Afcon 2019: Vumbi kutimka Jumamosi Uganda wakivaana na Tanzania, Kenya na Ghana

Chanzo cha picha, AFP/GETTY
Vumbi litatimuka Jumamosi jijini Kampala ambapo mataifa jirani ya Tanzania na Uganda wataminyana kutafuta nafasi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2019.
Kocha mpya wa Taifa Stars ya Tanzania mchezaji maarufu wa zamani wa Niigeria Emmanuel Amunike atakuwa na kibarua kigumu katika mechi ya kwanza kutokana na rekodi safi ya Uganda maarufu The Cranes.
The Cranes ndio timu pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki kushiriki mashindano hayo miaka miwili iliyopita nchini Gabon.
Timu hizo mbili zipo katika kundi L linaloongozwa na Uganda yenye pointi tatu baada ya kuifunga Cape Verde inayoshika mkia. Tanzania na Lesotho wote wana pointi moja baada ya kutoka sare jijini Dar es Salaam.
Uganda watakuwa wanamtegemea mshambuliaji wao Emmanuel Okwi ambaye anachezea klabu ya Simba ya Tanzania. Okwi alikuwa mfungaji bora wa ligi ya Tanzania msimu wa 2017/18.
Taifa Stars kwa upande wao wanamtegemea nahodha wao Mbwana Samatta ambaye anang'ara na klabu ya Genk ya Ubelgiji.

Chanzo cha picha, Getty Images
Historia inaibeba zaidi Uganda ambayo imeshinda mara 29 kati ya mechi 53 baina ya timu hizo mbili. Tanzania imeshinda mechi 10. Taifa Stars na Cranes wametoka sare mara 14.
Kenya vs Ghana

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa upande wa Kenya watashuka dimbani Moi Kasarani bila nahodha wao Victor Wanyama anaekipiga ligi ya England na klabu ya Tottenham Hotspurs.
Wanyama amekuwa majeruhi kwa muda mrefu na hivi karibuni ameripotiwa kuanza kufanya mazoezi.
Kenya maarufu kama Harambee Stars ina mtihani mgumu zaidi baada ya kushangazwa na Sierra Leone kwa kufungwa 2-1 katika mchezo wa awali wa kundi F.
Ghana, wanaofahamika kama Black Stars walianza kampeni yao kwa kuwabamiza Ethiopia kwa goli 5-0.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa namna yeyote ile mchezo wa kesho ni wa kufa na kupona kwa Kenya katika harakati za kutafuta nafasi ya kutinga fainali za mwakani zitakazopigwa nchini Cameroon.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa mwaka 2005 katika mechi ya kirafiki iliyomalizika kwa sare ya 2-2.
Timu mbili za juu katika makundi yote ndizo zitakazofuzu kwenye mashindano ya Afcon 2018.
Katika michezo mingine, Burundi itaminyana na Gabon Jumamosi pia. Siku ya Jumapili Rwanda watavaana na Ivory Coast huku DRC wakicheza dhidi ya Liberia.












