Netanyahu kuhusu Iran: Ukitupiga, tutakupiga

Netanyahu amesema Umoja wa Mataifa lazima "urejeshe" vikwazo dhidi ya Iran na "ni lazima sote tufanye kila tuwezalo kuhakikisha Iran haipati silaha za nyuklia".

Muhtasari

  • 'Hakuna sehemu nchini Iran' ambayo Israel haiwezi kufika - Netanyahu auambia Umoja wa Mataifa
  • Netanyahu: Israel 'haitapumzika' katika mashambulizi ya Hezbollah hadi raia wake warejee nyumbani
  • Netanyahu kuhusu Iran: Ukitupiga, tutakupiga
  • Mwanaharakati 'mgonjwa mahututi' wa Ghana anyimwa dhamanaPutin achora mstari mwekundu wa nyuklia kwa nchi za Magharibi
  • Shambulizi la Israel lawauwa wanajeshi 5 katika mpaka wa Syria na Lebanon
  • Ukraine yasema ndege zisizo na rubani 24 za Urusi zimedunguliwa huku moja ikiingia Romania
  • IDF yadai kuwaua viongozi wengine wakuu zaidi wa Hezbollah katika shambulizi lililopita
  • Shambulizi laua wanafamilia tisa nchini Lebanon - ripoti
  • Mamlaka ya Lebanon yatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja
  • Mazungumzo ya kusitisha mapigano yataendelea hata kama mapigano yanaendelea - Netanyahu
  • Alabama yatekeleza hukumu ya kifo ya pili ya gesi ya nitrojeni
  • Trump na Zelensky kukutana huku wanachama wa Republican wakiwa na hasira
  • Naomi Campbell apigwa marufuku kuwa mdhamini wa shirika la kutoa misaada
  • Israel yaishambulia Hezbollah kwa 'nguvu' yake yote licha ya wito wa kusitisha mapigano

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Na mpaka hapo ndio tunafikia mwisho wa matangazo yetu ya mubashara kwa leo, tukutane tena hapo kesho majaaliwa.

  2. 'Hakuna sehemu nchini Iran' ambayo Israel haiwezi kufika - Netanyahu auambia Umoja wa Mataifa

    f

    Chanzo cha picha, UN Web TV

    Netanyahu anarejelea tena "laana ya Oktoba 7" ambayo anasema ilianza wakati Hamas ilipovamia lakini, ameongeza kuwa, "haikuishia hapo".

    Amesema kuwa tarehe 8 Oktoba, Hezbollah ilishambulia Israeli kutoka Lebanon na tangu wakati huo imerusha zaidi ya roketi 8,000.

    Ameorodhesha wengine ambao wameishambulia Israeli ikiwa ni pamoja na Wahouthi wa Yemeni na kusema kwamba Aprili iliyopita, Iran iliishambulia moja kwa moja Israeli kutoka kwenye ardhi yake.

    Anasema "hakuna mahali nchini Iran" ambapo "mkono mrefu" wa Israeli hauwezi kufikia, na "hiyo kwa Mashariki ya Kati yote".

    Ameongeza pia kwamba: "Mbali na kuwa wanakondoo wanaoongozwa kwenye machinjo, askari wa Israeli wamepigana kwa ujasiri wa ajabu na kwa ushujaa, na nina ujumbe mwingine kwa mkusanyiko huu na kwa ulimwengu nje ya ukumbi huu - tunashinda."

    Unaweza pia kusoma:

  3. Netanyahu: Israel 'haitapumzika' katika mashambulizi ya Hezbollah hadi raia wake warejee nyumbani

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameliambia Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa vita hivi vinaweza kumalizika sasa ikiwa Hamas itajisalimisha.

    Lakini anaongeza kuwa Israel lazima pia iishinde Hezbollah nchini Lebanon.

    Anasema siku moja baada ya mashambulizi ya Hamas, Hezbollah ilirusha makombora na kuwalazimisha zaidi ya Waisraeli 60,000 kaskazini mwa Israel kuondoka makwao.

    "Inatosha - hatutapumzika hadi raia wetu warudi makwao."

    "Hatutakubali jeshi la kigaidi kwenye mpaka wetu wa kaskazini kutekeleza mauaji mengine ya mtindo wa Oktoba 7," amesema.

    Hezbollah ilirusha makombora na roketi kutoka kwenye shule, hospitali na nyumba za kibinafsi za raia wa Lebanon, amesema.

    Anasema kuwa Israel "haiko vitani na watu wa Lebanon", bali katika vita na Hezbollah ambayo "imeiteka nchi yako". Israel haina chaguo na ina kila haki ya kuondoa tishio hili, anasema.

    Unaweza pia kusoma:

  4. Netanyahu kuhusu Iran: Ukitupiga, tutakupiga

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Netanyahu amesema Umoja wa Mataifa lazima "urejeshe" vikwazo dhidi ya Iran na "ni lazima sote tufanye kila tuwezalo kuhakikisha Iran haipati silaha za nyuklia".

    Akihutumia Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa, Waziri huyo mkuu wa Israel amesema amekuwa akiionya dunia dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran, ambao anasema "imeuchelewesha" kwa takriban muongo mmoja lakini hajausimamisha.

    "Kwa ajili ya amani na usalama wa dunia nzima, hatupaswi kuruhusu hilo kutokea," anasema, akimaanisha Iran kupata silaha za nyuklia.

    "Nina ujumbe kwa wadhalimu wa Tehran," anaongeza. "Ukitupiga, tutakupiga."

    Awali alipoanza hotuba yake Netanyahu alisema kwamba "hakuwa na nia ya kuja" kwenye Baraza Kuu mwaka huu kwani nchi yake iko vitani "inapigania maisha yake".

    "Niliamua kuzungumza katika Umoja wa Mataifa baada ya 'uongo' kuhusu Israel," asema

    Hata hivyo, uamuzi wake wa kufanya hivyo ulifuatia kile alichokiita "uongo na kashfa" kuhusu nchi yake iliyosemwa na watu wengine waliosimama kwenye jukwaa, anasema.

    Anaongeza kuwa anataka kuja na "kuweka rekodi" kwamba Israeli inatafuta amani.

    Netanyahu alionyesha ramani huku akijaribu kutofautisha "baraka" ya maendeleo ya Israeli na "laana" ya ushawishi wa Iran katika eneo.

    Uchokozi wa Iran utahatarisha kila nchi katika Mashariki ya Kati - na dunia nzima, Netanyahu ameuambia Umoja wa Mataifa.

    "Iran inataka kulazimisha itikadi kali zaidi ya Mashariki ya Kati, na inatishia ulimwengu mzima."

    Ulimwengu umeituliza Iran, anasema, na kufumbia macho ukandamizaji wa ndani wa Iran na uchokozi wa nje.

  5. Mwanaharakati 'mgonjwa mahututi' wa Ghana anyimwa dhamana

    h

    Chanzo cha picha, Oliver Barker-Vormawor/Facebook

    Maelezo ya picha, Oliver Barker-Vormawor kwa sasa anatibiwa katika hospitali ya polisi

    Mwanaharakati wa Ghana aliyezuiliwa ambaye alikuwa mwandalizi mkuu wa maandamano ya hivi majuzi ya kupinga uchimbaji madini amenyimwa dhamana pamoja na wengine 11, licha ya kuwa mgonjwa mahututi.

    Oliver Barker Vormawor alifikishwa mahakamani siku ya Alhamisi na kukana mashtaka mengi, yakiwemo kukusanyika kinyume cha sheria na kumshambulia afisa wa umma.

    Bw Vormawor atazuiliwa na polisi kwa muda wa wiki mbili kisha afike mahakamani. Amekuwa akitibiwa katika hospitali ya polisi kwa ugonjwa ambao haukujulikana.

    Mwanaharakati huyo ambaye ni mhitimu wa Cho kikuu cha Cambridge alipanga maandamano ya siku tatu kupinga hatua dhidi ya uchimbaji haramu wa madini, unaojulikana kwa kienyeji kama "galamsey", ambao umelaumiwa kwa kuchafua 60% ya maji ya Ghana.

  6. Putin achora mstari mwekundu wa nyuklia kwa nchi za Magharibi

    g

    Chanzo cha picha, AFP

    Rais Vladimir Putin amechora "mstari mwekundu" kwa Marekani na washirika wake kwa kuashiria kwamba Moscow itafikiria kujibu silaha za nyuklia ikiwa watairuhusu Ukraine kushambulia ndani kabisa ya Urusi kwa makombora ya masafa marefu ya Magharibi. .

    Lakini wengine katika nchi za Magharibi wanauliza: je, ni kweli anamaanisha hivyo?

    Swali hili ni muhimu kujiuliza katika hali ya vita. Iwapo Putin anababaika, kama Ukraine na baadhi ya wafuasi wake wanavyoamini, basi nchi za Magharibi zinaweza kuhisi tayari kuongeza uungaji mkono wake wa kijeshi kwa Kyiv bila kujali vitisho vya Moscow.

    Iwapo anamaanisha anachokisema kuna hatari, kama inavyosemwa mara kwa mara na Moscow pamoja na Washington, kwamba mzozo unaweza kugeuka kuwa Vita vya Tatu vya Dunia.

    Katika matukio ya hivi punde ya ishara za onyo, Putin Jumatano aliongeza orodha ya matukio ambayo yanaweza kusababisha Urusi kutumia silaha za nyuklia.

    Inaweza kufanya hivyo, alisema, kujibu shambulio kuu la kawaida la kuvuka mpaka lililohusisha ndege, makombora au ndege zisizo na rubani.

  7. Shambulizi la Israel lawauwa wanajeshi 5 katika mpaka wa Syria na Lebanon

    f

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Wapiganaji wa Hezbollah wakionyesha baadhi ya silaha zao kwa vyombo vya habari

    Wizara ya ulinzi ya Syria imesema katika taarifa yake kwamba wanajeshi watano wameuawa na wengine sita kujeruhiwa kufuatia shambulio lililotekelezwa na Israel.

    Taarifa hiyo inaongeza kuwa shambulio hilo lililotokea mapema asubuhi, lililengwa katika moja ya maeneo yao ya kijeshi katika mpaka wa Syria na Lebanon katika eneo la mashambani la Damascus.

    Shambuli hili linadhaniwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa Israel kukata kuzuia usambazaji wa silaha za Iran zinazotolewa kwa Hezbollah kupitia Syria.

    Mapema wiki hii kamanda wa Jeshi la anga la Israel, Meja Jenerali Tomer Bar, alisema ingawa Israel imeharibu vibaya uwezo wa kijeshi wa Hezbollah, sasa inahitaji kusimamisha uwezo wa Hezbollah wa kuimarika tena. mfumo wa usamabazaji wa silaha kupitia Syria ni muhimu kwa hilo.

    "Nchini Lebanon tutazuia uwezekano wowote wa upelekaji wa silaha nchini Lebanon kutoka Iran," aliuambia mkutano wa maafisa siku ya Alhamisi.

    Hezbollah inapata msaada mkubwa wa kijeshi na kifedha kutoka Iran na ni mshirika wa rais wa Syria Bashar al-Assad.

    Unaweza pia kusoma:

  8. Ukraine yasema ndege zisizo na rubani 24 za Urusi zimedunguliwa huku moja ikiingia Romania

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Urusi imeishambulia Ukraine kwa ndege 32 zisizo na rubani aina ya Shahed, pamoja na makombora mawili ya Kh-22 na kombora moja la balistiki la Iskander-M, jeshi la anga la Ukraine liliripoti.

    Kulingana na ripoti ya asubuhi, ndege 24 kati ya 32 za kamikaze zilidunguliwa.

    Jeshi la anga linasema ndege moja isiyo na rubani iliingia kwenye anga ya Romania na nyingine "ilitoweka ndani."

    Romania imekiri ukiukaji wa anga lake wa ndege ya Urusi isiyo na rubani.

    Ndege isiyo na rubani ya Urusi huenda ilikiuka anga ya Romania kwa "kipindi kifupi sana", "chini ya dakika tatu" Ijumaa usiku wakati wa shambulio dhidi ya nchi jirani ya Ukraine, wizara ya ulinzi ya Romania ilisema.

    Kufuatia shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye mji wa Izmail katika mkoa wa Odessa, ulio kwenye mpaka na Romania kwenye wa Danube, watu watatu waliuawa na 14 walijeruhiwa, ofisi ya mwendesha mashtaka wa mkoa wa Odessa ilisema Ijumaa. Jeshi la Urusi halikutoa maoni yoyote juu ya data hizi.

    "Mfumo wa rada wa Romania umebainisha uwezekano kwamba moja ya ndege zisizo na rubani zilizohusika katika shambulio la Ukraine zilivuka anga ya Romania kwa muda mfupi sana - chini ya dakika tatu - katika eneo la mpaka," wizara ya ulinzi ya Romania ilisema katika tangazo lake.

    Romania (mwanachama wa NATO) ilichukua ndege zake mbili za kivita za F-16, pamoja na ndege mbili za Uhispania F-18, ambazo zinafanya kazi ya kushika doria katika anga ya nchi hiyo. Wakaazi wa kaunti ya kusin mashariki ya Romania ya Tulcea walitahadharishwa kuchukua kutafuta hifadhi kufuatia tukio hilo, shirika la habari la Reuters linasema.

    Mamlaka katika eneo la Odessa hapo awali ziliripoti shambulio la ndege isiyo na rubani kwenye mji wa Izmail, ulioko kwenye mpaka na Romania karibu nae neo la Danube, ambalo liliwauwa raia watatu na kujeruhi wengine 12.

    Jeshi la Urusi halijatoa kauli yoyote kuhusu shambulio jipya la ndege zisizo na rubani dhidi ya Ukraine.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi

  9. IDF yadai kuwaua viongozi wengine wakuu zaidi wa Hezbollah katika shambulizi lililopita

    Jeshi la Israel linasema kuwa viongozi wakuu waandamizi wa Hezbollah waliuawa wakati wa mashambulizi katika eneo la Beirut siku ya Jumanne.

    Katika operesheni waliyoiita "Mishale ya Kaskazini" IDF hapo awali ilisema ilimuua mkuu wa makombora na Kikosi cha Roketi cha Hezbollah - Ibrahim Muhammad Qabisi.

    Katika taarifa zake za hivi punde jeshi la Israel linasema wakuu wengine wa kundi hilo waliuawa , akiwemo naibu wa Qabisi.

    Wakati hayo yakijiri aubuhi ya leo zimeshuhudiwa picha zinazoonyesha makombora juu ya Haifa yakizuiwa.

    Mfumo wa kupambana na makombora wa Iron Dome wa Israel ulikatiza safari za makombora juu ya Haifa, yaliyofyatuliwa kutoka Lebanon.

    IDF inasema baadhi ya roketi zimeanguka katika maeneo ya wazi.

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    f

    Chanzo cha picha, Reuters

    Reuters

    Chanzo cha picha, Reuters

    Unaweza pia kusoma:

  10. Shambulizi laua wanafamilia tisa nchini Lebanon - ripoti

    Shirika la habari la Reuters linaripoti kwamba shambulizi la usiku kucha la Israel limeua watu tisa, wakiwemo watoto wanne, wa familia moja.

    Wakimnukuu Meya Mohammad Saab, Reuters inasema shambulizi hilo lilifanyika katika mji wa Shebaa kusini mwa Lebanon.

    Hezbollah inasema ilirusha makombora hadi Tiberias na Haifa

    Hezbollah imedai hivi punde kwamba ilishambulia maeneo mawili nchini Israel - Tiberias na Kiryat Ata huko Haifa.

    Hapo awali tulikufahamisha kuhusu ving'ora vinavyolia katika maeneo hayo mawili ambayo yote yanapatikana kaskazini mwa Israel.

    Kundi linaloungwa mkono na Iran linasema katika taarifa yake kwamba lililenga Tiberias "kwa wingi wa makombora".

    Soma zaidi:

  11. Mamlaka ya Lebanon yatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano mara moja

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa mambo ya nje, Abdallah Bou Habib, amezungumza katika Umoja wa Mataifa na kusema nchi yake inavumilia mzozo unaotishia uwepo wake, na kwamba ilikuwa ni muhimu kuukomesha kabla haujafikia hatua ya kutozuilika.

    Hezbollah pia imeashiria kuwa haiko tayari kurudi nyuma, na inaendelea kurusha makombora dhidi ya Israel.

    Upande mwingine, Israel imesema itaendelea kuwalenga Hezbollah huku mazungumzo yakiendelea, katika mashambulizi ambayo tayari yameua mamia ya watu kote Lebanon na kuwalazimisha makumi ya maelfu kuyahama makazi yao.

    Huku kukiwa na shinikizo kubwa hospitalini na idadi inayoongezeka ya wakazi waliokimbia makazi yao, mamlaka ya Lebanon inaomba kusitishwa kwa mapigano mara moja.

    Soma zaidi:

  12. Mazungumzo ya kusitisha mapigano yataendelea hata kama mapigano yanaendelea - Netanyahu

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Mapema leo asubuhi, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ilitoa taarifa ikitaka "kufafanua mambo machache" kuhusu kile ilichokiita "taarifa nyingi potofu kuhusu mpango wa kusitisha mapigano unaoongozwa na Marekani".

    Taarifa hiyo inaeleza kuwa Israel "iko pamoja na malengo ya mpango unaoongozwa na Marekani wa kuwawezesha watu walio kwenye mpaka wetu wa kaskazini kurejea salama kwenye makazi yao".

    Inaongeza kuwa timu zilikutana Alhamisi, na inasema majadiliano yataendelezwa katika siku zijazo.

    Kauli hiyo inafuatia washirika wakiwemo Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano katika kipindi cha siku 21 "ili kutoa nafasi kwa diplomasia kuelekea kukamilika kwa suluhu la kidiplomasia" na kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.

    Kufikia Alhamisi, pendekezo hilo lilikuwa limekataliwa na wanasiasa wa Israel akiwemo waziri wa mambo ya nje Israel Katz ambaye alisema "hakutakuwa na usitishaji mapigano kaskazini".

    Ikulu ya White House baadaye ilisema pendekezo la kusitisha mapigano "limeratibiwa" na Israel, licha ya madai ya Netanyahu.

    Jeshi la Israel lasema limenasa kombora lililorushwa kutoka Yemen

    Jeshi la Ulinzi la Israel linasema kuwa limefanikiwa kunasa kombora lililorushwa kutoka Yemen, baada ya ving'ora vya mashambulizi ya anga kusikika katikati mwa Israel.

    Makundi ya Houthi ya Yemen mara kwa mara yamekuwa yakirusha ndege zisizo na rubani na makombora kuelekea Israel tangu vita vya Gaza kuanza.

    Mengi yamenaswa, lakini mtu mmoja aliuawa mwezi Julai baada ya ndege isiyo na rubani kushambulia Tel Aviv, na kombora kutua katika eneo lisilo na watu katikati mwa Israel mapema mwezi huu.

    Waasi wa Houthi, wanaoungwa mkono na Iran, hawajatoa maoni yoyote kuhusu uvamizi wa kombora usiku wa kuamkia leo.

    Soma zaidi:

  13. Alabama yatekeleza hukumu ya kifo ya pili ya gesi ya nitrojeni Marekani

    .

    Chanzo cha picha, Alabama Department of Corrections

    Jimbo la Marekani la Alabama limetekeleza hukumu ya kifo kwa Alan Eugene Miller - Mmarekani wa pili kuwahi kuuawa kwa kuvuta gesi ya nitrojeni.

    Miller, mwenye umri wa miaka 59, alihukumiwa kifo kutokana na mauaji ya Lee Holdbrooks, Christopher Scott Yancy na Terry Lee Jarvis mnamo mwaka 1999.

    Hukumu ya kifo kwake ni ya tano nchini Marekani ndani ya kipindi cha wiki moja - matumizi makubwa zaidi ya adhabu ya kifo katika zaidi ya miongo miwili.

    Pia mnamo Alhamisi, Emmanuel Littlejohn alidungwa sindano ya sumu huko Oklahoma baada ya gavana wa jimbo hilo kukataa ombi la kuhurumiwa la dakika ya mwisho.

    Mauaji ya Miller ni ya 18 hadi sasa mwaka huu - na wengine saba wamepangwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyosalia ya 2024.

    Pia ni adhabu ya 1,600 ya kifo nchini Marekani tangu mahakama ya juu zaidi ya taifa hilo kurejesha hukumu ya kifo mnamo 1976.

  14. Trump na Zelensky kukutana huku wanachama wa Republican wakiwa na hasira

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Donald Trump amesema atakutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini New York siku ya Ijumaa.

    Mgombea huyo wa urais wa chama cha Republican aliambia mkutano wa wanahabari kwamba wawili hao watakutana mwendo wa 09:45 ET (14:45 BST) katika jengo la Trump Tower.

    Mkutano huo unatazamiwa kuendelea licha ya ripoti za awali kuwa ulifutwa huku kukiwa na hasira kutoka kwa wana Republican baada ya Zelensky kutembelea jimbo muhimu la Marekani la Pennsylvania.

    Siku ya Alhamisi, Zelensky alikutana na Rais wa Marekani Joe Biden na Makamu wa Rais Kamala Harris katika Ikulu ya White House kujadili "mpango wake wa ushindi", ambao anatumai utaishinikiza Urusi kukubali kumalizika kwa vita hivyo kidiplomasia.

    Soma zaidi:

  15. Naomi Campbell apigwa marufuku kuwa mdhamini wa shirika la kutoa misaada

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwanamitindo Naomi Campbell amepigwa marufuku kuwa mdhamini wa shirika moja la kutoa misaada baada ya uangalizi kugundua kuwa fedha za shirika hilo zilitumika katika hoteli za kifahari na kwa huduma za saluni.

    Uchunguzi wa Tume ya shirika hilo uligundua kuwa shughuli za maonyesho ya mitindo kwa ajili ya usaidizi hazikufanyika kwa kiasi kikubwa cha pesa kilichopatikana kama ilivyotakiwa.

    Badala yake zilitumika kwa ununuzi wa sigara na usalama wa Campbell na malipo mengine ambayo hayajaidhinishwa kwa mmoja wa wadhamini wenzake wa shirika hilo.

    "Nimegundua leo kuhusu ugunduzi huo, na nina wasiwasi mkubwa," Campbell, 54, aliliambia shirika la habari la AP.

    Aliongeza kuwa yeye sio mtu "aliyekuwa na udhibiti" wa shirika hilo la kutoa misaada.

    Ahadi za kuchangisha pesa hazijatekelezwa

    Amepigwa marufuku kujihusisha na shirika hilo kwa miaka mitano huku wadhamini wengine wawili, Bianka Hellmich na Veronica Chou, wakipigwa marufuku kwa miaka tisa na minne mtawalia.

    Wawakilishi wa mwanamitindo huyo wa Uingereza wamewasiliana na BBC.

    Uchunguzi uligundua kuwa malipo yasiyoidhinishwa ya jumla ya £ 290,000 kwa huduma za ushauri yalifanywa kwa Bi Hellmich, ambayo ilikuwa ni ukiukaji wa katiba ya shirika hilo.

    Ingawa Bi Hellmich alikuwa amependekeza kurejesha fedha hizo, wasimamizi wa muda walioteuliwa na Tume walifanikiwa kurejesha malipo kwa shirika hilo

  16. Israel yaishambulia Hezbollah kwa 'nguvu' yake yote licha ya wito wa kusitisha mapigano

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameliambia jeshi la nchi hiyo kuendelea kupigana kwa "nguvu" yake yote dhidi ya kundi lenye silaha la Hezbollah, licha ya wito kutoka kwa Marekani na washirika wengine wa kusitisha mapigano.

    Wizara ya afya ya Lebanon imesema takriban watu 92 waliuawa katika mashambulizi ya anga ya Israel siku ya Alhamisi, huku mamia ya wengine wakiuawa tangu mashambulizi hayo yalipoongezeka siku ya Jumatatu.

    Hezbollah imethibitisha kuwa shambulizi la anga kwenye jengo la ghorofa kusini mwa Beirut lilimuua mkuu wa kitengo cha ndege zisizo na rubani, Mohammad Surur.

    Hofu ya kutokea kwa vita kila mahali kati ya Israel na Hezbollah imetanda, baada ya kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon tangu Jumatatu.

    Ongezeko hilo la uhasama lilisababisha jumuiya ya watu 12 - ikiwa ni pamoja na Marekani, Uingereza na EU - kupendekeza kusitishwa kwa mapigano kwa wiki tatu kati ya Israel na Hezbollah siku ya Jumatano.

    Pendekezo hilo awali lilipokelewa kwa matumaini baada ya balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon, kusema nchi yake "iko wazi kwa mazungumzo".

    Lakini kufikia Alhamisi pendekezo hilo lilikuwa limekataliwa kabisa na wanasiasa wa Israel.

    Akitua New York kwa ajili ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw Netanyahu alisema Israel "haitasitisha" shughuli zake nchini Lebanon hadi ifikie malengo yake yote, "ya muhimu miongoni mwao ni kurejea kwa wakaazi wa kaskazini salama katika makazi yao."

    Ikulu ya White House baadaye ilisema pendekezo la kusitisha mapigano "limeratibiwa" na Israel, licha ya madai ya Bw Netanyahu, saa chache baadaye, kwamba nchi yake itaendelea na mapigano.

    Soma zaidi:

  17. Bila shaka hujambo msomaji wetu, karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 27/9/2024