Putin apendekeza sheria mpya kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia

Vladimir Putin anasema Urusi itachukulia shambulio kutoka kwa taifa lisilo la nyuklia ambalo liliungwa mkono na lenye silaha za nyuklia kuwa "shambulio la pamoja", katika kile kinachoweza kuzingatiwa kuwa tishio la kutumia silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine.

Muhtasari

  • Israel inapigana kwa 'nguvu' yake yote na haijaitikia wito wa kusitisha mapigano - Ofisi ya Netanyahu
  • Israel yasema imeshambulia maeneo lengwa 75 ya Hezbollah usiku kucha
  • Vita inaweza tu kumalizika kwa kusambaratisha Hezbollah - waziri wa Israel
  • Mfungwa aliyehukumiwa kifo kwa muda mrefu zaidi duniani aachiliwa huru
  • Watu wawili wakamatwa baada ya mwanamke kufariki akiongezwa 'makalio'
  • Elon Musk hakualikwa kwenye mkutano mkuu wa uwekezaji wa Uingereza
  • Marekani na washirika wake watoa wito wa kusitishwa kwa vita mara moja kwa siku 21

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Putin apendekeza sheria mpya kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia

    Rais wa Urusi aliwahi kutishia matumizi ya silaha za nyuklia lakini pendekezo lake jipya linapanua hali hizo.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Vladimir Putin anasema Urusi itachukulia shambulio kutoka kwa taifa lisilo la nyuklia ambalo liliungwa mkono na lenye silaha za nyuklia kuwa "shambulio la pamoja", katika kile kinachoweza kuzingatiwa kuwa tishio la kutumia silaha za nyuklia katika vita vya Ukraine.

    Katika hotuba yake muhimu Jumatano usiku, rais wa Urusi alisema serikali yake inazingatia kubadilisha sheria na masharti ambayo Urusi itatumia zana zake za nyuklia.

    Ukraine ni taifa lisilo la nyuklia ambalo hupokea msaada wa kijeshi kutoka kwa Marekani na nchi nyingine zenye silaha za nyuklia.

    Maoni yake yanakuja wakati Kyiv inatafuta idhini ya kutumia makombora ya masafa marefu ya Magharibi dhidi ya maeneo ya kijeshi nchini Urusi.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesafiri kwenda Marekani wiki hii na anatazamiwa kukutana na Rais wa Marekani Joe Biden mjini Washington siku ya Alhamisi, ambapo ombi la Kyiv linatarajiwa kuwa ajenda kuu.

    Ukraine imeingia katika ardhi ya Urusi mwaka huu na inataka kulenga ngome ndani ya Urusi ambayo inasema inatuma makombora nchini Ukraine.

    Akijibu matamshi ya Putin, mkuu wa wafanyakazi wa Zelensky Andriy Yermak alisema Urusi "haina kitu kingine chochote zaidi ya ulaghai wa nyuklia wa kutisha ulimwengu".

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alielezea maoni hayo kama "ya kutowajibika kabisa" katika mahojiano ya televisheni ya MSNBC.

    Mshirika wa Urusi, China pia imetoa wito wa utulivu, huku ripoti kuwa Rais Xi Jinping amemuonya Putin dhidi ya kutumia silaha za nyuklia.

  2. Kiongozi wa vuguvugu la kujitenga Cameroon akamatwa Norway

    Lucas Ayaba Cho

    Chanzo cha picha, Ambazonian Defence Forces

    Kiongozi wa Cameroon anayetaka kujitenga amekamatwa nchini Norway kwa madai ya kuhusika katika mzozo wa silaha unaoendelea katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

    Lucas Ayaba Cho alikamatwa Jumanne kutokana na shutuma kuhusu " matamshi yake mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii", wakili wake aliiambia BBC.

    Cho ni mtu mwenye ushawishi mkubwa katika vuguvugu la Anglophone (wazungumza kiingereza) linaloshinikiza uhuru kutoka kwa Cameroon, ambapo zaidi ya watu 6,000 wameuawa na wengine karibu milioni moja kuhama makazi yao tangu mapigano yalipoanza mnamo 2016.

    Baadhi ya watu katika mikoa miwili ya nchi inayozungumza Kiingereza wanasema wanabaguliwa na watu wengi wanaozungumza Kifaransa.

    Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeshutumu wanajeshi wa serikali na wale wanaojitenga kwa mauaji, ubakaji na mateso kwa raia.

    Afisa mmoja wa Cameroon aliiambia BBC kwamba Norway na Cameroon walikuwa na makubaliano ya kiusalama, ambayo yanaweza kumfanya Cho arudishwe katika siku zijazo.

    Tangu kuzuka kwa mzozo, serikali ya Cameroon imekuwa ikizitaka nchi za kigeni zinazowakaribisha viongozi wanaotaka kujitenga kuwarejesha nyumbani ili kujibu kesi zao kuhusu jukumu lao katika ghasia zinazoendelea.

  3. Jeshi la Sudan lashambulia maeneo ya mji mkuu Khartoum

    Moshi ulionekana ukifuka Khartoum siku ya Alhamisi wakati wa mapigano hayo

    Chanzo cha picha, Reuters

    Jeshi la Sudan limefanya mashambulizi makubwa dhidi ya kundi lenye nguvu la kijeshi linalopigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, likilenga maeneo ya mji mkuu iliyopoteza mwanzoni mwa mzozo huo.

    Katika mashambulizi ya alfajiri siku ya Alhamisi, vikosi vya serikali vilishambulia kambi za Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika mji mkuu Khartoum, na Bahri kaskazini mwake.

    Sudan imetumbukia katika vita tangu jeshi na RSF lilipoanza mapambano makali ya kuwania madaraka mwezi Aprili 2023, na kusababisha kile ambacho Umoja wa Mataifa umekiita mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.

    Takribani watu 150,000 wameuawa katika mzozo huo huku zaidi ya watu milioni 10, karibu theluthi moja ya watu, wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

    Mashahidi waliripoti mashambulizi makali ya angani na mapigano makali siku ya Alhamisi wakati wanajeshi walipovuka madaraja mawili muhimu juu ya Mto Nile, ambayo yalikuwa yametenganisha maeneo yanayodhibitiwa na serikali huko Omdurman na mikoa inayodhibitiwa na RSF.

    Tangu mwanzoni mwa vita, wanamgambo wamekuwa wakidhibiti karibu mji mkuu wote.

    Unaweza kusoma;

  4. Hakuna usitishaji vita, hakuna njia rahisi kwa Israel au Hezbollah

    Mashambulizi

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kama tulivyoripoti, Benjamin Netanyahu amewaambia wanajeshi wa Israel kuendelea kupigana kwa "nguvu" nchini Lebanon.

    Na tangu lengo jipya la vita la Israel lilipowekwa wazi wiki iliyopita, kurejea nyumbani kwa zaidi ya watu 60,000 waliokimbia makazi yao kaskazini, lugha ya uongozi imezidi kuakisi mawazo ambayo lengo hilo linaweza kufikiwa tu kupitia hatua ya kijeshi ambayo imekuwa ikiongezeka.

    Kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah anasema mashambulizi dhidi ya Israel yataisha pale tu kutakapokuwa na usitishaji vita huko Gaza, jambo ambalo hawezi kuliepuka kirahisi, licha ya ongezeko kubwa la vita dhidi ya raia wa Lebanon.

    Nasrallah anadai kukaribisha matarajio ya uvamizi wa ardhini ndani ya Lebanon, akisema itakuwa fursa nzuri kwa vikosi vyake na kushindwa kwa Israel.

    Lakini pande zote mbili zinajua kuna maumivu makubwa na hatari. Hezbollah imedhoofika, huku idadi kubwa ya watu waliouawa na milipuko mikali ya vifaa vya mawasiliano wiki iliyopita ikifedhehesha kundi ambalo mara nyingi husifiwa kama jeshi lenye uwezo zaidi lisilo la serikali katika Mashariki ya Kati.

    Lakini mashambulizi ya anga ya Israel hayajatimiza malengo, huku Hezbollah wiki hii ikipeleka zaidi mashambulizi Israel.

    Licha ya taarifa kutoka kwa jeshi la Israel kuashiria uvamizi wa ardhini unaweza kukaribia, uongozi unafahamu kwamba uvamizi wa hapo awali umeshindwa kufikia malengo ya Israel, au kuiharibu Hezbollah.

  5. Video: Tazama jengo likiporomoka ndani ya mto nchini India

    Maelezo ya video, Wakati ambapo Jumba liliporomoka mtoni kufuatia mafuriko India

    Video inaonyesha jengo la orofa mbili likiporomoka kwenye mto Ganges unaofurika katika jimbo la kaskazini mwa India la Bihar.

    Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo lililotokea mapema wiki hii katika wilaya ya Bhagalpur.

    Takriban watu 10 wamefariki mjini Bihar baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mafuriko katika maeneo kadhaa ya jimbo hilo. Timu za kutoa misaada na uokoaji zimetumwa katika maeneo yaliyoathiriwa.

  6. White House 'haijavutiwa' na mapendekezo mapya ya Zelensky - WSJ

    Zelensky

    Chanzo cha picha, EPA

    Utawala wa Biden haufurahishwi na "Mpango wa Ushindi" uliopendekezwa na rais wa Ukraine, Jarida la Wall Street Journal linaripoti.

    Utawala wa Biden una wasiwasi kuwa "Mpango wa ushindi" hauna mkakati kamili, na mapendekezo yanahusu kutoa silaha zaidi na kuondoa vikwazo kwa makombora ya masafa marefu.

    "Sijavutiwa, hakuna mpya huko," mmoja wa maafisa wa utawala wa Marekani alisema. Vyanzo vya WSJ vilibainisha kuwa mapendekezo ya Zelensky hayakubaliani, na sehemu zinazohusu diplomasia na siasa hazina maelezo mengi kuliko maombi ya silaha.

    "Mpango wa Ushindi" ambao Zelensky anakusudia kuwasilisha kwa uongozi wa Marekani bado haujawekwa wazi.

    Hata hivyo, BBC imeandika hapo awali kuhusu mambo makuu ya waraka huu.

  7. Israel inapigana kwa 'nguvu' yake yote na haijaitikia wito wa kusitisha mapigano - Ofisi ya Netanyahu

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameliambia jeshi la Israel kuendelea kupigana kwa "nguvu" yake yote na halijaitikia wito wa jana usiku wa kusitisha mapigano, ofisi yake inasema.

    Kujibu pendekezo la kusitisha mapigano lililotolewa na washirika 12 wa kimataifa, ofisi ya Netanyahu inasema:

    "Taarifa kuhusu kusitisha mapigano - sio kweli. Hili ni pendekezo la Marekani na Ufaransa, ambalo hata waziri mkuu hakujibu.

    Taarifa kuhusu maagizo yanayodhaniwa ya kudhibiti mapigano upande wa kaskazini pia ni kinyume cha ukweli.

    " Waziri mkuu aliagiza IDF kuendeleza mapigano kwa nguvu yake yote, na kulingana na mipango iliyowasilishwa kwake. Pia, mapigano huko Gaza yataendelea hadi malengo yote ya vita yatimie."

    13 wauawa katika mashambulizi ya usiku kucha - Lebanon

    Wizara ya afya ya Lebanon imesema watu tisa wameuawa na wengine 11 kujeruhiwa katika shambulio la Israel la usiku kucha huko Younine kaskazini-mashariki mwa Lebanon, karibu na Baalbek.

    Mamlaka zinasema kazi inaendelea kuondoa vifusi.

    Hapo awali, wizara ilitangaza vifo vya watu wengine wanne kusini zaidi, huko Qana na Aita el Shaab.

    Soma zaidi:

  8. Israel yasema imeshambulia maeneo lengwa 75 ya Hezbollah usiku kucha

    Katika taarifa mpya, Jeshi la Ulinzi la Israel linasema limeshambulia takriban maeneo lengwa 75 ya Hezbollah kwa usiku mmoja.

    Inasema mashambulizi hayo yalitokea eneo la Bekaa, karibu na mpaka wa Syria, na kusini mwa Lebanon, na kulenga maghala ya silaha, vifaa vya kurushia roketi, majengo ya kijeshi na miundombinu.

    Moshi waongezeka kusini mwa Lebanon baada ya mashambulizi ya Israel

    Wakati huo huo, moshi unaendelea kuongezeka wakati jeshi la Israel linadai kufanya kile inachokiita "kusambaratisha na kuharibu uwezo wa Hezbollah na miundombinu ya kigaidi".

    Picha hizi mpya zinaonyesha moshi ukifuka eneo la juu kusini mwa Lebanon, baada ya mashambulio ya Israeli.

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Pia unaweza kusoma:

  9. Vita inaweza tu kumalizika kwa kusambaratisha Hezbollah - waziri wa Israel

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Kiongozi wa upinzani wa Israel Yair Lapid anasema Israel "inapaswa kukubali pendekezo la kusitisha mapigano la Biden-Macron, lakini kwa siku 7 pekee".

    Mtazamo huo hauungwi mkono na Bezalel Smotrich, waziri wa fedha wa mrengo mkali wa kulia katika serikali ya Benjamin Netanyahu.

    Anasema Hezbollah "isipewe muda wa kujikwamua", na kwamba njia pekee ya kuwarudisha wakaazi waliokimbia makazi yao kaskazini mwa Israel ni "kujisalimisha kwa Hezbollah - au vita".

    Anasema kampeni ya Israel "inapaswa kuisha katika hali moja tu - kusambaratisha Hezbollah na kumaliza uwezo wake wa kuwadhuru wakazi wa kaskazini".

    Soma zaidi:

  10. Mfungwa aliyehukumiwa kifo kwa muda mrefu zaidi duniani aachiliwa huru

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mzee wa miaka 88 ambaye ndiye mfungwa aliyehukumiwa kifo kwa muda mrefu zaidi duniani ameachiliwa huru na mahakama ya Japan.

    Iwao Hakamada, ambaye amekuwa akisubiri kunyongwa kwa zaidi ya nusu karne, alipatikana na hatia mwaka wa 1968 kwa kumuua bosi wake, mkewe na watoto wao wawili vijana.

    Hivi majuzi alikubaliwa kesi yake kusikilizwa tena huku kukiwa na tuhuma kwamba wachunguzi wanaweza kuwa walimsingizia ushahidi uliosababisha ahukumiwe kwa mauaji ya watu wanne.

    Uamuzi huo unahitimisha mojawapo ya kesi ndefu na maarufu za kisheria nchini Japani.

    Mnamo mwaka wa 2014, Hakamada aliachiliwa kutoka jela na kuruhusiwa kusikilizwa tena na mahakama ya Japan, baada ya mawakili wa upande wa utetezi kuonyesha kuwa DNA kutoka kwa chembechembe za damu iliyopatikana kwenye nguo inayodaiwa kuvaliwa na muuaji haikulingana na yake.

    Tangu wakati huo amekuwa akiishi chini ya uangalizi wa dada yake, kutokana na hali yake ya akili kuwa mbaya.

    Kesi za muda mrefu za kisheria zilimaanisha kwamba ilichukua hadi mwaka jana kwa kesi hiyo kuanza tena - na hadi Alhamisi asubuhi kwa mahakama kutangaza kama Hakamada atafutiwa mashtaka, au atanyongwa.

    Hakamada ni mfungwa wa tano tu katika hukumu ya kifo kupewa fursa ya kesi kusikilizwa upya katika historia ya baada ya vita nchini humo.

  11. Watu wawili wakamatwa baada ya mwanamke kufariki akiongezwa 'makalio'

    .

    Chanzo cha picha, Family handout

    Watu wawili wametiwa mbaroni kufuatia kifo cha mwanamke anayesadikiwa kufanyiwa urekebishaji wa kuongeza makalio usiohusisha upasuaji.

    Alice Webb, 33, alifariki katika Hospitali ya Gloucestershire asubuhi ya Jumanne, baada ya kuanza kuhisi vibaya.

    Polisi wa Gloucestershire walisema walipigiwa simu na huduma ya ambulensi saa 11:35 za eneo siku ya Jumatatu, na uchunguzi - unaoongozwa na Timu Kuu ya Upelelezi wa Uhalifu - unaendelea.

    Watu hao wawili waliokuwa wamekamatwa kwa tuhuma za kuua bila kukusudia, wameachiliwa kwa dhamana ya polisi.

    Save Face, sajili ya kitaifa ya wahudumu wa afya walioidhinishwa ambao hutoa matibabu ya vipodozi yasiyo ya upasuaji ilisema hiki ni "kisa cha kwanza cha kifo kilichoripotiwa cha urekebishaji umbo kwa njia isiyo ya upasuaji nchini Uingereza".

    Matibabu yameratibiwa ili kufanya makalio kuwa makubwa zaidi, mviringo zaidi au kuinuliwa na kuwekwa mafuta au matibabu maalum ambayo mtu hudungwa kwenye makalio ili kubadilisha ukubwa au umbo.

    Wakati urekebishaji umbo usio wa upasuaji sio kinyume cha sheria nchini Uingereza, mwaka jana Halmashauri ya Jiji la Wolverhampton ilizuia kampuni kutekeleza utaratibu huo baada ya kubaini hatari zinazohusiana na michakato yao, ikiwa ni pamoja na kuganda kwa damu, magonjwa ya bakteria, na uwezekano wa tishu za mwili kuacha kufanya kazi.

    Mamlaka tano za mitaa huko Essex na Glasgow zilifuata mkondo huo na zimepiga marufuku kampuni fulani kutekeleza mchakato wa urekebishaji umbo kwa njia isiyo ya upasuaji katika eneo lao.

    Soma zaidi:

  12. Elon Musk hakualikwa kwenye mkutano mkuu wa uwekezaji wa Uingereza

    ,

    Mtu tajiri zaidi duniani, Elon Musk, hajaalikwa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa serikali ya Uingereza ikiwa ni hatua ya kujibu ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii wakati wa ghasia za mwezi uliopita, kulingana na uwelewa wa BBC.

    Ghasia zilienea kote Uingereza baada ya shambulio la kisu huko Southport, ambapo watoto watatu waliokuwa wakihudhuria darasa la kucheza densi waliuawa.

    Mjasiriamali huyo wa teknolojia aliweka kwenye mtandao wa X, ambao zamani ulijulikana kama Twitter, ujumbe akitabiri vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Uingereza na kumshambulia mara kwa mara waziri mkuu.

    Mkutano wa kilele mwezi Oktoba ni wakati muhimu ambapo Waziri Mkuu Keir Starmer anatumai kuvutia makumi ya mabilioni ya fedha kwa ajili ya biashara kutoka kwa wawekezaji wakubwa duniani.

    Bw Musk alihudhuria hafla ya mwaka jana na kuchukua jukumu muhimu katika mkutano wa akili mnemba - AI wa Novemba, ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya kusisimua ya pembeni na Waziri Mkuu wa wakati huo Rishi Sunak.

    Serikali na Bw Musk wametafutwa ili kutoa maoni yao.

    Wakati wa ghasia za Agosti, Bw Musk alishirikisha, na baadaye kufuta maoni yake kuhusu fikra za njama ya Uingereza kujenga "kambi za kizuizini" katika Visiwa vya Falkland kwa ajili ya waasi, kwenye mtandao wa X - jukwaa analomiliki.

    Wakati huo mawaziri walisema maoni yake "hayana msingi wowote" na ni "ya kusikitisha sana."

    BBC inafahamu kuwa hii ndiyo sababu hajaalikwa kuungana na mamia ya wawekezaji wakubwa duniani katika hafla hiyo ya tarehe 14 Oktoba.

    Soma zaidi:

  13. Marekani na washirika wake watoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika mpaka wa Lebanon na Israel

    .

    Washirika wakiwemo Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya wametoa wito wa kusitishwa mapigano kwa muda nchini Lebanon, kufuatia kuongezeka kwa mapigano kati ya Israel na Hezbollah.

    Umoja huo wenye wanachama 12 ulipendekeza kusitishwa kwa vita mara moja kwa siku 21 "ili kutoa fursa kwa diplomasia kuelekea kukamilika kwa suluhu la kidiplomasia" na kusitishwa kwa mapigano huko Gaza.

    Katika taarifa ya pamoja, walisema uhasama huo "hauvumiliki" na unaleta "hatari isiyokubalika" ya kuongezeka zaidi kwa vita hadi maeneo mengine ya ukanda" ambayo hayako kwa maslahi ya watu wa Israel au Lebanon.

    Hili linawadia baada ya mkuu wa jeshi la Israel kuwaambia wanajeshi kwamba mashambulizi makubwa ya anga nchini Lebanon yakilenga Hezbollah yanaweza kuwafungulia njia ya "kuingia katika eneo la adui".

    Matamshi ya Luteni Jenerali Halevi ni dalili ya wazi zaidi kutoka kwa kiongozi mkuu kwamba uvamizi wa ardhini huko Lebanon unaweza kuwa umekaribia.

    Taarifa hiyo ya pamoja ilitiwa saini na Marekani, Australia, Canada, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uingereza na Qatar.

    Ilifuatia mkutano wa viongozi wa dunia katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

    Walisema: "Ni wakati wa kuhitimisha suluhu ya kidiplomasia ambayo itawawezesha raia wa pande zote za mpaka kurejea makwao kwa usalama.

    "Diplomasia hata hivyo haiwezi kufanikiwa huku kukiwa na ongezeko la mzozo huu."

    Soma zaidi:

  14. ila shaka hujambo msomaji wetu, karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 26/9/2024