Uchaguzi Tanzania 2020: Uchaguzi ulioacha maswali mengi kuliko majibu

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Nafasi, BBC Swahili

Tanzania imefanya uchaguzi wake mkuu Oktoba 28, 2020, na Rais John Pombe Magufuli, akachaguliwa kwa mara ya pili kuongoza serikali ya awamu ya tano ya nchi hiyo, baada ya kushinda kwa asilimia 84 ya kura zote.

Huu ulikuwa uchaguzi mkuu wa sita wa Kidemokrasia tangu mfumo wa vyama vingi uasisiwe nchini humo mwaka 1992.

Uchaguzi mkuu wa kwanza ulikuwa mwaka 1995, uliomuingiza madarakani, rais wa awamu ya tatu, hayati Benjamin Mkapa.

Mkapa akachaguliwa tena mwaka 2005 kabla ya kumkabidhi kijiti rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete aliyeshinda uchaguzi mkuu wa nne mwaka 2005 na wa tano mwaka 2010.

Chaguzi zote zilizopita tangu taifa hilo lipate uhuru wake mwaka 1961, zikiwemo za wakati wa chama kimoja, zilizomuweka madarakani Rais wa kwanza wa taifa hilo, Hayati Julius Kambarage Nyerere na Rais wa awamu ya Pili, Ally Hassan Mwinyi, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ulikuwa ni uchaguzi wa kipee zaidi kuwahi kutokea nchini humo, ukiacha maswali mengi zaidi.

Idadi kubwa ya wagombea Urais, Inamaanisha nini?

Wagombea urais 16, walijitokeza katika Uchaguzi mkuu wa Tanzania wa 2020.

Idadi hii ni kubwa kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kulikua na wagombea 8 pekee, 2010 walikuwa 7 na ule wa mwaka 2005, kulikuwa na wagombea 10 wa urais.

Wachambuzi wanasema idadi hiyo na mazingira ya uchaguzi yaliyokuwepo, lazima kuibuka na maswali ya aina hiyo.

Maswali hayo lazima watu wajiuliza, lakini muhimu watu kufahamu Demokrasia, sio tu idadi ya wagombea, ama idadi ya vyama kushiriiki katika uchaguzi, demokrasia ni mfumo huru wa uchaguzi, watu kujieleza, kukosoa na kukosolewa", anasema Beatrice Kimaro, Mchambuzi wa siasa za Tanzania.

Wadadisi wa siasa kama huyu, wanatoa picha kwamba demokrasia ni jambo pana sana. Ni zaidi ya namba, ni Zaidi ya idadi ya watu kushiriki ama kushirikishwa kwenye Uchaguzi.

Wagombea hao 16 wa Urais wanafanya watu kuhoji, Je ni kweli wote walikuwa na dhamiria ya kushinda Urais?

Idadi hiyo ni ishara ya ukuaji wa demokrasia ya taifa hilo? Au kuna jambo lililojificha?

Kwa nini Uchaguzi Unung'unikiwe?

Katika Uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020, kulikua na manung'uniko mengi juu ya zoezi lenyewe la uchaguzi na matokeo ya uchaguzi huo, uliompa ushindi wa asilimia 84 Rais John Pombe Magufuli. uchaguzi ambao Chama cha Mapinduzi kimeshinda kwa kishindo.

Manung'uniko haya yalitoka ndani na ya nje ya nchi.

Vyama vikubwa vya upinzani nchini humo, bara na visiwani Zanzibar vya ACT Wazalendo na CHADEMA vilikataa matokeo, vikisema uchaguzi ulivurugwa, haukuwa huru na wa haki.

Chama cha ACT Wazalendo kikafika mbali zaidi na kupeleka malalamiko ya ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, ICC.

Jumuiya za Kimataifa pia zilieleza wasiwasi wao kuhusu uchaguzi wa Tanzania.

Chama cha wananchi CUF, chenyewe pamoja na kunung'unikia Mchakato wa Uchaguzi na matokeo, kilijiapiza kutoshiriki tena Uchaguzi mkuu wowote wa nchi hiyo, mpaka pale itakapoundwa tume huru ya Uchaguzi.

Kwanini malalamiko na Manung'uniko haya?

Ingawa kila uchaguzi manung'uniko yanakuwepo, lakini Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 malalamiko yalionekana kuwa mengi zaidi.

Wapo wanaosema, kulikuwa na wizi wa wazi wa kura, kuondolewa kwa baadhi ya wagombea wa udiwani na ubunge wa vyama vya upinzani na kuondolewa kwa mawakala wa vyama vya upinzani kwenye vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (NEC), ambayo ndiyo inayosimamia na kuendesha zoezi la uchaguzi mkuu nchini humo, ilisema kwamba uchaguzi ulikuwa huru na haki, na imefuata sheria kwenye kusimamia uchaguzi huo.

Ushindi wa kishindo wa CCM, Je ni mwanzo wa mwisho wa upinzani?

Lingine lililojitokeza katika uchaguzi mkuu wa Tanzania 2020 ni kuhusu ushindi wa kishindo wa Chama tawala cha Mapinduzi (CCM).

Karibu katika ngazi zote, imepata ushindi mkubwa, ikizoa karibu viti vyote vya ubunge, kama sio zaidi ya asilimia 95, ushindi ambao haujawahi kutokea katika historia ya uchaguzi mkuu wa vyama vingi.

Vigogo wa kutazamwa wa vyama vya Upinzani akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Kiongozi mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na Mkwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia wote walipoteza viti vyao, tena kwa tofauti kubwa kabisa ya kura ambayo usingeweza kudhania.

Vigogo wa upinzani kama Godbless Lema, Halima mdee, Joseph Mbilinyi au Mchungani Msigwa walishindwa kwa tofauti kubwa ya kura, kwenye maeneo ambayo ndiyo ngome ya Upinzani.

Mikoa ya kanda ya Kaskazini (Arusha, Kilimanjaro na Manyara), kanda ya Magharibi (Kigoma na Kagera), kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya na Iringa), na kanda ya Pwani hasa mkoa wa Dar es Salaam, majimbo yote yamechukuliwa na Chama tawala (CCM).

Wengi wanabaki kujiuliza, Ushindi huu wa CCM, Je ni kweli CCM imeimarika kiasi hicho? Ama vyama vya upinzani vimeporomoka kisiasa? Au kuna nini jambo nyuma ya pazia?

Sura ya Mijadala Bungeni itakuwaje?

Bunge la 12 la Tanzania tayari limezinduliwa rasmi na Rais John Magufuli huku likiwa na wabunge wengi zaidi wa CCM.

Haijapata kutokea Bunge kuwa na wabunge wote karibu wa chama Kimoja.

Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, Wabunge wa upinzani wameonekana kuwa wakosoaji wakubwa wa masuala ya kitaifa yanayoibuka.

Mawazo yao mbadala, yanasaidia kujenga miswada yenye macho mbalimbali na mawazo mbalimbali.

Haimaanishi kwamba wakati wa mabunge yaliyopita hoja zao zilibebwa na serikali, lakini wadadisi wa siasa wanaona uwepo wao bungeni una mantiki.

"Lakini kwa utamaduni wa kibunge, uwepo wao unasaidia kuchachusha mijadala wakati wa kupitisha miswada mbalimbali. Maswali hayo yanakuja kwa sababu ya utamaduni huo huo, wanajiuliza inawezekana kukatokea mbunge wa CCM kuikosoa serikali ya CCM? anasema Kimaro

Pamoja na hayo, Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai, alisema hiyo ni dhana tu, na kwamba bunge hilo litatekeleza wajibu wake vyema, na wabunge wake wanapaswa kuwa huru kuisimamia serikali.

Nani alizima Mitandao siku chache kabla na baada ya uchaguzi?

Swali lingine ambalo halina majibu ya moja kwa moja ni kuhusu Kuzimwa ama kuzimika kwa intanet na mitandao ya Kijamii.

Siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu kufanyika Oktoba 28, 2020 intaneti haikuwa inapatikana kama kawaida na Mitandao ya Kijamiii kama Twitter, Whatsapp na Instagram nayo ilikua shida kupatikana ama haipatikani kabisa.

Njia hiyo ndo njia yenye umaarufu zaidi katika kupashana habari katika kipindi cha miaka 10 iliyiopita. Maswali mengi watu wanajiuliza , kulikuwa na tatizo la kiufundi?

Kwanini mitandao izime wakati huo ama mitandao ya kijamii isipatikane wakati huo muhimu wa Uchaguzi? Kila mtu ana jibu lake.

BBC wakati huo iliwatafuta Mamlaka zinazohusika bila mafanikio, ili kupata majibu ya hayo.

Nani mkweli katika sakata la wabunge 19 wa viti Maalumu Chadema?

Maswali mengine watu wanajiuliza ni kuhusu chama kikuu cha Upinzani, CHADEMA kutimua wanachama wake 19 walioapa kuwa wabunge wa viti maaalumu wakiongozwa na Mwenyekiti wake wa Baraza la wanawake la Chama hicho, na mmoja wa wanasiasa nguli wanawake wa chama hicho, Halima Mdee.

Chama hicho kikatangaza, hakijapeleka majina ya wabunge hao kuapishwa, na kimewafuta uanachama.

Ingawa wanachama hao kupitia Halima Mdee, walijibu kwamba watakata rufaa kupinga uamuzi huo wa chama kuwafukuza.

Pamoja na yote, Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai akaweka bayana kwamba wanachama hao 19 licha ya hatua zilizopo ni wabunge halali, mpaka itakavyokuwa vinginevyo.

Kauli yake inapingana na kauli ya Spika wa zamani wa Bunge la nchi hiyo, Pius Msekwa aliyesema kwamba kikatiba Mbunge akitimuliwa na chama chake, maana yake ubunge wake pia unakoma.

Sasa ukisikiliza pande zote hizo kuanzia upande wa CHADEMA, upande wa wanachama waliofukuzwa, kina Halima Mdee, Spika wa sasa Job Ndugai na Spika mstaafu, Pius Mseka, unabaki kujiuliza maswali nani mkweli na nani muongo?

Anayedanganya anafanya hivyo kwa faida ya nani?

Na nini hatma ya ubunge wa wanawake hao 19?

Ukweli wa haya, utabainika muda si mrefu wakati huu, wanachama hao wakiwa katika mchakato wa kukata rufaa kwenye vyombo vya juu vya chama hicho.

Mwisho wa maalim Seif katika Siasa za Zanzibar?

Hivi karibuni, MaalimSeif Sharif Hamad, mgombea Urais wa upinzani kutoka Chama cha ACT Wazalendo ameapa na kukubali kuwa makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.

Kikatiba anaunda serikali ya Umoja wa Kitaifa na Rais Hussein Mwinyi wa Chama tawala cha Mapinduzi kuongeza serikali ya awamu ya nane ya Visiwa hivyo.

Kwa namna Maalim Seif alivyokuwa na misimamo kuhusu mchakato mzima wa uchaguzi Zanzibar, akipinga wazi na kuitisha hata maandamano ya Amani kwa wafuasi wake, leo kukubali kuwa sehemu ya Serikali anayoikosoa sana, Je ni mwisho wa siasa zake Visiwani humo?

Ataendelea kuaminika na wafuasi wake?

Na Je atawezaje kusimama na kesi waliyoifungua mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai, kama ACT Wazalendo katika mazingira aliyopo sasa?

Mwenyewe baada ya kuapishwa alisema, ameamua kujiunga na Serikali, baada ya kujadiliana na wanachama lakini yote ni kwa maslahi ya Zanzibar na kusaidia kuponyesha machungu ya wafuasi wake.

Ni kweli Upinzani unachelewesha kasi ya maendeleo?

Uchaguzi umekwisha, na Rais John Magufuli anaendelea na awamu yake ya pili ya miaka mitano ya uongozi wake, mara nyingi amenukuliwa wakati wa kampeni akisema kwamba akipewa wabunge wengi kutoka chama chake cha CCM, maendeleo yatapaa zaidi bila vikwazo, na bila kuacha msemo wake wa wakati wote pia kwamba, maendeleo hayana chama.

Sasa chama chake kimeshinda tena kwa kishindo kikubwa na kupata wabunge na madiwani wengi Zaidi.

Wananchi wanasubiri kwa hamu kuona maendeleo ya kasi, na huenda chama hicho kitapimwa kwa kasi hiyo ya maendeleo katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025.

Na swali linalobaki kichwani mwa watu: Je ni kweli Upinzani ulikuwa unazuia kasi ya maendeleo? 2025 huenda ukawa wakati mzuri wa kujadili hoja hii.