiyo hivyo, wakati mwingine tunaomba wadogo zetu watusaidie au watoto wetu watusaidie wakitoka shule japo kwa muda mfupi, kwani muda mrefu tunabaki wenyewe tunateseka tu’’

Anasema wanapobaini wameibiwa au kudhulumiwa wakihoji wahusika huwajibu kwa kebehi kwamba wao ni vipofu hawajui kitu na hawawezi kuwafanya kitu hivyo hawawezi kuwachukulia wahusika hatua sababu mara nyingine hushirikiana na watu ambao walidhani wangekuwa walinzi na wasaidizi wao.

“Hatuwezi kumchukulia mtu hatua sababu hatuoni hata kama tuna uwezo wa kuwatambua kwa sauti mtu anakana na kukuhoji, wewe unaniona, nina rangi gani? unakuwa huna la kusema.

Mimi nimezaliwa 1978 nina akili ninajua anayenitendea jema na baya wanatufanyia vile sababu hawatutaki sijui baya tulilowatendea”

Utambuzi wa fedha kwa kupapasa ni changamoto kubwa zaidi kwao mara nyingi hupewa fedha pungufu wakiamini wamepewa kubwa au wakati mwingine kurudisha albaki (chenji) kubwa kuliko ilivyostahili.

Unaweza pia kusoma

Leila ambaye kwa sasa ni bibi wa mjukuu mmoja, anasema maisha yake na mwenza wake ni ya kuhangaika kwa sababu hata yeye hana kazi ya kuaminika bali hutegemea kazi ndogondogo ambazo zina ujira duni.

“Maisha ya ndoa yanaendelea hivyo hivyo tu si unajua vijana wa siku hizi leo atakuchangamkia siku zinakwenda na wewe huoni hutafuti makubwa”

Kwa sasa wanaishi kwenye nyumba ya urithi ya babu yao na mara kadhaa wamekuwa wakiingia kwenye migogoro ya kifamilia ya mara kwa mara kutokana na wingi wao eneo moja lakini kila mmoja kuona ana haki zaidi na uhalali wa kuwepo eneo hilo zaidi ya wengine.

mm
Maelezo ya picha, Mtoto wake wa kiume ndio tegemeo lake licha ya kuwa pia naye haoni vizuri

Tumaini pekee lillobaki kwa Leila kwa sasa ni mtoto wake mvulana ambaye alikuwa anasoma shule ya ufundi Tanga ambaye ameshindwa kuendelea na masomo kutokana na kutofanya vyema kwenye mitihani ya kidato cha pili baada ya kukaa nyumbani kwa muda mrefu kutokana na kutokuwa na ada.

Mtoto huyo pia ana uoni hafifu. Licha ya jitihadi za kimatibabu zilizofanywa na wazazi wake na walimu shuleni bado hali yake haijabadilika na sasa yupo nyumbani akisubiri mama yake apate msaada kutoka kwa wasamaria wema ili aweze kurejea shuleni na kutimiza ndoto yake ya kuwa fundi umeme.

Imehaririwa na Florian Kaijage na kuchapishwa na Esther Namuhisa