Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Arsenal 0-2 Manchester City: Pep Guardiola asema City wataimarika hata zaidi
Meneja wa Manchester City Pep Guardiola amesema klabu hiyo itaimarika hata zaidi kadiri siku zinavyosonga.
Alisema hiyo hata baada yao kuwazidi nguvu Arsenal mechi yao ya kwanza msimu huu Ligi Kuu England kwa kuwacharaza 2-0 Jumapili.
Gunners walikuwa wanacheza mechi yao ya kwanza ya ushindani bila Arsene Wenger ambaye alikuwa amewaongoza tangu 1996 kabla ya kustaafu mwishoni mwa msimu uliopita.
Lakini hawakujiweza dhidi ya mabinga hao watetezi uwanjani Emirates.
Raheem Sterling aliwaweka City kifua mbele dakika ya 14 na kisha Bernardo Silva akaongeza la pili dakika ya 64.
Upande wa Arsenal Pierre-Emerick Aubameyang na nguvu mpya Alexandre Lacazette ndio waliokaribia kufunga lakini bahati haikusimama.
"Tuna wachezaji wengi sana ambao bado hawajafikia kiwango chao cha juu cha uchezaji lakini tumekuwa pamoja kwa misimu miwili na tunajua tunafaa kufanya nini," Guardiola aliambia BBC Sport baada ya mechi hiyo.
"Tumecheza vyema sana kwa jumla na siku baada ya siku tutaendelea kuimarika na kuimarika.
"Nina furaha kuwa meneja wa Manchester City. Wamenipa kikosi kizuri sana. Siwezi kulalamika hata dakika moja."
City wameonyesha makali yao
City wakiwa na Pep Guardiola walionekana kuwa na makali sana wakati wa mechi ya Ngao ya Jamii ambapo waliwalaza Chelsea 2-0 na Jumapili walionekana imara sana.
Walimnunua mchezaji mmoja pekee wa kikosi cha kwanza, Riyad Mahrez waliyemnunua £60m kutoka Leicester dirisha kuu la kuhama wachezaji, na alichezeshwa mechi yao ya kwanza Liig ya Premia.
Aliwasaidia sana safu ya kati. Sterling alichezeshwa wingi ya kushoto badala la Leroy Sane ambaye aliingizwa kama nguvu mpya na mchezaji huyo wa England akawafaa kwa bao la kwanza na lake la 50 Ligi ya Premia.
"Kila msimu huwa ni msimu muhimu na mechi hii ilikuwa ngumu sana lakini tulicheza soka ya kiwango cha juu sana. Tuliunda nafasi nyingi sana na uchezaji wetu ulikuwa mzuri. Tutaendeleza safari hii," alisema Guardiola.
"Tumeridhika kwa sababu nyingi, nyingi sana.
"Mambo yakiwa 1-0 tulipata bao ambalo pengine hatukustahiki, lakini kipindi cha kwanza tulistahili kufunga mabao mengine mawili au matatu hiyi."
Meneja wa Arsenal alisema nini?
Arsenal walianza vyema mechi dakika za kwanza tano na pia wakakamilisha kipindi cha kwanza vyema Aubameyang na Henrikh Mkhitaryan wakikaribia kufunga.
Waliwachezea wachezaji wawili wapya, Mgiriki Sokratis Papastathopoulos beki wa kati aliyetokea Borussia Dortmund, na kiungo wa kati kinda wa miaka 19 Guendouzi aliyekuwa akichezea Lorient ya Ufaransa.
Guendouzi alicheza vyema na anataraiwa kuchezeshwa zaidi na Emery Unai msimu huu.
"Ilikuwa mechi yake ya kwanza Ligi ya Premia. Ana sifa nzuri na ustadi pia na akiwa uwanjani ataimarika haraka zaidi," alisema meneja wa Arsenal.
Kulikuwa na dalili kwamba Arsenal ambao walicheza kwa mfumo wa 4-2-3-1 wanahitaji muda zaidi kuzoea mfumo huo mpya.
"Matokeo yalikuwa 2-0 lakini nafikiri kwa jumla katika dakika hizo 90 tulikuwa tunaimarika," Emery alisema.
"Kipindi cha kwanza hatukucheza tulivyotaka. Tulizungumza wakati wa mapumziko kuhusu kuwajibika zaidi kipindi cha pili, kujituma zaidi. Tulitaka tuimarisha udhibiti wa mpira na kuzuia pasi zao. Nafikiri katika kipindi cha pili tulicheza zaidi jinsi tulivyotaka."
Meneja huyo wa zamani wa Sevilla na Paris St-Germain alisema alifurahia mandhari Emirates.
"Tulitaka kuanza hapa na wafuasi wetu. Tulitaka kuonyesha ustadi wetu lakini ni wazi kwamba mikononi mwa Manchester City hatungeweza kuwapa (mashabiki) ushindi. Lakini nafikiri hapa mambo yatakuwa sawa sana."
Nini kinafuata?
Arsenal na Unai Emery walikuwa na ratiba ngumu ya mechi kwani sasa wanajiandaa kwa safari ya Stamford Bridge kukutana na Chelsea Jummaosi. City watakuwa wenyeji wa Huddersfield Jumapili.