Urusi yafungiwa miaka minne kushiriki michuano mikubwa duniani ikiwemo michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020 na kombe la dunia mwaka 2022

Chanzo cha picha, Getty Images
Urusi imefungiwa kwa miaka minne kushiriki michezo yoyote mikubwa ya kimataifa na wakala wa kupambana na dawa za kusisimua misuli (Wada).
Inamaanisha kuwa bendera ya Urusi haitapepea wala wimbo wao wa taifa wa nchi yao hautapigwa kwenye michuano kama ya Olimpiki ya mwaka 2020 na michuano ya kandanda ya kombe la dunia ya mwaka 2022 nchini Qatar.
Lakini kwa wanamichezo ambao watathibitisha kutotumia dawa hizi wataruhusiwa kushiriki lakini kwa kigezo cha kutoiwakilisha Urusi.
Kamati kuu ya Wada imefanya maamuzi haya katika mkutano wake mjini Lausanne, Switzerland.
Hatua hii inakuja baada ya wakala wa kupambana na dawa za kusisimua misuli nchini Urusi (Rusada) kutajwa kutotii na kuziharibu sampuli za wanamichezo wa Urusi Januari 2019.
Hata hivyo ilitakiwa kusiwasilisha sampuli hizo kwa Wada baada ya tuhuma zilizopelekea kufungiwa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2018.
Wada inasema Rusada ina siku 21 kukata rufaa. Kama haitofanya hivyo pendekezo hilo litafikishwa katika mahakama kuu ya michezo (Cas).
Makamu Rais wa Wada Linda Helleland amesema zuio hili ''halitoshi''
''Binafsi nilitaka kuwepo vikwazo ambavyo vitakua vikali zaidi,'' alisema.''Tunapaswa kuwasafisha wanamichezo ambao hawahusiki na vikwazo hivi kwa kadri tuwezavyo''
Unaweza pia kusoma
Jumla ya wanamichezo 168 wa Urusi walishiriki kama wanamichezo huru katika michuano ya Olimpiki mwaka 2018 mjini Pyeongchang kufuatiwa kufungiwa kwa nchi yao katika michuano ya mwaka 2014 iliyofanyika mjini Sochi. Wanamichezo wa Urusi walishinda medali 33 mjini Sochi, 13 kati yake zikiwa za dhahabu.
Urusi ilizuiliwa kama taifa kushiriki michuano mikubwa tokea mwaka 2015.
Licha ya kufungiwa huko, Urusi itaruhusiwa kushiriki michuano ya Euro 2020 katika jiji la St Petersburg ambao utakua mwenyeji wa michuano hiyo kwa sababu chama cha soka Ulaya Uefa hakihusiki moja kwa moja katika kesi zinazohusu dawa za kusisimua misuli.












