Kepa Arrizabalaga: Chelsea wakaribia kuvunja rekodi ya dunia kwa kumnunua kipa wa Athletic Bilbao kwa £71m

Kepa Arrizabalaga anayelinda lango Athletic Bilbao

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kepa Arrizabalaga anayelinda lango Athletic Bilbao

Chelsea wamepiga hatua sana katika mazungumzo yao ya kutaka kumnunua mlinda lango Kepa Arrizabalaga kutoka klabu ya Athletic Bilbao ya Uhispania katika uhamisho ambao utavunja rekodi ya nunua ya ununuzi wa golikipa.

Mlinda lango huyo mwenye miaka 23 anatarajiwa kununuliwa kujaza nafasi ya Thibaut Courtois ambaye anaonekana kutokuwa tayari kusalia katika klabu hiyo ya Stamford Bridge.

Ada hiyo itazidi £66.8m ambazo Liverpool walilipa mwezi Julai kumchukua kipa wa Brazil Alisson.

Courtois, ambaye huchezea timu ya taifa ya Ubelgiji, bado hajarejea mazoezini huku tetesi zikimhusisha na kuhamia Real Madrid.

Mchezaji huyo mwenye miaka 26 alikuwa ametarajiwa kujiunga na wenzake kwa mazoezi ya kuanza msimu Jumatatu lakini hakufika.

Inadaiwa anataka kulazimisha uhamisho wake kwa kuwa klabu yake haikuwa inataka kumuuza.

Alipoulizwa kuhusu Kepa baada ya Chelsea kuwashinda Lyon wa Ufaransa kwa mikwaju ya penalti Jumanne, meneja wa Chelsea Maurizio Sarri alisema: "Nilimwona mwaka mmoja uliopita. Maoni yangu ya kwanza yalikuwa kwamba yeye ni kipa mzuri sana, wa umri mdogo, lakini mzuri sana."

Thibaut Courtois

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Courtois aliibuka kipa bora wa michuano ya Kombe la Dunia Urusi akichezea Ubelgiji

Iwapo ununuzi wa Kepa utafanikiwa, basi itakuwa ni rekodi pia kwa klabu hiyo ya London katika ununuzi wa wachezaji.

Bei yake itazidi £58m walizowalipa Real Madrid kumchukua mshambuliaji Mhispania Alvaro Morata mwaka jana.

Kepa kipa msaidizi wa De Gea

Kepa ni kipa nambari mbili katika timu ya taifa ya Uhispania, akiwa nyuma ya kipa wa Manchester United David de Gea, na amechezea timu ya taifa mechi moja pekee.

Kepa Arrizabalaga amechezea timu ya taifa ya Uhispania mechi moja pekee

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kepa Arrizabalaga amechezea timu ya taifa ya Uhispania mechi moja pekee

Amekaa misimu miwili katika kikosi cha kwanza cha Bilbao na kuwalindia lango katika mechi 53 La Liga.