Mzozo Ukraine: Kupigana nchini Ukraine ni bora kuliko kuishi Nigeria

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati Urusi ilipoivamia Ukraine mwezi uliopita, Mnigeria Ottah Abraham mwenye umri wa miaka 27 anasema alipata hasira sana.
Alichukua simu yake na kuandika katika kurasa yake ya tweeter: "Nataka kujiunga na timu ya mapambano."
Alikuwa umbali wa kilomita 8,700 (maili 5,400) kutoka eneo la vita, katika nyumba ndogo katika jiji kuu la Nigeria, Lagos.
Mhitimu huyo wa falsafa ni mmoja kati ya mamia ya Waafrika, kutoka nchi kama Nigeria, Kenya, Senegal, Afrika Kusini na Algeria, ambao wanasema wako tayari kuchukua silaha katika vita dhidi ya Urusi, ili kuepukachangamoto nyingi zinazowakabili vijana wengi.
"Tunajua kuwa ni vita, sio mchezo wa watoto," aliiambia BBC. "Lakini kuwa mwanajeshi nchini Ukraine itakuwa bora kuliko kuwa hapa.
"Labda nitaruhusiwa kubaki hapa ikiwa vita itaisha, na nitakuwa shujaa na kupigana na adui."

Watu wanaojitolea wapatao 20,000 kutoka duniani kote wameripotiwa kujiandikisha baada ya Rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky kutoa wito wa kimataifa kwa wapiganaji wa kigeni "kwenda na kuwa bega kwa bega na Waukreni".
Serikali imefuta kwa muda mahitaji yake ya viza na mshahara kwa wale walio na pasipoti halali na mafunzo ya kijeshi.
Ingawa hakujawa na uthibitisho rasmi kwamba wapiganaji wa kigeni wataruhusiwa kubaki nchini humo baada ya vita.
Kereti Usoroh, Mnigeria anayeishi katika mji mkuu, Abuja, alisema motisha zake za kujitolea hazihusiani na faida ya kifedha au matarajio ya uraia.
"Tayari ninaishi maisha ya starehe. Ikiwa ningetaka kwenda Ulaya, ningefanya hivyo kupitia elimu, sio vita," mwanasheria huyo mwenye umri wa miaka 29 alisema.
"Hii ni kuhusu kumpiga mnyanyasaji - mtu mmoja akikosa haki ni wote tumekosa."
Siku chache baada ya tangazo la Rais Zelensy, watu kadhaa wa kujitolea wenye matumaini walielekea kwenye ubalozi wa Ukraine mjini Abuja, wakiwa na nia ya kujiandikisha.
Mamluki hawakaribishwi
Lakini ubalozi wa Ukraine nchini Nigeria - kama mataifa mengine barani Afrika - imelazimika kuweka vikwazo kwani serikali nyingi za bara hilo hazitaki raia wao kupigana nchini Ukraine.
"Nigeria inalaani matumizi ya mamluki popote pale duniani na haitavumilia jambo hilo," wizara ya mambo ya nje ya Nigeria iliandika katika taarifa yake.
Bohdan Soltys, afisa wa ubalozi wa Ukraine nchini Nigeria, alisema kuwa hawatawalipa Waafrika kupigana - na watu watalazimika kulipia safari zao za ndege ili kufika Ulaya.
"Kuna utofauti kati ya wafanyakazi wa kujitolea wa kigeni na mamluki," aliiambia BBC.

Chanzo cha picha, Getty Images
Baadaye alifafanua kuwa aliagizwa kuwafukuza watu wa kujitolea waliofika katika ubalozi huo.
Senegal pia iliwaonya raia wake dhidi ya kujiandikisha katika vita hivyo na kumwamuru balozi wa Ukraine kutupilia mbali chapisho la Facebook ambalo lilikuwa limewataka watu wa kujitolea wa Senegal, akiziita harakati za kuadikisha watu ni"haramu na kinyume kisheria."
Wizara ya mambo ya nje ya Algeria ilitoa amri sawa na ubalozi wake wa Ukraine.
"Nchi yangu inasema siruhusiwi kwenda. Nilijaribu kuiandikia wizara ya mambo ya nje. Hawakunijibu, lakini nitajaribu tena," Belhadj Hani Amir wa Algeria mwenye umri wa miaka 28 aliambia BBC.
"Nataka kwenda Ukraine, lakini pia natumani kuwa vita hivi vitakwisha haraka iwezekanavyo."
Balozi wa Ukraine nchini Afrika Kusini, Msumbiji na Botswana Liubov Abravitova aliiambia BBC kwamba mamia ya watu kutoka mataifa ya kusini mwa Afrika walijitolea kupigana au kufanya kazi katika hali ya kibinadamu - lakini hakuweza kufanyia kazi ombi lao kwani alikuwa akisubiri maagizo kutoka kwenye serikali yao. Afrika Kusini ina sheria kali dhidi ya mamluki.
Kwa hakika, tovuti rasmi ya Ukraine ya kuajiri "kikosi cha kimataifa" cha watu wa kujitolea, ambacho hutoa maelezo ya mawasiliano ya balozi za ndani duniani kote, haijumuishi tena misheni katika nchi za Afrika.
Mwakilishi anayefanya kazi kwenye tovuti alithibitisha kuwa baadhi ya nchi za Afrika ziliondolewa kwa sababu ya "vizuizi vya udhibiti".
"Ndugu wa Urusi"
Algeria, Senegal na Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi 17 kati ya 54 za Afrika ambazo hazikupiga kura katika Umoja wa Mataifa kulaani uvamizi wa Ukraine, kwa sababu zilitaka kuzuia uadui wa Urusi.

Chanzo cha picha, AFP
Na Urusi si bila msaada katika Afrika. Imeongeza ushawishi wake katika bara - hasa kijeshi, kwa kusaidia nchi kama Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Libya, Mali na Sudan kupambana na waasi au wapiganaji wa Kiislamu.
Video inayodaiwa kuwaonesha wanajeshi kutoka CAR wakiapa kujiunga na "ndugu zao wa Urusi" pia imekuwa ikisambazwa mtandaoni, ingawa BBC haikuweza kuthibitisha chanzo na afisa wa serikali hajajibu ombi la maoni yake.
Ijumaa iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alisema kuwa "zaidi ya wapiganaji 16,000" kutoka Mashariki ya Kati walijitolea kupigana na jeshi la Urusi - haijulikani ikiwa hii inajumuisha yoyote kutoka Afrika Kaskazini.
Lakini huku serikali za Kiafrika zikishikilia kuwaandikisha raia wao wenyewe, haijawekwa wazi kama yeyote kati ya watu hao wataingia vitani - na afisa wa Ukraine anayehusika na kusajili watu wa kujitolea wa kigeni aliiambia BBC kwamba hakuna Waafrika waliofika.
Kukatishwa tamaa
Baadhi ya watu kama David Osagie Adeleke kutoka jimbo la Oyo kusini-magharibi mwa Nigeria, hili lilikuwa pigo kubwa.

Chanzo cha picha, Prince Nkem Nduche
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye amefanya kazi kama mhudumu wa uokoaji wa dharura wa Shirika la Msalaba Mwekundu, alikuwa akijiandaa kujiandikisha kama mpiganaji, baada ya kukusanya nyaraka zinazohitajika, ikiwa ni pamoja na barua ya mapendekezo.
"Nilikwenda moja kwa moja kituo cha polisi kuchukua nyaraka zangu," alisema na kueleza kuwa rekodi safi ya uhalifu ni mojawapo ya mahitaji ya kuandikishwa.
"Nimesikitishwa kusikia kwamba ubalozi sasa unasema hautatuchukua sisi Waafrika."
Huku barua pepe zake kwa ubalozi wa Ukraine zikirejea, anatafuta njia mbadala za kufika kwenye mpaka wa nchi hiyo.
"Nimefanya mahojiano na ubalozi wa Poland nchini Nigeria," alisema.
Prince Nkem Nduche, ambaye alikuwa miongoni mwa wale katika ubalozi wa Ukraine mjini Abuja, ana ujuzi zaidi kuliko wengi kuhusu hali ya Ukraine.
Kiukweli alikaa nchini Urusi kwa muda akiwa kijana, ana uraia wa nchi mbili na hata alijiandikisha katika chuo cha kijeshi cha Urusi - lakini alifungwa jela kwa muda mfupi, akishutumiwa kuwa jasusi baada ya kuonekana katika ubalozi wa Marekani.
Alisema aliikimbia nchi miaka saba iliyopita, kupitia Ukraine - na angepigana kwa furaha dhidi ya Urusi, lakini anakubali kuwa sivyo.
"Nilitaka kwenda peke yangu lakini kama serikali ya Nigeria ilisema hatuwezi kwenda... nitawatii," aliiambia BBC.

Unaweza kusoma pia:
- YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
- UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
- UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
- KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
- ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
- PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
- SILAHA:Mzozo wa Ukraine:Makombora ya stinger na silaha nyingine kali zinazotumiwa Ukraine
















