Champions League: Man United yakubali kipigo mbele ya Juventus

Dyabala akifunga goli

Chanzo cha picha, Getty Images

Manchester United wameangukia pua katika uga wao wa Old Trafford kwa kukubali kichapo cha goli moja bila majibu kutoka kwa miamba Juventus wa Italia.

Nyota mpya wa Juventus ambaye amewahi kukupiga na United hapo awali Cristiano Ronaldo aligeuka mwiba mchungu kwa mashabiki wake wa zamani Jumatano usiku.

Krosi ya Ronaldo ndiyo ilizaa goli lilofungwa na Paulo Dybala katika dakika ya 17 ya kipindi cha kwanza.

Juve maarufu kama Bibi Kizee wa Torino waliwakaba koo United maarufu kama Mashetani Wekundu kwa kumiliki mpira kwa 70%. Juve pia ilifanya mashambulizi makali 10 na United kuambulia shambulizi moja.

Mashetani wekundu waliamka kiasi mwanzoni mwa kipindi cha pili na kufanya shambulizi la maana kupitia kiungo Paul Pogba lakini shuti lake liligonga mwamba.

Usiku wa jana ulikuwa mgumu kwa kocha wa Manchester United Jose Mourinho ambaye alifanyiwa kebehi na mashabiki wa Juve.

Kipigo cha jana kilikuwa cha pili kwenye mashindano ya Ulaya toka mwaka 2013 kwa Manchester United wakiwa nyumbani Old Trafford.

Mwaka 2013 United walifungwa na Real Madrid na Ronaldo alipachika bao la ushindi.

Ronaldo na Dyabala

Chanzo cha picha, Getty Images

Juve na United watacheza mechi ya marudio katika uga wa Allianz Novemba 7. Iwapo Juve yenye alama 9 na kushika usukani wa Kundi H itashinda mchezo huo itafuzu katika hatua ya mtoano (16 bora).

United wanasalia katika nafasi ya pili na alama zao 4. Valencia wana alama 2 na Young Boys wanashikilia mkia wakiwa na alama 1.

Mourinho amekubali kushindwa akisema Juve walikuwa na kiwango bora Zaidi. "…Juventus wapo katika kiwango cha tofauti nasi. Yanipasa kuwa muwazi. Ubora, ukomavu na uzoefu wao ni wa kiwango cha juu. Ilikuwa mechi ngumu sana kwetu. Nilifikiri tungeambulia kitu lakini haikuwezekana."