Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Urusi imeweka idadi kubwa ya Majeshi na Vifaa mpakani na Ukraine - Je inajiandaa kulivamia taifa hilo?
Wakati dunia ikiendelea kushuhudia mzozo wa wahamiaji katika mpaka wa Belarus na Poland, hali nyingine ambayo inaweza kuleta mtafaruki inatokea mashariki mwa Ulaya.
Kwa siku kadha, Urusi imeanza kuongeza idadi ya wanajeshi na silaha zinazoenda katika mpaka wa Ukraine, kufikia mpaka serikali nyingine ikiwemo Marekani na Umoja wa Ulaya kutoa angalizo la shambulio wakati wa baridi.
Kiev na Moscow wamekuwa katika vita kwa kipindi cha zaidi ya miaka saba wakati Putin alipoivamia na kuiteka Crimea na mgogoro wa mpakani huku wanajeshi wa Urusi wakiwa katika eneo hilo kila mara.
Uhalisia ni kuwa msimu uliopita ,angalizo lilitolewa wakati Urusi ilipopeleka silaha katika mpaka wa Ukraine.
Hata hivyo , vyanzo kadhaa vya kijasusi vya nchi za magharibi vimeeleza wasiwasi wao kuhusu hali ilivyo kwa sasa.
Wizara ya Ulinzi ya Ukraine inakadiria kuwa zaidi ya wanajeshi 114,000 wa Urusi wamepelekwa katika eneo la mpaka kaskazini-mashariki, mashariki na kusini mwa Ukraine, ikiwa ni pamoja na askari wa kawaida 92,000 , wanaanga na wanamaji.
Wiki iliyopita Washington ilidai kuwa na ripoti za kijasusi ambazo zilionesha kwamba Kremlin ilikuwa "inajiandaa kwa uvamizi" na siku ya Jumatatu mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, alitoa wito wa kuzingatia "mkusanyiko mkubwa wa jeshi la Urusi.
Tunaona mkusanyiko usio wa kawaida wa askari na tunajua kwamba Urusi imekuwa tayari kutumia aina hii ya uwezo wa kijeshi kabla ya kufanya vitendo vya kichokozi dhidi ya Ukraine," Stoltenberg alisema katika mkutano wa waandishi wa habari.
Siku ya Jumanne, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alizungumza na mwenzake wa Urusi kueleza namna ambavyo Ufaransa iko tayari "kutetea mamlaka ya eneo la Ukraine," wakati Ujerumani pia ikionya "matokeo makubwa" katika tukio ambalo Moscow ilishambulia nchi hiyo jirani.
Awali, mkuu wa Majeshi ya Uingereza, Jenerali Nick Carter, aliliambia gazeti la Times kwamba Uingereza inapaswa "kuwa tayari" kwa vita na Urusi.
Ikulu ya Kremlin haijakanusha hatua hizo za kijeshi, lakini imesema mapendekezo ya uchochezi na imeilaumu NATO kwa kufanya mazoezi ya kijeshi katika pwani ya Crimea.
Vita vya mwaka 2014, ambavyo vilisababisha Urusi kuivamia Crimea, hadi sasa vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 14,000, kulingana na takwimu rasmi.
Pande hizo zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano hayo zaidi ya mwaka mmoja uliopita, ambapo walipunguza kasi ya ya mzozo huo.
Hata hivyo, majira ya kiangazi, Kremlin ilifanya mazoezi ya kijeshi huko Crimea na kisha kutumwa kwa vifaa vizito vya kijeshi karibu na eneo la Dombás, eneo la mpaka mashariki mwa Ukraine ambako mzozo ulianza.
Wiki chache baadae walizirudisha silaha zao.
"Wakati huu ni mgumu zaisi kuelezea upelekwaji wa idadi kubwa ya silaha nzito kutoka katikati ya mji hadi magharibi ambako ni karibu na mpaka wa Ukraine," Zhanna Bezpiatchuk , mwandishi wa BBC huko Kiev .
Kwa mujibu wa Bezpiatchuk, ambaye aliripoti kuhusu upelekwaji wa jeshi katika eneo hilo anasema, kwa upande mwingine mazoezi na harakati za kijeshi zilikuwa zinaendelea ingawa operesheni hiyo mpaka sasa haijawekwa wazi kuwa ya nini.
Ripoti ya hivi karibuni kutoka Carnegie Endowment for International Peace imebaini kuwa "ukifanya uchunguzi kwa makini"kwa viongozi wa Urusi kuhusu Ukraine wanapendekeza kila upande ina uhalali wa jeshi lao kukaa katika eneo hilo.
"Viashiria vya muda mfupi na vya muda mrefu vinapendekeza kwamba Kiev na Washington zina sababu nzuri ya kuwa na wasiwasi," maandishi hayo yalisema.
Bezpiatchuk anabainisha kuwa, pamoja na hali ya uvamizi "kwa kisingizio cha kutetea raia wa Urusi" wanaoishi katika maeneo yanayodhibitiwa na Moscow, Kremlin pia inaweza kutaka kuishinikiza Ulaya kusamehe bomba la gesi la Urusi la North Stream-2 kutoka kwa mamlaka za Ulaya. .
Jumanne hiyo, mdhibiti wa nishati wa Ujerumani alisimamisha uidhinishaji wa bomba la gesi lenye utata linalotoka Urusi hadi Ujerumani, ikizingatiwa kuwa kabla ya kuthibitishwa lazima lizingatie sheria za ndani.
Urusi imesema nini?
Serikali ya Urusi imehoji kile inachokichukulia kama mhemko wa nchi za Magharibi na kuhoji sababu ya harakati za kijeshi ya hivi karibuni ya jeshi la NATO katika pwani ya Black Sea.
Katika muonekano wa televisheni ya taifa mwishoni mwa juma, rais Vladimir Putin alisema Moscow ilikuwa na wasiwasi kuhusu mazoezi ambayo hayajatangazwa kwa kile kuhusisha kikundi chenye nguvu cha wanamaji, na wana anga ambao walikuwa wamebeba silaha za nyukila.
Katika maoni yake , hii iliwakilisha changamot kubwa ya Urusi.
"Mna hisia kwamba hawatatuacha tulete ulinzi wetu. Naam, wajue kwamba hatutapunguza ulinzi," aliongeza.
Uhusiano kati ya Moscow na NATO umekuwa mbaya katika wiki za hivi karibuni, baada ya Kremlin kusimamisha kazi yake katika makao makuu ya baraza hilo huko Brussels Oktoba 18, baada ya muungano huo kuwafukuza wawakilishi wanane wa Urusi wanaotuhumiwa kwa ujasusi.
Ukraine ilisema nini?
Bezpiatchuk anasema kuwa serikali ya Ukraine iliacha siku zipite wakati huu kabla ya kuanza harakati zake.
"Ilichukua siku 10 kuthibitisha mkusanyiko wa askari," anasema.
Watu mbalimbali katika serikali ya Ukraine akiwemo rais na maafisa wakuu wamejitokeza kuihoji Urusi kuhusu harakati hizo za wanajeshi.
"Imekuwa kawaida kwa Ukraine kwa miaka saba kuishi na vitisho kutoka kwa Urusi. Labda matukio ya hivi karibuni yanaonesha namna ambavyo Ukraine imechoshwa na vita ," anasema Bezpiatchuk.
Rais wa Ukraine Vlodomir Zelensky ameomba uungwaji mkono kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kimataifa katika kukabiliana na kutumwa kwa jeshi la Urusi.
Mvutano uliopo katika eneo la Dombás pia unaongeza wasiwasi katika eneo la Dombás katika siku za hivi karibuni, baada ya Oktoba 26, jeshi la Ukraine kuthibitisha kwamba limetumia ndege isiyo na rubani iliyotengenezwa Uturuki, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Kiev kutumia teknolojia hii katika mapigano na kusababisha maandamano huko Moscow.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alilaani uuzaji wa ndege zisizo na rubani za Uturuki kwa Ukraine na kuzingatia kuwa kupatikana kwao "kumeyumbisha" hali ya eneo hilo.
Kwanini kinachoendelea Belarus ni muhimu kujua?
Wakati haya yakiendelea katika mpaka wa mashariki mwa mpaka wa Ukraine upande wa kaskazini, mzozo wa wahamiaji wa Belarus pia unaangaliwa kwa wasiwasi.
Wiki iliyopita , waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alisema nchi yake inahofia Urusi na Belarus kutumia kigezo cha wahamiaji kuanzisha operesheni Ukraine.
"Tumeona huko nyuma vikosi vya Urusi katika mipaka ya Ukraine wakitumia kisingizio cha uchochezi na kisha kuvamia wakati ni jambo ambalo walipanga kwa muda mrefu," anasema Blinken.
Lakini kwa mujibu wa Bezpiatchuk, anasema hatari haiishii hapo.
Na Ukraine ina mpaka wa zaidi ya kilomita 1,000 km kuelekea Belarus ambao una mabwawa, visima, misitu na mashamba. Hakuna vikwazo vinavyowazuia katika mpaka huu na kiukweli , ni rahisi sana kuingia katika himaya ya Ukraine ukitokea Belarus.
Mwandishi wa BBC anasema, hali hiyo inafanya taifa hilo kuwa hatarini kama rais wa Belarus, Alexander Lukashenko atawaelekeza wahamiaji Ukraine.
"Hali hii inashindwa kueleweka na wengi nchini Ukraine iwapo Poland atafunga mipaka yake na wahamiaji kupoteza nafasi ya mwisho ya kuvuka na kuingia Umoja wa Ulaya. Basi watatafuta hifadhi Ukraine eneo ambalo walikuwa wanapita tu ," alisema.
Kwa maoni yake , anaona hali hii italeta mvutano katika pande hizo mbili katika serikali ya Ukraine.
Lukashenko, mshirika wa karibu wa Putin, hivi karibuni aliishutumu Marekani kwa kujenga kambi ya NATO katika Ukraine kwa kudai kuwa kilikuwa kituo cha mafunzo .
Na mwezi Septemba, Urusi na Belarus walifanya mazoezi ya kijeshi karibu na mpaka wa Ukraine.
"Licha ya kwamba Belarus haihusiki katika mgogoro huo, wengi wanaamini kuwa inafuata mkondo wa Urusi," anasema Bezpiatchuk