Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran kuipa Urusi ndege zisizo za rubani ili kuisambaratisha Ukraine
Iran inapanga kuipatia Urusi mamia ya ndege za kivita zisizo na rubani kwa ajili ya vita yake nchini Ukraine, baadhi zikiwa na uwezo mkubwa wa wa kivita, afisa wa Marekani amesema.
Moja kwa moja
Rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu aghadhabishwa na uchunguzi dhidi ya mke wake
Rais wa zamani wa Zambia Edgar Lungu ameishutumu serikali kwa kumtesa, baada ya mkewe kuitwa kuhojiwa.
Esther Lungu anatakiwa kuhojiwa na Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya (DEC) kuhusiana na nyumba 15 anazomiliki mjini Lusaka. Tume hiyo inadai kuwa mali hizo huenda zimepatikana kwa njia isiyo halali, jambo ambalo anakanusha.
Akiwahutubia wabunge wa chama tawala cha zamani, Patriotic Front, walioenda kumtembelea yeye na mkewe kuonyesha mshikamano, Bw Lungu alisema familia yake inalengwa kwa njia isiyo ya haki.
"Si lazima uwe na akili sana kujua kwamba anayeandamwa sio [Esther Lungu] ni mimi. Kwa hivyo hii ni njama, ni kama kumenya vitunguu hivyo niko tayari," alisema Bw Lungu, ambaye watoto wake wawili hivi majuzi pia waliitwa kuhojiwa.
Kwa upande wake, Bi Lungu ametangaza kuwa hana hatia.
Chama cha Bw Lungu mwaka jana kilipoteza mamlaka kwa aliyekuwa madarakani Hakainde Hichilema wa United Party for National Development.
Maafisa kadhaa wa zamani wa serikali wamekuwa wakifika kuhojiwa na baadhi ya mali zao kuchukuliwa kama sehemu ya vita vya serikali mpya dhidi ya ufisadi.
Afrika kutawala kwa ukuaji wa watu duniani hadi 2050 - UN
Nchi za Kiafrika zinatazamiwa kutawala ongezeko la watu duniani hadi mwaka 2050, kulingana na ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya nusu ya makadirio ya ongezeko la idadi ya watu duniani itashuhudiwa katika nchi nane, tano kati ya hizo ziko barani humo.
Nchi hizo ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ethiopia, Nigeria na Tanzania.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Nigeria kwa sasa ni nchi ya sita kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu duniani, na ifikapo mwaka 2050 inatarajiwa kuwa na idadi ya watu sawa na Marekani, watu milioni 375. Hali ambayo itaifanya nchi ya nne yenye watu wengi zaidi duniani.
Ifikapo mwaka 2050 Ethiopia na DR Congo pia zinatarajiwa kuwa katika orodha ya nchi 10 zenye watu wengi zaidi duniani.
Teksi lililoishiwa na mafuta lapatikana na ''kondoo wa kuibwa''
Polisi wa Afrika Kusini wamemkamata mwanamume mmoja baada ya kukamata teksi ndogo iliyokuwa imebeba kondoo 21 wanaoshukiwa kuibiwa.
Walisema uchunguzi wa awali ulionyesha basi hilo liliishiwa petroli huku watu waliokuwa ndani wakisafiri kutoka Kuruman Kaskazini mwa Cape ambako mifugo hiyo inadaiwa kuibiwa.
Gari hilo lilinaswa na polisi waliokuwa wakishika doria barabarani mwishoni mwa juma.
"Walipokaribia gari na kulikagua, polisi waliwaona watu wawili wakikimbia kutoka eneo la tukio na kumwacha mtu mwenye umri wa miaka 43," Huduma ya Polisi ya Afrika Kusini ilisema katika taarifa siku ya Jumatatu.
Mshukiwa huyo alikamatwa na kuzuilwa pamoja na kondoo hao, polisi waliongeza.
Walisema uchunguzi unaendelea kwani mshukiwa alitakiwa kufika mahakamani siku ya Jumatatu.
Mali yawataja kuwa mamluki wanajeshi 49 wa Ivory Cost wanaozuiliwa
Serikali ya kijeshi nchini Mali imetangaza kuwa wanajeshi 49 kutoka Ivory Coast, waliozuiliwa katika uwanja wa ndege wa Bamako walipowasili siku ya Jumapili, walikuwa mamluki.
Hata hivyo ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Mali, MINUSMA, umesema watu hao walikuwa sehemu ya kitengo kilichotoa msaada wa kawaida wa vifaa kwa kikosi cha kijeshi cha Ivory Coast cha MINUSMA.
Serikali nchini Mali inasema kesi hiyo itawasilishwa kwa mamlaka ya mahakama.
Mwandishi wa habari wa eneo hilo aliambia BBC kwamba serikali ya kijeshi ya Mali - ambayo imeahidi kurejesha utawala wa kiraia - imekuwa na uhusiano mbaya na Umoja wa Mataifa.
Uchunguzi waondoa hofu ya Dos Santos kuuawa- Mwanasheria Mkuu wa Angola
Mwanasheria Mkuu wa Angola Helder Pitta Gros anasema uchunguzi wa maiti ya aliyekuwa Rais wa Angola José Eduardo dos Santos umedhibitisha hakuwekewa sumu.
Mahakama ya Barcelona iliidhinisha uchunguzi wa maiti kufuatia ombi kutoka kwa binti yake Tchize dos Santos, ambaye alidai kuwa aliuawa.
Bw Dos Santos alifariki katika hospitali ya Barcelona siku ya Ijumaa, ambapo alikuwa akipatiwa matibabu.
Mawakili wa familia hiyo wameshutumu hatua za serikali ya Angola kurudisha mwili wa marehemu nyumbani kwa ajili ya mazishi ya kiserikali, wakisema alitaka mazishi ya kibinafsi nchini Uhispania.
Soma:
Mmoja wa mapacha waliotenganishwa Tanzania afariki dunia
Mmoja wa mapacha walioungana viungo vya mwili na kufanyiwa upasuaji wa kutenganishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) nchini Tanzania amefariki dunia baada ya hali yake kubadilika ghafla.
Neema ambaye alitenganishwa na mwenzake Rehema amefariki Jumapili ya July 10 baada ya hali yake kubadilika ghafla wakati akiendelea na matibabu.
Taarifa ya Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano imeeleza kuwa hali ya Neema ilibadilika ghafla akiwa katika Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU).
"Nasikitika kukufahamisha kuwa mtoto Neema ambaye alitenganishwa na mwenzake Rehema amefariki jumapili ya tarehe 10 Julai saa 3 asubuhi. Akiwa ICU hali yake ilibadikika gafla, madaktari walijitahidi kurudisha hali yake bila mafanikio" ilieleza
Muhimbili ilifanikisha upasuaji wa kuwatenganisha watoto hao waliokuwa wameungana Rehema na Neema Julai 1 mwaka huu.
Pacha mwenzie Rehema bado yupo ICU akiendelea na matibabu
- Hospitali ya Taifa Muhimbili yawatenganisha pacha walioungana
- Sababu za kifo cha Maria na Consolata
- Pacha walioshikana Tanzania
DR Congo yajiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jumatatu imekuwa rasmi mwanachama wa saba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya kupeleka hati za kuridhia kwa makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Arusha, Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje Christophe Lutundula aliwasilisha nyaraka hizo kwa Katibu Mkuu wa EAC, Peter Mathuki, ambaye alieleza kuwa maendeleo hayo ni muhimu kwa DR Congo na jumuiya.
Nchi wanachama ziliidhinisha ombi la DR Congo kujiunga na umoja huo mwezi Aprili na bunge la nchi hiyo liliidhinisha uamuzi huo mwezi Juni.
Urais wa DR Congo uliweka ujumbe kwenye Twitter kuhusu maendeleo ya hivi punde:
DR Congo inaungana na Burundi, Kenya, Uganda, Rwanda, Sudan Kusini na Tanzania na kuwa nchi ya pili katika shirika hilo.
EAC tayari inajishughulisha na juhudi za kumaliza ghasia mashariki mwa DR Congo, huku kikosi cha kikanda kinatarajiwa kutumwa huko.
Soma zaidi:
Ugonjwa usiojulikana wa kutokwa na damu puani na kuanguka wakumba kusini mwa Tanzania, Rais athibitisha
Mikoa ya kusini mwa Tanzania imekumbwa na ugonjwa wa ajabu usiofahamika, ambao usababisha watu kutokwa damu puani na kuanguka.
Rais wa taifa hilo, Samia Suluhu amekiri kuwepo kwa ugonjwa huo leo wakati akizungumza na viongozi wa dini katika Mkutano mkuu wa 20 wa Shirikisho la mabaraza ya maaskofu wa Kanisa Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA unaofanyika jijii Dar es Salaam.
'nilikuwa nazungumza na waziri mkuu juzi, ametoka ziara kule mikoa ya kusini, Lindi ananiambia ameona kuna maradhi yameingia, wanadamu wanatokwa tu na damu za pua na wanadondoka', alisema Rais Samia
Rais Samia hakusema ni watu wangapi mpaka sasa wameathirika na haijulikani ni aina gani ya ugonjwa uliolikumba eneo hilo liloloko mpakani na nchi ya Msumbiji.
'hatujui ni kitu gani, wanasayansi wataalamu wa afya wote wamehamia huko wanaangalia ni kitu gani' alisema Rais na kuongeza 'kwanini mwanadamu atokwe tu damu za pua adondoke, angekuwa mmoja wawili tungesema presha imepanda veins zimebasti (mishipa imepasuka) anatokwa damu za pua, lakini ni wengi kwa mfululizo, ni maradhi ambayo hatujawahi ona, na yote ni kwa sababu tuna haribu makazi ya viumbe kule walikoumbwa na mungu, tunawasogeza kwetu na kutuletea aina yote hiyo ya maradhi'.
Rais Samia alikuwa akizungumza kwenye mkutano huo wa AMECEA, shirkisho linaloundwa na nchi 8 ambazo ni Zambia, Malawi, Kenya, Uganda, Sudan, Ethiopia, Eritrea na mwenyeji Tanzania, ambapo pamoja na mambo mengine umejiegemeza kwenye masuala ya utunzaji wa mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu ya binadamu.
Vita vya Ukraine: Iran inapanga kuipatia Urusi ndege zisizo na rubani, Marekani yaonya
Iran inapanga kuipatia Urusi uwezekano wa mamia ya ndege zisizo na rubani kwa vita vyake nchini Ukraine, baadhi zikiwa na uwezo wa kivita, afisa wa Marekani amesema.
Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House Jake Sullivan alisema taarifa zilizopokelewa na Marekani zinaonyesha kuwa Iran inajiandaa kutoa mafunzo kwa vikosi vya Urusi kutumia ndege hizo zisizo na rubani.
Aliongeza kuwa haijulikani ikiwa Iran imezifikisha ndege hizo.
Ndege zisizo na rubani zimekuwa muhimu kwa vita vinavyoendelea kwa Ukraine na Urusi.
Wiki iliyopita tu, Ukraine iliomba michango ya maelfu ya ndege zisizo na rubani kusaidia juhudi zake za vita.
Bw Sullivan aliongeza kuwa taarifa za kijasusi zilizopokelewa na Marekani zinaunga mkono maoni kwamba shambulio la Urusi mashariki mwa Ukraine ‘’linagharimu udumishaji wa silaha zake yenyewe’’.
Pia aliona kwamba ndege zisizo na rubani za Iran hapo awali zilitumiwa na waasi wa Houthi wa Yemen kushambulia Saudi Arabia.
Maoni yake yalikuja kabla ya ziara ya Rais wa Marekani Joe Biden nchini Israel na Saudi Arabia wiki hii.
Hakuna nchi hadi sasa imejiunga na vikwazo dhidi ya Urusi kutokana na vita vyake nchini Ukraine.
Israel inaiona Iran, ambayo inataka kuondolewa kwake, kama tishio kubwa zaidi la kikanda.
Marekani na washirika wengine wameipatia Ukraine silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola tangu uvamizi huo mwezi Februari.
Bw Sullivan alisema Marekani itaendelea ‘’kudumisha ulinzi madhubuti wa Ukraine.’’
Soma zaidi:
Shinzo Abe: Waombolezaji wa Japan watoa heshima za mwisho kwa Waziri Mkuu wa zamani wakati wa mazishi
Maelfu ya waombolezaji wanajitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa waziri mkuu wa zamani wa Japan Shinzo Abe siku ya Jumanne.
Mazishi ya faragha, ambayo yako wazi kwa marafiki na familia ya karibu pekee, yanaendelea katika hekalu la Zojoji la Tokyo.
Kufuatia mazishi, gari la kubebea maiti lililobeba mwili wa Abe litaelekea katikati mwa jiji la Tokyo.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 67 aliuawa kwa kupigwa risasi Ijumaa iliyopita alipokuwa akitoa hotuba ya kampeni huko Nara kusini mwa Japani.
Ndani ya hekalu la Zojoji, ibada za Wabudha zinafanywa.
Nje na kote Tokyo, bendera zinapepea nusu mlingoti.
Msafara wa mazishi Jumanne alasiri utapita kwenye maeneo muhimu kama vile jengo la bunge, ambalo Abe aliingia kwa mara ya kwanza kama mbunge mnamo 1993, na ofisi ambayo aliongoza taifa kama waziri mkuu.
Soma zaidi:
Abe alikuwa waziri mkuu wa Japan aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi baada ya vita na mmoja wa wanasiasa wake wenye ushawishi mkubwa.
Polisi walisema mtu huyo mwenye silaha alimlenga kutokana na malalamiko aliyokuwa nayo na kundi la kidini ambalo aliamini kuwa Abe alikuwa sehemu yake.
Shambulio hilo lilileta mshtuko katika taifa ambalo matukio ya unyanyasaji wa bunduki ni nadra sana.
Vita vya Ukraine: Ujerumani inahofia kukatwa kwa gesi ya Urusi kunaweza kuwa ya kudumu
Usambazaji wa gesi asilia ya Urusi kwenda Ujerumani kupitia bomba la Bahari ya Baltic Nord Stream 1 umesimamishwa kwa siku 10 kwa kazi ya matengenezo ya kila mwaka.
Lakini Waziri wa Uchumi wa Ujerumani Robert Habeck alionya kwamba nchi za EU lazima ziwe tayari ikiwa usafirishaji wa gesi hautaanza tena.
Ameishutumu Urusi kwa kutumia gesi ‘’kama silaha’’ kujibu vikwazo vya Umoja wa Ulaya kuhusu vita vya Ukraine.
Bw Habeck alikiri Ujerumani imekuwa ikitegemea sana gesi ya Urusi.
Alieleza hilo kama ‘’kosa kubwa la kisiasa kama tunavyoona leo, ambalo tunajaribu kulitatua haraka tuwezavyo.’’
Alisema vituo viwili vya kuelea kwa ajili ya kusambaza gesi asilia kimiminika (LNG) vitakuwa tayari mwishoni mwa mwaka.
Soma zaidi:
Unaufahamu msikiti wa miujiza wa Japan?
Msikiti wa Kobe huko Japan, watu wengine wanauita Msikiti wa Miujiza. Hapo awali umenusurika mikasa nchini humo.
Ulinusurika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani huko Kobe wakati wa Vita vya pili vya dunia mnamo 1945.
Wakati huo, msikiti huo ulikuwa kimbilio salama kwa watu wengi huku mabomu yakiharibu miji ya Japan.
Baadhi ya watu wanautaja msikiti huu kuwa msikiti wa kwanza kujengwa nchini Japani.
Mnamo 1928, Waislamu walipoongezeka katika jiji la bandari la Kobe, walihitaji mahali pa ibada, wakaanza kuchangisha pesa za kujenga msikiti, na Waislamu, wengi wao kutoka India na Uturuki, walikuwa likizoni.
Msikiti huo wa orofa tatu ulibuniwa na mhandisi wa Czech Jan Josef Svagr.
Msikiti wa Kobe ulifunguliwa rasmi mwaka wa 1935, na sala zilitolewa na Waislamu wengi kutoka eneo la Kansai.Msikiti huo pia ulinusurika tetemeko la ardhi huko Japan mnamo 1995 ambalo liliua maelfu ya watu.
Pia, msikiti huo ulinusurika na mafuriko makubwa yaliyoathiri Kobe mnamo 1938, na hivyo kujulikana kama 'msikiti wa miujiza'.
Msikiti huo ni maarufu na ni mahali pa Waislamu wa eneo hilo kuabudu na kufanya sherehe na harusi za Waislamu.
Msikiti huo ulichukuliwa na jeshi la wanamaji la Japan mnamo 1943.Msikiti huu bado unatumika na Waislamu wengi, na uko katika eneo maarufu la watalii.
Siku ya Idadi ya Watu Duniani: India itaishinda China mwaka 2023, UN yasema
India inatazamiwa kuwa nchi yenye watu wengi zaidi duniani mwaka ujao, na kuipita China yenye watu wake 1.4bn, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Kufikia Novemba hii, sayari itakuwa nyumbani kwa watu 8bn.
Lakini ukuaji wa idadi ya watu sio haraka kama ilivyokuwa zamani.
Sasa iko katika kiwango cha polepole zaidi tangu 1950 na inakaribia kilele, inasema Umoja wa Mataifa, karibu miaka ya 2080 karibu 10.4bn ingawa baadhi ya wanademografia wanaamini kwamba inaweza kutokea hata mapema.
Lakini idadi ya watu duniani inaongezeka bila usawa.
Zaidi ya nusu ya ukuaji tutakayoshuhudia katika miaka 30 ijayo utafanyika katika nchi nane pekee - Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ethiopia, India, Nigeria, Pakistan, Ufilipino na Tanzania.
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja