'Maisha yangu yote nimeishi kwa utambulisho wa uongo'

Chanzo cha picha, Rachaphon Riansiri/BBC Thai
Laiti wangelijua mimi ni nani, wangelinitukana na kunikejeli,"Ek, (sio jina lake halisi) anasema.
Alizaliwa akiwa ana jinsia mbili ya kike na ya kiume ambayo (ilifichwa) ili kumtambulisha kama msichana tangu alipozaliwa.
Alipokua anakuwa hakujua kama ana uume ndani ya uke wake.
Alilelewa kama msichana, alivalia sketi akienda shule, lakini anakumbuka alikuwa na mtazamo wa vitu vingine kuwa vya 'kisichana'.
Mara kadhaa alijikuta akicheza na wavulana wengine na anakumbuka 'akitamani' angelikuwa mvulana.
Ek alianzia hapo safari ya mwendo mrefu katika jamii kutaka ombi lake liheshimiwe.
Kupigwa marufuku

Chanzo cha picha, Rachaphon Riansiri/BBC Thai
Alipokua shule ya upili, maumbile yake yalibadilika, mwili ukawa mkubwa na kupata misuli. Mabadiliko hayo yaligeuza maisha yake kabisa.
Alikuwa mwanariadha chipukizi na alifanya vyema sana katika mbio za mita 100 ambapo aliweka rekodi mpya ya mbio hizo katika shule yao.
Alishirika mashindano ya riadha kama msichana na alishinda mashindano yote ya ngazi ya mkoa na alikuwa anaelekea kuiwakilisha Thailand, kabla ya ndoto yake kukwamishwa ghafla.
Malalamishi ya kutaka uchunguzi wa kuthibitisha jinsia yake yaliwasilishwa. Matokeo ya uchunguzi huo ulibaini kuwa ana maumbile ya kiume, na hatimae kuondolewa katika mashindano hayo ya riadha.
Furaha moja kwa moja ikageuka karaha.
Kuchanganyikiwa

Chanzo cha picha, Rachaphon Riansiri/BBC Thai
"Baada ya kupokea matokeo ya uchunguzi, Nilihisi kana kwamba nimevuliwa nguo hadharani. Niliishi kama msichana maisha yangu yote na nilikuwa na jinsia ya kike kama wasichana wengine," Ek anauliza. "Mimi ni nani? Nimekuwa mtu wa aina? Nilichanganyikiwa na kudhalilika. Nilijitengaina watu."
Aliitwa majina na hata marafiki waliokuwa karibu naye pia, kuna wale walimuita "mtu aliye na uume uliogawanyika".
"Nilihisi kana kwamba maisha yangu yamefikia kikomo. Sikuelewa tena kama mimi ni mwanamke au mwanamume. Sikua na ufahamu kuhusu nafasi yangu duniani.
Nillijitenga, na kuepuka kuenda darasani kwa kuhofia kukejeliwa na wanafunzi wenzangu darasani. Familia yangu ilijua hali ninayopitia lakini haikufanya chochote. NiIiathirika sana na hali hiyo."
Maisha mapya

Chanzo cha picha, Rachaphon Riansiri/BBC Thai
Ek aliamua kuhamia Bangkok kuanza upya maisha, ambako alipata kazi aliyokua ameomba kama mwanamke.
Nchini Thailand, watu wa majina kulingana na jinsia yao.
Majina hayo ni rasmi na ni vigumu kubadilisha kutokana na mchakato wa kisheria.
Hata hivyo wafanyakazi wenzake, walimchukulia kama mwanaume na walipogundua aliomba kazi kama mwanamke, Walibadili mtazamo wao juu yake.
Wafanyakazi wenzake wa kike waliokua karibu nae pia walianza kumtenga, kwa kuhofia huenda wakadhaniwa kuwa wanashiriki mapenzi ya jinsia moja.
Alikabiliwa na wakati mgumu uliomlazumu kujitenga kwa miezi mitatu hadi pale alipopata kazi nyingine lakini alike iliwafanya na changamoto nyingine.

Chanzo cha picha, Rachaphon Riansiri/BBC Thai
"Mwanzoni ilikuwa rahisi kujificha, lakini niligunduliwa tena baada ya wiki kadhaa.
Wakati huo nilidhalilishwa mno. Wanaume walinishika kwa nguvu wakitaka kuthibitisha jinsia yangu. Nilipata msongo wa mawazo kutokana na tukio hilo."
Juhudi za kutaka kupata utambulisho rasmi zilipogonga mwamba, aliachana nayo na kuomba kazi kwa kutumia utambulisho wa uwongo - ili asigunduliwe na mamlaka, aliamuabkubadisha kazi kill baada ya miezi mitatu.
Alifanya hivyo kwa miaka mitatu, hali iliyomwezesha kujenga urafiki na watu kadhaa, miongoni mwao mwanamke aliyemtaja kama "mpenzi wa maisha yake".
"Maisha yangu yalibadilika tangu nilipokutana nae. Alinielewa na kunipa motisha ya kuendelea mbele na maisha licha ya maumbile yangu.
Japo niliendelea kubadili kazi kutoka moja hadi nyingine kila baada ya miezi mitatu alikuwa karibu nami."
Aliweka akiba iliyomwezesha kuanzisha biashara ya mboga na matunda. Pia alitumia ujuzi wakevwa kutengeneza vifaa vya umeme kupata fedha za ziada. Maisha yalimwendea vyema kwa miaka michache.
Baadaye mpenzi wake alitoweka, bila hata kumuaga.

Chanzo cha picha, Rachaphon Riansiri/BBC Thai
"Nilisononeka sana. Nikajiuliza maswali mengi. Nilikosea nini? Mbona akaniacha ghafla? Nilijaribu kumtafuta, lakini familia yake ilisema haina taarifa kuhusu aliko. Nikajaribu kuwasiliana nae kwa njia ya simu bila mafanikio. Nilimtafuta kwa wiki nzima. Mara nikaingiwa na mawazo ya kutaka kujitoa uhai, afadhali kufa."
Aliamua kujitoa uhai lakini, wakati wa jaribio hilo aligusa kwa bahati mbaya kifaa karibu na machine ya kutoa pesa benki ATM, ambayo iliwasilisha ujumbe wa dharura kwa polisi waliofika katika eneo la tukio.
Alikamatwa na kushitakiwa kwa wizi kwa sababu polisi hawakuamini hadithi yake ya kutaka kujitoa uhai.
Mahakama ilimpata na hatia na kuamua afungwe jela miezi sita.
Akiwa gerezani, alifanyiwa uchunguzi wa kitibabu, baadae madaktari na maafisa wa gereza hilo walijadiliana kwa muda mrefu kabla ya kuafanya uamuzi kuhusu jinsia yake.
Baadaye alipelekwa katika jela ya wanawake kwa kuhofia usalama wake katika jela ya wanaume.
"Walihofia nitabakwa kwa sababu nina sehemu ya siri ya mwanamke," Ek anasema.
Maisha gerezani
Maisha yake gerezani yalimwezesha kupewa matunzo mazuri, na wafungwa wenzake wa kike walimdekeza. Kwa mara ya kwanza ilijihisi kuwa na maisha mazuri.
"Maisha yangu gerezani yalikua mazuri," Ek anasema. "Walitaka kunijua, walisema nami, na kufanya kila wawezalo kuniridhisha. Sikuwahi kufanyiwa hivyo maishani mwangu."
Baada ya kukamilisha kifungo chake, alijipata katika maisha yake ya awali. Rekodi yake ya uhalifu ilimuathiri alipotuma maombi ya kazi, lakini anashukuru kulikuwa na wanahabari wakati polisi walipomkamata.
Wanahabari walikuwa katika eneo la tukio bila ufahamu wa polisi na walifanikiwa kunakili kila kitu alipokuwa anahojiwa.
Ek aliamua anataka kurejea jela, kwa hiyo aliingilia uhalifu wa kuharibu mitambo ya ATM.
Alikamatwa na kushitakiwa tena ambapo alihukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani.
"Wakati huu walinipeleka kagika jela ya wanawake. Niliamua sitawahi tena kutoa mguu wangu nje ya jela, kwa hivyo nilikiuka sheria zote zilizowekwa hadi wakaniongezea muda wa kusalia kifungoni."
Hata hivyo mpango wake ulifeli na hatimaye akaachiliwa huru.
Kujinasua
Akiwa jela, Ek alihudhuria warsha moja iliyoandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali ambalo liliangazia masuala ya jinsia, na kwa mara ya kwanza akasikia neno "jinsia mbili".
Kutokana na ushauri wa wa wataalamu na usaidizi wao, aligundua anaweza kuachana na jinsia yake ya kike kisheria na kutambuliwa kama mwanaume.
Ili kufikia azma hiyo, Ek alihitaji cheti cha matibabu kinachoonesha ana jinsia inayomtambulisha kama mwanamume, pamoja na stakabadhi inayoonesha amefanyiwa uchunguzi wa kiakili kuthibitisha kwamba hana akili punguani.
Alitumia miezi mitano kupata stakabathi hizo.
Hatimaye, siku aliyokua akiisubiri kwa hamu ikawadia.
Mshtuko

Chanzo cha picha, Rachaphon Riansiri/BBC Thai
Asubuhi ya tarehe 24 Juni, aliangalia nyaraka za utambulisho wake tena ili kuhakikisha kuwa hakuna alichokisahau.
Aliondoka ofisi ya wilaya aliyozaliwa, Udon Thani, kujiandikisha rasmi na utambulisho halisi wa jinsia yake.
Alikuwa na hofu kuwa ndoto zake zinaweza kuzimika ndani ya saa kumi na moja.
Lakini ikawa hivyo tena.
Afisa aliyekuepo zamu alikuwa hana nyaraka zote za kuthibitisha utambulisho wake.
Ek alitakiwa aende kuleta wazazi au rafiki yake tangu utotoni kuwa shaidi.
Hivyo ilimbidi arudi nyumbani na kujaribu tena.
Utambulisho
Siku iliyofuata, mama yake -ambaye alikuwa hakubaliani na suala la jinsia yake kutambuliwa kwa muda mrefu alimsindikiza katika ofisi za wilaya.
Afisa alitumia muda mrefu katika simu akizungumza na mhusika mkuu wa mji wa Bangkok kumuelezea namna ya kuidhinisha maombi hayo ambayo si ya kawaida.
Baada ya muda,maombi yake ya kubadilisha utambulisho wake yalipitishwa lakini kabla alitakiwa kufanya vipimo vya afya ili kupata cheti za kitabibu ambacho kitaelezea hali yake ya kuwa na jinsia mbili.
Hatimaye Ek aliweza kubadili jina na kuwa na jina linalomtambulisha kama mwanaume.
"Kwa sasa naweza kuwa huru na maisha yangu -najihisi kuwa juu ya dunia.Nataka kupiga kelele kusema nimeanza maisha mapya.Naondokana na utambulisho wa uongo na niko huru".












