Simba vs Yanga: Nani kuibuka mbabe dabi ya Kariakoo?

Chanzo cha picha, SIMBA
Hisia za mashabiki wa soka Tanzania zitaelekezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambako kutachezwa mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga kuanzia saa 11 jioni ikiwa ni ya mzunguko wa kwanza wa ligi kuu msimu huu.
Timu hizo zinakutana huku Yanga wakiongoza msimamo wa ligi wakiwa na pointi 19 na Simba ipo nafasi ya pili ikiwa imekusanya jumla ya pointi 17 huku kila timu ikiwa imeshacheza mechi saba.
Lakini tofauti na nyakati za nyuma ambapo mijadala katika kipindi kama hiki huwa ni ile inayohusu mechi hiyo kwa maana ya ufundi, mbinu na ubora wa wachezaji, safari hii suala ambalo limekuwa gumzo ni uamuzi wa uongozi wa Simba kuomba ufafanuzi kwa bodi ya ligi Tanzania (TPLB) baada ya kile walichotaja kuwa ni agizo la kutakiwa kuvaa jezi zenye nembo ya mdhamini mwenza wa Ligi Kuu, kampuni ya GSM katika mechi hiyo ya Jumamosi.
Uongozi wa Simba kupitia mtendaji wake mkuu, Barbara Gonzalez, mwanzoni mwa wiki hii uliandika barua kwenda kwa TPLB kuelezea wasiwasi wao juu ya mkataba huo baina ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na kampuni ya GSM wakidai una harufu ya mgongano wa kimaslahi.
Katika barua hiyo, Simba imetoa hoja tatu za kuonyesha mgongano wa kimaslahi uliopo baina ya kampuni ya GSM na klabu ya Yanga jambo ambalo inahofia linaweza kusababisha kutokuwa na usawa na haki katika usimamizi wa ligi.
Hoja ya kwanza ni lengo la kampuni ya GSM katika udhamini wake kwa Yanga ambalo ni kuhakikisha timu hiyo inatwaa ubingwa lakini ya pili ni Simba kutopewa taarifa juu ya hafla ya kusaini mkataba wa udhamini wa ligi baina ya kampuni hiyo na TFF tofauti na Yanga ambayo viongozi wake walihudhuria kwa idadi kubwa.

Chanzo cha picha, Simba/Instagram
Na hoja ya tatu ya Simba ni ukumbusho kwamba shughuli za uendeshaji wa Yanga sasa zinafanyika katika ofisi za GSM huku pia mwakilishi wa kampuni hiyo katika shughuli mbalimbali, Mhandishi Hersi Said akiwa pia ni makamu mwenyekiti wa kamati za usajili na mashindano za Yanga.
"Tunaandika barua hii tukiwa na wasiwasi mkubwa kutokana na uelewa wetu wa uhusiano uliopo baina ya Yanga na GSM. Tunaamini Yanga itakuwa na faida isiyo na usawa katika TPLB nje ya uhusiano wao na 'mdhamini huru' GSM. Yanga ina mahusiano ya moja kwa moja na GSM kinyume na kanuni za Ligi Kuu 2021.
Kanuni ya 16 (11.1) ya Ligi Kuu 2021 inasomeka: Hairuhusiwi kwa klabu/mchezaji/mwamuzi kufanya mawasiliano ya moja kwa moja na mdhamini wa Ligi bila ruhusa ya TFF kuhusu
masuala yanayohusu mkataba wa udhamini, yeyote atakayekiuka atafungiwa kipindi kati ya miezi mitatu na kumi na mbili au faini ya shilingi laki tano (500,000/-)," inasomeka sehemu ya barua hiyo ya Simba kwenda TPLB huku ikinukuu kifungu cha kanuni ya 16 ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kinachohusu udhamini.
Majibu ya Bodi ya Ligi
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania kupitia kwa mtendaji Mkuu wake Almas Kasongo umefafanua kuwa ulishaipa muongozo Simba na imeoneshwa kushangazwa na kitendo cha barua ya klabu hiyo kwenda bodi ya ligi, kuanikwa hadharani wakati ni nyaraka ya mawasiliano ya siri baina ya klabu na TPLB.
"Bodi ya ligi ni chombo cha vilabu na inasimama kwa ajili ya vilabu. Tuna utaratibu wetu wa kupeana habari zinazohusiana na bodi ya ligi.
Tuna jukumu la kuwafahamisha kilabu chochote kinachoendelea ikiwemo mkataba kati ya GSM na TFF na ndio maana ukiona barua ya Simba inaomba ufafanuzi baada ya sisi kuwaelezea yaliyomo katika mkataba na kwamba ni mambo gani ambayo vilabu vinapaswa kuyafanya," alisema Kasongo.
Mtendaji huyo wa bodi ya ligi kuu Tanzania alisema kuwa Simba na vilabu vingine vilishaelezwa kuhusu mkataba huo kwa njia rasmi za mawasiliano zilizoainishwa na mamlaka za soka.
"Na kwa sababu bodi ya ligi ipo kwa sababu ya vilabu, iliweza kukaa chini na kutoa ufafanuzi kama ambavyo Simba waliomba na kama ambavyo klabu kingine chochote kikiomba, bodi ya ligi ina wajibu wa kujibu kupitia njia sahihi za mawasiliano kwa mujibu wa utaratibu.
Hivyo itoshe kusema kuwa bodi ya ligi iliwasiliana na klabu zote 16 za Ligi Kuu juu ya mkataba huo," alifafanua Kasongo.

Chanzo cha picha, YANGA/INSTAGRAM
Nini kitajiri?
Kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara zinafafanua kwamba timu ambayo haitovaa nembo ya mdhamini katika mchezo wa ligi, itatozwa faini ya Shilingi milioni tatu na muendelezo wa kosa hilo unaweza kupelekea adhabu ya kushushwa daraja.
"Klabu inawajibika kuheshimu masharti ya udhamini wa Ligi Kuu kimkataba kwenye michezo yake kama inavyoelekezwa na TFF/TPLB, timu itakayokiuka itatozwa faini ya shilingi milioni tatu (3,000,000/-) kwa kila mchezo itakaokiuka na inaweza kuchukuliwa hatua zaidi ikiwemo kushushwa daraja na/au kufungiwa," inafafanua kanunia ya 16(1.7).
Lakini ibara ya kwanza ya kanuni hiyo inawapa nguvu Simba kwani inaeleza kuwa nembo ambayo klabu zinapaswa kuvaa ni ya mdhamini mkuu tu wa ligi na sio mwenza.
" Nembo ya Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu itawekwa kwa rangi zake halisi katika mkono wa kulia kwenye sare za timu za kuchezea, na timu zitalazimika kufanya hivyo kwa michezo yake yote ya Ligi Kuu," inafafanua ibara hiyo.
Utata wa kikanuni
Hata hivyo wakati ibara ya kwanza ya kanuni ya 16 ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiipa nguvu Simba, utangulizi wa kanuni hiyo unazipa mamlaka TFF na TPLB kutoa maelekezo ya udhamini kwa klabu ambayo yanatakiwa kufuatwa.
"TFF/TPLB itatoa maelekezo na mwongozo kuhusu masharti na makubaliano ya msingi kimkataba na Mdhamini ambapo Klabu, timu, wachezaji na wadau wengine watawajibika kuheshimu na kutekeleza," unafafanua utangulizi huo.
Ni kama ilivyo kwa ibara ya tatu ya kanuni hiyo inazilazimisha klabu kuweka nembo ya mdhamini pasipo kuzingatia kanuni za ligi kwa kuagizwa na mamlaka za soka hapa Tanzania.
"Timu zitalazimika kuweka nembo ya mdhamini kwenye vifaa vyake vya kuchezea kama inavyoelekezwa na Kanuni hizi au kwa maelekezo maalum ya TFF," inasema ibara hiyo.
Maoni ya wachambuzi wa soka
Mchambuzi wa soka wa kituo cha habari cha Clouds Media, Priva Abihudi alisema kuna mapungufu ya kisheria na kikanuni katika mkataba huo baina ya GSM na TFF hivyo Simba walikuwa na haki ya kuhoji na kutaka ufafanuzi.
"Katiba ya TFF inafafanua kwamba TFF itafuata na kuheshimu sheria za nchi na sheria za nchi upande wa mikataba zinasema kuwa mkataba wowote unaohusisha upande wa tatu kama ni mnufaika, upande wa tatu una haki ya kujua yaliyomo katika mkataba hivyo katika hili, Simba wana haki ya kujua kwa sababu wao wanawajibika kuutumikia mkataba.
Ninachoona tatizo kubwa ni kwamba viongozi wa klabu ambao ndio wanatakiwa kuwa na nguvu kupitia bodi ya ligi ambayo ndio chombo chao wamepoteza mamlaka katika kujisimamia hivyo wanajikuta hawana mamlaka ya kushiriki katika majadiliano ya mikataba na badala yake watekelezaji tu wa mkataba ambao hawajui una nini ndani yake," alisema Abihudi.
Mchambuzi wa soka wa kituo cha Wasafi Media, George Job alisema sababu mbili pengine ndio zimeibua sakata hilo.
"Kwanza kanuni za ligi zinazungumza na kufafanua maslahi ya mdhamini mkuu na hazijatoa muongozo kuhusu mdhamini mwenza hivyo inaleta ukakasi katika utekelezaji wa vipaumbele vya mdhamini mwenza.
Lakini kingine ni mdhamini kushindwa kujitofautisha uhusiano wake na klabu kwani mtendaji wa shughuli za mdhamini ndiye amekuwa akionekana katika uendeshaji wa Yanga," alisema Job












