Mwanadiplomasia
wa ngazi ya juu wa Umoja Wa Ulaya (EU) ameyaita madai ya Moscow kwamba Ukraine ilishambulia
majengo ya serikali ya Urusi kuwa ni "jaribio la
makusudi" la kuvuruga mchakato wa amani.
Kauli ya
Kaja Kallas kwenye mitandao ya kijamii ni kujibu madai ya Kremlin kwamba
Ukraine ilijaribu kushambulia moja ya makazi ya Vladimir Putin kwa kutumia
ndege zisizo na rubani.
"Hakuna
mtu anayepaswa kukubali madai yasiyo na msingi kutoka kwa mchokozi ambaye ameshambulia
ovyo miundombinu na raia wa Ukraine," Kallas aliandika kwenye mitandao ya
kijamii.
Mapema wiki
hii Moscow iliishutumu Ukraine kwa kuilenga nyumba binafsi ya Putin kwenye
Ziwa Valdai kaskazini-magharibi mwa Urusi.
Urusi imesema
itapitia upya msimamo wake katika mazungumzo ya amani yanayoendelea kutokana na
hilo.
Tangu Waziri
wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov alipotoa madai hayo kwa mara ya kwanza, vyombo
vya habari vya serikali ya Urusi na wanasiasa wamelijadili shambulio hilo kwa sauti
za uchochezi.
Andrei
Kartapolov, mkuu wa kamati ya ulinzi ya bunge la Urusi, amesema, “bada ya kile
ambacho [Ukraine] imekifanya, "hakutokuwepo kwa msamaha."
Ingawa
Kremlin awali ilisema haioni umuhimu wa kutoa ushahidi wa shambulio hilo,
lakini siku ya Jumatano jeshi la Urusi lilitoa kile ilichosema ni ushahidi wa
jaribio la shambulio hilo.
Ushahidi
unajumuisha ramani inayodaiwa kuonyesha ndege zisizo na rubani zikirushwa
kutoka maeneo ya Sumy na Chernihiv nchini Ukraine na video ya ndege isiyo na
rubani iliyoanguka kwenye msitu wenye theluji.
Mwanajeshi
aliyesimama karibu na mabaki ya ndege hiyo anadai ni ndege isiyo na rubani
ya Chaklun ya Ukraine.
BBC
haijaweza kuthibitisha video hiyo, wala kubaini mahali ilipodondoka.
Wasifu wa
ndege hiyo isiyo na rubani iliyoharibika unafanana na ndege aina ya
Chakluns zinazotengenezwa Ukraine - lakini vipande vya ndege iliyoonyeshwa
kwenye picha ni vya bei nafuu na vinapatikana kwa wingi mtandaoni, na inawiya
vigumu kuthibitisha kuwa ni kutoka jeshi la Ukraine.
Wizara ya ulinzi ya Urusi pia ilitoa video ya kile ilichosema ni mkazi alielezea kusikia kelele kama roketi wakati wa shambulio hilo.
Hata hivyo, chombo kimoja cha habari cha uchunguzi cha Urusi kilisema kimezungumza na zaidi ya wakazi kumi na wawili wa eneo linalozunguka makazi ya Putin na hakuna aliyesikia chochote kinachoweza kuonyesha kuwa ndege zisizo na rubani 91 zimeingia hapo au zimepigwa na ulinzi wa anga.
"Kama kitu hicho kingetokea, jiji lote lingekuwa likizungumzia," mtu mmoja aliambia kituo hicho.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ukraine alisema kile ambacho Urusi iliwasilisha kama ushahidi kilikuwa "cha kuchekesha." "Hawako makini hata kuhusu kutunga hadithi hiyo," Heorhii Tykhyi aliambia Reuters.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia amekanusha vikali madai hayo, akiyahusisha na mchakato unaoendelea unaoongozwa na Marekani wa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano nchini Ukraine.
Putin hajataja hadharani shambulio hilo linalodaiwa kuwa la ndege zisizo na rubani, lakini akihutubia wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine wakati wa hotuba yake ya mkesha wa mwaka mpya, alisema "tunawaamini nyinyi na ushindi wetu".