Gareth Bale awasaidia Real Madrid kutoka nyuma na kushinda 4-1, Ronaldo bado hajafunga Serie A

Gareth Bale akisherehekea kuwafunga Real Madrid

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Bale pia alifunga bao walipolaza Getafe

Gareth Bale alifunga bao kwa mechi yake ya pili mtawalia La Liga na kuwawezesha Real Madrid kutoka nyuma na kuwalaza Girona 4-1.

Wenyeji hao wa Catalonia walikuwa wamejiweka kifua mbele kupitia bao la Borja Garcia kabla ya Sergio Ramos kusawazisha kupitia penalti baada ya Marco Asensio kuchezewa visivyo eneo la hatari.

Real walijiweka kifua mbele kupitia penalti nyingine ambayo bado ilipatikana baada ya Asensio kufanyiwa madhambi eneo la hatari lakini mfungaji wakati huu akawa Mfaransa Karim Benzema.

Bale baadaye alifunga baada ya kupokea pasi kutoka kwa Isco.

Bale baadaye alimsaidia Benzema kufunga.

Nyota huyo wa Wales mwenye miaka 29 pia alikuwa amefunga katika mechi ya kwanza ya Real katika La Liga chini ya meneja wao mpya Julen Lopetegui wiki iliyopita, ambapo waliwalaza Getafe 2-0 uwanjani Santiago Bernabeu.

Girona, waliomaliza nafasi ya 10 msimu uliopita La Liga walikuwa wamewashinda Real 2-1 walipokutana nao mechi kama hiyo msimu uliopita.

Kulikuwa na dalili kwamba wangewashangaza tena baada ya Garcia kufunga kutokana na kutomakinika kwa walinzi wa Real.

Hata hivyo waliathiriwa na mikwaju ya penalti ambayo hawawezi wakamlaumu mwamuzi kwani Marc Muniesa alikosa kumakinika akimkaba Asensio, Pere Pons naye pia akarudia kosa kama hilo.

Wengi wamekuwa wakisubiri kuona iwapo Real watajimudu bila mshambuliaji wao nyota Cristiano Ronaldo aliyehamia Juventus na meneja wao Zinedine Zidane aliyejiuzulu baada ya msimu uliopita kumalizika.

Ronaldo aliondoka na ushindi mechi yake ya kwanza ya nyumbani ligini Serie A Juve walipopata ushindi wa 2-0 dhidi ya Lazio, mabao yakifungwa na Miralem Pjanic na Mario Mandzukic.

Ronaldo, aliyenunuliwa £99.2m kutoka Real Madrid, hajafunga bao hata moja katika mechi mbili za Serie A walizocheza kufikia sasa.

Cristiano Ronaldo na Mario Mandzukic

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Cristiano Ronaldo na Mario Mandzukic

Katika mechi hiyo dhidi ya Lazio, mashabiki waliinua mabango yenye jina lake.

Aligusa mpira mara moja pekee eneo la hatari la wapinzani uwanjani Allianz kipindi cha kwanza, na muda mfupi kabla ya bao la pili la Juve alikuwa amepiga shuti kali lakini likarushwa nje na kipa Thomas Strakosha.

Ronaldo ndiye aliyekuwa amefikiwa na mpira ndani ya eneo la hatari kutoka kwa krosi ya Joao Cancelo lakini akashindwa kuupiga vyema na badala yake ulipodunga na kurejea uwanjani Mandzukic akafunga dakika ya 75.

Edinson Cavani, Kylian Mbappe na Neymar

Chanzo cha picha, Getty Images

Ufaransa, washambuliaji watatu nyota wa Paris St-Germain - Edinson Cavani, Kylian Mbappe na Neymar - wote walifunga na kuwawezeshamabingwa hao watetezi kuwalaza Angers 3-1 mechi ya Ligue 1.