Riyad Mahrez ajiunga na Manchester City kwa Paundi milioni 60

Manchester City imevunja rekodi yake kwa kumsajili winga wa Leicester City Riyad Mahrez kwa Paundi milioni 60.
Mahrez mwenye miaka 27 amesaini mkataba wa miaka 5 na kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na City tokea ichukue ubingwa msimu uliopita.
City ilijiondoa katika mbio za kumuwania Mahrez mwezi Januari baada ya Leicester kumzuia kuondoka.
Mahrez amesema aina ya uchezaji wa City inavutia na ni timu ambayo kila mchezaji anatamani kuichezea.

''Kuwaona wakicheza limekua jambo la kuvutia sana,'' alisema Mahrez.
''Pep Guardiola ni kocha ambaye anapenda soka la kushambulia, na kiwango cha City msimu uliopita kilikua kizuri sana.
''Nafikiri tutafanikiwa zaidi miaka ya mbeleni na ninaamini aina yangu ya uchezaji inaweza kuwa nzuri zaidi chini ya uongozi wa Pep.''

Mahrez alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka baada ya Leicester kuwashangaza wengi kwa kuwa mabingwa wa England msimu wa 2015-16 akiondoka klabuni hapo kwa rekodi ya ufungaji wa magoli 48 katika michezo 179.
Leicester inasema ''Alicheza kwa moyo mmoja akiwa karibu sana na amashabiki kwa miaka minne na nusu ndani ya klabu.''
''Kumbukumbu yake itadumu daima katika historia na mioyoni mwa mashabiki''.
Mahrez aliomba kuhama Leicester mwezi Januari lakini ikashindikana baada ya Manchester City kukataa kutoa Paundi milioni 95 iliyokua ikihitajika na Leicester.














