Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Vitendo vya Urusi nchini Ukraine ni vya kuchukiza, asema Biden

Rais wa Marekani Joe Biden asema kuwa "katika mwaka jana dunia yetu imepata msukosuko mkubwa" na "vita vya kikatili visivyo na maana vilivyoamuliwa na mtu mmoja".

Moja kwa moja

  1. Tunakomea hapo kwa leo. Kwaheri.

  2. Habari za hivi punde, Vitendo vya Urusi nchini Ukraine ni vya kuchukiza, asema Biden

    Rais wa Marekani Joe Biden anasema kuwa "katika mwaka uliopita ulimwengu wetu umepata msukosuko mkubwa" na "vita vya kikatili visivyo na maana vilivyochaguliwa na mtu mmoja".

    Akizungumzia suala la vita vya Ukraine katika Baraza la Umoja wa Mataifa Biden amesema mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Urusi, alivamia jirani yake na "kukiuka bila aibu" kanuni za msingi za katiba ya Umoja wa Mataifa.

    Biden aidha amesema Vladimir Putin amejaribu "kufuta nchi huru kwenye ramani" na kuuita mpango wa Urusi wa kuandaa kura za maoni "za uwongo" katika sehemu za Ukraine kwa sasa unadhibiti "ukiukaji mkubwa wa katiba ya Umoja wa Mataifa".

    "Putin anadai ilibidi achukue hatua kwa sababu Urusi ilitishiwa lakini hakuna aliyeitishia Urusi na hakuna mtu mwingine isipokuwa Urusi iliyotafuta migogoro." Alisema Biden.

    Biden pia amesema Putin ametoa vitisho vya nyuklia dhidi ya Ulaya, anaita wanajeshi zaidi kupigana na kujaribu kuchukua sehemu za Ukraine.

    "Ulimwengu unapaswa kuona vitendo hivi vya kuchukiza jinsi vilivyo."

    Soma zaidi:

  3. Mzozo wa DRC na Rwanda: Kagame ataka UN kukomesha michezo ya lawama

    Rais wa Rwanda Paul Kagame ameutaka Umoja wa Mataifa kutafuta suluhu ya ukosefu wa usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)

    Katika hotuba yake kwa viongozi katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, rais Kagame alishutumu Umoja huo kwa kutumia michezo ya lawama baada ya kushindwa kutafuta suluhu ya ukosefu wa ya usalama ya DRC.

    Awali Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi alishutumu Rwanda kwa uchokozi wa wazi na kurudia shutuma hizo alipokuwa akihutubia Umoja wa Mataifa.

    Tshisekedi alidai kuwa licha ya nia yake njema kwa watu wa Congo katika kushughulikia suala la amani, baadhi ya majirani wanayaunga mkono makundi yenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Ripoti ya Umoja wa Mataifa mnamo Agosti 2022 ilisema kwamba chombo hicho kimepata ushahidi thabiti kwamba Bw Kagame aliunga mkono kundi la waasi la M23 kwa kutoa wanajeshi na silaha.

    Kundi la M23, ambalo lilidhibitiwa mwaka 2013, liliibuka na kuanza mapambano mwishoni mwa mwaka jana huku wakiishutumu serikali ya Kinshasa kwa kutoheshimu makubaliano ya kuwaondoa na kuwajumuisha tena wapiganaji jeshini.

    Maelezo zaidi:

  4. Tanzania yatoa tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ebola

    Wizara ya Afya nchini Tanzania imewashauri wananchi wake kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa ebola siku moja baada ya nchi jirani ya Uganda kuthibitisha mlipuko mpya wa virusi vya ugonjwa huo.

    Naibu Waziri wa afya Dk Godwin Mollel imewaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini kuimarisha utoaji wa elimu, ufuatiliaji wa ugonjwa, uchunguzi wa kitaalam na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na kinga muhimu katika maeneo yao.

    "Vilevile, nimewaelekeza kuimarisha uchunguzi wa wageni wanaoingia nchini kupitia mipaka yetu ikiwemo matumizi ya vipima joto" ilisema taarifa hiyo.

    Hata hivyo amewataka wananchi kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kugusa mwili au majimaji ya mwili wa mhisiwa au mgonjwa wa Ebola na kuepuka safari zisizo za lazima kutembelea maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huo September 20.

    Uganda ilithibitisha mlipuko wa virusi vya Ebola baada ya mwanaume mwenye umri wa miaka 24 aliyeambukizwa Ebola kufariki dunia katika mlipuko mpya uliothibitishwa na maafisa wa afya.

  5. Naibu waziri ashtakiwa kwa rushwa Rwanda,

    Naibu Waziri wa vijana na utamaduni Edouard Bamporiki ameshtakiwa kwa makosa ya rushwa.

    Katika kesi hiyo iliyoendeshwa na mahakama mjini Kigali, mshtakiwa amekiri makosa na kuomba radhi.

    Mwandishi wa BBC Yves Bucyana aliyekuwa mahakamani anasema kuwa, Mwendesha mashtaka ameiambia mahakama kuwa msingi wa mashtaka dhidi ya Bw. Bamporiki ni kuwa alipokea franga milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara Gatera Norbert ili kuingilia kati na kupangua hatua ya manispaa ya jiji la Kigali ya kufungia kiwanda chake cha pombe.

    Mwendesha mashtaka alifichua kwamba mshtakiwa alifumaniwa katika hoteli moja mjini Kigali akipokea hongo ya franga milioni 5 ambazo ni nusu ya kiasi walichokuwa wamekubaliana.

    Bwana Bamporiki amekiri kupokea pesa hizo lakini akasisitiza kwamba hakukusudia kupokea ama kutoa rushwa badala yake alikuwa mpatanishi tu kati ya mfanyabiashara huyo na manispaa ya jiji la Kigali.

    Pia ameshtakiwa kwa kosa la matumizi mabaya ya mamlaka.

    Mwendesha mashtaka amesema kwamba mshukiwa aliahidi kuingilia kati katika kuachiliwa kutoka gerezani mke wa mfanyabiashara huyo na baadaye kupewa mlungula wa franga milioni 10.

    Mshukiwa amekiri kupokea franga hizo lakini akasema ni zawadi aliyopewa baada ya kumshauri mfanyabiashara huyo njia ya kutumia ili mkewe aweze kuachiliwa huru.

    Mwendesha mashtaka amependekeza hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela dhidi ya mshukiwa na kutozwa faini ya kitita cha franga milioni 200 ambazo ni sawa na dola laki 2.

    Hata hivyo, wakili wa mshtakiwa amesema kuwa mapendekezo hayo dhidi ya mteja wake ni makali mno huku mshukiwa akiomba radhi.

    Bwana Edouard Bamporiki aliachishwa kazi na Rais Paul Kagame mapema mwezi wa 5 mwaka huu na tangu wakati huo amekuwa katika kizuizi cha nyumbani.

  6. Nigeria: Mafuriko yabeba mamia ya miili kutoka kwenye makaburi

    Mafuriko yamebeba zaidi ya makaburi 1,500 kwenye eneo la maziara katikati mwa Nigeria mji wa Mariga, jimbo la Niger.

    Zaidi ya makaburi 500 yamesombwa na mafuriko katika muda wa wiki moja pekee iliyopita.

    Imamu mkuu wa mji huo, Alhassan Musa Na’ibi, aliambia BBC takriban miili 1,000 iliyooza imezikwa upya.

    Mafuriko hayo yalifuatia siku kadhaa za mvua kubwa katika eneo hilo.

    Imamu huyo alisema makaburi hayo hayajawahi kupata uharibifu wa aina hiyo tangu kuanzishwa kwake miaka 500 iliyopita.

    Makaburi hayo yako karibu na mto.

    Wakazi wanasema shughuli za hivi majuzi za uchimbaji wa dhahabu karibu na makaburi hayo pia zimeifanya eneo hilo kuwa hatarini - kwani ardhi inadhoofika.

    Nigeria inakabiliwa na wimbi baya zaidi la mafuriko katika muongo mmoja - na kuathiri majimbo 29 kati ya 36 yake.

    Tangu mwisho wa Julai, zaidi ya watu 300 wameuawa na wengine zaidi ya 100,000 wamelazimika kuyahama makazi yao.

    Madaraja na mashamba makubwa pia yameharibiwa.

    Mamlaka inasema mafuriko zaidi yanatarajiwa katika wiki zijazo huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha.

    Soma zaidi:

  7. Tanzania: Miaka 20 ya kusubiri kuingia kwenye tuzo ya Oscar yafika mwisho

    Filamu ya Kitanzania imeorodheshwa kuwania tuzo ya Oscar - na hivyo kuhitimisha miongo miwili ya nchi hiyo kusubiri kuingia katika tuzo hizo.

    Filamu ya Vuta N’kuvute - imeorodheshwa katika kitengo cha 95 cha Filamu Bora ya Kimataifa ya Oscar.

    Filamu hiyo iliyotolewa kwa Kiswahili na waigizaji wengi weusi, inasimulia kisa cha msichana mdogo wa Kihindi-Mzanzibari ambaye mapenzi yake yanastawi kutokana na uasi wa kisiasa katika siku za mwisho za utawala wa kifalme wa Uingereza.

    ‘’Mustakabali wa sinema ya Tanzania hatimaye uko mikononi mwetu. Wimbi la wasanii wa filamu za Kiswahili linakua na fahari, akili na ujasiri kila siku, Amil Shivji, mtayarishaji mwenza wa filamu hiyo, alichapisha kwenye Instagram.

    Mnamo Septemba 2021, Vuta N’kuvute iliandika historia kama filamu ya kwanza ya Kitanzania kuwahi kuonyeshwa katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Toronto (TIFF).

    Tanzania iliingia kwa mara ya kwanza kwenye tuzo za Oscar ilikuwa filamu ya Maangazi: The Ancient One, mwaka wa 2002.

    Filamu za nchi hiyo za Kiswahili za Bongo ni maarufu Afrika Mashariki.

    Soma zaidi:

  8. Raia wa Ukraine wanakabiliwa na ukatili - Papa Francis

    Papa Francis amezungumzia mzozo wa Urusi na Ukraine katika hotuba yake ya kila wiki, akisema kwamba raia wa Ukraine walikuwa wakikabiliwa na ukatili, unyama na mateso.

    Bila kuitaja Urusi, Papa aliwaambia wasikilizaji wake kwa ujumla katika uwanja wa St. Peter's kwamba Waukraine ni watu wa‘’maadili’’ wasio na kosa wanaouawa.

    Pia alizungumza kuhusu mazungumzo aliyofanya na Kadinali Konrad Krajewski, mkuu wake wa shirika la kutoa misaada nchini Ukraine.

    Vyombo vya habari vya Vatikani vilisema Krajewski, ambaye ni raia wa Poland, alipigwa risasi na watu wengine wiki iliyopita alipokuwa akitoa msaada.

    Pia alitembelea makaburi ya halaiki.

    Soma zaidi:

  9. Kukusanya wanajeshi wa akiba niishara ya udhaifu – Balozi wa Marekani

    Kukusanya wanajeshi wa akiba ambako kumeagizwa na Rais wa Putin ni ishara ya ‘’udhaifu,’’ amesema balozi wa Marekani nchini Ukraine.

    ‘’Kura za maoni na kukusanya wanajeshi wa akiba ni ishara za udhaifu, kushindwa kwa Urusi,’’ Bridget Brink ameandika kwenye Twitter.

    ‘’Marekani haitatambua kamwe madai ya Urusi ya kutwaa eneo la Ukraine, na tutaendelea kusimama na Ukraine kwa muda wote itakavyochukua,’’ anaongeza.

    Soma zaidi:

  10. Ethiopia yakataa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili wa Tigray

    Serikali ya Ethiopia imekataa ripoti ya tume ya Umoja wa Mataifa, na kuielezea kuwa ‘’isiyo kamili, isiyo na msingi na isiyo na uthibitisho’’ na ina nia ya kuihujumu Ethiopia.

    Tume inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne iliangazia kile ilichokiita taarifa za kuaminika za mauaji makubwa yaliyofanywa na jeshi la ulinzi la taifa la Ethiopia.

    ‘’Serikali inajutia njia ya haraka, isiyo na viwango, na inayoendeshwa na ajenda [Tume ya Kimataifa ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu juu ya Ethiopia], iliyochagua kutekeleza wajibu wake’’ Iliongeza kuwa ripoti hiyo ilikuwa ‘’taarifa ya kisiasa’’.

    Serikali ilijitetea ikisema imewafikisha wahusika wa ukiukaji wa haki za binadamu mbele ya sheria.

    Serikali ya shirikisho na vikosi vya waasi vya Tigray vimeshutumu kila mmoja kwa ukiukaji wa haki za binadamu huku vita katika eneo la kaskazini la Tigray vikiendelea.

    Soma zaidi:

  11. Habari za hivi punde, Putin akusanya wanajeshi wa ziada kwa ajili ya vita Ukraine

    Rais wa Urusi Vladimir Putin ametangaza kukusanya wanajeshi wa ziada kwa ajili ya vita nchini Urusi - kulingana na shirika la habari linalomilikiwa na serikali TASS.

    Anasema kuwa nchi za Magharibi zimeonyesha kuwa lengo lake ni kuiangamiza Urusi na kwamba zimejaribu kuwageuza watu wa Ukraine kuingia kwenye vita kwa lazima.

    Lengo letu ni kuikomboa Donbas, anasema.

    Rais Putin anasema nchi za Magharibi zimeonyesha kuwa hazitaki amani kati ya Ukraine na Urusi.

    Putin pia anasema kuwa atatoa hadhi ya kisheria kwa ‘’wanaojitolea’’ wanaopigana huko Donbas.

    Putin ametangaza kuwa kuanzia leo ni muhimu kuchukua uamuzi wa haraka ili kulinda watu katika ‘’ardhi zilizokombolewa’’.

    “Ndiyo maana niliiomba wizara ya ulinzi kukusanya jeshi kwa ajili ya vita,” anasema.

    Amesema agizo hilo tayari limetiwa saini na linaanza kutekelezwa leo.

    Amesema kuwa raia wote ambao watakusnywa watakuwa na hadhi kamili ya jeshi.

    Putin ameongeza kuwa nchi za Magharibi zimekuwa zikiichafua Urusi lakini Urusi ina silaha nyingi za kujibu.

    “Tutatumia rasilimali zote tulizonazo kuwatetea watu wetu,” anasema.

    ‘’Nina imani na msaada wako,’’ anahitimisha.

    Soma zaidi:

  12. Wasomali kati ya makumi walioshtakiwa nchini Marekani kwa ulaghai

    Raia wa Kisomali wanaoishi Marekani walio na uhusiano na Kenya ni miongoni mwa watu 47 walioshtakiwa nchini Marekani kuhusiana na wizi wa $250m (£220m) katika madai ya mpango wa ulaghai wa kukabiliana na Covid-19.

    Wanadaiwa kuiba kutoka kwa mpango unaolenga kutoa chakula kwa watoto wakati wa janga hilo.

    Mamlaka ya shirikisho la Marekani Jumanne ilitangaza kwamba washukiwa hao wanahusishwa na Aimee Bock - mwanzilishi na mkurugenzi mkuu wa Feeding Our Future, shirika lisilo la faida ambalo lilikuwa mfadhili linaloshiriki katika Mpango wa Shirikisho wa Lishe ya Mtoto huko Minnesota.

    Hata hivyo, Bi Bock alikanusha kutekeleza makosa yoyote.

    Kama sehemu ya mpango unaodaiwa, wafanyakazi wa ‘Feeding Our Future’ waliajiri watu binafsi na mashirika kufungua tovuti za Mpango wa Shirikisho wa Lishe ya Mtoto katika jimbo lote la Minnesota.

    Tovuti hizi, zilizoundwa na kuendeshwa na washtakiwa na wengine, zilidai kuwa zinatoa chakula kwa maelfu ya watoto kwa siku ndani ya siku chache au wiki baada ya kuundwa.

    Washukiwa hao wanadaiwa kutoa bili za milo ambayo hawakuwahudumia watoto ambao hawakuwapo, ilisema Idara ya Haki (DoJ) katika taarifa.

    Idara hiyo inadai washtakiwa walitumia pesa hizo kununua magari ya kifahari, mali isiyohamishika ya makazi na biashara huko Minnesota pamoja na mali huko Ohio na Kentucky, mali isiyohamishika katika pwani ya Kenya na Uturuki, na kufadhili safari za kimataifa.

    Mmoja wa washukiwa hao, Mohammed Jama Ismail, alikamatwa nchini Marekani mwezi Aprili alipokuwa akijaribu kuondoka nchini humo kuelekea Kenya kupitia Amsterdam.

    Alikiri kosa la ulaghai wa paspoti mwezi uliopita.

    ‘’Mashtaka ya leo yanaelezea njama mbaya ya kuiba fedha za umma zilizokusudiwa kutunza watoto wanaohitaji kwa kiasi ambacho ni sawa na mpango mkubwa zaidi wa ulaghai wa kukabiliana na janga,’’ alisema mkurugenzi wa FBI Christopher Wray.

    Washukiwa hao wanashtakiwa kwa kula njama, wizi wa fedha, utakatishaji fedha na hongo.

    Minnesota ni mwenyeji wa jumuiya kubwa ya wahamiaji kutoka Afrika Mashariki, hasa Wasomali na Waethiopia.

  13. Japan:Mwanamume ajichoma moto katika maandamano ya mazishi ya Abe

    Mwanamume mmoja wa Japan amejichoma moto kama njia ya kupinga mazishi ya serikali ya aliyekuwa Waziri Mkuu Shinzo Abe, ambaye aliuawa mwezi Julai.

    Mamia ya viongozi wa kigeni wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo tarehe 27 Septemba.

    Siku ya Jumatano, mashahidi waliwaita polisi baada ya kumuona mtu akiwaka moto karibu na ofisi ya waziri mkuu mjini Tokyo.

    Maafisa walizima moto huo, na kumpeleka mtu huyo hospitalini, vyombo vya habari vya ndani viliripoti.

    Kiwango cha majeraha yake na hali yake ya sasa haijulikani.

    Ripoti za vyombo vya habari vya Japan zinasema kuwa mwanamume huyo anaaminika kuwa na umri wa miaka 70.

    Serikali bado haijatoa maoni yoyote kuhusu maandamano hayo.

    Lakini upinzani wa umma dhidi ya kufanyika kwa mazishi ya serikali umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni, huku kura za maoni zikionyesha wapiga kura wengi kutofurahishwa na matumizi ya shughuli nzima ya mazishi.

    Abe aliuawa kwa kupigwa risasi tarehe 8 Julai, akiwa na umri wa miaka 67, katika mkutano wa kampeni wa chama chake cha kisiasa.

    Mauaji ya waziri mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi nchini Japan yalilaaniwa kimataifa na kuishtua Japan, nchi yenye rekodi ndogo ya ghasia za kisiasa na uhalifu wa kutumia bunduki.

    soma zaidi:

  14. 'Panya Road' watuhumiwa sasa kufikishwa mahakamani TZ,

    Zaidi ya watuhumiwa 100 wa uhalifu wa kundi la panya road nchini Tanzania wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayohusu uhalifu.

    Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema kulingana na taarifa iliyotolewa jana inaendelea kuwashikilia zaidi ya vijana 100 wanaodaiwa kuhusika kwenye matukio ya uhalifu katika vitongoji mbalimbali ndani ya jiji hilo.

    Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar-es-Salaam alizungumza na BBC na kueleza kuwa wanaendelea na operesheni maalum ili kukomesha vitendo vya uhalifu jijini Dar es Salaam.

    “Taarifa ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, jana ilielezea hatua ambazo serikali na Jeshi la Polisi imejielekeza. Pia Jeshi la Polisi inaendela na uchunguzi na upelelezi ukikamilika, watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria…

    ”Suala zima la uhalifu litakoma kwa kushirikiana kati ya wananchi na sisi Polisi. wahalifu wako kwenye jamii yetu, wanatekeleza matukio leo, wanarudia kesho na zaidi ya hapo. cha msingi wananchi watoe taarifa,” alisema Kamanda Muliro.

    Doria saa 24, magari kila kitongoji

    Kutokana na kukithiri kwa matukio ya uhalifu yanayosababishwa na Panya road na matukio mengine ya kihakifu, Mapema jana Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama mkoa wa Dar-Es-Salaam, ambaye pia ni mkuu wa mkoa huo Amos Makalaalitoa msimamo wa kamati yake imeshaagiza vituo vyote kufanya kazi saa 24 kwa siku lakini pia kila kitongoji kitapitiwa na gari la polisi kwaajili ya kurahisisha operesheni ya kusaka waalifu.

    ”Hakuna kituo cha polisi kitakachofanya kazi kwa saa 12 tu, sasa polisi watakuwa saa 24, magari yapo na kutakuwa vikao shirikishi kati ya wananchi, viongozi wa serikali, polisi na polisi jamii kila wiki vyenye lengo la kutathmini hali ya usalama katika mtaa husika jijini Dar es Salaam,” alisema.

    Matukio yaliyohusisha kundi hilo hivi karibuni

    Panya Road hivi karibuni wanadaiwa kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja wa chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sambamba na kujeruhi baadhi ya wananchi katika wilaya ya Temeke.

    Hata hivyo polisi ilifanikiwa kuwaua watu sita wanaotajwa kuwa wa kundi hilo waliopambanana polisi kwenye mapambano mwishoni mwa wiki iliyopita.

    Panya road ni kundi gani?

    Panya road ni kundi la uhalifu lililopata umaarufu kutokana na matukio mbalimbali ya kunyakua mali za watu pamoja na kujeruhi wananchi katika mkoa wa Dar es Salaam.

    Kundi hilo lilianza kupata umaarufu mwaka 2016 kutokana na matukio hayo yauhalifu jijini Dar es Salaam ambapo walifahamika kwa kutumia visu, mapanga na vyuma chakavu wanapovamia wananchi kwa lengo la kuwajeruhi na kunyanganya mali zao.

    Hata hivyo kundi hilo huwa linapotea pale polisi wanapofanya msako, na huibuka kisha kupotezwa tena.

  15. AU: Zimbabwe iondolewe vikwazo

    Rais wa Senegal Macky Sall ametoa wito wa kuondolewa vikwazo dhidi ya Zimbabwe katika hotuba yake kwenye Mkutano Mkuu wa 77 wa Umoja wa Mataifa mjini New York.

    Kiongozi huyo wa Senegal, na mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, alisema hatua kali dhidi ya Zimbabwe zinazidisha mateso ya watu.

    Bw Sall alikuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kuhutubia Baraza Kuu. Alilitaka Baraza la Usalama kushughulikia mizozo barani Afrika kwa njia sawa na kushughulikia mizozo mingine.

    Pia alitoa wito wa mageuzi katika baraza hilo ambayo yatalifanya kuwa shirikisha zaidi na pengine kuipa Afrika kiti cha kudumu. Bw Sall pia alitoa wito kwa Afrika kupewa kiti katika kundi la G20, linalojumuisha viongozi wa mataifa 20 makubwa kiuchumi duniani.

    Viongozi zaidi wa Afrika wanatarajiwa kuhutubia mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano katika siku ya pili ya mjadala huo wa ngazi ya juu.

  16. Marekani inasema inafuatilia harakati za wanajeshi wa Eritrea katika eneo la Tigray

    Marekani inasema inafuatilia harakati za wanajeshi wa Eritrea katika eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia baada ya waasi wa huko kusema mashambulizi makali yanaendelea.

    Mjumbe maalum wa Marekani katika Pembe ya Afrika, Mike Hammer, alielezea ripoti hizo kuwa za kuhuzunisha sana.

    Alisema vikosi vya nje vinapaswa kuepuka kuchochea mzozo unaoendelea huko Tigray.

    Eritrea imekuwa ikishirikiana na wanajeshi wa serikali ya Ethiopia katika vita vyao vya miaka miwili dhidi ya waasi wa Tigray.

    Bw Hammer alisema kuwepo kwa wanajeshi wa Eritrea kulichochea tu hali ya kutisha.

    Hapo awali, msemaji wa kundi la waasi la TPLF Getachew Reda alisema kulikuwa na mapigano makali katika maeneo kadhaa ya mpakani.

    Wakati huohuo ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaishutumu Ethiopia kwa ukatili wa Tigray

    Ripoti inasema ukiukaji wa haki za binadamu umefanywa na pande zote.

    Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema wanaamini kuwa serikali ya Ethiopia ndiyo inayohusika na uhalifu dhidi ya binadamu unaoendelea katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo.

    Katika ripoti yake, Tume ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu nchini Ethiopia iliangazia kile ilichokiita taarifa za kuaminika za mauaji makubwa yaliyofanywa na jeshi la ulinzi la taifa la Ethiopia, ambayo yaliwalenga wanaume na wavulana wa Tigray walio katika umri wa kupigana.

    Serikali ya Ethiopia ilikanusha ripoti hiyo. Wachunguzi wanasema pia kuna ushahidi kwamba njaa inatumiwa kama silaha ya vita.

    Ripoti hiyo inasema ukiukaji wa haki za binadamu umefanywa na pande zote tangu mapigano yalipozuka karibu miaka miwili iliyopita.