Eliud Kipchoge: Je, ni hatua gani zimesalia kwa mfalme wa mbio za marathoni?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Na Rebecca Adams
- Nafasi, BBC Sport Africa
Yeye ndiye anayeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za marathon na mwanamume pekee aliyekimbia umbali huo - ingawa si rasmi - kwa chini ya saa mbili hadi alipotetea taji lake la Olimpiki mnamo Septemba Eliud Kipchoge aliamini kuwa amepata urithi wake wa michezo.
Ni wazi kwamba mwanariadha huyu mwenye umri wa miaka 37- anaheshimiwa sana na mashabiki wa spoti, wengi wao tayari wanachukulia Mkenya huyo kuwa mwanariadha bora zaidi wa kiume katika historia.
Kando na orodha yake ndefu ya ufanisi, ushindi wake mjini Sapporo, Japan, ulimfanya ajiunge nakunde la wakimbiaji wenye ujuzi , na kuwa mtu wa tatu kuhifadhi taji la marathon ya Olimpiki
Ni mwanariadha mashuhuri wa Ethiopia Abebe Bikila pekee katika miaka ya 1960 na Waldemar Cierpinski wa Ujerumani Mashariki, mwaka wa 1976 na 1980, ambao wamefanikiwa kushinda tuzo hiyo kama Kipchoge, aliyeteuliwa kuwania tuzo ya BBC ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka wa Afrika.
"Nilifurahia sana kushinda dhahabu ya Olimpiki kwa mpigo," Kipchoge aliambia BBC Michezo Afrika. Nimefanya mengi, lakini dhahabu ya Tokyo 2020 iliimarisha kila kitu. Iliimarisha kile nimekuwa nikifanya."
Ushindi wake - uliopatikana kwa tofauti kubwa zaidi ya ushindi katika mbio za marathon za Olimpiki kwa wanaume katika miongo mitano - ulikuwa wa kuvutia sana na kushawishi Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki kumchagua Kipchoge kama mwanariadha wao wa kiume wa Michezo hiyo.
Michezo ya Olimpiki ilipangwa kwa kuzingatia kauli mbiu inayoendana na hulka ya Kipchoge, ambayo ni imani kwamba chochote kinawezekana.
"Ilikuwa muhimu sana kutupa tumaini na kumwambia kila mtu kwamba kama wanadamu, kwa bahati nzuri tuna ujuzi na uwezo wa kukabiliana na hali ya kutokuwa na uhakika wowote," alisema.
Haishangazi kwamba Kipchoge ana nia ya kutaka kuibua hali mpya, kwani imekuwa sifa kuu ya taaluma yake.
Gwiji wa Marathon
Dhahabu ya Kipchoge nchini Japan ilikuwa medali yake ya nne ya Olimpiki kwa ujumla, huku mwanariadha wa zamani wa mita 5000 akiwa amenyakua shaba na fedha katika Michezo ya 2004 na 2008 mtawalia.
Medali hizo zinaongeza wasifu unaojumuisha rekodi rasmi ya dunia ya mbio za saa mbili dakika moja na sekunde 39, ambayo aliweka mjini Berlin mwaka wa 2018 alipoboresha alama ya zamani kwa sekunde 80.
Mwaka mmja baadaye, alikimbia mbio za marathon za kwanza kabisa za chini ya saa mbili, katika hali ya kusaidiwa, kama sehemu ya INEOS 1:59 Challenge mjini Vienna.
"Mbio yangu kuu ni ya kuvunja kizuizi cha masaa mawili," alisema. "Sababu ya kwanza ni kwamba aliandikisha historia na kuwaambia watu kwamba chochote unachotaka na kukifanyia kazi, utakipata."
Licha ya umri wake na mafanikiyo aliyopata, Kipchoge hajaonesha dalili ya kupunguza kasi - kinyume kavisa kwa kweli.
"Bado kuna mengi katik akapu langu lakini kikubwa zaidi ni kukimbia mbio kuu zote sita za marathon na kushinda zote - hiyo ni changamoto yangu inayofuata."
Kipchoge tayari ameshinda mataji katika mashindano matatu ambayo ni sehemu ya mbio kuu za dunia za marathon, kwa ushindi huko London, Berlin na Chicago, kumaanisha kuwa bado anahitajika kushinda mbio za Boston, New York na Tokyo.
Kocha Patrick Sang, ambaye amesimamia mabadiliko ya kustaajabisha ya Kipchoge kutoka kwa bingwa wa dunia wa mita 5000 hadi mvunja rekodi ya mbio za marathon, anaamini kuwa huhudi zake, na kazi aliyofanya naye kwa miongo miwili, inaweza kufanikisha hili.
"Bila shaka kutakuwa na wakati atastaafu, lakini kwa sasa bado ana kile anachohitaji kufanya katika kiwango cha juu sana," anasisitiza Sang, ambaye alishinda medali ya fedha ya Olimpiki ya kuruka viunzi mwaka 1992.
"Tutarajie mengi zaidi kutoka kwake miaka ijayo."
Jicho la uhifadhi

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa urithi wa Kipchoge katika michezo huenda tayari umepatikana, haijalishi atafanya nini siku zijazo, kuna eneo lingine ambalo anataka kuacha alama ya kudumu.
"Ningependa kuacha urithi ambapo watu watanikumbuka wanapoona sura yangu," alisema. "Jina langu linahusu mada za usawa, uhifadhi na elimu."
Mnamo Septemba, alianzisha Wakfu wa Eliud Kipchoge ili kuzingatia mambo hayo matatu - 'ambayo ni muhimu sana kwangu'.
"Kuna utafiti unaosema usifanye mazoezi mahali ambapo kuna hewa chafu au palipo na hewa chafu, na ufanye mazoezi tu pale ambapo tuna hewa safi," alieleza.
"Tunajaribu kuwaambia watu watoke nje ya mlango na kukimbia kwa ajili ya utimamu wa mwili na afya. Wakfu wangu pia unajenga maktaba na lengo letu, ni kuwa maktaba katika kila shule ya chekechea, msingi na sekondari."
Mbali na shughuli zake zauhifadhi mazingira, anataka watu zaidi kujiunga na mchezo wake.
"Kukimbia kwangu ni maisha kwani - bila riadha, hakuna maisha," alisema. "Riadha imenifikisha mahali kwingi; kukimbia kumenisaidia kuweka chakula mezani kwa watoto wangu na ndugu zangu"
"Kukimbia kumeniwezesha kuhamasisha watu zaidi na kuwaambia watu kwamba hakuna mwanadamu aliye na mipaka."
Kinachompatia motisha, anasema, ni mapenzi yake kwa mchezo huo lakini pia hamu ya 'kuhamasisha watu zaidi, watoto na vijana kila siku'.
Kwa hivyo wakati mwanariadha anapostaafu, usitarajie atapumzika - bali ataanzae mbio mpya za marathon, wakati huu kuhubiri ujumbe wa kujenga sayari bora katika siku zijazo.
"Kama sikuwa na kazi nyingi za kufanya, ningependa kuzunguka ulimwengu kuwatia moyo vijana, kuwatia moyo watoto kupenda kukimbia," alisema.
"Ningeenda ziara ya kuangazia zaidi kuhusu uhifadhi na mazungumzo ya michezo na elimu. Nitapambana na mechi."
Ikiwa ataifanya vizuri kama vile anavyokimbia maili 26.2, ulimwengu unaweza kuwa mahali pazuri zaidi.
Tafadhali Mpigie kura Mwanamichezo Bora wa Afrika wa BBC 2021 ambapo pia utapata sheria na ilani ya faragha. Upigaji kura utafungwa Jumapili Disemba 19 2021 saa 23:59 GMT."
Mahojiano na Eliud Kipchoge yamefanywa na Michelle Katami.














