Jose Mourinho: Manchester United hawako tayari kutawala EPL

Chanzo cha picha, Reuters
Manchester United "hawako tayari kuwa timu babe" kwa sasa na mashabiki wanafaa kusahau ubabe uliokuwa na timu hiyo enzi za Sir Alex Ferguson, meneja wa sasa Jose Mourinho ameambia BBC Sport.
United walishinda mataji 13 ya Ligi Kuu ya Uingereza chini ya Ferguson, lakini Mourinho amesema kwa sasa ni vigumu kuwa na ubabe wa aina hiyo.
Alipoulizwa iwapo anaweza kurejeshea klabu hiyo ukuu wake kama awali, Mreno huyo alijibu: "Msahau hilo".
"Msijaribu kurudi nyuma miaka 10, 20 iliyopita kwa sababu hilo haliwezekani tena.
Kwenye mahojiano ya kina na Gary Lineker, Mourinho pia alisema:
- United hawahitaji kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ndipo wawavutie wachezaji wa haiba ya juu
- Hangewauwa wachezaji Angel di Maria, Javier Hernandez na Danny Welbeck iwapo angelikuwa meneja wa United walipokuwa wanauzwa
- Haijakuwa rahisi kwa kiungo wa kati Paul Pogba kuzoea tena soka ya Uingereza
Mourinho, 54, alitia saini mkataba wa miaka mitatu Mei mwaka jana kuchukua nafasi ya Louis van Gaal, aliyefutwa kazi licha ya kushinda Kombe la FA.
Mashetani hao Wekundu wamemaliza nambari saba, nne na tano misimu mitatu iliyofuata baada ya Ferguson kustaafu.
Msimu huu wamekwama nambari sita tangu tarehe 6 Novemba.
Mourinho haamini wanakaribia kushinda Ligi ya Premia karibu kila mwaka, lakini hataki klabu hiyo ilegee baada ya kushinda Kombe la EFL msimu uliopita.
"Hatuko tayari kuwa Manchester United," alisema.

Chanzo cha picha, PA
"Hatuko tayari kuwa klabu babe. Hatuko nayati kujaribu kushinda kila kitu.
"Kwa sababu ya sifa za klabu zenyewe, na mimi binafsi, tuko tayari kupigania kila mechi, kila alama. Lakini kuna pengo kubwa kati ya ndoto za jumla za klabu kubwa kama hii na uhalisia."

Chanzo cha picha, PA















