Waraibu wageukia dawa za usingizi Tanzania

Teja akijidunga mihadarati

Chanzo cha picha, Getty Images

Waraibu wa mihadarati nchini Tanzania wamegeukia dawa za usingizi kama njia mbadala baada ya kuadimika kwa dawa za kulevya.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Tanzania imekaza nati kwenye vita dhidi ya dawa za kulevya na matokeo yake ni kupungua kwa uingizwaji wa mihadarati kama heroine na cocaine.

Baadhi ya waraibu wa mihadarati, maarufu kwa jina la mtaani kama mateja, wamejisalimisha hospitali kupata msaada wa kitabibu ili kuachana na matumizi ya dawa hizo.

Hata hivyo, kwa wengine upungufu huo umewafanya watafute mbinu mpya za kusalia na uraibu wao kwa kutumia dawa za hospitali, ikiwemo dawa za usingizi.

Baadhi ya dawa hizo kupatikana kwake ni mpaka uwe na cheti cha daktari kwa wagonjwa wenye matatizo ya kukosa usingizi pamoja na wale wenye maumivu makali baada ya kufanyiwa upasuaji.

Kijana Khalfani Mshangama mkazi wa Magomeni jijini Dar es salam ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitumia mihadarati ameiambia BBC kuwa kutokana na ugumu wa kupata madawa hayo kwa sasa amegeukia dawa za usingizi hasa valium.

Mshangama hubugia mpaka vidonge 20 kwa mkupuo."Kawaida nahitaji kunywa vidonge vingi ili nipate stimu (uraibu) kama ya cocaine'' alisema kijana huyo.

Kamili Muharam mkazi wa Mwananyala jijini Dar es salaam anasema kutokanan na dawa hizo za usingizi kutopatikana kwa urahisi,hutumia mbinu ya kujifanya mgonjwa afikapo kwenye maduka ya dawa.

"…kuna maduka maalumu ambayo tayari wameshanizoea. Haiwi ngumu sana kwangu kupata vidonge."

Dozi ya Valium, ambayo huwa ni vidonge 10 huuzwa kwa Sh500 tu. Na ili pate vidonge 20 huhitaji Sh1000 ambayo ni karibia nusu dola tu.

Opioids

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Dawa za kupunguza maumivu za Opioids pia husababisha uraibu iwapo matumizi yake yatakuwa kupita kiasi

Daktari bingwa wa matibabu ya uraibu kutoka hospitali ya rufaa ya Temeke jijini Dar s Salaam Isaac Rugemarila ameiambia BBC kuwa kitaalamu mtu akikosa dawa ambayo ameizoea hutafuta dawa nyingine ambayo hufanana na aliyoizoea (cross addiction) ambayo humletea hali ya uraibu.

Kwamujibu wa Dkt Rugemarila dawa hizo za usingizi ambazo hupatikana kenye maduka ya dawa hutolewa kwa wenye matatizo ya akili,usingizi na maumivu makali baada ya kufanyiwa upasuaji.

Hata hivyo,amekiri kuwa wapo baadhi ya wafamasia wasio waadilifu na huzitoa bila ya kuzingatia kuzitoa kwa watu bila ya kuzingatia hilo.

"Licha ya dawa hizo kama valium(Diazepam) kutumika kwa wagonjwa kwa njia nzuri lakini zimekuwa na madhara kwa mtumiaji iwapo zitatumiwa kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kupata uraibu,na hata huenda zikasababisha kifo ikiwapo zitatumika na kilevi kingine kama pombe," ameonya Dkt Rugemarila.

Kwa upande wake meneja uhusiano na elimu kwa umma wa mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) Gaudensia Simwanza anasema mamlaka hiyo imeweka mifumo ambayo huanisha utaratibu wa kununua dawa kutoka katika maduka ya dawa kwani zipo dawa ambazo ni lazima zitolewa kwa mgonjwa kwa cheti cha daktari hvyo ni lazima wafamasia kuzingitia maelekezo hayo.

Sindano na chupa za heroine
Maelezo ya picha, Kuadimika kwa heroine kumesababisha waraibu kutafuta ulevi mbadala

Aidha bi Simwanza anasema kuwa katika kuhakikisha kuna kuwa na udhibiti wa dawa zote zenye uraibu ambazo hupatikana katika maduka ya dawa,TFDA hutoa vibali vya dawa hizo kwa baadhi tu ya maduka ya dawa nchini na pia wanapaswa kuweka kumbukumbu ya dawa zote zilizouzwa na wanapotaka kibali kingine ni lazima wapeleke ripoti ya dawa za mwanzo.

"Tunatoa vibali kwa maduka maalum na wanapaswa kutuletea kumbukumbu ya matumizi ya dawa hizo kila baada ya miezi sita,'' alisisita Simwanza.

Katika mkutano wa 28 wa kimataifa wa kupambana na madawa ya kulevya unaondaliwa na Umoja wa mataifa uliofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni,waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alisema matumizi ya madawa ya kulevya yamepungua kwa 90% huku changamoto kubwa ikiwa ni matumizi ya dawa za usingizi kama dawa mbadala za kulevya.

Majaliwa alisema kuwa vijana wengi sasa wameanza kuharibikiwa kwa matumizi ya dawa hizo,hivyo kuzitaka mamlaka zote zinazohusika na udhibiti wa dawa kuongeza nguvu ili kunusuri nguvu kazi ya taifa.