Gor Mahia yaichapa Simba 2-0 mchezo wa fainali kombe la SportPesa

Gor Mahia ya Kenya wamefanikiwa kutetea ubingwa wao kwa kuifunga Simba ya Tanzania mabao 2-0
Maelezo ya picha, Gor Mahia ya Kenya wamefanikiwa kutetea ubingwa wao kwa kuifunga Simba ya Tanzania mabao 2-0

Bingwa mtetezi Gor Mahia ya Kenya imehifadhi ubingwa wa mashindano ya kandanda ya SportPesa Super Cup ambayo yamemalizika leo hii katika uwanja wa Afraha Stadium, Nakuru eneo la bonde la ufa nchini Kenya.Gor Mahia imeshinda Simba ya Tanzania mabao 2-0, wafungaji wakiwa ni Meddie Kagere na Jacques Tuyisenge wote kutoka Rwanda.

Kwa matokeo hayo Gor Mahia sasa imejikatia tiketi ya kusafiri England mwezi ujao kupambana na Everton katika uwanja wao wa Goodison Park.

Wakicheza mbele ya halaiki ya mashibi, Gor Mahia walitawala mechi kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Wachezaji wa Gor Mahia wakiwa na furaha tele
Maelezo ya picha, Wachezaji wa Gor Mahia wakiwa na furaha tele

Kocha wa Simba Masoud Djuma amesema hawatumia nafasi zao za kufunga kikamilifu.

"Tunakubali Gor Mahia wametuzidi nguvu.lakini ndio hali ya mchezo,'' alisema Djuma.Naibu wa kocha wa Gor Mahia Zedekiah Otieno alikua anatembea juu ya keki.

"Siku kubwa leo kwa Gor, Simba tumewaonyesha ngoma ya hali ya juu sasa tunajiandaa kwa safari ya England," alisema Otieno

Singida United na Kakamega Homeboys

Katika mechi ya nusu fainali Gor Mahia ilishinda Singida ya Tanzania mabao 2-0, na Simba ikaiondoa Kakamega Homeboyz ya Kenya kwa mabao 5-4 ya penalti.

Singida United imeibuka mshindi wa tatu
Maelezo ya picha, Singida United imeibuka mshindi wa tatu

Singida United FC iliichapa Kakamega Homeboys 4-1 kwa mikwaju ya Penati katika na kuwa mshindi wa tatu katika michuano hiyo

Timu hizo mbili zilikuwa sare ya 1-1 kabla ya Homeboys kuzidiwa kete na Singida kwenye mikwaju ya penati kisha kunyakua ushindi wa tatu na kitita cha doa za Marekani 7500 huku Homeboys waliomaliza washindi wa nne wakizawadiwa dola 5000.

Bao la kwanza la Kakamega Homeboys lilifungwa dakika ya 10 na Wycliffe Opondo .Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Homeboys wakiwa kifua mbele kwa bao moja bila majibu.

Katika dakika ya 60 kipindi cha pili, Danny Lyanga aliisawazishia Singida United bao.

Mchezaji wa bora wa mechi kati ya Singida United na Kakamega Homeboys
Maelezo ya picha, Mchezaji wa bora wa mechi kati ya Singida United na Kakamega Homeboys

Mpaka dakika 90 za mchezo timu hizo zilikuwa zimetoshana nguvu kwa bao 1-1, hivyo mshindi akaamuliwa kwa mikwaju ya penati.

Jumla ya timu nane,nne za Kenya na nne za Tanzania zilishiriki mashindano haya ya wiki moja.