Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta asisitiza kuwa hatarajii kusalia kwenye Ligi ya Ubelgiji msimu ujao

Samatta

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 2

Nahodha wa Taifa Stars Mbwana Samatta amesisitiza kuwa hatarajii kusalia kwenye klabu yake ya Genk msimu ujao na badala yake kuchezea Ligi ya Primia ya England.

Samatta ambaye ni kinara wa ufungaji wa klabu ya Genk ambao ni mabingwa wa Ligi ya Ubelgiji, anawaniwa na klabu kadhaa za England.

Akizungumza na runinga ya Azam TV, mshambuliaji huyo amesema yupo tayari kuchukua nafasi ya Romelu Lukaku wa Man United endapo atapata nafasi.

Lukaku amekuwa na wakati mgumu Old Trafford msimu uliopita na amekuwa akihusishwa na mipango ya kutaka kuhamia klabu ya Inter Milan.

Alipoulizwa na Azam TV endapo anaweza kuvaa viatu vya Lukaku Samatta alijibu: "Kwanini nishindwe? Naweza kuvaa. Mafanikio yanaweza yasiwe kama niliyopata Genk, lakini naweza kucheza, sababu mpira ni uleule. Tayari nipo Ulaya na najua nini natakiwa kufanya kwenye ligi za Ulaya. Itakuwa ni klabu kubwa na presha itaongezeka mara dufu, yaweza kuwa vigumu kuzoea mwanzoni lakini mwisho nitazowea."

Ruka X ujumbe
Ruhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)

Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue

Onyo: Imetoka kwingine na inaweza kuwa na matangazo

Mwisho wa X ujumbe

Samatta ameendelea kuficha ni klabu gani za England ambazo uongozi wake unafanya majadiliano nazo kwa sasa.

"Kwa sasa hivi siwezi kusema sana, ni kitu ambacho kipo kwenye mchakato nasubiria kitakapokuwa tayari na wakati utakapofika nitaweza kukizungumza. Lakini sijioni tena Genk, namuomba Mwenyezi Mungu litimie, lakini ikishindikana bado nina mkataba na Genk."

Katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari mwaka huu, klabu ya Cardiff ilituma ofa ya Pauni milioni 13 kumng'oa Genk, lakini uhamisho huo ukakwama.

Hata hivyo Cardiff imeshuka daraja.

Mwezi uliopita Samatta aliliambia gazeti la Mwanchi kuwa: "Ndiyo, nitaondoka mwishoni mwa msimu huu...(klabu ya England) moja inanifukuzia sana na imekuwa ikipiga simu kwa wakala wangu kila siku."

Samatta

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Samatta amefunga zaidi ya magoli 30 msimu huu akaiwa na klabu ya Genk.

Streka huyo mwenye miaka 26, ameifungia Genk magoli 23 na kumaliza kama mshambuliaji bora wa ligi. Pia ameifunga magoli 9 kwenye michuano ya ligi ya Europa.

Jina la Samatta limekuwa likiimbwa na mashabiki wa Genk, na wamekuwa wakimuomba mshambuliaji huyo kusalia klabuni hapo kucheza ligi ya Mabingwa Ulaya.

"Hawa jamaa (Genk) hawajacheza Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2011 enzi za akina (Kevin) De Bruyne, najua wanataka nicheze msimu ujao lakini Ligi Kuu ya England ina heshima yake...ni ligi ambayo tayari imepiga hatua kubwa sana kulinganisha na Ligi Kuu ya Ubelgiji. Ni ligi ambayo inapendwa na watu wengi duniani, Ligi inayoonekana sehemu kubwa duniani. Yaani kwa vitu vingi iko mbali," amesema Samtta.

Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.

Kabla ya kujiunga na Mazembe alikuwa akiichezea klabu ya Simba ya Tanzania.