Jose Mourinho: Nimepata ofa tatu za kuwa mkufunzi lakini pia 'siegeshi basi'

Chanzo cha picha, Reuters
Jose Mourinho anasema kuwa amekataa ofa tatu za kuwa mkufunzi tangu alipofutwa kazi na Man United huku akipinga madai kwamba anapendelea sana mtindo wa kuegesha basi.
Raia huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 55 alibwaga manyanga baada ya klabu hiyo kusema kuwa hakuna hatua aliyopiga kutokana na matokeo duni ya mechi , mtindo ama hata kuwaimarisha wachezaji chipukizi.
Mchezaji wa zamani wa Man United Gary Neville alisema kuwa hakuna anayestahili kuamua kuhusu filosofia ya klabu hiyo.
Gary Neville hajui Filiosofia yangu, Mourinho aliambia Bein Sports.
''Filosofia yangu inategemea. Ningependa kuwa katika klabu ambayo itanipatia mazingira sawa na yale ambayo mkufunzi wa liverpool anapata na mwenzake wa Manchester City''.
''Tayari nimekataa ofa tatu za kazi kwasababu nahisi sio ninachotaka''.
Maourinho ambaye aliiongoza Man United kushinda kombe la ligi pamoja na lile la bara Ulaya , anaeleweka kuwa na kandarasi ya kuondoka katika klabu hiyo ambayo inamzuia kuzungumzia kuhusu kuondoka kwake katika klabu hiyo.
Lakini alizungumzia kuhusu maswala kadhaa akiwa mgeni katika chombo cha habari za michezo cha Bein Sports:
- Jinsi ambavyo mchezaji mmoja alimwambia kutokosoa wachezaji katika mazoezi.
- Kukana madai kwamba yeye haegeshi basi, park the bus.
- Jinsi ambavyo hakuungwa mkono kama vile Guardiola na Klopp wanavyofanyiwa na klabu zao.
- Jinsi ambavyo siku za kuwa mkufunzi mwenye uwezo mwingi zimeisha.

Chanzo cha picha, Reuters
''Mchezaji mmoja alinitaka kutomkosoa''
Katika visa tofauti Mourinho alikuwa akimkosoa winga Anthony Martial, beki wa kushoto Luke Shaw na mshambuliaji Marcus Rashford, ambaye mchezo wake umeimarika tena chini ya ukufunzi wa Ole Gunner Solskjier.
Laikini alisisitiza kuhusu mchezaji mmoja ambaye alimtaka kutomkosoa huku Mourinho akihisi kwamba ni ishara ya wachezaji wa kisasa kuwa na hisia nyingi.
''Hivi majuzi nilipokuwa nikifunza mchezaji mmoja aliniambia tafadhali unaponikosoa nikosoe katika faragha sio mbele ya wachezaji wengine'' , alisema.
''Nilimuuliza kwa nini? alinijibu ''kwa sababu kwa hadhi yangu mbele ya wachezaji wengine unaponikosoa sihisi vyema''.
''Siku hizi lazima uwe mwerevu katika kuwasoma wachezaji wako, na kujaribu kuunda mazingira bora''.
Alilinganisha hali hiyo na ile ya mshambuliaji wa Chelsea Didier Drogba , ambaye alishirikiana naye katika uwanja wa Stamford Bridge aliposhinda ligi mara mbili 2005 na 2006.
''Drogba ni mchezaji ambaye unapozidisha shinikizo kwake ndipo anavyozidi kuimarika katika mchezo wake'', alisema Mourinho.
''Kuna wachezaji ambao unapowapatia shinikizo ndiposa wanapozidi kuimarika''.
''Kuna wengine ambao mafikra yao na tabia zao sio nzuri. Walilelewa katika mazingira tofauti , kwa wao kufikia kilele cha soka kila kitu walipata kwa urahisi. Kuna wengine hawatoa hisia sawa, hutoa maneno machafu na mara nyengine wengine ni hatari''.

Chanzo cha picha, PA
Manchester City na Liverpool zinaungwa mkono
Mourinho alisema kuwa kuwa filisofia yake ilitegemea timu aliyokuwa akiifunza, lakini akapinga shutuma kwamba kikosi chake kilipendelea sana kucheza mchezo wa kulinda lango ama ''Park the Bus''.
Alizungumza kuhusu mtindo wa soka aliocheza akiwa Chelsea na kusema: Je unajua sifa hyo ya 'park the bus' ilianza wapi?
''Ni wakati nilipokuwa bingwa na Real Madrid nikiwa na pointi 100 na magoli 106, rekodi nilioweka katika ligi hiyo''.
Pia alisema kuwa hakuungwa mkono sawia na wakufunzi wenzake katika klabu ya Liverpool na Manchester City.
Hiyo ni licha ya kutumia dau lilivonja rekodi la £75m kumnunua Romelu Lukaku. Anasema kwamba katika klabu ya Man City, Guardiola hakushinda ligi.
''Lakini katika msimu wa pili, Guardiola alifanya uamuzi muhimu lakini uliungwa mkono''.
''Katika klabu ya liverpool ni wachezaji wangapi walikuwepo kabla ya kuwasili kwa Klopp? iwapo wewe ni mkufunzi na una uwezo wa kuchagua wachezaji wanaoweza kufuata mawazo yako hicho ni kitu kimoja. upande mwengine ni iwapo huwezi kufanya hivyo''.
Siku za kuwa mkufunzi mwenye uwezo mwingi zimeisha.
Ijapokuwa Mourinho alionekana kuwa mkorofi kuhusu rekodi yake na mbinu zake hakuelezea iwapo alikuwa amepata funzo akiifunza Man United.
Klabu hiyo ipo katika harakati ya kumuajiri mkurugenzi wa soka ili kusaidia ushirikiano kati ya bodi na usimamizi wa timu.
Na raia huyo wa Ureno aliongezea: Wakati ambapo mkufunzi alikuwa katika kilele cha timu na mwenye uwezo mkubwa umekwisha na sasa unahitaji kila mtu katika klabu.












