Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lalaani kushambuliwa kwa Padri Kitima

TEC imelitaka jeshi la polisi na vyombo vingine kuchukua hatua za haraka kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Mwanamke Uingereza abainika kufungwa kimakosa katika hospitali ya magonjwa ya akili kwa zaidi ya miaka 40

    h

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Akiwa bado msichana mwenye usonji na matatizo ya kujifunza,Kasibba alilazwa kimakosa katika hospitali ya magonjwa ya akili nchini Uingereza kwa miaka mingi, wizara ya afya imesema. Alichukuliwa akiwa na umri wa miaka 7, na sasa ana umri wa miaka 50.

    Mwanamke huyo, ambaye anatoka Sierra Leone alipewa jina la Kasibba na mamlaka kwa usalama wake, pia alilazimika kukaa miaka 25 katika kifungo cha upweke.

    Kasibba ambaye alipelekwa katika kituo cha afya akiwa na umri wa miaka 7 alipoteza uwezo wa kuongea, na hapakuwa na familia ya kumsaidia kujadili hali yake ya kiafya.

    Mwanasaikolojia mmoja alisema ilichukua miaka tisa kumuondoa katika mazingira hayo.

    Wizara ya afya ya Uingereza imeambia BBC kwamba hali ya watu wengi wenye ulemavu ambao bado wako katika hospitali za magonjwa ya akili haikubaliki, na kwamba marekebisho ya sheria za afya ya akili zitazuia tatizo hili.

    Zaidi ya watu 2,000 wenye usoni na ulemavu wa kujifunza bado wako katika hospitali za magonjwa ya akili nchini Uingereza. Inasemekana kuwa karibu 200 kati yao ni watoto.

  2. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lalaani kushambuliwa kwa Padri Kitima

    Padre Kitima

    Chanzo cha picha, TEC

    Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limeeleza kusikitishwa kwake sana na limelaani tukio baya na la uovu la kuvamiwa na kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padri Charles Kitima.

    Waraka wa Baraza hilo umesema Padri Kitima alipata majeraha makubwa na kuwa amelazwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.

    Katika waraka wake, TEC imelitaka jeshi la polisi na vyombo vingine kuchukua hatua za haraka kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

    ''Uchunguzi wa tukio hilo ufayike haraka na taarifa zitolewe kwa uwazi bila upotoshaji wowote ili kurudisha imani na matumaini kwa watu wetu''. Ilisema sehemu ya waraka huo.

    Waraka wa TEC

    Chanzo cha picha, TEC

  3. FA yapiga marufuku wanaume waliobadili jinsia kwenye soka la wanawake

    H

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Chama cha Mpira wa Miguu (FA) ni chombo kinachoongoza soka la Uingereza

    Wanaume waliobadili jinsia na kuwa wanawake hawataweza tena kucheza soka la wanawake nchini Uingereza kuanzia tarehe 1 Juni, limetangaza Shirikisho la Soka.

    Limefanyia marekebisho sheria zake tarehe 11 Aprili, na kusema ni wale tu waliozaliwa kibaolojia wanawake ndio watakaoruhusiwa kucheza.

    Mahakama ya Juu ya Uingereza tarehe 15 Aprili ilifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria mwanamke ni ile jinsia ya kibayolojia.

    "Tunaelewa kuwa hili litakuwa gumu kwa watu wanaotaka kucheza mchezo wanaoupenda kwa jinsia ambayo wanajitambulisha, na tunawasiliana na wanawake waliosajiliwa ambao walibadilisha jinsia na wanacheza sasa ili kuwaelezea juu mabadiliko hay na jinsi watakavyoweza kuendelea kuhusika katika michezo," imesema FA.

    FA ilisema siku ya Alhamisi kwamba kuna wachezaji takribani 30 waliobadili jinsia waliosajiliwa miongoni mwa mamilioni ya wachezaji wanaocheza bila malipo.

    Lakini hakuna waliobadili jinsia waliosajiliwa katika ligi za kulipwa kote Uingereza.

    FA ya Uskoti pia inatazamiwa kufuata uamuzi wa FA kwa kuwapiga marufuku waliobadili jinsia katika soka la wanawake nchini Scotland.

    Vyanzo vya habari vimeiambia BBC Sport kwamba Bodi ya Kriketi ya Uingereza na Wales (ECB) pia inatarajiwa kuwapiga marufuku waliobadili jinsia kwenye mchezo wa wanawake.

    Siku ya Alhamisi Netiboli ya Uingereza pia ilibadilisha miongozo yake kwa kuwapiga marufuku waliobadili jinsia katika michezo ya wanawake.

    Sera ya awali ya FA ilikuwa inasema wanawake waliobadili jinsia wanaweza kuendelea kushiriki katika soka la wanawake kwa kufuata vigezo fulani.

    Ikiwemo kuthibitisha kupitia rekodi za matibabu kwamba viwango vyao vya testosterone viko chini ya viwango vilivyowekwa kwa angalau miezi 12 iliyopita, na kutoa rekodi ya tiba ya homoni na mapitio ya kila mwaka ya matibabu.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Chama cha DA cha Afrika Kusini kimelaani kuondolewa kwa wanajeshi wa SADC DRC

    SADC

    Chanzo cha picha, EPA

    Chama cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini, mwanachama wa Serikali ya Umoja ambayo pia inajumuisha ANC, kimelaani namna ambavyo wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) wanajiondoa kutoka Goma.

    Ilisema kuwa M23 wanakagua vifaa vyao wanapotoka, gazeti binafsi la The Citizen liliripoti jana.

    "Habari za kutisha zinaonesha kwamba waasi wa M23, wanaoaminika kuungwa mkono na Rwanda, wanakagua zana za kijeshi za SANDF [Jeshi la Ulinzi la Kitaifa la Afrika Kusini] wakati misafara hiyo ikipita," msemaji wa ulinzi wa DA, Chris Hattingh, alisema akiongeza kuwa kikosi hicho kimelazimika kujadiliana kupita salama.

    "Wanajeshi wenye uwezo wa kukabiliana haraka na hali zinazoendelea, (QRF) kwa kawaida kusaidia vitengo washirika vinavyohitaji usaidizi.

    Wameelezea uzoefu huu kama wa kukatisha tamaa na kufedhehesha." Pia alitaja mipango mbovu na ukosefu wa uwazi katika mchakato huo.

    "Kile ambacho kilipaswa kuwa ni kuondoka kwa uratibu na kimkakati badala yake imekuwa mchakato wa kuchanganyikiwa na hatari, unaowaweka askari wetu hatarini na kuliacha taifa na maswali mengi kuliko majibu."

    Takribani wanajeshi 57 waliondoka Goma tarehe 29 Aprili wakielekea Tanzania kupitia Rwanda baada ya Sadc kufanya mazungumzo na nchi hiyo ya mwisho kwa njia salama katikati ya mwezi wa Aprili.

    Unaweza kusoma;

  5. Polisi Tanzania yachunguza tukio la kushambuliwa kwa Padri Charles Kitima

    Polisi

    Chanzo cha picha, Polisi Tanzania

    Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la kushambuliwa kwa Padri Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), ambaye alijeruhiwa kichwani usiku wa kuamkia Mei Mosi, 2025 katika eneo la maliwato ya kantini ya TEC, Kurasini.

    Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tukio hilo lilitokea majira ya saa nne na robo usiku.

    Padri Kitima alikuwa ametoka kuhudhuria kikao cha viongozi wa dini kilichodumu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni.

    Baada ya kikao hicho, aliendelea kubaki katika kantini ya Baraza kwa ajili ya kupata kinywaji, ambapo baadaye alielekea maliwatoni na ndipo alipovamiwa na kushambuliwa na watu wawili waliotumia kitu butu.

    Padri Kitima alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu na hali yake inaelezwa kuwa inaendelea vizuri. Kabla ya kuhamishiwa Aga Khan, alipatiwa huduma ya kwanza katika kituo kidogo cha afya kilichopo ndani ya eneo la TEC.

    Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja, Rauli Mahabi (maarufu kama Haraja), mkazi wa Kurasini, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa mara moja.

    Mashuhuda waliokuwepo katika eneo la tukio wameripoti kuwa Padri Kitima alionekana akizungumza na watu kadhaa kabla ya kuondoka kuelekea maliwatoni, na muda mfupi baadaye waliona watu wakikimbia eneo hilo, huku yeye akiomba msaada akiwa anatokwa damu.

    Padri Charles Kitima mbali na kuwa Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), mbali na nafasi yake ndani ya Kanisa Katoliki, Padri Kitima anajulikana kwa misimamo yae ya kukosoa na kuwa mstari wa mbele katika masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria na uwajibikaji wa kijamii.

  6. Zelensky ahimiza shinikizo zaidi kwa Urusi baada ya mashambulio ya usiku kucha

    Zelensky

    Chanzo cha picha, getty

    Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amezungumza dhidi ya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Urusi zilizotokea jana usiku.

    Anasema mji wa Odesa ulikumbwa na ndege 21 zisizo na rubani, na kusababisha "moto mwingi kuzuka" na kusababisha vifo.

    Anaongeza kuwa maeneo mengine, ikiwa ni pamoja na Kyiv na Sumy, pia yalishambuliwa. Zelensky anasema Urusi imekuwa "ikipuuza" mapendekezo ya Marekani ya kusitisha mapigano kikamilifu na bila masharti, hivyo "shinikizo la kuendelea" kwa Urusi linahitajika ili kuyaleta kwenye meza ya mazungumzo.

    Kama ukumbusho, Urusi haijatoa maoni yoyote kuhusu shambulio hilo, na gavana wake aliyewekwa rasmi huko Kherson anasema watu saba waliuawa na shambulio la Ukraine jana usiku.

    Unaweza kusoma;

  7. Marekani yazitaka India na Pakistan kupunguza hali ya wasiwasi baada ya mauaji ya Kashmir

    Askari

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Marekani imezitaka India na Pakistan kufanya kazi pamoja ili "kupunguza hali ya wasiwasi" baada ya shambulio baya la wanamgambo katika eneo la Kashmir linalotawaliwa na India wiki iliyopita kuwaua raia 26.

    Waziri wa mambo ya nje Marco Rubio alifanya mazungumzo tofauti na waziri wa mambo ya nje wa India na waziri mkuu wa Pakistan siku ya Jumatano na kuwataka "kudumisha amani na usalama katika Asia Kusini".

    India inaishutumu Pakistan kwa kuunga mkono wanamgambo baada ya shambulio la Aprili 22 kwenye eneo la karibu na mji wa mapumziko wa Pahalgam.

    Islamabad inakanusha madai hayo. Siku ya Jumatano India pia ilitangaza kufungwa kwa anga yake kwa ndege zote za Pakistani, katika msururu wa hatua za piga nikupige zilizochukuliwa na pande zote mbili.

    "Wahusika, waungaji mkono na wapangaji" wa shambulio la Pahalgam "lazima wafikishwe mbele ya sheria", Waziri wa Mambo ya Nje wa India S Jaishankar aliandika kwenye X baada ya kuzungumza na mwenzake wa Marekani kwa njia ya simu, huku Rubio akielezea masikitiko yake na kuthibitisha uungaji mkono wa Washington katika mapambano ya India dhidi ya ugaidi.

    Wakati huohuo, mwanadiplomasia mkuu wa Marekani alieleza haja ya "kulaani shambulio la kigaidi" katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif. Aliitaka Islamabad kushirikiana "katika kuchunguza shambulio hili". Wakati wa mawasiliano hayo ya simu, Sharif alikataa "majaribio ya Wahindi kuhusisha Pakistan na tukio hilo", taarifa iliyotolewa na ofisi yake ilisomeka.

    Waziri Mkuu wa Pakistani pia aliitaka Marekani "kuishinikiza India kufuta matamshi hayo na kuchukua hatua kwa uwajibikaji".

  8. Israel yashambulia "kundi lenye itikadi kali" Syria

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Israel yaishambulia "kundi lenye itikadi kali" Syria

    Israel ilisema ilifanya shambulizi nchini Syria dhidi ya "kundi lenye itikadi kali" ambalo liliwashambulia watu wa jamii ya Druze, kufuatia ahadi ya kutetea kundi hilo la walio wachache huku ghasia mbaya za kidini zikienea karibu na Damascus siku ya Jumatano.

    Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria ilikataa "aina zote za uingiliaji wa kigeni" katika masuala ya ndani ya Syria, bila kutaja Israel, na kutangaza kujitolea kwa Syria kulinda makundi yote ya Syria "ikiwa ni pamoja na madhehebu ya Druze."

    Hii ni mara ya kwanza kwa Israel kutangaza shambulio la kijeshi la kuunga mkono Druze wa Syria tangu kuondolewa madarakani kwa Bashar al-Assad, ikionyesha kutokuwa na imani kubwa na Waislam wa Kisunni waliochukua nafasi yake na kutoa changamoto zaidi kwa juhudi za Rais wa mpito Ahmed al-Sharaa za kuweka udhibiti wa taifa hilo lililotetereka.

    Chanzo cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria kililiambia shirika la habari la Reuters kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Israel yalilenga vikosi vya usalama vya serikali, na kumuua mmoja wa wanachama wao, katika mji wa Druze wa Sahnaya nje kidogo ya Damascus.

    Katika taarifa yao, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Israel Katz walisema jeshi la Israel limefanya "operesheni ya onyo na kulishambulia kundi lenye itikadi kali".

    "Wakati huo huo, ujumbe ulipitishwa kwa utawala wa Syria - Israel inatarajia kuchukua hatua ili kuzuia madhara kwa Druze," walisema.

    Tangu Assad aondolewe madarakani mwezi Disemba, Israel imeteka eneo la kusini-magharibi, na kuapa kuilinda Druze.

  9. Traore ashukuru nchi zilizoandamana kumuunga mkono

    .

    Chanzo cha picha, Captain Ibrahim Traoré/ X

    Kiongozi wa utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, ametoa shukurani zake za dhati kwa nchi zilizoandamana duniani kote jana Jumatano, akisema mshikamano huo umeimarisha imani yao kwamba mapigano wanayopigania ni kupatikana kwa ulimwengu mzuri na usawa zaidi na wenye haki.

    "Napenda kutoa shukrani zangu kwa wazalendo wote wanaopenda amani, wapenda uhuru na wapendelea Afrika wote ambao waliandamana ulimwenguni kote Jumatano Aprili 30, 2025 kuunga mkono kujitolea kwetu na maono yetu ya Burkina Faso mpya na Afrika mpya, kujiweka huru kutoka kwa mikono ya ubeberu na ukoloni," Traore aliandika katika akaunti yake ya X.

    Aliahidi kutobadilisha msimamo hata wakati anapopitia changamoto, badala yake "nitasimama kidete hadi watu wetu watakapokombolewa."

    Maelfu ya raia barani kote Afrika kote waliandamana chini ya wito wa "Hands Off the AES!" kuonyesha mshikamano wao na Burkina Faso na kiongozi wake wa kijeshi, Kapteni Ibrahim Traoré.

    Maandamano yalifanyika Burkina Faso, Ghana, na Liberia na kwengine yakiongozwa na mashirika ya mashinani.

    Waandamanaji walilaani vikali uingiliaji wa mataifa ya kigeni na kusisitiza kuunga mkono nchi hiyo dhidi ya ubeberu.

    Wimbi hili la mshikamano barani Afrika linafuatia ufichuzi wa hivi majuzi wa mamlaka ya kijeshi ya Burkina Faso kwamba ilizima "njama kubwa" ya kumpindua Traore Aprili 21.

    Serikali ya Burkina Faso ilielezea njama hiyo kama juhudi ya "kuzua machafuko" na kubadilisha utawala chini ya uongozi wa Traoré.

    "Chini ya Kapteni Traoré, Burkina Faso imekuwa ishara ya utu na ukakamavu wa Afrika," lilisema Vuguvugu la Kisoshalisti la Ghana ambalo liliandaa maandamano nchini Ghana.

    "Tunasimama na watu wa Burkina Faso ambao wanapigania kurejesha utajiri wao na mustakabali wao kutoka kwenye makucha ya ukoloni mamboleo."

    Soma zaidi:

  10. Wanajeshi wa Israel wapinga vita dhidi ya Gaza

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Katika wiki za hivi karibuni, maelfu ya askari wa akiba wa Israel - kutoka matawi yote ya jeshi - wametia saini barua wakiitaka serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kusitisha mapigano na kujikita zaidi katika kufikia makubaliano ya kuwarudisha mateka 59 waliosalia wanaoshikiliwa na Hamas.

    Miezi kumi na minane iliyopita, Waisrael wachache walitilia shaka mantiki ya vita: kuwashinda Hamas na kuwarudisha mateka.

    Kwa wengi, usitishaji vita wa Januari na kurudi kwa mateka zaidi ya 30 kuliweka matumaini kwamba vita vinaweza kuisha hivi karibuni.

    Lakini baada ya Israel kurejea vitani katikati ya mwezi Machi, matumaini hayo yalikatizwa.

    "Tulifikia hitimisho kwamba Israel inaenda mahali pabaya sana," Danny Yatom, mkuu wa zamani wa shirika la kijasusi la Mossad alisema.

    "Tunaelewa kwamba kinachomsumbua zaidi Netanyahu ni maslahi yake mwenyewe. Na katika orodha ya vipaumbele, maslahi yake na maslahi ya kuwa na serikali imara ndiyo ya kwanza, na sio mateka."

    Wengi wa wale wanaotia saini barua za hivi majuzi ni, kama Yatom, wakosoaji wa muda mrefu wa waziri mkuu. Baadhi walihusika katika maandamano ya kuipinga serikali yaliyotangulia kuzuka kwa vita tarehe 7 Oktoba 2023 kufuatia mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel.

    Lakini Yatom anasema hiyo sio sababu ya kuamua kuzungumza.

    "Nilisaini jina langu na ninashiriki maandamano si kwa sababu yoyote ya kisiasa, lakini kwa sababu ya kitaifa," alisema.

    "Nina wasiwasi sana kwamba nchi yangu itapoteza mwelekeo."

    Soma zaidi:

  11. Jeshi DRC lataka Rais wa zamani Kabila ondolewe kinga ya kisheria

    .

    Chanzo cha picha, Joseph Kabila - PR

    Mfumo wa haki za jeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, umetuma ombi rasmi kwa bunge la Seneti kuomba kuondolewa kwa kinga ya Joseph Kabila.

    Rais wa zamani, sasa ni seneta wa kudumu, anashukiwa kuwa na uhusiano na Congo River Alliance, muungano wa makundi ya waasi.

    Anashtakiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu, na kushiriki katika harakati za uchochezi.

    Mfumo wa haki za kijeshi unaangazia hadhi ya Joseph Kabila kama seneta wa kudumu kuanzisha kesi hiyo.

    Vitendo hivyo vinadaiwa kutokea baada ya muda wake wa urais. Waziri wa Sheria Constant Mutamba anasema kwamba ushahidi huo upo sasa.

    "Mfumo wa Sheria imekusanya ushahidi mwingi uliowazi na usioweza kukanushwa ambao unaonyesha wazi kuhusika kwa Seneta wa kudumu Joseph Kabila Kabange katika uhalifu wa vita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, na mauaji ya raia, raia wa kawaida na wanajeshi katika sehemu ya mashariki ya nchi kwa sasa. Tunamkaribisha kiongozi huyo wa zamani serikalini kuja na kukabiliana na mfumo wa haki wa Congo", Waziri wa Sheria wa Congo alitangaza Jumatano, Aprili 30.

    Chama cha Joseph Kabila, kilichosimamishwa na serikali, kinakanusha madai hayo.

    Kwa wiki kadhaa, imekuwa ikiyataja madai ya uwongo.

    Soma zaidi:

  12. Padri Kitima wa Tanzania avamiwa na kujeruhiwa Polisi yamshikilia mtu mmoja

    a

    Chanzo cha picha, Jambo

    Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la kushambuliwa kwa Padri Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), ambaye alijeruhiwa kichwani usiku wa kuamkia Mei Mosi, 2025 katika eneo la maliwato ya kantini ya TEC, Kurasini.

    Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, tukio hilo lilitokea majira ya saa nne na robo usiku.

    Padri Kitima alikuwa ametoka kuhudhuria kikao cha viongozi wa dini kilichodumu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja jioni. Baada ya kikao hicho, aliendelea kubaki katika kantini ya Baraza kwa ajili ya kupata kinywaji, ambapo baadaye alielekea maliwatoni na ndipo alipovamiwa na kushambuliwa na watu wawili waliotumia kitu butu.

    Padri Kitima alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya matibabu na hali yake inaelezwa kuwa inaendelea vizuri. Kabla ya kuhamishiwa Aga Khan, alipatiwa huduma ya kwanza katika kituo kidogo cha afya kilichopo ndani ya eneo la TEC.

    Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja, Rauli Mahabi (maarufu kama Haraja), mkazi wa Kurasini, kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio hilo huku uchunguzi wa kina ukiendelea ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha hatua kali zinachukuliwa mara moja.

    Mashuhuda waliokuwepo katika eneo la tukio wameripoti kuwa Padri Kitima alionekana akizungumza na watu kadhaa kabla ya kuondoka kuelekea maliwatoni, na muda mfupi baadaye waliona watu wakikimbia eneo hilo, huku yeye akiomba msaada akiwa anatokwa damu.

    Padri Charles Kitima mbali na kuwa Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), mbali na nafasi yake ndani ya Kanisa Katoliki, Padri Kitima anajulikana kwa misimamo yae ya kukosoa na kuwa mstari wa mbele katika masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria na uwajibikaji wa kijamii.

  13. Serikali ya Tanzania yakanusha ukiukwaji wa Sheria kesi ya Lissu kusikilizwa kwa mtandao

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Serikali ya Tanzania imesema hakuna sheria iliyokiukwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam ilipoamua kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kwa njia ya mtandao.

    Hayo yameelezwa Ijumaa Bungeni mjini Dodoma na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2025/26. “Ukifuatilia kilichotokea tarehe 24, Procedures (taratibu) zile zilikuwa properly lollowed (zimefuatwa inavyotakiwa), sasa huyu mtu anayetokea anayesema kuna uvunjifu wa sheria, sheria ipi sheria si ndiyo hii?,” alihoji Johari na kuongeza: “hii ndiyo sheria, na mimi ninayezungumza hapa ndiye Mwanasheria Mkuu wa Serikali.”

    Akifafanua zaidi, Johari alisema Mahakama inaweza kuendesha kesi kwa njia ya mtandao iwapo imeona kuna tishio lolote baada ya kufanya tathmini.

    “Mahakama itaassess (tathmini) mazingira yaliyopo siku hiyo na kuona kwamba tuisikilizeje shauri hili na hasa kama kuna mazingira katika mitandao zinarushwa habari za ajabu ajabu zingine ni za kutisha, kwa hiyo mahakama iki-assess (tathmini) mazingira inaweza kuamua, na ni kwa mujibu wa sheria,” alieleza.

    Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, alizungumzia suala hili kwa kusema kuwa huduma ya Mahakama Mtandao itaendelea, hasa kunapokuwepo na viashiria vya matishio ya kiusalama.

    “Kama kuna matishio, kwa mfano wenzetu walikuwa wanasema kwenye maandamano wanaenda kukinukisha na kwa sababu za kiusalama ikaonekana ni vizuri kesi ikasikilizwa kwa njia ya mahakama mtandao,” alisema Bashungwa jijini Dodoma, alipoambatana na Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), kukagua Makasha ya kisasa ya Mahakama Mtandao yanayowezesha usikilizaji wa mashauri kwa njia ya kiteknolojia katika Gereza la Isanga, Dodoma.

    Hata hivyo Maelezo haya ya Serikali yamekosolewa na baadhi ya watu, ikionekana kama kuingilia Muhimili wa Mahakama ambao umepanga kutoa maamuzi Mei 6, 2025. Mmoja wa waliokosoa kupitia mtandao wake wa X ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche.

    "Nilifikiri uamuzi wa kutumia mtandao kwenye kesi ya Lissu ni uamuzi wa Mahakama. Anachozungumza Bashungwa ni kama maamuzi hayo walifanya wao. Anasema hatuwezi kuruhusu!!! Bashungwa ni nani kwenye kesi hii?", alihoji Heche.

    Aprili 24, 2025, Lissu ambaye pia ni mwanasheria alipinga kesi yake kusikilizwa siku hiyo kwa njia ya mtandao akitaka iwe ya wazi, huku wanasheria wake wakiongozwa na Peter Kibatala wakisema utaratibu uliotumika kutaka kesi hiyo isikilizwe kwa njia ya mtandao umekiuka sheria.

    Kufuatia mabishano ya kisheria mahakamani hapo kati ya upande wa utetezi na ule wa mashitaka wakiwemo mawakili wa serikali, Mahakama ilisema itatoa uamuzi Mei 6, iwapo kesi hiyo itaendeshwa kwa njia ya mtandao ama mshitakiwa huyo ataletwa Mahakamani.

    Kabla ya kuahirishwa kwa kesi, nje ya Mahakama kulitokea mzozo kati ya Polisi na viongozi na wafuasi wa CHADEMA waliopanga kwenda kusikiliza kesi hiyo, ambapo CHADEMA kupitia kwa Katibu Mkuu wake, John Mnyika, ilidai kukamatwa kwao na karibu watu 24 walipatwa na majeraha.

    Polisi ilikiri kuwakamata baadhi ya viongozi akiwemo Makamu Mwenyekiti, John Heche na Katibu Mkuu, Mnyika.

    Kwa mara ya kwanza Lissu alifikishwa Mahakamani Aprili 10, na kusomewa mashtaka ya uchapishaji wa taarifa za uongo na uhaini katika Mahakama ya Kisutu.

    Soma zaidi:

  14. Mbunge apigwa risasi Kenya

    .

    Chanzo cha picha, BUNGE

    Mbunge mmoja nchini Kenya ameuawa kwa kupigwa risasi na mtu asiyejulikana.

    Charles Ong’ondo alikuwa ametoka bungeni muda mchache tu kabla ya kushambuliwa akiwa ndani ya gari lake kwenye barabara iiliyo na shughuli nyingi mjini Nairobi.

    Polisi wamesema gari la mbunge huyo Charles Ong'ondo liliandamwa na watu wawili waliokuwa wakiendesha pikipiki- kisha mmoja wao akasimama na kumfyatulia risasi kadhaa.

    Dereva wake alinusurika shambulio hilo.

    Marehemu ni mbunge wa chama cha mwanasiasa mkongwe Raila Odinga.

    Polisi wangali wanachunguza kisa hicho huku waliotenda uhalifu huo wakiwa bado hawajakamatwa na nia ya mauaji hayo haikubainika mara moja.

    Dereva wa gari na abiria wa kiume, ambao hawakujeruhiwa walifanikiwa kumkimbiza mbunge huyo katika Hospitali ya Nairobi, ambapo alitangazwa kuwa amefariki wakati anawasilishwa.

    Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wa polisi Muchiri Nyaga, alithibitisha kwamba mbunge huyo aliuawa kwa kupigwa risasi Jumatano jioni kando ya Barabara ya Ngong karibu na mzunguko wa chumba cha kuhifadhi maiti cha City na mtu aliyekuwa na bunduki.

    "Asili ya uhalifu huu inaonekana kuwa alilengwa na ulipangwa," msemaji wa polisi aliongezea.

    Muchiri alisema makamanda wakuu wa polisi na wapelelezi walitembelea eneo hilo kuchunguza kilichotokea.

    Huduma ya Polisi ililaani kitendo hicho cha ufyatuaji risasi na kukitaja kama "uhalifu mbaya na usio na maana" na kuhakikishia umma kwamba hakuna kitakachozuia uchunguzi.

  15. Video : Tazama Donald Trump akisema ‘anataka kuwa papa’

    Maelezo ya video, Tazama: Trump afanya mzaha kwamba 'angependelea kuwa papa'

    Rais wa Marekani Donald Trump amefanya mzaha kwamba 'angependelea kuwa papa ajaye' wakati alipoulizwa na maripota ni nani ambaye angependelea kuwa kiongozi mpya wa kanisa Katoliki.

    Rais huyo wa Marekani alisema hana pendekezo lolote lakini akaunga mkono kadinali wa Marekani anayetoka mjini New York kuwa chaguo lake kwa wadhfa huo.

    Kufuatia kifo cha Papa Francis Jumatatu ya Pasaka, mchakato wa kumchagua Papa mpya utaanza tarehe 7 mwezi Mei.

    Pia unaweza kusoma:

  16. Marekani imesaini mkataba wa kupata madini ya Ukraine

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Marekani imetia saini mkataba na Ukraine wa pamoja wa rasilimali zake za nishati na madini, baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo yenye mvutano.

    Nchi hizo mbili zimekubaliana kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa ujenzi ili kuchochea ufufuaji wa uchumi wa Ukraine kutokana na vita vyake na Urusi.

    Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema ilionyesha pande zote mbili zimejitolea kudumisha amani na ustawi wa kudumu nchini Ukraine.

    Kwa Kyiv, mpango huo unaonekana kuwa muhimu katika kupata msaada wa kijeshi wa Marekani.

    Ukraine inaaminika kuwa na akiba kubwa ya madini muhimu kama grafiti, titanium na lithiamu. Uhitaji wa madini hayo ni mkubwa kwa sababu ya matumizi yake katika nishati mbadala, kijeshi na miundombinu ya viwanda.

    Makubaliano hayo yanakuja huku kukiwa na vita vya kibiashara vya Marekani na China.

    Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Wizara ya Fedha ya Marekani Jumatano alasiri, Mfuko mpya wa Uwekezaji wa Ujenzi mpya wa Marekani-Ukraine unatambua "msaada mkubwa wa kifedha na nyenzo" ambao Marekani imeipa Ukraine tangu Urusi ilipovamia Februari 2022.

    Waziri wa Fedha wa Marekani alisema katika taarifa yake ya video kwamba mpango huo utasaidia "kufungua ukuaji wa Ukraine".

    Taarifa hizo zinaonyesha mshikamano zaidi na Ukraine kuliko ilivyo kawaida katika utawala wa Trump.

    Inarejelea "uvamizi kamili wa Urusi" na inaongeza kuwa "hakuna serikali au mtu ambaye alifadhili au kusambaza silaha kwa Urusi ataruhusiwa kufaidika na ujenzi mpya wa Ukraine".

    Urusi bado haijajibu makubaliano hayo.

    Soma zaidi:

  17. Hujambo msomaji wetu, karibu katika matangazo ya moja kwa moja ikiwa ni tarehe 1/05/2025