Madaktari Uganda wathibitisha Judith kutolewa figo akiwa kwa mwajiri wake Saudi Arabia

m

Madaktari nchini Uganda wamethibitisha kuwa mwanamke aliyekuwa akifanya ya nyumbani nchini Saudi Arabia, aliondolewa figo yake ya kulia na sio ajali ya gari kama ilivyoarifiwa awali na mwajiri wake.

Wizara ya mambo ya ndani nchini humo imethibitisha hilo, baada ya kupewa ripoti ya uchunguzi kutoka Hospitali kuu ya kitaifa ya Mulago.

Kufuatia taarifa hiyo ya uchunguzi sasa familia ya mwanamke huyo inaiomba serikali kusimamia suala hilo hadi haki itakapopatikana.

Judith Nakintu mwenye umri wa miaka 38 ana watoto watano na alichukuliwa na kampuni ya Nile Treasure Gate mnamo mwaka 2019 kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za nyumbani huko Jeddah nchini Saudi Arabia.

Baada ya kufanya kazi karibu miezi miwili, mawasiliano yake na familia yake yalikatika, ndipo mama yake mzazi alipoanza kufuatilia karibu miezi mitatu ndipo akaambiwa mwanae amepata ajali.

'Alitufahamisha kwa simu kwamba alipata ajali nilikuwa nataka kufahamu familia yake, nikamuuuliza alipata ajali bila kampuni iliyompeleka kujua? Nikawapigia simu kampuni yake nikawaeleza, wakasema hawana habari wala taarifa', alisema mama huyo.

Kampuni ya Nile Treasure Gate ilimpigia mama wa Nakintu simu…mnamo tarehe 30 Oktoba 2021. Mwanae alikuwa anatarajia kuwasili katika uwanja wa ndege wa Entebe siku hiyo. Aliondoka mpaka kwenye uwanja huo wa ndege kwa ajili ya kumpokea mwanae.

Alipowasili alimuona mwanae akiletwa kutoka kwenye ndege akiwa kwenye kiti cha wagonjwa cha magurudumu, hawezi kutembea na kuingizwa kwene gari la wagonjwa hadi Hospitali kuu ya Mulago.

Maelezo ya sauti, Masaibu ya wana Afrika Mashariki waliokwenda uarabuni kutafuta ajira

Kesho yake wakaruhusiwa kwenda nyumbani, lakini yeye hakuamini ripoti aliyopewa.

'Tulipolala hospitali maafisa wa kampuni waliyomchukua wakamleta daktari kufanya uchunguzi wa wa kitabibu wakasema yupo sawa hana tatizo, mimi sikuridhishwa, siku ya Jumatatu nikarudi Mulago wakamfanyia uchunguzi upya nikaambiwa figo moja imetolewa', alisema mama huyo.

Afisa mratibu wa kuzuia ulanguzi wa binadamu kutoka Idara ya Uhamiaji Uganda, Agness Igoye, amewaeleza waandishi wa habari kwamba, Hospitali kuu ya Mulago imethibitisha kwamba alitolewa figo moja.

Uchunguzi wa madaktari nchini Uganda umethibitisha figo yake ya kulia ilitolewa , uchunguzi wa awali wa Polisi umetambua muajiri wake wa nchini Saudi Arabia kwa jina la Sadaffa Muhamed, alitoa ripoti bandia za kitabibu kuwadanganya wanafamilia ya muathiriwa. Zilionyesha sehemu zake zote za viungo zipo sawa wakati sio kweli'.

Ripoti ya awali kutoka Polisi wa Saudi Arabia zilionyesha Nakintu ambaye amepooza, alipata ajali .

Maelezo ya video, Kwanini wasichana wa Uganda wanavuka mpaka kutafuta kazi Kenya?

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na mtandao wa Indepent nchini Uganda, Kampuni ya Nile Treasurer, siku chache baadaye ilipokea taarifa kuwa watoto wawili wa waajiri hao wamefariki dunia kutokana na ajali hiyo, bahati nzuri Nakintu alinusurika ingawa ameumia sana na kusababisha damu yake kuganda.

Kwa upande wake, Rais wa Migrant Workers Voice, inayoshughulikia masuala ya wafanyakazi wahamiaji, Abdallah Kayonde, amesema ameiandikia Kampuni hiyo kulipa fidia ya shilingi milioni 600 za Uganda kwa kitendo cha kutolewa figo ya muathirika huyo kinyume cha sheria na kuuzwa.

Hata hivyo Kampuni hiyo imenukuliwa ikipinga kuhusika na kutolewa kwa figo ya mwanamke huyo.