Wilder v Fury: Tyson Fury asema 'dunia inajua bingwa halisi ni nani' baada ya pambano kuwa sare

Deontay Wilder (l) and Tyson Fury

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Tyson Fury (kulia) Deontay Wilder (kushoto) wote hawajawahi kupoteza pambano

Bondia Tyson Fury amesema "dunia inajua bingwa halisi wa ndondi za uzani wa juu ni nani " na anaamini kuwa matokeo ya sare yalikuwa ni "maamuzi ya zawadi" kwa bondia Deontay Wilder.

Fury, 30, ambaye ni raia wa Uingereza alirejea ulingoni jijini Los Angeles baada ya muda mrefu kuka nje na kupambana vyema, kiasi wachambuzi wengi wa mchezo huo wakiamini alishinda.

Tayri promota Frank Warren amesema yeye pamoja na bodi ya masumbwi ya Uingereza wataiandikia shirikisho la WBC barua ya kutaka pambano la marudio la mabondia hao. Wilder ni raia wa Marekani.

Akiongea jana jumapili kuhusu pambano liliopigwa alfajiri ya jumamosi kwa saa Afrika Mashariki, Fury amesema: "Kwa kweli sijawahi ona maamuzi mabovu kama haya maishani mwangu. Sijui ni pambano gani walikuwa wanaliangalia (majaji)."

Mabondia kadhaa ambao ni mabingwa wa zamani wa dunia kama Floyd Mayweather, Lennox Lewis, Tony Bellew na Carl Froch wanaamini Fury alishinda.

Fury aliangushwa mara mbili katika pambano hilo la raundi 12 lakini mara zote alinyanyuka na kuendelea na mpambano.

Baada ya pambano kuisha, jaji wa kwanza alimpa Wider ushindi wa alama 115 dhidi ya 111 za Fury, jaji wa pili alimpa ushindi Fury wa alama 114 dhidi ya 112 za Fury na jaji wa tatu na wa mwisho akatoa alama sare za 113-113.

Alejandro Rochin ndiye jaji aliyempa alama za juu Wilder na Fury amesema jaji huyo hafai.

Fury na Wielder

Chanzo cha picha, Getty Images

"Sijui alikuwa anaangalia kitu gani," ameng'aka Fury na kuongeza. "Vitu kama hivi ndivyo vinaupa mchezo wa masumbwi jina baya. Vyombo vyote vya habari vitaandika habari mbaya. Kila mdau wa masumbwi atasema neno baya. Inabidi afungiwe maisha kujihusisha na masumbwi."

"Dunia inajua bingwa halisi wa ndondi za uzani wa juu ni nani. Wilder amepewa zawadi ya matokeo akiwa nchini mwake. Itakuwa anaishukuru nyota yake ya bahati kwa kubaki na mikanda ya kijani na dhahabu ambayo mimi ndiye mmiliki halisi."

Fury amedai atarudi nyumbani kama "shujaa".

Akizungumza namna alivyoweza kunyanyuka baada ya kuangushwa na konde la Wilder, Fury amesema alikuwa kama "mzimu wa phoenix akinyanyuka kutoka kwenye majivu".

Fury aliangushwa na kurejea tena katika pambano

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Fury aliangushwa na kurejea tena katika pambano

"Tumpe sifa yake. Alinipata wakati muafaka. Nilinyanyuka, sijui niliwezaje. Hauwezi kwenda kuogelea na usilowe."

Fury amesema mkufunzi wake Ben Davison mwenye miaka 26 anastahili kupewa tuzo ya thamani ya mkufunzi bora wa mwaka kwa wa jarida la Ring.

Davison amemsaidia Fury kurudi katika ubora wake baada ya kukaa nje ya ulingo kwa miezi 30. Pambano lake la mwisho lilikuwa mwaka 2015 kwa kumtandika Wladimir Klitschko. Baada ya hapo bondia huyo alipambana dhidi ya msongo wa mawazo na kukubali kifungo cha kujihusisha na mchezo huo kwa kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni.