Ligi Kuu England: Fulham wamchukua Andre Schurrle kutoka Borussia Dortmund

Andre Schurrle

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Schurrle amefunga mabao matatu katika mechi 33 alizowachezea Dortmund

Fulham wamemchukua mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Chelsea Andre Schurrle kutoka klabu ya Borussia Dortmund inayocheza Ligi Kuu ya Ujerumani.

Mchezaji huyo alishinda Kombe la Dunia akiwa na timu ya taifa mwaka 2014. Hata hivyo hakujumuishwa katika kikosi kilichokuwa Urusi mwaka huu.

Schurrle mwenye miaka 27 atakuwa na klabu hiyo ya Craven Cottage kwa misimu miwili kwa mkopo.

"Nasubiri sana kuanza," amesema.

"Ni lazima nipiganie nafasi yangu na nahitajika kuonyesha ustadi ili niwe mchezaji anayeweza kuisaidia timu."

Schurrle aliwachezea Chelsea msimu wa 2013-15 na alitunukiwa nishani ya mshindi wa Ligi ya Premia mwaka 2015 licha ya kwamba alikuwa amehamia Wolfsburg ya Ujerumani katikati ya msimu.

Amekuwa na Dortmund tangu Julai 2016 ambapo amewachezea mechi 33 na kufunga mabao matatu.

Amechezea timu ya taifa ya Ujerumani mechi 57.

Fulham walipandishwa daraja tena kucheza Ligi Kuu ya England Mei mwaka huu baada ya kuwashinda Aston Villa katika mechi ya muondoano ya baada ya msimu ya kufuzu kwa EPL kutoka ligi ya Championship.

Walifanya hivyo kwa kuandikisha ushindi wao wa kwanza kabisa uwanjani Wembley katika kipindi cha miaka 139 kwenye mechi hiyo iliyochezwa 26 Mei, 2018.