Mtoano Afcon: Uganda yakabidhiwa Senegal

Chanzo cha picha, Getty Images
Ratiba ya hatua ya mechi za mtoano, ama 16 bora ya Afcon tayari ipo wazi, na mwakilishi pekee wa Afrika Mashariki Uganda ataminyana na Senegal.
Senegal ambayo ilikuwemo kwenye kundi C pamoja na nchi mbili za Afika Mashariki, Kenya na Tanzania.
Senegal ilizifunga timu hizo bila huruma; Tanzania 2-0 na Kenya 3-0.
Uganda na Senegal zitashuka dimbani Ijumaa usiku na mshindi wa mechi hiyo atasonga mbele mpaka raundi ya robo fainali.
Swali ni je, Uganda itanyolewa na Senegal kama ilivyotokea kwa jirani zake, ama italipa kisasi kwa niaba ya Afrika Mashariki?

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika mechi nyengine kali za hatua hiyo ya mtoano, miamba miwili ya soka barani Afrika, Cameroon na Nigeria wataumana jijini Alexandia siku ya Jumamosi.
Wenyeji Misri watakutana na Afrika Kusini, huku Ghana ikiminyana na Tunisia.
Ratiba kamili ya mtoano

Chanzo cha picha, Getty Images
Ijumaa, Julai 5
Morocco vs Benin
Uganda vs Senegal
Jumamosi, Julai 6
Nigeria vs Cameroon
Misri vs Afrika Kusini
Jumapili, Julai 7
Madagascar vs DR Congo
Algeria vs Guinea
Jumatatu, Julai 8
Mali vs Ivory Coast
Ghana vs Tunisia
Timu zilizofanya vibaya

Chanzo cha picha, CAF/TWITTER
Jumla ya timu nane zimefungasha virago kwa kutolewa katika hatua ya makundi, tatu kati ya hizo zimefungwa mechi zote.
Tanzania ndiyo timu iliyofanya vibaya zaidi katika mashindano hayo kitakwimu.
Tanzania imefungwa jumla ya magoli nane na kufunga mawili, hivyo wamemaliza wakiwa na uwiano wa magoli wa -6.
Timu inayofuata kwa kufanya vibaya ni Namibia ambayo pia ilifungwa mechi zote na kumaliza na uwiano wa magoli wa -5, kisha Burundi yenye alama sifuri pia na uwiano wa magoli wa -4.
Timu nyengine zilizofungasha virago ni Guinea-Bissau yenye alama 1, Zimbabwe alama 1, Mauritania alama 2, Angola alama 2 na Kenya yenye alama 3.
Timu nne zimefuzu katika raundi ya mtoano kama timu bora kati ya wale walioshindwa. Mataifa hayo ni Guinea, DR Congo, Afrika Kusini na Benin.












