Urusi na Ukraine: Zijue athari za vita ya Ukraine kwa Afrika

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Ezekiel Kamwaga
- Nafasi, Mchambuzi
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson na Rais wa Marekani, Joe Biden, tayari wameeleza hatua ya Russia kuivamia Ukraine kijeshi kama "janga na doa katika masuala ya uhusiano wa kimataifa". Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameelezea uvamizi huo kama ni hatua ya mwanzo ya mlolongo wa vita zitakazofuata katika eneo la Ulaya Mashariki.
Ni rahisi kuona kwa upande wa Ulaya na Marekani ni kwa vipi uvamizi huo ni tukio la kihistoria. Tangu kumalizika kwa Vita Kuu vya pili vya Dunia 1939-1945, hakuna nchi ya Ulaya iliyoivamia kijeshi nchi nyingine na kwa kiasi kikubwa ilionekana masuala ya kupigana vita yatabaki katika vitabu vya historia pekee.
Hotuba ya Rais Vladmir Putin alfajiri ya Februari 24 mwaka huu imebadili upepo. Katika hotuba yake ya kutangaza uvamizi, Rais huyo wa Russia alitoa sababu kubwa mbili za uvamizi - mosi kutimiza matakwa ya kimkakati ya kijeshi na pili kuondoa hatari ya siasa za kibaguzi kwa nchi hiyo jirani.
Katika dunia ya sasa ya utandawazi, ni wazi kwamba eneo muhimu kidunia kama Ulaya Mashariki likipata 'chafya' ya namna hii, ni lazima maeneo mengine dunia yashikwe na 'mafua'. Pasi na shaka yoyote, Afrika, kama ilivyo kwingineko duniani, itaathirika na mgogoro huu.
Ni kwa vipi Afrika itaathirika?
Mpaka sasa, sauti kubwa rasmi ambayo imepigwa na Afrika kuhusiana na mgogoro wa Ukraine ni hotuba ya Mwakilishi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa (UN), Martin Kimani, aliyeonya kwamba hatua ya Urusi kutoheshimu mipaka iliyowekwa kwa sheria za kimataifa ni hatari kwa amani na utulivu wa dunia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukraine ilikuwa sehemu ya Urusi ya Kisovieti kwenye miaka ya nyuma na Kimani alionya kwamba kwa bara kama la Afrika ambalo mipaka baina ya nchi zake iliwekwa na wakoloni, Russia inaweza kuchochoea nchi nyingine nazo ziamue kuvamiana kwa kuzingatia historia za miaka ya nyuma badala ya taratibu za kisasa zinazohusika na masuala ya mipaka.
Huo ni upande mmoja wa shilingi. Matatizo ya mipaka yanaweza kutokea kwenye miaka ijayo lakini kwa sasa - kwa wakati huu ambapo tayari vita vimelipuka huko Ukraine, Afrika tayari imeingia katika matatizo ambayo haikuwa nayo mwishoni mwa mwaka jana.
Jambo la kwanza ambalo litaanza kuiumiza Afrika ni kupanda kwa bei za mafuta. Mara tu baada ya kuanza kwa vita, bei ya mafuta tayari imepanda kufikia zaidi ya dola 100 kwa pipa - kiwango kikubwa zaidi cha kupanda kwa bei tangu mwaka 2014. Urusi ni miongoni mwa wasambazaji wakubwa wa nishati ya gesi na mafuta duniani na mgogoro huu utaathiri uzalishaji wake ama kwa vikwazo ambavyo tayari vimewekwa na taifa moja moja kama vila Marekani na Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya au kwa changamoto za kivita.
Afrika tayari inapitia katika kipindi kigumu kiuchumi. Wiki iliyopita, BBC Swahili iliripoti kuhusu kupanda kwa gharama za uchumi nchini Kenya kiasi cha kuzua malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi. Ni wazi kupanda kwa bei ya mafuta kutaongeza bei zaidi ya bidhaa mbalimbali na kufanya hali kuwa ngumu zaidi.
Wiki tatu zilizopita, Waziri wa Nishati wa Tanzania, January Makamba, alionya bungeni jijini Dodoma kuhusu uwezekano wa kupanda zaidi kwa bei ya mafuta kutokana na mgogoro huu. Kupanda kwa bei ya mafuta huanzisha mnyororo wa kupanda kwa bei za uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa. Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba sasa nchi zitalazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza mafuta kuliko kawaida na hili huathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kwenye mambo mengine muhimu.
Hali ni mbaya zaidi Kaskazini mwa Afrika

Chanzo cha picha, BASHIR AHMED/TWITTER
Pengine kuliko eneo lolote la Afrika, upande wa Kaskazini utaathirika zaidi kiuchumi na vita hivi kuliko eneo lingine lolote. Jambo la kwanza kuzingatia ni kwamba kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Kilimo ya Marekani, kabla hata ya vita hivi, viwango vya mfumuko wa bei vilivyopo sasa katika eneo hilo vinakaribiana na vile vilivyokuwepo wakati wa mapinduzi yaliyopewa jina la Arab Springs takribani miaka 11 iliyopita.
Urusi na Ukraine ndiyo wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Misri, nchi yenye watu wengi na ushawishi mkubwa zaidi katika eneo la Kaskazini mwa Afrika ndiyo mwagizaji mkuu wa ngano duniani. Ngano ni muhimu kwa taifa hilo kiasi kwamba waandamanaji waliomng'oa madarakani Rais Hosni Mubarak walikuwa wakililia zaidi mambo mawili tu; mkate na uhuru.
Uagizwaji wa bidhaa na nafaka nyingi kutoka Urusi na Ukraine hufanyikia kupitia Bahari Nyeusi (Black Sea) na kama vita hivi vitasababisha vikwazo au masharti ya usafirishaji kupitia njia hiyo, itabidi njia nyingine itafutwe. Hilo litaongeza gharama maradufu kwa kutumia njia tofauti katika mazingira ambayo bei tayari zitakuwa zimepanda.
Tayari Mpango wa Chakula Duniani (WFP) umeonya kwamba mgogoro wa Urusi na Ukraine unaweza kuwa na athari mbaya za kupandisha bei za vyakula na kusababisha njaa kwa masikini katika eneo la Kaskazini mwa Afrika. Taarifa iliyotolewa na WFP hivi karibuni iliweka bayana kwamba pengine huu ni wakati mbaya zaidi kuwa na mgogoro wa kivita kwenye eneo muhimu kwa uzalishaji wa chakula.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika eneo la Afrika Mashariki, Kenya itapata pia athari za kiuchumi. Yenyewe ni mwagizaji mkuu wa ngano kutoka Urusi katika ukanda huu lakini yenyewe pia ni muuzaji mkubwa wa chai yake kwa taifa hilo. Mwaka 2021 pekee, Kenya iliuza chai yenye thamani ya shilingi za Kenya bilioni 6.2 kwa Urusi katika kipindi cha kati ya Januari mpaka Novemba 2021. Biashara hii sasa inaingia shakani kutokana na vita hivi.
Masuala ya Kijeshi, Diplomasia na Usalama kwa Afrika
Vita ya Russia na Ukraine vinaliweka bara la Afrika katika nafasi ngumu kwenye uhusiano wake na nchi kubwa duniani. Ingawa inaonekana kama ni mgogoro baina ya nchi mbili, lakini huu ni mgogoro kati ya Russia na nchi za Magharibi.
Katika miaka ya karibuni, Urusi imeanza kujitanua Afrika. Imeanza kutoa misaada ya kijeshi kwa nchi za Afrika kuanzia katika eneo la Mashariki, Pembe ya Afrika na Afrika ya Kati. Nchi nyingi za Afrika tayari zina makubaliano na mikataba ya kijeshi na nchi za Magharibi kama Uingereza na Marekani ambazo ziko tofauti na Urusi kwenye mgogoro huu.
Isivyo bahati, Afrika haina nchi yenye hadhi ya taifa kubwa (super power) na kuchagua upande katika mgogoro huu si jambo lenye afya kidiplomasia. Namna pekee ya kuendelea kubaki na marafiki wote ni kufuata siasa za kutofungamana na upande wowote. Kwa namna hii, nchi za Afrika zitakuwa na urafiki wa kuendelea na mikataba na makubaliano yake ya awali na mahasimu wote wanaopambana katika vita hii.

Chanzo cha picha, AFP
Tatizo kubwa zaidi kwa Afrika sasa litakuwa ni namna mgogoro huu utakavyohamisha matatizo yote ya dunia katika eneo moja. Kihistoria, maisha ya watu wa Ulaya huwa na thamani kuliko ya Waafrika au kwingine duniani na hili litafanya jitihada zote za masuala ya haki za binadamu, njaa, ulinzi na usalama kuangalia kwenye eneo hilo la Bahari Nyeusi.
Hii maana yake ni kwamba maeneo kama Sudan, Somalia, Sudan Kusini, Mali, Msumbiji na kwingine ambako kulianza kutazamwa kwa kina, sasa kutapunguzwa umuhimu wakati jamii ya kimataifa ikitazama Ukraine. Ni vigumu kubashiri kwa kina nini hasa itakuwa athari ya hili kwenye masuala ya ulinzi na usalama kwa Afrika.
Kwa sababu Urusi na Ukraine ni ndugu, hakuna msemo wa Kiswahili unaosadifu nyakati hizi kama ule usemao; "ndugu wakigombana chukua jembe ukalime, na wakipatana chukua kapu ukavune". Huu ni wakati wa Afrika kujikita kwenye mambo ya kuondoa utegemezi wa nafaka na mazao kutoka Ulaya, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kutumia vyema akiba yake ya fedha za kigeni iliyopo.
Jambo moja ambalo liko wazi ni kwamba chafya ya Ukraine tayari italeta mafua makali.













