Tshisekedi amesema 'hakuna tashwishi' kwamba Rwanda inasaidia M23

Rais Felix Tshisekedi wa DR Congo siku ya Jumapili alitangaza kwamba hakuna tashwishi kwamba serikali ya Rwanda inawaunga mkono wapiganaji wa M23 , lakini akasisitiza kwamba walitaka kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda.
Hii ni mara ya kwanza tangu kuzuka kwa mgogoro kati ya mataifa hayo mawili kwamba ameishtumu waziwazi Rwanda kwa kulisaidia kundi hilo.
Mamlaka ya Rwanda imekana madai hayo ikisema kwamba suala la M23 ni tatizo la DR Congo yenyewe.
Akizungumza wakati wa ziara yake nchini Congo Brazzaville ambapo alikutana na mwenjeji wake rais Denis Sassou Nguesso, katika hotuba iliopeperushwa na runinga, bwana Tshisekedi alisema:
''Kila ninapohisi kwamba tunahitaji kujenga madaraja badala ya mipaka, lakini tumerudi palepale''
''Natumai Rwanda imejifunza, kwasababu ni wazi kwamba imelisaidia kundi la M23 kushambulia DRC''

Chanzo cha picha, FLICKR.COM/PAULKAGAME
Kesi ya DR Congo dhidi ya Rwanda imesababisha kusimamishwa kwa usafiri wa kampuni ya ndege ya RwandAir kuelekea DR Congo huku biashara ya mipakani ikiathiriwa katika siku za hivi karibuni.
Mapigano kati ya wapiganaji wa M23 na vikosi vya serikali yalifikia kikomo baada ya waasi hao kutangaza wiki iliopita kwamba wameondoka katika eneo walilokuwa wakikalia.
Kuchipuka kwa kundi la M23 linalotekeleza mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni kumesababisha hali ya wasiwasi kati ya mataifa hayo mawili.

Kundi la wapiganaji wa M23 liliuteka mji wa Goma 2012 kabla ya kujiondoa katika muungano, na baada ya kupoteza katika vita vya 2013, wanachama wake walitorokea Rwanda na Uganda.
Kufikia 2021, kundi la wapiganaji wa M23 linaloongozwa na Sultani Makenga lilikuwa limerudi na kukita kambi katika milima ya Rushturu na wakaanza kupigana na vikosi vya serikali - huku kila kundi likililaumu jingine kwa uchokozi
Wikendi iliopita , msemaji wa waasi hao alitoa taarifa akisema kwamba vikosi vya serikali vilikuwa vinajiaanda kwa mashabulizi mapya.
Rais wa Angola Joao Lourenco , wakati huohuo amezindua jitihada kuwakutanisha rais Tshisekedi na Paul Kagame ili kutafuta suluhu ya mzozo huo.
Katika matamshi yake, Tshisekedi alimshukuru rais Lourenco , Macky Sall, rais wa muungano wa bara Afrika na rais Deniss Sassou Nguesso kwa juhudi zao za kuzipatanisha serikali za DR Congo na Rwanda kulingana na ofisi ya rais wa DRC.

Chanzo cha picha, kulu ya Congo Brazaville
Rwanda imeishutumu DR Congo kwa kuwaficha waasi wa FDLR dhidi ya Kigali mbali na kushirikiana na vikosi vya wapiganaji wa maeneo kadhaa nchini humo.
Baada ya Tshisekedi kuchukua mamlaka DR Congo, kulikuwa na wakati wa uhusiano mzuri na Rwanda na wapiganaji wa mataifa hayo mawili waliungana kukabiliana na FDLR, na kuwauwa baadhi ya viongozi wake.
M23 ni nani? Wanataka nini?

Chanzo cha picha, AFP
Ukizungumzia M23, inawakumbusha wengi kuwahusu watu kama Sultani Makenga na wengine kama Bosco Ntaganda, huku wengine wakirudi nyuma na kumkumbuka Laurent Nkunda.
Tangu mwaka 2004, Jenerali Nkunda amejiondoa katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na wanajeshi wake katika vilima vya Rutshuru na kuunda CNDP, ambayo imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali na mji wa Goma.
Sababu za vita vyake ni kulinda watu wa kabila lake na aliendeleza mapambano dhidi ya makundi mengine ya waasi ambayo pia yanatokana mapigano ya kikabila na ni miongoni mwa sababu zilizotolewa na Nkunda na wapiganaji wake wakiwemo Makenga na Ntaganda.
Wote watatu walikuwa wanachama wa waasi wa zamani wa APR waliochukua mamlaka nchini Rwanda mwaka 1994, kabla ya kuendeleza vita vyao nchini DR Congo mwishoni mwa miaka ya 1990.
Nkunda alikamatwa nchini Rwanda mapema mwaka 2009 na kufungwa, huku CNDP ikiongozwa na Ntaganda ikijadiliana na serikali ya Kabila katika makubaliano ya Machi 23, 2009.
Miaka minne baada ya kusitishwa kwa mapigano, kundi la watu wanaojiita wapiganaji wa M23 lilizaliwa mwaka 2012, likiongozwa na Ntaganda na Makenga, ambao wanasema makubaliano ya serikali na CNDP Machi 23 hayajafuatwa.
Serikali za Rwanda na Uganda zimeshutumiwa na wataalam wa UN kwa kuwa nyuma ya makundi ya waasi, lakini wameendelea kukanusha.












