Ramla Ali: Mwanamke wa kwanza anaye azimia kuiwakilisha Somalia katika masumbwi Olimpiki

Chanzo cha picha, Richard Moore
Wakati mwanamasumbwi Ramla Ali aliposhinda mataji ya Uingereza na England mnamo 2016, familia yake haikutazama mapigano hayo.
Sio kwamba hawakuweza kutazama kuhofia kuumizwa kwake - hawakujua kabisa.
Kwa mara ya kwanza mwanamke muislamu kuwahi kushinda pigano la England ameificha siri hiyo kwa muda mrefu kutoka kwa familia yake akiamini kuwa hawatopendelea, kama ambavyo bado wengine hawalipendelei hilo.
" Nakumbuka nilishindana katika fainali ya pigano la kitaifa," Ali, binti wa imamu ameiambia BBC Sport Africa. "Wazazi wangu wanaishi Bethnal Green [mjini London] na fainali zilikuwa zinafanyika katika mtaa jirani wa York Hall.
"Nakumbuka nikimpa kocha begi langu na nikamwambia: 'Tutakatana huko baadaye'. NIkasema: 'Mama nakwenda nje kukimbia, tutaonana baadaye' - na kwa wakati wote, nilikuwa nakwenda kushindana kimataifa, ndicho kiasi cha hali iliyokuwa ikinikabili."
Ali alianza kupigana masumbwi akiwa msichana mdogo na alimuambia mamake anafanya mazoezi tu, na sio kushiriki mashindano.
Ni hadi alipotimia miaka zaidi ya 20 ndipo maisha yake ya siri yalipofichuka.

Chanzo cha picha, Charles Hyams
'Kwanini unauonyesha mwili wako?'
"Nakumbuka nikirudi kutoka kwenye mazoezi na kila mtu alikuwa sebuleni," anaeleza mwanamasumbwi aliyeiwakilisha England kabla ya kubadili uwakilishi kuwa wanyumbani alikozaliwa Somalia.
"Nilijiulizat: 'nini kinachoendelea hapa? kwa kawaida hatukai chini pamoja na wakaniambia: 'Sikiliza ni lazima uache tabia hii.Ni kwanini unauonyesha mwili wako? Sio sawa kwa msichana wa kiislamu, ni mchezo wa wanaume, je jamii itakufikiriaje?'
"Nilivunjika moyo kwa kweli waliponiambia hivyo."
Ili kuifurahisha familia yake, mpiganaji huyo wa uzani wa featherweight aliacha kupigana - kama alivyowahi kuacha na kurudi tena mara kadhaa katika maisha yake ya kupigana.
Kwa wakati mmoja, Ali aliingia kufanya kazi katika kampuni ya uwakili, akilizimika kuzama katika kazi hadi usiku wa manane jambo lililomzuia kupigana, lakini hilo halikudumu baada ya miezi sita alirudi katika mchezo huo ambao umeyabadili pakubwa maisha yake.
Kuitoroka Mogadishu
Ali alikuwa mtoto mdogo wakati familia yake ilipoutoweka mji mkuu wa Somalia Mogadishu katikam iaka ya 1990 baada ya kakake wa miaka 12 kuuawa na kombora alipokuwa akicheza nje wakati wa vita vya kiraia.
Kwamba amefanikiwa kuishi mpaka sasa ni kama miujiza kutokana na namna mamake anavyoeleza walivyoutoroka mji mkuu huo.

Chanzo cha picha, Reuters
"Tuliyawacha makaazi yetu, nyaraka zetu muhimu kila kitu," anasema Anisa Maye Maalim. " Kulikuwana milipuko na watu walitupiga risasi , waliwaua baadhi ya watu waliokuwa ndani ya gari letu."
Baada ya kuponea safari hatari ya siku 9 kuingia Kenya wakati ambapo Maalim anasema abiria wengi katika boti lililojaa walikufa kwa njaa, walifanikiwa kuishi kwa msaada wa chakula kutoka kwa Umoja wa mataifa mjini Mombasa kabla ya kuwasili England kama wakimbizi.
Waliishia London ambako Ali, aliyekuwa anazungumza Kisomali tu alianza kusoma.
Kwa miaka michache, mwanamasumbwi huyo wa siri alianza kushindana katika mashindano rasmi, huku familia yake ikiwa gizani isipokuwa tu kakae mdogo aliyemsaidia kutoroka.

Chanzo cha picha, Getty Images
'Umenipa fahari kubwa'
Lakini mwaka jana, Ali aliamua kuiwakilisha Somalia jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kutoka na kwamba nchi hiyo imekuwa ikitajwa kama iliyoshindwa kutoka katika vita, na haina shirikisho la ndondi.
Lakini shinikizo la Ramla na mumewe Richard Moore limechangia kuidhinishwa kwa shirikisho la ndondi la Somalia mnamo Februari, na Moore kuwa kocha wa kitaifa.
Huku Ramla na Richard wakifukuzia ndoto yao, mahojiano katika TV ya kisomali yalichangia maisha yake kubadilika pakubwa.

Chanzo cha picha, Richard Moore
Mjombake alitazama mahojiano hayo.
"Alisema: 'Umenipa fahari kubwa. Unachofanya ni kitu kizuri mno ,na nasikitika umelizimika kuliweka siri kwa muda huu wote. Usijali nitamuambia mamako, kwamba ni jambo zuri na sio baya '," anatabasamu.
Hatimaye mamake aliridhia - aliyeshawishika kwa mambo mazuri yanayoweza kutokana na hilo kwa ajili ya Somalia inayokumbwa na mzozo.
"Nilimuambia tu ajifunike mtandio kichwani, ili watu wajue ni msichana mzuri wa kiislamu." amesema Maalim.

Kioo cha jamii
Ali anaungwa mkono pakubwa kutoka kwa jamii ile ile ambayo kwa wakati mmoja mamake alikuwana wasiwasi nayo.
Licha ya kwamba bado kuna baadhi wasiolipendelea, wakiwemo nduguze wakubwa, lengo ni kupiga hatua zaidi mbele.
Somalia haijawahi kutuma mwanamasumbwi kwenda kushiriki katika Olimpiki na haijawahi kushinda medali - lakini Ali analenga kutimiza yote mawili ifikapo 2020.
Iwapo atashinda au atashindwa, anaamini kwamba tayari amefanikiwa.













