Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Marekani washindwa kufuzu Kombe la Dunia Urusi
Marekani hawatashiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka ujao nchini Urusi baada ya kulazwa 2-1 na Trinidad & Tobago mechi ya kufuzu kwa michuano hiyo Jumanne.
Panama waliingiza mchanga kitumbua cha Marekani kwa kuandikisha ushindi dhidi ya Costa Rica.
Vijana hao wa Bruce Arena walianza mechi wakiwa katika nafasi ya tatu ya kufuzu kwa Kombe la Dunia lakini bao la ushindi la Roman Torres dakika ya 88 liliwafikisha Panama kwa michuano hiyo kwa mara ya kwanza.
Marekani hawakupata hata nafasi ya kucheza michuano ya muondoano ya kufuzu dhidi ya Australia, kwani nafasi hiyo iliwaendea Honduras waliowalaza Mexico.
Mara ya mwisho kwa Marekani kukosa kushiriki fainali za Kombe la Dunia ilikuwa mwaka 1986.
Marekani walilaza Panama 4-0 Ijumaa iliyopita lakini licha ya kucheza dhidi ya Trinidad & Tobago waliokuwa na alama tatu pekee kutoka kwa mechi tisa walizocheza awali za kufuzu, walicheza vibaya sana na hakukuwa na matumaini yao ya kushinda.
Matokeo kamili mechi za Jumanne:
- Trinidad & Tobago 2-1 USA
- Honduras 3-2 Mexico
- Panama2-1 Costa Rica