Matokeo UEFA Valencia 2-1 Manchester United, Manchester City 2-1 Hoffenheim: Paul Pogba apoteza bao la wazi, Leroy Sane afunga mawili UEFA

Fedor Chalov

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, CSKA Moscow walitupwa nje licha ya ushindi wao dhidi ya Real Madrid

Manchester United walipokezwa kichapo na klabu ya Valencia ya Uhispania katika mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Jumatano baada ya nyota wao Paul Pogba kupoteza bao la wazi.

Kiungo Phil Jones alijifunga na kuchangia ushindi huo wa Valencia ambao uliwanyima Man utd nafasi ya kumaliza wakiwa kidedea katika Kundi H.

United walikuwa tayari wamefuzu kwa hatua ya muondoano na ushindi ungewawezesha kumaliza juu ya Juventus ya Italia waliochapwa 2-1 na Young Boys ya Uswizi.

Lakini vijana hao wa Jose Mourinho walicheza mchezo duni sana na wakachapwa na klabu ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya 15 katika ligi kuu ya Uhispania, La Liga, ambao walikuwa wanachezesha kikosi cha kubabaisha kwa kuwa walikuwa tayari wanajua wangemaliza wakiwa nafasi ya tatu.

Paul Pogba

Chanzo cha picha, Rex Features

Carlos Soler aliufikia mpira wa kichwa uliokuwa umetokea kwa Jones na kufunga bao la kwanza dakika ya 17 kabla ya Jones kufanya masihara tena na kumbwaga kipa wake Sergio Romero dakika ya 47 hata baada ya kipa huyo kuonekana kuwa katika nafasi nzuri ya kuunyaka mpira huo.

Pogba alikuwa amepoteza nafasi ya wazi ya kufunga mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kupokea mpira kutoka kwa Marouane Fellaini.

Wachezaji watatu nguvu mpya walioingia uwanjani kipindi cha pili walijaribu kuokoa jahazi la United na kufunga bao la kufutia machozi dakika ya 87.

Presentational grey line

Matokeo mechi za UEFA Jumatano 12 Desemba, 2018

  • Real Madrid 0-3 CSKA Moscow
  • Viktoria Plzen 2-1 Roma
  • Ajax 3-3 Bayern Munich
  • Benfica 1-0 AEK Athens
  • Man City 2-1 Hoffenheim
  • Shakhtar Donetsk 1-1 Lyon
  • Valencia 2-1 Man Utd
  • Young Boys 2-1 Juventus
Presentational grey line

Marcus Rashford alifunga kwa kichwa kutoka kwa krosi ya Ashley Young baada ya Jesse Lingard kufanikiwa kuuzuia mpira usitoke nje.

Hali kwamba wamemaliza wa pili kwenye kundi ina maana kwamba watapangwa kukutana na klabu iliyomaliza kidedea katika makundi mengine hatua ya muondoano. Wanaweza kukutana na klabu kama vile Barcelona, Borussia Dortmund, Paris St-Germain, Porto, Real Madrid na Bayern Munich.

Valencia v Manchester United

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Manchester United walikuwa wanapigania kushinda mechi yao ya tatu mtawalia ugenini Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya

Iwapo wangelimaliza kileleni, United wangekutana na mmoja kati ya Atletico Madrid, Roma, Schalke, Ajax na Lyon.

Watarejea uwanjani tena Anfied Jumapili kucheza mechi ya Ligi ya Premia dhidi ya mahasimu wao wa jadi ambao pia wamefuzu hatua ya muondoano Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya Liverpool.

Matokeo ya United Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu:

  • Kushinda v Young Boys (ugenini) 0-3
  • Sare v Valencia (nyumbani) 0-0
  • Kushindwav Juventus (nyumbani) 0-1
  • Kushinda v Juventus (ugenini) 2-1
  • Kushinda v Young Boys (nyumbani) 1-0
  • Kushindwa v Valencia (ugenini) 2-1
Group H

Chanzo cha picha, BBC Sport

Manchester City wafuzu wakiwa viranja

Leroy Sane (left)

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha, Wachezaji wa Hoffenheim waliokuwa wamejenga ukura Leroy Sane akipiga frikiki yake

Pep Guardiola alisema hatua ya Manchester City kufuzu kwa hatua ya 16 bora Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ni ufanisi usio na kifani baada yao kumaliza kileleni Kundi F kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Hoffenheim ya Ujerumani.

Leroy Sane alifunga mawili na kuwawezesha miamba hao wa England kufika hatua ya muondoano kwa msimu wa sita mtawalia.

"Mameneja ni wazuri sana na klabu bora zaidi Ulaya zipo hapa," alisema Guardiola.

"Baadhi ya klabu kubwa, kubwa sana zimetupwa nje. Inter Milan ni klabu nzuri lakini sasa watacheza Europa League.

"Siku moja ukilala kidogo utajipata Europa League, na ndiyo maana nina furaha sana kuwa katika 16 bora.

City waliunga nafasi nyingi lakini Hoffenheim ndio waliotangulia kufunga kupiria penalti iliyopigwa na Andrej Kramaric dakika ya 16.

Gabriel Jesus na Nicolas Otamendi walitikisa mwamba wa goli kwa mipira ya kichwa, naye John Stones akazimwa na kipa Oliver Baumann.

Sane aliwasawazishia kwa frikiki aliyoipiga akiwa hatua 25 kutoka kwenye goli ambapo ukuta wa wapinzani ni kama uliyeyuka dakika ya 45+1. Alifunga la pili dakika ya 61 kwenye kaunta.

City ndiyo klabu pekee ya England iliyoongoza kwenye kundi lake, na kwa hivyo wanaweza tu kukabidhiwa klabu nne pekee hatua ya 16 bora ambazo ni Atletico Madrid, Schalke, Roma au Ajax.

Leroy Sane

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha, Sane alikuwa mchezaji bora wa mechi

Real Madrid wapokezwa kipigo kikali zaidi Ulaya

Real Madrid walipokezwa kipigo chao kikubwa zaidi nyumbani kwao mechi za Ulaya baada ya kulazwa 3-0 na CSKA Moscow.

Mabingwa hao wa Ulaya walitumia kikosi hafifu sana mechi hiyo ya Kundi G na wakaadhibiwa kwa hilo. Kikosi hicho hata hivyo kilikuwa na Thibaut Courtois, Marcelo, Isco na Karim Benzema.

Real walimuingiza uwanjani Gareth Bale kipindi cha pili lakini akaumia kwenye kifundo cha mguu, ingawa aliweza kucheza kipindi kilichosalia cha mechi baada ya kupokea matibabu uwanjani.

Walizomewa na mashabiki wao baada ya mechi kumalizika.

Ilikuwa mara yao yakwanza kushindwa nyumbani mechi ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika kipindi cha miaka tisa.

CSKA Moscow, ambao mechi zao pekee walizoshinda ligi zilikuwa dhidi ya wamejipata nje baada ya kushika mkia kutokana na Viktoria Plzen kuwalaza Roma 2-1 na kumaliza nafasi ya tatu iliyowahakikishia nafasi ya kucheza Europa League.

CSKA ndiyo timu ya kwanza kuwashinda Real nyumbani na ugenini kwenye kundi tangu Juventus walipofanya hivyo msimu wa 2008-09.