Uganda yathibitisha wagonjwa sita wapya wa Ebola
Maafisa wanasema wagonjwa waliothibitishwa kuwa na virusi vya ebola wanatokea wilaya ya kati ya Mubende.
Moja kwa moja
Iran: Baba yake Mahsa Amini ashutumu mamlaka kwa kuficha ukweli

Chanzo cha picha, FAMILIA YA MAHSA AMINI
Baba yake na Mahsa Amini, mwanamke mwenye umri wa miaka 22 ambaye kifo chake kimesababisha wimbi la maandamano kote Iran, ameshutumu mamlaka kwa kusema uwongo.
Katika mahojiano na BBC, Amjad Amini alisema hakuruhusiwa kuona ripoti ya uchunguzi wa mwili wa bintiye na amekanusha kuwa alikuwa na afya mbaya.
Alisema mashahidi waliiambia familia kuwa alipigwa chini ya ulinzi wa polisi. Mamlaka za Iran zimekanusha hili.
Mahsa Amini aliwekwa kizuizini kwa madai ya kuvunja sheria za kuvaa hijabu.
Mwanamke huyo wa Kikurdi kutoka mji wa kaskazini-magharibi wa Saqez, alifariki hospitalini huko Tehran siku ya Ijumaa, baada ya kukaa siku tatu bila fahamu.
"Niliwaomba wanionyeshe kamera za mwilini za maafisa wa usalama, waliniambia kamera zimeishiwa na betri.
Maafisa wa Iran wamesema kuwa Bi Amini alikuwa amevaa nguo zisizo na heshima wakati wa kukamatwa kwake.
Ingawa baba yake anasema kwamba muda wote alikuwa akivaa koti refu.
Pia alisema alizuiliwa mara kwa mara na wahudumu wa afya kuona mwili wa binti yake baada ya kifo chake. "Nilitaka kumuona binti yangu, lakini hawakuniruhusu," alisema
Alisema alipoomba kuona ripoti ya uchunguzi wa maiti aliambiwa na daktari: "Nitaandika chochote ninachotaka na hakina uhusiano wowote na wewe."
Mamlaka ya Iran inasema kuwa Bi Amini hakutendewa vibaya lakini alipatwa "ghafla na tatizo la moyo" baada ya kuwekwa kizuizini mjini Tehran na polisi wa maadili wa nchi hiyo.
Rais wa Zambia aapa kuondoa sheria inayopinga kumtukana rais

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Zambia Hakainde Hichilema ameiambia BBC kuwa atashinikiza kutupiliwa mbali kwa sheria tata inayoharamisha kumtusi rais.
Hii Inafuatia kilio cha mashirika ya kutetea haki za binadamu ambayo yanasema takriban watu kumi na wawili, wakiwemo wanaharakati wa upinzani, wamekamatwa na kushtakiwa kwa kuvunja sheria wakati wa mwaka wa kwanza wa Rais Hichilema madarakani.
Bw Hichilema aliahidi kufanya mabadiliko dhidi ya uongozi uliopita alipoingia madarakani mwaka jana. Mafanikio yake yalijumuisha kupungua kwa mfumuko wa bei kwa nusu, kupokea dhamana kutoka IMF ya dola bilioni na kuanzisha ushuru wa chini na elimu bila malipo.
Lakini wakosoaji wanasema licha ya ahadi za uchaguzi, serikali imekuwa ikichelewa kukomesha sheria ya matusi ya wakati wa ukoloni ambayo mara nyingi ilitumika kuwanyamazisha wakosoaji.
Hichilema aliambia BBC kwamba sheria hiyo itafutwa, lakini hadi wakati huo, itaendelea kutumika. "Kuna sheria hapo.
Jambo la kwanza kati ya mambo muhimu tuliyosema tutafanya, ni kurejesha utawala wa sheria.
"Sheria hiyo ni moja ya zile ambazo tumezitenga ambazo zinapaswa kufanyiwa marekebisho na inapitia taratibu zinazostahili. Kabla ya kufanyiwa marekebisho ni sheria na itatumika," alisema.
Mataifa ya Afrika Mashariki kwenye hali ya tahadhari kufuatia mlipuko wa Ebola Uganda

Chanzo cha picha, AFP
Nchi za Afrika Mashariki zimetoa tahadhari baada ya kutangazwa kwa mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola nchini Uganda.
Nchi jirani ya Tanzania imesema tayari imeweka timu za ufuatiliaji kwenye vituo muhimu vya kuingilia ikiwemo viwanja vya ndege na vituo vya mpakani. Katibu Mkuu wa Afya Abel Makubi aliambia BBC kwamba timu hizo zilikuwa zikiwachunguza watu wote wanaokuja nchini.
Wizara ya afya ya Kenya ilisema imezitaka mamlaka za kaunti, haswa katika maeneo ya mpakani, kuwa macho na kuimarisha ufuatiliaji.
Ilisema timu za kushughulikia zimewekwa ili kukagua watu ambao wanaweza kuwa hatarini, pamoja na wasafiri na wafanyikazi wa afya. Pia iliwataka wananchi kuwa waangalifu.

Mchungaji akiri kuhusika katika mauaji ya muuguzi mwanafunzi wa Ghana
Mchungaji mmoja amekamatwa baada ya kuwaambia polisi kwamba alimsaidia chifu wa eneo kumteka nyara, kumuua na kumzika muuguzi mwanafunzi katikati mwa Ghana.
Georgina Asor Botchwey, 22, alipotea zaidi ya wiki moja iliyopita na arifa zilishirikishwa kote kwa matumaini ya kumpata:
Ruka X ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Mwili wake ulitolewa baadaye na polisi katika nyumba ya chifu wa eneo hilo Nana Clarke huko Mankessim, ambapo waliongozwa na mchungaji.
Begi la mwathiriwa, viatu, na mali nyingine pia zilipatikana, kulingana na tovuti ya Joy Online.
Bw Clarke hajulikani alipo huku polisi wakisema wameanzisha msako wa kumtafuta.
Uganda yathibitisha wagonjwa wapya sita vya Ebola

Chanzo cha picha, AFP
Wizara ya afya ya Uganda imethibitisha wagonjwa wapya sita wa Ebola baada ya maafisa kuthibitisha mlipuko wa ugonjwa huo nchini humo mapema wiki.
Visa hivyo vipya vya maambukizi viliripotiwa katika wilaya ya kati ya Mubende ambapo mwanamume mwenye umri wa miaka 24 alithibitishwa kufariki Jumanne baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa huo.
Msichana wa mwaka mmoja pia anashukiwa kufariki kutokana na ugonjwa huo siku ya Jumanne.
Kati ya wagonjwa hao sita, mmoja aliripotiwa kutoka wilaya jirani.
Huu ni mlipuko wa tatu wa ugonjwa wa ebola nchini Uganda.
Zaidi ya watu 40 ambao walitangamana na familia iliyopatikana na maambukizi ya viru wamefuatiliwa.
Kumi na moja kati yao wametengwa, alisema Kyobe Henry Bbosa,kamanda wa usimamizi wa matukio kutoka wizara ya afya.
Nchi jirani zilisema ziko katika hali ya tahadhari iwapo ugonjwa huo utasambaa katika mipaka.
Wataalamu wanasema kuwa wana ebola ya Sudan kihistoria ina viwango vya chini vya maambukizi na vifo ikilinganishwa na aina ya Ebola ya Congo.
Mamlaka ya Uganda inaendelea kuhakikishia umma na jumuiya ya kimataifa kwamba wana uwezo wa kudhibiti janga hili.
Wanaume wa Urusi wanakimbia kuvuka mpaka hadi Georgia

Chanzo cha picha, b
Katika kituo cha ukaguzi cha Upper Lars kwenye mpaka wa Georgia na Urusi, magari mengi yenye nambari za leseni ya Kirusi yanavuka kwenye bonde la mlima linalopeperushwa na upepo.
Watu wawili ambao walivuka hivi majuzi waliambia BBC kwamba foleni ya takriban kilomita 5 (maili 3.1) ilishuhudiwa upande wa Urusi.
Katika gari moja dogo kutoka jiji la Urusi la Stavropol, abiria waliokuwa wamelala, wengi wao wakiwa vijana, walipumzika baada ya kungoja kwa saa saba.
Walitaka kutafuta intaneti ili kuwafahamisha jamaa wa nyumbani kwao kwamba walikuwa wamefika salama.
Mtu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema ameamua kuondoka mara baada ya Vladimir Putin kutangaza mpango wa kusajili wanajeshi wa ziada kuongeza juhudi zake katika vita vya Ukraine jana asubuhi.
Mtu huyo anayekimbia alisema hakuwa na wakati wa kukusanya vitu vyake.
Alichukua tu pasi yake ya kusafiria na kuondoka kwa sababu alikuwa amefikisha vigezo vya kuingia kwenye kundi la wale wanaosajiliwa.
Georgia ni mojawapo ya nchi chache zilizobaki ambazo Warusi wanaweza kuingia bila visa.
Takriban raia 140,000 wa Urusi wameingia Georgia tangu kuanza kwa vita, na wito unaongezeka kutoka kwa wanasiasa wa upinzani wa Georgia kwa serikali kuanzisha utaratibu wa visa kudhibiti wimbi la raia wa Urusi wanaoingia.
Kremlin inapuuzilia mbali ripoti za wanaume wa Urusi waliokimbia baada ya wito wa uhamasishaji
Hata hivyo, awali msemaji wa urusi alisema kuwa ripoti za wanaume kutoroka nchi wale ambao wanaweza kusajiliwa kama wanajeshi wa akiba chini ya mipango mipya iliyotangazwa na rais ‘’ inaongezwa chumvi’’.
Ripoti hizo ziliwadia baada ya hotuba ya Rais Putin hapo jana, ambapo alisema usajili wa wanajeshi wa akiba ni sehemu muhimu katika kuhakikisha uadilifu kwenye eneo la Urusi - huku wanajeshi 300,000 wa akiba wakikabiliwa na kupelekwa kupigana Ukraine.
Soma zaidi:
Katika picha: Wafungwa walioachiliwa jana usiku
Katika hali isiyotarajiwa, Ukraine na Urusi jana usiku zilibadilishana wafungwa wa vita waliokuwa wakiwazuilia, pamoja na baadhi ya wafanyakazi wasiokuwa wanajeshi.
Raia watano wa Uingereza, Mmorocco mmoja, Msweden mmoja, Mcroatia mmoja, na Wamarekani wawili walisafirishwa hadi Saudi Arabia - baada ya nchi hiyo kusaidia kubadilishana uhuru wao - kabla ya kurejea katika makazi yao.
Huko Ukraine, zaidi ya wanajeshi 200 walibadilishwa kwa wanajeshi 55 wa Urusi na mbunge wa zamani wa Ukraine Viktor Medvedchuk.
Hizi ni baadhi ya picha:

Chanzo cha picha, Saudi Press Agency
Maelezo ya picha, Wafungwa kumi wa vita waliwasili Riyadh jana usiku baada ya Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman kusaidia wakala wa makubaliano ya kuwaachilia huru. 
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Wafungwa wa vita waliobadilishana - akiwemo raia wa Uingereza Shaun Pinner aliyevaa fulana ya rangi ya chungwa - wamekaa baada ya kuteremka kutoka kwa ndege yao kuelekea Saudi Arabia, kabla ya kurejea katika nchi zao. 
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Zaidi ya wanajeshi 200 wa Ukraine walibadilishana na wanajeshi 55 wa Urusi, na mwanasiasa Viktor Medvedchuk, jana usiku. 
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kateryna Polishchuk, ambaye alitekwa na vikosi vya Urusi wakati akitetea kiwanda cha utengenezaji vyuma cha Azovstal huko Mariupol, alivyoonekana kwa simu kufuatia mazungumzo hayo. 
Chanzo cha picha, Reuters
Maelezo ya picha, Kateryna Polishchuk, ambaye alitekwa na vikosi vya Urusi wakati akitetea kiwanda cha utengenezaji vyuma cha Azovstal huko Mariupol, alivyoonekana kwa simu kufuatia mazungumzo hayo. Soma zaidi:
Polisi nchini Urusi wakamata raia wanaopinga wito wa Putin wa kuongeza wanajeshi wa akiba

Chanzo cha picha, Reuters
Polisi wa Urusi wameripotiwa kuwakamata mamia ya waandamanaji waliokuwa wakiandamana kupinga uamuzi wa Urusi wa kuongeza maelfu ya wanajeshi wa ziada kupigana nchini Ukraine.
Kikundi cha haki za binadamu cha Urusi OVD-Info kiliweka jumla ya idadi ya waliokamatwa kuwa zaidi ya 1,300.
Idadi kubwa zaidi ya waliokamatwa walikuwa raia wa St Petersburg na Moscow.
Nchini Urusi, mikutano isiyoidhinishwa ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kupinga maandamano.
Jana, ofisi ya mwendesha mashitaka ya Moscow ilionya kwamba wito kwenye mtandao wa kujiunga na maandamano yasiyoidhinishwa ya mitaani, au kushiriki katika maandamano hayo, inaweza kusababisha hadi miaka 15 jela.
Soma zaidi:
Ukraine na Urusi zabadilishana wafungwa hatua ambayo haikutarajiwa

Chanzo cha picha, Reuters/State Security Service of Ukraine
Maelezo ya picha, Mkuu wa Idara ya Usalama wa Jimbo la Ukraine Vasyl Maliuk akimkumbatia mfungwa wa vita baada ya mabadilishano yaliyofanyika katika mkoa wa Chernihiv nchini Ukraine. Huku kukiwa na mvutano unaoongezeka, Ukraine na Urusi zimefanya mabadilishano ya wafungwa ambayo hayakutarajiwa, ikiwa ndio mpango mkubwa zaidi tangu vita kuanza.
Urusi iliwaachilia huru wafungwa 215 wa vita, wakiwemo makamanda wa Kikosi cha Azov.
Kwa muda wa wiki kadhaa, waliongoza upinzani katika jiji la Mariupol, wakiwa wamejichimbia kwenye nguzo na vichuguu vya ujenzi wa chuma wa Azovstal, na wanaonekana kama mashujaa nchini Ukraine.
Wageni kumi waliotekwa nchini Ukraine pia waliachiliwa.
Kwa upande wake, Ukraine iliwarudisha wapiganaji 55 wa Urusi na mwanasiasa anayeunga mkono Urusi Viktor Medvedchuk, ambaye alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Andriy Yermak, mkuu wa ofisi ya Rais Zelensky, alisherehekea ‘’mafanikio makubwa’’ ya mazungumzo baada ya ‘’kazi kubwa’’, ambayo ilifanyika kwa msaada wa Uturuki na Saudi Arabia.
Muda ambao mabadilishano hayo yamefanyika ni wa kuvutia.
Ilitokea saa chache baada ya rais wa Urusi, Vladimir Putin, kutoa hotuba kwenye televisheni akitangaza kuongeza wanajeshi wa akiba kwa ajili ya vita na kile kinachoitwa kufanya ‘kura ya maoni juu ya kujiunga na Urusi’ ikipangwa na vikosi vinavyoungwa mkono na Urusi katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Ukraine.
Matukio hayo yanaonekana kama Urusi kuongeza kasi katika vita inapokabiliwa na hasara vitani huku kukiwa na mashambulizi ya vikosi vya Ukraine kurudisha eneo lake.
Mabadilishano hayo yamezua swali: kwa nini sasa?
Soma zaidi:
Floyd Mayweather kupigana tena na Conor McGregor 2023

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Floyd Mayweather alimshinda Conor McGregor kwa urahisi katika pambano lake la mwisho kama mtaalamu. Floyd Mayweather anasema anataka kupigana na nyota wa UFC Conor McGregor katika pambano la maonyesho mwaka ujao.
Mayweather, 45, alimsimamisha McGregor katika raundi ya 10 ya pambano la mwisho la taaluma yake mwaka 2017.
Akiwa ameshiriki katika maonyesho kadhaa tangu astaafu, Mayweather anasema yuko kwenye mazungumzo ya kupigana tena na McGregor.
‘’Hatujui ikiwa itakuwa maonyesho au vita vya kweli,’’ aliambia Daily Mail.
‘’Ningependelea maonyesho.’’
McGregor baadaye aliweka picha kwenye Instagram kutoka kwenye pambano lao la awali na kuandika ‘’#notinterested’’.
Mayweather alipendekeza Uwanja wa Allegiant, nyumbani kwa Washambuliaji wa NFL wa Las Vegas, kama mahali panapowezekana kwa mechi yake ya marudiano na McGregor.
‘’Tayari walizungumza nami kuhusu nitakachopokea,’’ Floyd aliiambia TMZ na kuongeza, ‘’nambari zitakuwa 9.’’
‘’Unajua tunapaswa kuanza angalau kwa milioni 100 kwa Floyd Mayweather.’’
Ruka Instagram ujumbeRuhusu maudhui? (Mitandao ya kijamii)Onyo: BBC haihusiki na maudhui ya njeMkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa Instagram ujumbe
Mayweather anachuana katika mpambano mwingine wa maonyesho wikendi hii nchini Japan atakapochuana na nyota wa MMA Mikuru Asakura.
Mmarekani huyo, ambaye alistaafu ndondi bila kushindwa kwa rekodi ya 50-0, ametokea katika mapambano kadhaa ya maonyesho, ikiwa ni pamoja na dhidi ya nyota wa YouTube, Logan Paul mwaka jana.
McGregor alirejea UFC baada ya kupoteza dhidi ya Mayweather, lakini amejitahidi kugundua upya kilichompelekea kuwa bingwa wa kwanza wa UFC mara mbili.
Raia huyo wa Ireland, 34, amepoteza mapambano matatu kati ya manne ya mwisho ya UFC na kwa sasa anaendelea kupata nafuu kutokana na kuvunjika mguu katika mchezo wake dhidi ya Dustin Poirier mwaka mmoja uliopita.
Soma zaidi:
Korea Kaskazini yakanusha kusambaza silaha kwa Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Maelezo ya picha, Vladimir Putin wa Urusi na Kim Jong-un wa Korea Kaskazini walikutana mara ya mwisho mwaka 2019 Korea Kaskazini yasema haijawahi kuiuzia Urusi silaha na haina mpango wa kufanya hivyo katika siku zijazo, kufuatia ripoti za Marekani kwamba Moscow ilikuwa ikigeukia Pyongyang ili kujaza akiba yao ya silaha.
Maafisa wa Marekani walisema hapo awali kwamba Urusi inaweza kununua roketi na makombora ya mizinga kutoka Korea Kaskazini.
Walisema hatua hizo, pamoja na madai ya ununuzi wa silaha za Iran, zinaonyesha vikwazo vya Magharibi vinazuia juhudi za Urusi katika vita vya Ukraine.
Hata hivyo, Moscow ilikanusha ripoti hizo wakati huo.
Harakati zozote za silaha kati ya nchi hizo mbili zitakuwa zinakiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Siku ya Alhamisi, katika taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari vya serikali ya Korea Kaskazini KCNA, afisa ambaye hakutajwa jina katika wizara ya ulinzi ya Korea Kaskazini alisema: ‘’Hatujawahi kusafirisha silaha au risasi kwa Urusi hapo awali na hatutapanga kuziuza.’’
Ilishutumu Marekani, na ‘’vikosi vingine vya uhasama’’, kwa kueneza uvumi ‘’kutekeleza malengo yake ya kisiasa na kijeshi’’.
Mapema Septemba, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema ununuzi wa Urusi wa Korea Kaskazini ‘’unaweza kujumuisha mamilioni ya roketi na makombora ya mizinga.’’
Lakini msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa John Kirby baadaye alionekana kupuuza kauli hiyo, kwa kusema ununuzi ulikuwa bado haujakamilika na hakuna ushahidi wa kupendekeza silaha hizo zingetumika katika vita vya Ukraine.
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari umethibitisha gharama kubwa kwa jeshi lake, licha ya kutumia silaha za hali ya juu kama vile makombora.
Vikosi vya Ukraine, vinavyotumia silaha za nchi za Magharibi ambazo vimeingizwa nchini humo katika miezi ya hivi karibuni, vimesababisha hasara kubwa.
Silaha nyingi za Korea Kaskazini zilizoundwa na Urusi zilitoka enzi ya Usovieti, lakini ina makombora yanayofanana na yale ya Urusi.
Mnamo Julai, Korea Kaskazini ilikuwa moja ya nchi chache ambazo zilitambua rasmi maeneo mawili ya kujitenga yanayoungwa mkono na Urusi mashariki mwa Ukraine.
Katika kulipiza kisasi, Ukraine ilikata uhusiano wote wa kidiplomasia na Pyongyang.
Mapema mwezi huu, rais wa Urusi Vladimir Putin aliapa kupanua ‘’uhusiano wao wenye tija’’ katika barua kwa mwenzake Kim Jong-un.
Soma zaidi:
Macron awakutanisha Kagame na Tshisekedi kujadili ukosefu wa usalama

Chanzo cha picha, sERIKALI YA RWANDA
Maelezo ya picha, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron awakutanisha Kagame na Tshisekedi Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amewakutanisha marais Félix Tshisekedi wa DR Congo na Paul Kagame wa Rwanda kujadili ukosefu wa usalama mashariki mwa DR Congo pembezoni mwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York.
Siku ya Jumanne, Bw Tshisekedi aliikashifu vikali Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 mbele ya mkutano wa Umoja wa Mataifa.
Siku ya Jumatano, Bw Kagame aliambia bunge kwamba ‘’mchezo wa kurushiana lawama hausuluhishi matatizo’’, saa chache kabla ya wote wawili kukutana chini ya mpango wa Bw Macron.
Kwa mkutano huo, Bw Kagame aliunga mkono mchakato wa kikanda kama suluhu la mzozo huo lakini akasema ‘’utahitaji usaidizi thabiti wa kifedha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa’’.
Mamlaka za kikanda zimekubali kuunda kikosi cha kikanda ili kupambana na makundi ya waasi mashariki mwa DR Congo, bado haijafahamika ni lini kikosi hicho kitaanza hatua.
Kundi la waasi la M23 linadhibiti sehemu za Jimbo la Kaskazini mwa Congo tangu Juni.
Rwanda imekuwa ikikanusha kuunga mkono kundi hilo.
Soma zaidi:
Kifo kingine chahusishwa na Ebola Uganda

Chanzo cha picha, EPA
Wizara ya afya ya Uganda inasema mtoto wa mwaka mmoja anashukiwa kufariki kutokana na Ebola katika wilaya ya kati ya Mubende siku ya Jumanne.
Alikuwa miongoni mwa watu kumi na moja waliowekwa karantini kufuatia kisa kilichothibitishwa cha mwanamume mwenye umri wa miaka 24, aliyefariki Jumatatu.
Lakini kifo cha msichana mdogo bado hakijathibitishwa kuwa kilitokana na Ebola, kwa sababu maafisa bado wanasubiri matokeo kutoka kwa sampuli zilizochukuliwa kutoka kwa watu waliowekwa karantini.
Siku ya Jumanne, maafisa wa Uganda walithibitisha kuzuka kwa homa ya virusi ya Ebola katika kijiji cha wilaya ya Mubende, zaidi ya kilomita 150 kutoka mji mkuu Kampala.
Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kuwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha takriban muongo mmoja kwa kesi ya Ebola kuthibitishwa nchini humo.
Hii ni mara ya tano Uganda kupata mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, mara ya kwanza ulikuwa mbaya zaidi mwaka 2000 na kuua watu 224, na mlipuko wa mwisho nchini ilikuwa mwaka 2018. Milipuko mingine ilitokea 2014 na 2017.
Soma zaidi:
Tanzania na Msumbiji zatia saini mikataba ya ulinzi na usalama

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
Msumbiji na Tanzania zimesaini mikataba miwili ya ushirikiano mjini Maputo inayolenga kupambana na ugaidi na uhalifu.
Msumbiji kwa sasa inapambana na wanamgambo wa Kiislamu katika eneo lenye utajiri wa gesi kaskazini mwa Cabo Delgado nchini humo.
Mikataba hiyo ilisainiwa ikiwa ni sehemu ya ziara rasmi ya siku tatu ambayo Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anafanya nchini Msumbiji.
''Katika kuhakikisha tunapambana na magaidi, kupitia mahusiano haya leo tumeweza kutia saini katika eneo la usalama na ulinzi, na hii ni hatua muhimu sana katika kusonga mbele'' amesema rais Samia.
Mbali na kupambana na wanajihadi, Rais Filipe Nyusi alisema nchi hizo mbili kwa sasa zimejikita katika unyonyaji wa hidrokaboni ambayo ni nyenzo za ujenzi wa vyanzo muhimu vya nishati kama makaa ya mawe na gesi.
Rais Samia pia alisisitiza haja ya nchi zote mbili kuimarisha usalama kwa sababu ya mpaka wa pamoja wanaoshiriki.
Volodymyr Zelensky : Urusi lazima ikabiliane na "adhabu ya haki"

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais Volodymyr Zelensky ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York kuwa Urusi lazima ipewe adhabu kwa uvamizi wake Ukraine.
Katika video iliyorekodiwa awali, kiongozi huyo wa Ukraine alitoa wito wa kuundwa kwa mahakama maalum ya vita na kueleza kwa kina kuhusu uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa na Urusi.
Pia aliweka "mkakati" wa amani, ikijumuisha usaidizi zaidi wa kijeshi na kuiadhibu Urusi kwenye jukwaa la dunia.
Hotuba yake ilipata shangwe kutoka kwa wahudhuriaji wengi wa kikao hicho.
Katika hotuba yake ya utangulizi, Bw Zelensky aliishutumu Urusi kwa kusababisha "msukosuko mkubwa" na "vita vyake haramu".
Alizungumza siku yajana Rais wa Urusi Vladimir Putin aliwaita wanajeshi 300,000 wa akiba, hatua ambayo ilisababisha maandamano katika baadhi ya mitaa ya Urusi.
Bw Zelensky alisema hatua hiyo ilionyesha adui yake hakuwa makini kuhusu mazungumzo ya amani.
Alilaani mipango iliyotangazwa hivi majuzi katika maeneo yanayokaliwa na Urusi ya nchi yake kufanya kile kinachoitwa kura ya maoni juu ya kujiunga na Urusi - mpango uliolaaniwa na viongozi wa Magharibi katika Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne.
Soma zaidi:
