Afcon2019: Uganda itaweza kuandika historia ya pili leo kwa kuifunga Zimbabwe?

Kikosi cha Uganda

Chanzo cha picha, CAF

Muda wa kusoma: Dakika 1

Uganda inashuka dimbani saa mbili usiku wa leo dhidi ya Zimbabwe katika mchezo wa pili wa Kundi A.

Endapo Uganda itashinda mchezo huo, itaandika historia ya pili katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Africa (Afcon).

Siku ya Jumamosi Uganda iliandika historia kwa kushinda mchezo wake wa kwanza wa Afcon, ikiwaadhibu jirani zao DR Congo goli 2-0.

Mwaka 2017 Uganda ilishiriki Afcon lakini ilishindwa kuandika ushindi walau kwenye mchezo mmoja.

Leo hii wanavaana na Zimbabwe, Uganda wanahitaji ushindi kwa hali na mali ili wafuzu moja kwa moja hatua ya mtoano.

Katika mechi ya kwanza dhidi ya DRC Uganda hawakupigiwa sana upatu kuondoka na ushindi.

DRC kwa takwimu za ubora wa viwango ipo juu ya Uganda, ina wachezaji wenye uzoefu zaidi na ni mabingwa mara mbili wa kombe hilo.

Lakini magoli ya Patrick Kaddu katika dakika ya 14 na Emmanuel Okwi katika dakika ya 48 yalitosha kuzamisha jahazi la DRC.

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Wenyeji Misri pia wapo kwenye Kundi A, na mchezo wa kwanza walipata ushindi mwembamba wa goli moja dhidi ya Zimbabwe.

Japo Zimbabwe wanaonekana ni vibonde katika kundi hilo, kufungwa goli moja na wenyeji Misri inaonesha kuwa si timu ya kubeza.

Tayari kocha wa Uganda, Sebastien Desabre amekanusha kuidharau Zimbabwe na kusema anatarajia mchezo mgunu hii leo.

Kwa Uganda, wakishindwa kupata ushindi, walau sare itawafaa katika kujiimarisha na hesabu za kufuzu kwa hatua ya mtoano.

Katika mpambano mwengine hii leo, wenyeji Misri watacheza na DRC.

Mchezo huo utapigwa kuanzia saa tano usiku.

Misri, itataka kuonesha kiwango bora zaidi kulinganisha na mechi dhidi ya Zimbabwe, na kupata ushindi utakaowavusha mpaka hatua ya mtoano.

DRC wao wanataka kuonesha kuwa bado ni timu nzuri ambayo kwa kiwango chao hawawezi kufungwa mechi mbili mfululizo.