Edward Lwidiko: Simulizi ya daktari anayeleta mapinduzi ya kisayansi Tanzania

    • Author, Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC Swahili

Inawezekana kizazi cha sasa kinaweza kuvutiwa na masomo ya sayansi zaidi kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma…

Licha ya kwamba ilikuwa ni kawaida miaka ya nyuma kuona watoto wakijijengea nyumba za matope au kutengeneza vitu vya udongo kama vile watu, vyungu na kadhalika katika michezo yao ya kila siku.

Kwa sasa ni nadra kuona michezo ya aina hiyo watoto wakicheza mtaani.

Baadhi ya maeneo nchini Tanzania ilikuwa mtoto au kijana kuona maabara kwa mara ya kwanza ni mpaka aanze kidato cha kwanza na wengine wanaweza wasizione kabisa labda waende hospitali kwa ajili ya kupata tiba.

Hata hivyo kukua kwa teknolojia kumeweza kubadilisha hali ya maisha kwa baadhi ya jamii, kuanzia watoto mpaka wakubwa.

Lakini nini kinachorudisha nyuma matamanio yao ya ubunifu na kuwa wanasayansi

Ni kawaida kwa shule kuwa na safari za vitendo katika somo kama la historia; baadhi ya shule hutembelea makumbusho, kwenye upande wa siasa wanatembelea bunge na shule nyingi wanatembelea mbuga za wanyama.

Lakini sasa masomo ya sayansi nayo yanamabadiliko yake, Tanzania sasa ina kituo kikubwa cha sayansi ambacho kinawapa fursa watoto kujifunza kwa vitendo masomo ya sayansi.

STEM Park- ikiwakilisha teknolojia, Uhandisi, hesabu na sayansi.

Hii ni 'ndoto iliyotimia' ya daktari wa kitanzania, Edward Lwidiko.

Dkt.Edward Lwidiko ni muasisi wa mradi wa vijana wa Project Inspire anaongoza mabadiliko haya kwa kutumia taaluma yake , na anataka kizazi kijacho kiwe na mwanga mpya kwenye taaluma ya sayansi, teknolojia , uhandisi na hesabu.

Kwanini kituo cha sayansi kwa watoto ni muhimu?

Dunia ikiwa kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda, bila shaka Sayansi na Teknolojia inachukua nafasi kubwa na mataifa yanayoendela kama Tanzania imeonekana kuchukua hatua ya kutokubaki nyuma katika kuhakikisha vizazi vijavyo vinakuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu ndani ya mabadiliko na kazi zao za kiubunifu Ulimwenguni.

Edward Lwidiko ni daktari wa binadamu anaendesha mradi unaochochea sayansi na teknolojia kwa vijana wadogo wa Kitanzania ujulikanao kama 'Projekt Inspire', kikiwa ndio kituo cha kwanza cha Sayansi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Dkt. Lwidiko anasema aliona kulikuwa na haja ya watoto kujifunza kwa njia rafiki zaidi.

Fursa alizokosa wakati anakuwa ni moja ya chachu iliyomsukuma kuanzisha kituo cha aina hiyo.

Anasema akiwa Sweden akisomea masomo ya sayansi, aliona watoto wengi wa nchi hiyo wakiwa wanapewa mafunzo kwa vitendo.

"Kwenye pita pita zangu huko duniani nilipata kuona watoto wakijifunza kwa vitendo kwenye vituo maalum vya sayansi, ni kitu cha kawaida huko Ughaibuni nikaona Tanzania inaweza ikapata fursa ya kuwa na kituo kama hicho kwa kuzingatia mazingira yake." Dkt. Lwidiko anaeleza.

Wataalamu mbalimbali katika bara la Afrika wamekuwa mstari wa mbele katika kusaidia watu kutoka kwenye jamii zao kufahamu kuhusu umuhimu wa sayansi na teknolojia, lakini bado kwenye mitaala ya elimu pamoja na sheria imeendelea kurudisha nyuma juhudi hizo.

Una maana gani unaposema ni kituo cha kwanza kikubwa cha sayansi kwa watoto Afrika Mashariki?

Kituo cha sayansi cha Projekt Inspire chenye uwezo wa kupokea vijana wadogo zaidi ya 1000, huku wakiamini kuwa ipo haja ya kuibua ile hali ya sayansi ndani yao kwani kila mtoto ni mwanasayansi.

Udadisi unaofanywa na vijana wadogo watu wengi ni vigumu kutilia maanani, ila ndio chimbuko la sayansi lenyewe, Lwidiko anasema kuwa kichochezi kikubwa ni kuwa mtu yeyote amezaliwa kufahamu jambo lolote kwa undani na pengine hata ni la hatari kiasi gani atatamani kujua kwa kujaribu ili kupata majibu zaidi.

"Vijana wadogo ni wanasayansi tangu wanazaliwa, unapomtazama mtoto namna anavyoyaangalia mazingira yake vitu vilivyo mbele yake ataona moto ni lazima atajiuliza anachokiona ni kitu gani hapo anakuwa ametengeneza swali la kisayansi." Ameongeza Lwidiko.

Jamii nyingi zimekuwa kikwazo katika kuchochea sayansi na hii ni kutokana na tabia ya kidadisi ambayo inatambulika kuwa ni hatari hasa kwa vijana wadogo.

Kituo hicho kina miaka mitano sasa, na kinatumia wataalamu wa sayansi kuwafundisha vijana wadogo, utaratibu wao wa kutumia elimu ambayo wanaisoma darasani na kuiweka kwenye vitendo, wazazi wameonekana kuwa karibu zaidi na kushawishika kupeleka watoto wao.

"Watoto kuanzia umri wa miaka 12 kushuka chini na pia watoto wa Sekondari ambao wanakuja na mawazo yao ya kisayansi na kiteknolojia na sisi tunatengeneza mazingira tunawapa vifaa ambavyo wanaweza wakatumia kujifunza,"

Vitu vinavyopatikana kwenye mazingira ya kila siku na yanayomzunguka mtoto ndio elimu ya sayansi kwa vitendo inayofundishwa na hapa wanaeleza kwa undani, pia vitu ambavyo havina madhara hasa pale wanapotumia kemikali.

Projekt Inspire inavyochochea ufaulu wa masomo ya sayansi

Wazazi wengi ambao watoto wao wamekuwa wakishiriki kwenye kituo hicho wamekuwa wakitoa ushuhuda wa namna vijana wao walivyobadilika, hatahivyo ukuaji wa ubunifu baina ya watoto.

Uanzishwaji wa programu maalum ya katika shule za sekondari ambayo huandaa kambi za sayansi kila mwaka, " mwaka huu tuna mpango wa kuandaa kambi kwenye kituo chetu cha sayansi."

Ikiwa bado Dunia inapitia changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, nchi nyingi Ulimwenguni zimekuwa zikihimizwa kutumua umeme mbadala kutoka kwenye vyanzo ambavyo haviharibu mazingira kama umeme wa maji, kituo kiliibua watoto ambao walionesha nia yao katika mabadiliko hayo.

"Kuna mmoja alitengeneza 'solar pump' ambayo inatumia umeme wa jua kwaajili ya kuvuta maji ili kupunguza visima vilivyokuwa wazi ambavyo havikuwa salama." amesema Lwidiko.

Suluhisho la matatizo kutoka kwenye mtandao wa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati

Matatizo ya mataifa mengi, kama Tanzania yanaweza kutatulika hasa yale yanayohitaji zaidi elimu na utalaamu wa kisayansi, Dkt.Lwidiko anasema kuwa njia pekee ni kutambua kuwa sayansi inao uwezo na pia uwezashaji wa kuibua na kufanyia kazi matatizo ndio suluhisho pekee.

Wazazi wanazungumziaje mapinduzi haya ya kisayansi

Florence Kitunga , ni mzazi ambaye huwa anampeleka mtoto wake katika kituo hicho cha STEM Park mkoani Tanga anasema kituo hicho kimewasaidia wazazi na watoto.

"Kituo kimekuwa msaada mkubwa kwa watoto katika tasnia ya sayansi, tumeona utofauti kwa watoto katika kujituma, kujiamini na kjitegemea na vilevile kituo kimekuwa msaada kwa watoto wakati wa likizo katika kujiepusha na mazingira magumu na kuzingatia elimu zaidi."

Anthony Mhina anasema yeye kama mzazi anaona ni wakati muafaka sasa kwa shule kuanzisha mitaala ya elimu ya vitendo kwa kuzingatia mazingira na uhalisia wa maisha ambayo tunayoishi sasa.

Anasema ni muhimu mtoto kujifunza kwa vitendo badala ya kusubiri mpaka amalize chuo kikuu, "ni vyema kuwa na vituo kama hiki cha StemPark lakini shule nazo zinapaswa kufuata mkondo huo".

"Umuhimu wa wanafunzi kujifunza kwa vitendo upo tena sana, tuchukulie mfano wazazi ni wajasiriamali, watoto wanakuwa wakiwaona wazazi wakiwa wanafanybiashara tangu wakiwa wadogo, licha ya kujifunza shuleni kuhusu biashara ila nyumbani anajifunza biashara na kutunza fedha, hivyo utaona wazi mtoto anajifunza kwa kuona na inaweza kurahisisha upatikanaji ajira na utendaji wake," Anthony anaeleza.