Thierry Henry alimshauri Alexis Sanchez aondoke Arsenal kwenda Man Utd?

Thierry Henry and Alexis Sanchez

Chanzo cha picha, Getty Images

Mchezaji maarufu wa zamani wa Arsenal Thierry Henry amekanusha kwamba alimwambia Alexis Sanchez aihame klabu hiyo na kujiunga na Manchester United.

Sanchez, aliyejiunga na United Jumatatu kwa makubaliano ya kubadilishana wachezaji ambapo Henrikh Mkhitaryan alihamia Arsenal, amesema alikuwa amezungumza na Mfaransa huyo.

"Nakumbuka leo, mazungumzo niliyokuwa nayo na Henry, ambaye alibadilisha klabu kwa sababu sawa na leo ni zamu yangu," Sanchez aliandika kwenye Instagram.

Henry, aliyehamia Barcelona mwaka 2007, alijibu Jumanne na kusema: "Hakuna wakati hata mmoja ambao nilimwambia Alexis Sanchez aondoke Arsenal."

Akijibu shutuma dhidi yake, Henry, ambaye anashikilia rekodi ya ufungaji mabao Arsenal aliongeza kwenye ujumbe wa Twitter kwamba: "Sikuwa na habari kwamba alikuwa ahajiunga na Man Utd hadi nilipoona kwenye vyombo vya habari sawa nanyi."

Henry, 40, alihamia Nou Camp baada ya kukaa misimu minane Arsenal kwa £16.1m.

Thierry Henry

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Thierry Henry alifungia Arsenal mabao 228

Akiwa Barca alishinda mataji mawili ya La Liga na kombe moja la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Sanchez, 29, kutoka Chile alikuwa amekaribia sana kuhamia Manchester City Agosti mwaka jana lakini alitia saini mkataba wa miaka minne unusu Manchester United ambapo atakuwa analipwa £14m kwa mwaka baada ya kutozwa ushuru.