Jurgen Klopp: Kocha wa Liverpool asema 'watapata tabu' kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Barcelona

Jurgen Klopp

Chanzo cha picha, PA

Maelezo ya picha, Liverpool chini ya Jurgen Klopp ilifika fainali msimu uliopita na kuchapwa na Real Madrid

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amesema timu yake 'itataabika' leo usiku kwenye mchezo wa nusu fainali ya Klabu Bingwa Ulaya djhidi ya Barcelona.

Klopp pia amesema anaamini timu yake itapata nafasi katika mchezo huo utakaopigwa nyumbani kwa Barcelona, dimbani Nou Camp.

"Je, tutakuwa wakamilifu? Hilo haliwezekani. Tutafanya makosa? Hakika. Tutaabika, naam kwa asilimia 100," amesema kocha huyo raia wa Ujerumani.

"Kutakuwa na nyakati ambazo tutapata nafasi mchezoni? Kabisa, kwa asilimia 100. Natumai tutazitumia nafasi, na hicho ndicho tutajaribu kufanya."

Klopp, ambaye aliiongoza Liverpool mpaka fainali msimu uliopita pia amesema: "Tutakuwa huru kucheza mchezo wetu lakini wapinzani wetu ni timu nzuri sana."

"Sisi tulikuwa kwenye mpambano mwaka jana, lakini wao wamekuwa kwenye mpambano kwa miaka karibu 20 sasa. Itakuwa mechi ngumu lakini naisubiri kwa hamu zote... Natumai wachezaji wangu nao wana ari kama yangu."

Kama ilivyo kwa Liverpool, Barcelona nao ni mabingwa mara tano wa kombe la Klabu Bingwa Ulaya.

Hata hivyo, Barcelona wameshinda makombe matatu ndani ya miaka 13 iliyopita. Wakati Liverpool imeshinda kombe lake la nne mwaka 1984 na la tano mwaka 2005.

Licha ya Liverpool kuwa na kikosi kikali chenye safu imara ya mashambulizi, Barcrlona hawajafungwa wakiwa nyumbani kwenye michuano hiyo kwa michezo 31 mfululizo sasa.

"Naweza sema tukipata sare hayatakuwa matokeo mabaya duniani, lakini si kama ndio tukitakacho, lakini itakuwa sawa tu," amesema Klopp ambaye pia aliiongoza Borussia Dortmund mpaka fainali ya michuano hiyo mwaka 2013.

Messi

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Lionel Messi alikuwa mwiba mkali kwa Manchester United katika hatua iliyopita, na je leo pia 'atawatenda' Liverpool?

"Watu wengi wamekuja Barcelona na mipango yao lakini kufika hapa wakagonga mwamba," amesisistiza Klopp.

Liverpool pia wanapambana ili kushinda ubingwa wa Ligi ya Primia baada ya miaka 29. Wanachuana vikali na Manchester City waliopo kileleni kwa tofauti ya alamambili huku ikisalia michezo miwili iliyosalia ligi kuisha.

Wakati Liverpool ikisubiria City wapoteze alama ili wao wachukue ubingwa, Klopp amekataa kusema kuwa wanaitazamia mechi ya leo kama nafasi adimu ya kushinda walau kikombe kimoja kikubwa msimu huu.

"Twatakiwa kupambana na Barcelona. Tuna nafasi katika michuano yote miwili. Sielewi kwanini watu wanapendelea kuongelea matokeo ya mchezo hata kabla ya kuchezwa."

"Kwa sasa sina haja ya kujua kipi ni bora kwetu kushinda. Tutajaribu kucheza kwa kiwango bora kabisa, kisha tutaona tunaweza kushinda kitu gani mwishoni mwa msimu.

"Tutakaporejea nyumbani (England) hatutakuwa na mchezo kati yetu na City, tutakuwa na mpambano dhidi ya Newcastle. Lakini hatutakiwi kuwafikiria Newcastle wakati tunaenda kuchuana na Barca. Litakuwa ni kosa kubwa sana kukutana na Barcelona huku vichwani mwetu kwa 15% au 20% tukiwaweka Newcastle."