Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Marekani 2020: Je hatma ya uchaguzi Marekani kuafikiwa mahakamani?
Mgombea urais wa chama cha Democrat Joe Biden ana njia ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi wa Marekani lakini mpinzani wake Donald Trump anakosoa shughuli ya kuhesabu kura katika majimbo manne muhimu.
Hivyo ni nini kinachoweza kutokea?
Kampeni ya Trump imedai, bila kutoa ushahisi kwamba kumekuwa na udanganyifu katika zoezi hilo na kuamuru zoezi la kuhesabu kura lisimame kwenye majimbo ya Pennsylvania, Wisconsin, Georgia na Michigan.
Tunazungumza na wataalamu wa sheria kujua hii ina maanisha nini- na nini kitakachofuata.
Tunaweza kuwa na matokeo wakati huu?
Ndio na hapana.
Kwa kawaida, data zinapoonesha mgombea anaongoza kwa kura ambazo hawezi kuzidiwa, mgombea huyo hutangazwa mshindi.
Hatua hii hufanyika saa za mapema asubuhi baada ya siku ya kupiga kura.
Haya si matokeo rasmi, matokeo rasmi- ni makadirio, na matokeo rasmi mara nyingi huchukua siku kadhaa kuhesabu.
Lakini mwaka huu kura nyingi za posta zinamaanisha kuwa kuhesabu kura kunachukua muda mrefu, hasa katika maeneo yenye upinzani mkali, hawajaruhusiwa kuhesabu kabla ya siku ya uchaguzi.
Kulikuwa na vikwazo kabla ya kura
Kabla ya uchaguzi wa Jumanne kulikuwa na kesi 300 katika majimbo 44 kuhusu kura za posta na uchaguzi wa mapema mwaka huu.
Malalamiko yalijikita katika masuala kama muda wa mwisho wa kutuma na kupokea kura, sahihi za mashahidi zilizohitajika na bahasha zilizotumika kutuma kura hizo.
Majimbo yanayoongozwa na Republican yalisema masharti hayo yalikuwa ya lazima ili kuzuia udanganyifu wa kura.
Lakini Democrats walisema masharti haya ni majaribio ya kuwanyima watu kutumia haki yao ya kimsingi.
Ni changamoto gani zilizotolewa na Trump?
Wisconsin
Kampeni ya Trump imesema imeomba kura zihesabiwe tena Wisconsin "kwa sababu ya dosari zilizoonekana" siku ya Jumanne.
Haijulikani zoezi hili la kuhesabu upya litafanyika lini, hatahivyo, kwa kuwa zoezi hili halifanyiki mpaka maafisa wa kaunti wamalize kuhesabu kura.
Shughuli nzima ya uhesabuji kura inapaswa kukamilika tarehe 17 mwezi Novemba.
Profesa wa Chuo cha sheria cha Columbia Richard Briffault amesema zoezi la kuhesabu kura liliwahi kurudiwa Wisconsin mwaka 2016, na kulikuwa na mabadiliko ya kura karibu 100".
''Kurudia kuhesabu kura hakuna maana kukosoa uhalali wa kura,'' anaeleza. ''kunamaanisha kuhakikisha kuwa hesabu ziko sawasawa.''
Michigan
Bw. Trump alishinda jimbo hilo mwaka 2016 ulikuwa ushindi mwembamba wa zaidi ya kura 10,700.
Tarehe 4 mwezi Novemba, kampeni yake ilitaka kusimamishwa kwa zoezi la kuhesabu kura, ingawa 96% ya kura bado hazijahesabiwa rasmi na maafisa wa uchaguzi.
Maelfu ya kura bado hazijahesabiwa na nyingi zinatoka katika miji ambayo kihistoria ni ya chama cha Democratic, lakini vyombo vya habari vya Marekani na BBC vinakisia ushindi kwa Biden.
Pennsylvania
Changamoto hapa inategemea uamuzi wa jimbo kuhesabu kura ambazo zimewekwa alama ya siku ya Uchaguzi lakini hufika hadi siku tatu zikiwa zimechelewa.
Republican wanatafuta kukata rufaa.
Matthew Weil, Mkurugenzi wa kituo cha mradi wa utafiti wa sera, anabainisha kuwa maafisa wa jimbo walituma ujumbe kabla ya siku ya uchaguzi ukiwataka wapigakura kuwasilisha kura zao katika vituo badala ya kutuma kwa posta.
''Hivyo ninahisi sio idadi kubwa ya kura zilizotupiliwa mbali kama hali ilikuwa hivyo."
Prof. Briffault pia ameeleza kuwa kura zinazowasili kwa kuchelewa zinahesabiwa peke yake, na amesema kama Biden ataongoza bila kura hizo kuhesabiwa, haoni msingi wa madai haya .
Lakini Kampeni ya Trump imedai kupata ushindi kwenye jimbo hili ingawa kuna zaidi ya kura milioni moja hazijahesabiwa.
Hakuna mitandao yoyote mikubwa iliyotaja mshindi.
Georgia
Kampeni ya Bw.Trump na chama cha Republican wamesema wamefungua kesi katika kaunti ya Chatham jimboni Georgia kusimamisha shughuli za kuhesabu kura.
Mwenyekiti wa chama cha Republican jimboni humo David Shafer aliandika katika ukurasa wa twitter kuwa waangalizi wa chama walimuona mwanamke mmoja ''akichanganya zaidi ya kura 50 kwenye kasha la kura za posta ambazo hazikuhesabiwa''.
Malalamiko haya yanaweza kufika mahakama ya juu?
Mapema Jumatano, Bw. Trump pia alidai kuwepo kwa udanganyifu wa kura bila kutoa ushahidi, na aliongeza: "Tutakwenda kwenye mahakama ya juu tunataka mchakato wote wa kura usimame."
Kura zilishasimama- vituo vilifungwa siku ya uchaguzi, ingawa kuna swali kuhusu kura zilizochelewa kama jimboni Pennsylvania.
Bw. Weil anasema: "Mahakama ya juu haina nguvu kuzuia mchakato wa kisheria wa kuhesabu kura."
Prof Briffault pia anasema kuwa kampeni zinaweza kuweka pingamizi katika majimbo muhimu, lakini "bado lazima wawe na [kesi] ambayo inaleta maswali ya kikatiba" ili ifikie Mahakama Kuu.
Ikiwa matokeo yatakataliwa, hatua hiyo itahitaji wanasheria kupeleka malalamiko kwenye mahakama za majimbo. Majaji wa majimbo watatoa amri ya kura kuhesabiwa tena, na mahakama ya juu inaweza kubatilisha hukumu.
Hatima ya mchakato wa kura.
Vyovyote itakavyokuwa, tarehe 20 mwezi Januari, kwa mujibu wa katiba muhula mpya wa urais unatakiwa kuanza kazi.
"Mchana , tunapaswa kumuapisha mtu kuwa rais. Ikiwa hakuna badala yake tutaingia kwenye mpango wa kurithisha," anasema bwana Weil.
Mfano kumuidhinisha makamu wa rais, kama hakuna makamu wa rais basi spika ( wa sasa wa Democrat, Nancy Pelosi).