Mohamed Salah: Mchezaji aliyesaidia kuwafikisha Misri Kombe la Dunia

Mohamed Salah

Mohamed Salah huenda amefunga mabao chungu nzima lakini atakumbukwa nchini Misri kwa kitu kimoja- bao la dakika za lala salama dhidi ya Congo mwezi Oktoba.

Bao hilo liliwawezesha Mafirauni kufuzu kwa mara ya kwanza kwa michuano ya Kombe la Dunia baada ya kipindi cha robo karne.

Misri walifanikiwa kuwa mabingwa wa Afrika mara saba lakini walikuwa hawajawahi kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia tangu 1990, na ikiwa katika dakika za lala salama walishinda penalti huku ikiwa matokeo ni 1-1 hatua iliyozua hisia zisizokuwa za kawaida nje na hata ndani ya uwanja.

Na mchezaji huyo ambaye alikuwa ametulia na kutobabaishwa alifunga bao hilo lililowafurahisha mashabiki wengi wa nyumbani na kumlazimu Rais Abdul Fattah Al Sisi kumpongeza kwa kuweza kuhimili shinikizo za raia milioni 80 wa Misri.

Bao hilo lilimpatia umaarufu wa kuwa mfalme wa Mafirauni 2017, huku timu hiyo ikipewa jina la utani ''Misri ya Salah'' kutokana mchezo wa kasi wa mshambuliaji huyo ambaye aliiwezesha Misri kuwika.

Kwa mfano Salah alifunga mabao matano kati ya mabao saba yaliyofungwa wakati timu hiyo ikitafuta kufuzu kwa Kombe la Dunia la Urusi.

Alipata umaarufu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2017 wakati alipopewa fursa katika timu ya michuano hiyo baada ya kufunga mabao manne kati ya matano yaliyofungwa na Misri, akifunga mara mbili huku timu hiyo ya Afrika Kaskazini ikitinga fainali kabla ya kupoteza kwa Cameroon.

Mchezo mzuri wa 'mchawi' huyo wa Misri haukusita katika mechi za kitaifa pekee kwani katika safu ya kimataifa amewika akiichezea Roma na Liverpool kwa kufunga mabao.

Maelezo ya video, AFOTY 2017: Safari ya Salah kufikia ufanisi

Baada ya kujiunga na Liverpool mnamo mwezi Juni, umahiri wa mshambuliaji huyo ulionekana mapema baada ya kutangazwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Agosti na Septemba.

Bao lake katika mechi yake ya kwanza, lilitangulia tu. Alifunga mengine saba katika mechi 11 za ligi ya Uingereza huku akifunga mabao matano katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika mechi sita alizoshiriki.

Mchezo wake mzuri katika ligi kuu ya England ni msururu wa muendelezo wa mchezo wake nchini Italia ambapo Salah alikuwa kiungo muhimu katika kikosi bora cha Roma katika kipindi cha miaka saba.

Alifunga mabao 15 na kutoa usaidizi wa mabao 11 katika ligi iliyo na umaarufu wa kuweka ulinzi mkali huku Roma au Giallorossi ikimaliza ya pili nyuma ya mabingwa Juventus kwa pointi nne pekee.

Akipewa jina la utani 'Special' na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thierry Henry, Je Salah anaweza kutumia uteuzi wake wa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa Afrika ya BBC kuwa mshindi wa kwanza wa Misri tangu Mohammed Aboutrika 2008?