Mzozo wa Ukraine na Urusi: Bei za mafuta zapanda kutokana na hofu ya usambazaji, huku mataifa yakiiwekea vikwazo Urusi

Petrol pump

Chanzo cha picha, Getty Images

Bei ya mafuta na gesi ilipanda Jumanne kwa hofu kwamba mzozo wa Ukraine na Urusi utatatiza usambazaji kote ulimwenguni.

Bei ya mafuta yasiyosafishwa ilipanda zaidi kwa miaka zaidi ya dola 99 (£73) kwa pipa baada ya Rais Vladimir Putin kuagiza wanajeshi kuingia mashariki mwa Ukraine.

Lakini bei baadaye zilidhibitiwa, licha ya nchi za Magharibi kutangaza vikwazo vya kiuchumi na hatua za kuzuia bomba kuu la gesi la Urusi.Hisa pia zilisababisha hasara ya mapema.

Baada ya kushuka kwa zaidi ya asiliamia 1.5 katika biashara ya mapema Jumanne, Wall Street ilirejea shughuli kufuatia matamshi ya Rais wa Merika Joe Biden akielezea majibu ya Marekani. Hisa za Dow zilifunga kwa asilimia 1.4, hata hivyo hisa za S&P 500 zilishuka kwa asilimia 1 huku za Nasdaq zikianguka kwa asilimia 1.2.

Hapo awali, soko la hisa la Japan lilifunga kwa asilimia 1.7 chini, na la China likipungua karibu asilimia 1, huku masoko la hisa huko Ulaya na Uingereza yakifunga .

Maumivu upande wa mafuta

Urusi ni nchi ya pili kwa mauzo ya mafuta nje ya nchi baada ya Saudi Arabia na mzalishaji mkuu wa gesi asilia duniani.

Hatua za kulazimisha nchi kupunguza uzalishaji mafuta yasiyosafishwa au gesi asilia zitakuwa na "madhara makubwa" kwa bei ya mafuta na uchumi wa dunia.

"Uamuzi wa Urusi kuivamia Ukraine tayari unasababisha bei ya mafuta kupanda na bila shaka itasababisha kupanda kwa bei ya mafuta hadi pauni 1.50 kwa lita [ya petroli isiyo na risasi]," kulingana na msemaji wa kampuni ya mafuta ya RAC Simon Williams.

"Hii inaleta habari mbaya kwa madereva nchini Uingereza wanaotatizika kumudu kuweka mafuta kwenye magari yao."

Lakini hatua zilizotangazwa na Marekani, Uingereza na Ulaya kufikia sasa hazifikii kile kilichotishiwa katika tukio la uvamizi.

Vikwazo hivyo vinalenga taasisi za fedha, wasomi na mashirika mengine ya serikali nchini Urusi, kwa sehemu ikilenga kuzuia uwezo wa serikali ya Urusi kukusanya pesa kwenye masoko ya fedha ya Magharibi.

Siku ya Jumanne, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz pia alichukua hatua muhimu ya kuzuia uidhinishaji wa bomba la Nord Stream 2 ambalo lingesambaza gesi moja kwa moja kutoka Urusi hadi Ujerumani.

"Ikiwa Urusi itaendelea zaidi na uvamizi huu, tunasimama tayari kwenda mbali zaidi," Rais wa Marekani Joe Biden alisema katika hotuba yake kutoka Ikulu ya White House.

Pia alionya kuwa kutetea eneo la Nato kunaweza kuwagharimu umma kwa njia ya bei ya juu ya nishati.

A Ukrainian service member uses a periscope while observing the area at a position on the front line near the village of Travneve in Donetsk region

Chanzo cha picha, Reuters

Tangu mwanzo wa mwezi Februari, bei ya mafuta tayari imepanda kwa zaidi ya asilimia 10 wakati wa mvutano.

Maike Currie, mkurugenzi wa uwekezaji huko Fidelity International, alisema bei ya mafuta inaweza kupanda hadi zaidi ya dola 100 kwa pipa kutokana na mgogoro wa Ukraine, majira ya baridi kali nchini Marekani, na ukosefu wa uwekezaji katika usambazaji wa mafuta na gesi duniani kote.

"Urusi inachangia moja kati ya mapipa 10 ya mafuta yanayotumiwa duniani kote, hivyo ni mhusika mkuu linapokuja suala la bei ya mafuta, na bila shaka, itawaumiza watumiaji kwenye pampu za petroli," alisema.

Mpango wa Urusi kukabiliana na vikwazo vipya

Urusi imetumia miaka mingi kujiandaa kwa wakati huu.

Mnamo mwaka wa 2014, wakati wanajeshi wa Urusi walipohamia Crimea, na kuteka sehemu ya Ukraine, ilizua raundi ya kwanza ya vikwazo vya kimataifa, na hiyo ikawa fundisho muhimu kwa Urusi.

Tangu wakati huo imekuwa ikiweka ulinzi, ikiacha kutegemea dola, na kujaribu kuukinga uchumi wa Urusi kutokana na vikwazo.

Rais Putin anaweza kuwa anaweka dau kuwa anaweza kustahimili vikwazo kwa muda mrefu zaidi ya inavyodhaniwa na nchi za Magharibi.

Sehemu kubwa ya mafuta na gesi ambayo Uingereza inaagiza haitoki Urusi, lakini itaathiriwa na kupanda kwa bei ya kimataifa.

Bei ya wastani ya dizeli nchini Uingereza ilifikia 152.51p kwa lita siku ya Jumatatu, chini ya rekodi ya Jumapili ya 152.58p.

Bei ya jumla ya gesi ya Uingereza pia imepanda, bei ya Uingereza kwa utoaji wa Aprili imeongezeka kwa asilimia 9.

Utegemezi wa kiuchumi kati ya Urusi na Ulaya huenda ukazuia hatua za Magharibi kuendelea, alisema Shaistah Akhtar, mtaalamu wa sheria za vikwazo kutoka kampuni ya sheria ya Uingereza Mishcon de Reya.

Edward Gardner, mchumi wa bidhaa katika Capital Economics alisema mvutano huo huenda ukafanya bei ya mafuta iwe juu, hata kama nchi za Magharibi hazitachukua hatua kali zaidi.

"Si kwa maslahi ya kiuchumi ya Urusi au Magharibi kutumia biashara ya nishati kama silaha dhidi ya kila mmoja, lakini hiyo haimaanishi kuwa haitafanyika," aliandika katika barua Jumanne.

"Hata kama nchi za Magharibi hazitatekeleza vikwazo vya moja kwa moja kwa mauzo ya nje ya nishati ya Urusi, mvutano na Urusi unaweza kuweka bei ya mafuta kuwa juu kwa muda mrefu."