Urembo: Mwanadada avimba mdomo baada ya kudungwa sindano ya kuibadilisha muonekano

.

Chanzo cha picha, SHAUN WHITMORE/BBC

Maelezo ya picha, Harriet Green anasema alikuwa na uchungu mwingi zaidi na aibu baada ya kudungwa sindano ya kuongeza midomo

Wakati Harriet Green alipoondoka kwenye saluni baada ya kudungwa sindano ya kubana mdomo, alihakikishiwa kwamba uvimbe wa ziada uliojitokeza utaisha baada ya siku chache, lakini miezi mitatu baadaye midomo yake ilikuwa bado imevimba kweli kweli.

Midomo yake ilikuwa imevimba kiasi cha kushindwa hata kuufunga mdomo wake vizuri.

Harriet, 22, kutoka Uingereza, aliambiwa na madaktari kwamba sasa alihitaji taratibu tatu tofauti za kurejesha midomo yake, iliyogharimu zaidi ya £700 kwa jumla.

"Midomo yangu ilikuwa mibaya sana kiasi kwamba sikuweza hata kufunga mdomo wangu kwa sababu nilikuwa na uvimbe mgumu kwenye midomo yangu," anasema.

Harriet, ambaye anafanya kazi kama mdhibiti simu kwa wateja, hakuwahi kufanyiwa upasuaji wa urembo kabla ya kudungwa sindano ya kufanya midomo yake kuwa mikubwa mnamo mwezi Desemba.

Jukumu la washawishi wa Instagram na TikTok

Baada ya kuona watu wenye ushawishi katika mitandao ya kijamii wakizungumzia na kushawishi watu juu ya kupata sindano za kujaza mashavu, kuzuia makunyanzi na kufanya midomo kuwa na nyamanyama kwenye Instagram na TikTok, Harriet aliamua kuifanya midomo yake ivutie kwa matumaini kwamba hisia hasi kuhusu midomo yake itafika mwisho'

"Kwa ubora na ukubwa wa kizazi chetu kwenye mitandao ya kijamii siku hizi, nilidhani pia mimi ningeweza kufanya hivyo," anasema.

'Kuna shinikizo kubwa kuhusu hilo na tumesikia mambo mengi, inaonekana kama jambo la kawaida kufanya.'

Lakini Harriet sasa anatambua kuwa huko ni 'uwanja hatari na kwamba picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii 'hazionyeshi ukweli wakati wote.'

'Madhara yake yanaweza kuwa mabaya. Huwezi kupata matokeo unayotaka kila wakati. Bado sijihisi salama ninapotabasamu kama ilivyokuwa hapo awali.'

.

Chanzo cha picha, HARRIET GREEN

Maelezo ya picha, Midomo ya Harriet ilikuwa imevimba

'Tatizo ni kubwa kuliko kubwa'

Matibabu ya awali yaligharimu £165 lakini kufikia sasa Harriet amemlipa Dk Saba Raja, ambaye anaendesha kliniki yake ya urembo huko Norwich, zaidi ya £700 kurekebisha midomo yake.

Dk. Raja analazimika kufanyiwa matibabu kadhaa ili kuponya midomo ya Harriet.

"Kila mwezi mimi hujibu maswali kutoka kwa wasichana wadogo ambao wameenda kwa ajili ya kuongezasehemu ya chini ya macho au kuongeza ukubwa wa midomo na sasa wana matatizo," anasema.

Dk Raja anaelezea tasnia hiyo kama pori lenye giza, huku watu wanaowadunga sindano wakiwa 'wamekaa kwenye magari yao' na 'jikoni'.

Alisema, 'Sindano za kuzuia makunyanzi zinaweza kupatikana tu kwa agizo la daktari, lakini mtu yeyote anaweza kununua na kumdunga mtu.

Viongeza ngozi ya (midomo na uso) vinaweza kununuliwa kutoka kwa tovuti au mahali pengine na mtu yeyote ambaye amefanya kozi ya siku moja.'

.

Chanzo cha picha, SHAUN WHITMORE/BBC

Maelezo ya picha, Dk. Saba Raja anashinikiza kuwepo kwa kanuni zaidi na viwango vya mafunzo kwa sekta hii

"Wadaktari wengi wasio wa matibabu wananunua dawa za bei rahisi mtandaoni, hawajui zinatoka wapi na ubora wake uko vipi," anasema.

Tunahitaji kanuni kali na viwango vya juu vya mafunzo.

'Uchunguzi wa kila mwaka wa Chuo cha Uingereza cha Dawa za Urembo uligundua kuwa asilimia 82 ya wanachama wake 400 walikuwa wamewatibu watu ambao walikuwa na matatizo kutoka kwa mtu mwingine asiye daktari katika mwaka uliopita.

Utafiti huo uligundua kuwa takriban kesi 2,000, au asilimia 59 ya kesi hizo, zilitokana na urembo.

'Hatari ya upofu wa kudumu'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Dawa za kudungwa sindano ili kurekebisha maumbo zinashababisha matatizo zaidi.

Mnamo 2021, mmoja kati ya watu watano waliofanya urekebishaji wa maumbo vilikumbwa na matatizo.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa 'hii inathibitisha jinsi dawa zinazotumika kurekebisha maumbo kwenye ngozi ya mwanadamu zinaweza kuwa katika mikono hatari.'

Dk Tamara Griffiths wa Muungano wa Madaktari wa Ngozi wa Uingereza anaamini kuwa tatizo kubwa ni dawa za ujazo wa ngozi kwa sababu 'mtu yeyote anaweza kujidunga' na ni 'hatari kubwa' kuliko taratibu nyingine za urembo.

Alisema kuwa 'upofu wa kudumu ni moja ya hatari zinazowezekana kutokea.

Ingawa hii hutokea mara chache. Lakini kuna mfano nchini Uingereza.'

Pia husababisha kuziba kwa mishipa ya damu.

Aliongeza kuwa madaktari wa ngozi wamekuwa na wasiwasi kwa muda mrefu kuhusu "sekta hii isiyodhibitiwa na ambayo inaweza kuwa hatari sana".

'Kuna kundi la watu ambao wako kwenye Instagram siku moja wanadunga watu sindano, siku ya pili wametoweka wakitoa madai ya uwongo ya umahiri wao.'

Utafiti kabla hujafanyiwa upasuaji au kuongeza ukubwa wa viungo vya mwili

.

Chanzo cha picha, DR TAMARA GRIFFITHS

Maelezo ya picha, Dk Tamara Griffiths wa Jumuiya ya Madaktari wa Ngozi ya Uingereza

Anaongeza kuwa wale wanaotaka marekebisho ya viungo vya mwili kwa ajili ya urembo bila kufanyiwa upasuaji au kupitia taratibu husika, wafanye utafiti kwanza wao wenyewe na kwenda kwa kampuni iliyosajiliwa au mtu anayetambulika na aliye katika taasisi ya kitaaluma.

Mapema mwaka huu, serikali ilikataa mwito wa wabunge wa kuunda mpango wa lazima wa kutoa leseni ili kudhibiti taratibu za urembo zisizo za upasuaji nchini Uingereza.

Idara ya Afya na Utunzaji wa Jamii inasema bado inafanyia kazi mpango ambao utafanya kuwa kosa kutekeleza baadhi ya taratibu zisizo za upasuaji bila leseni.

.

Chanzo cha picha, SHAUN WHITMORE/BBC

Maelezo ya picha, Dr. Raja akiitibu midomo ya Harriet

Msemaji alisema: "Mtu yeyote anayezingatia kufanya marekebisho ya umbo bila kufanyiwa upasuaji wa urembo anapaswa kufikiria juu ya athari inayoweza kutokea kwa afya yake ya mwili na kiakili na, ikiwa ataamua kuendelea nayo.

Wakati wa kuamua, chukua muda kutafuta daktari anayeheshimika, aliyehitimu.'

Mpango huo unawadia kuchelewa sana kwa Harriet lakini baada ya taratibu tatu hatimaye anafurahishwa na midomo yake na anajaribu kurejesha imani yake tena.

Anatumai uzoefu wake utawaelimisha wanawake wengine na kuchukua tahadhari.

'Ikiwa unataka kuongeza midomo au kitu kingine chochote, fanya utafiti wako kwanza na usifanye tu kwa kuona picha kwenye mitandao ya kijamii, kwa sababu hakuna ukweli wa picha hizo.