Kombe la Dunia 2018: Nzige watishia viwanja vya mpira Urusi

Locusts

Chanzo cha picha, Getty Images

Maafisa wa serikali ya Urusi wametahadharisha kwamba huwenda nzige wakashambulia viwanja vya mpira wa miguu nchini humo na kuzua kashfa kubwa wakati wa Kombe la Dunia.

Pyotr Chekmarev amesema takriban hektari milioni moja za ardhi kusini mwa Urusi zimevamiwa na wadudu hao.

Volgograd, mji ambao England watachezea dhidi ya Tunisia mnamo 18 Juni, ni moja ya maeneo ambayo yameathiriwa.

"Tumejifunza kukabiliana na nzige, lakini tutakwepa vipi kutumbukia katika kashfa ya dunia kutokana na nzige mwaka huu?" amesema Chekmarev.

"Ulimwengu wote utafika hapa. Viwanja vya mpira wa miguu vimejaa majani. Nzige hupenda maeneo ambayo kuna majani na rangi ya kijani.

"Utawazuia vipi kufika eneo ambalo mpira unachezewa?" aliongeza Chekmarev, mkuu wa idara ya ukulima katika wizara ya kilimo.

Volgograd Arena

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, England watacheza mechi yao ya ufunguzi katika uwanja wa Volgograd Arena

Kombe la Dunia 2018 litaanza mnamo 14 Juni na mechi zitachezewa viwanja 12 katika miji 11 Urusi.