Maafisa wa Umoja wa Mataifa washtushwa na video ya ngono ndani ya gari la UN Israel

Umoja wa Mataifa unasema kwamba 'umeshtuka na kukerwa' na kanda ya video ya tendo la ngono lililofanyika ndani ya gari moja la Umoja huo nchini Israel.

Kanda hiyo inamuonesha mwanamke alievalia rinda jekundu akimkaribia mwanamume mmoja katika kiti cha nyuma cha gari hilo jeupe lenye nembo ya UN.

Kanda hiyo ya video iliosambazwa sana katika mitandao ya kijamii ilidaiwa kunaswa katika barabara kuu mjini Tel Aviv.

Umoja wa mataifa umesema kwamba inakichunguza kisa hicho na unakaribia kumtambua mtu aliehusika.

Wale waliohusika wanaaminika kuwa maafisa wa kulinda amani nchini Israel, Umoja huo umesema.

Abiria mwengine anaonekana amekaa mbele lakini dereva haonekani huku gari likiendeshwa.

Stephane Dujarric, msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa , Antonio Guterres , alikitaja kitendo hicho kinachoonekana katika kanda ya pili kama kinachochukiza.

''Tabia kama hiyo ni kinyume na chochote kile tunachokiamini'', bwana Dujarric aliambia BBC siku ya Ijumaa.

Alipoulizwa iwapo kitendo hicho ni cha makubaliano ama kilihusisha malipo, bwana Dujarric alisema maswali hayo ni miongoni mwa uchunguzi unaoendelea.

Umoja wa Mataifa una sera kali dhidi ya tabia za ngono miongoni mwa wafanyakazi wake.

Wafanyakazi wanaweza kupewa adhabu iwapo watapatikana wamekwenda kinyume na sheria za Umoja huo.

''Wanaweza kurudishwa kwao ama hata kupigwa marufuku katika ujumbe huo wa walinda amani, lakini ni jukumu la mataifa yao kuwachukulia hatua zaidi ama hata kuwaadhibu''.

Umoja wa mataifa umekuwa ukichunguzwa kufuatia madai ya vitendo vya ngono kuripotiwa miongoni mwa walinda amani na wafanyakazi wengine.

Kumekuwa na madai chungu nzima katika miaka ya hivi karibuni. Katibu mkuu ameahidi kutowakubali wale watakaohusika na tabia hiyo mbovu.

Je msemaji huyo wa UN amesema nini kuhusu kanda hiyo?

"Tumeshtushwa na kushangazwa na kile kinachoonekana katika video hii," Mr Dujarric said.

Alisema uchunguzi ulioongozwa na afisi ya UN ya Internatal Oversight ulikuwa unafanyika kwa haraka.".

Bwana Dujarric alisema eneo la kitendo hicho limetambuliwa na utambuzi wa waliohusika katika video hiyo unakaribia kukamilika.

Kutokana na majumba yalionaswa katika video hiyo , kanda hiyo inaonekana kunaswa katika barabara ya HaYarkon, eneo ambalo lina biashara nyingi.

"Tunatarajia uchunguzi huo kukamilika hivi karibuni ili kuweza kuchukua hatua dhidi ya wahusika'', alisema Dujarric.

Je rekodi ya UN kuhusu masuala ya ngono ni ipi?

Heather Barr, mshirikishi wa masuala ya haki za kibinadamu katika shirika la Human Rights Watch alisema, ''hakushangazwa na kanda hiyo kutoka Israel''.

Bi Bar, ambaye alifanya kazi na UN nchini Burundi na Afghanistan , alisema ''ni vyema wanachunguza , lakini akaongezea kwamba UN ina matatizo makubwa zaidi ya kanda hiyo".

''Tatizo ni kuhusu madai ya unyanyasaji wa kingono unaotekelezwa na wafanykazi wa UN'', alisema bi Barr.

Mwaka 2019 , kulikuwa na madai 175 ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wafanyakazi wa UN, ripoti moja ilisema.

Kati ya madai hayo, 16 yalikuwa na ushahidi , 15 yalikosa ushahidi na mengine yote yaliosalia yanafanyiwa uchunguzi.