Trump alinganisha ushuru wa kimataifa na athari za soko kama ‘unywaji dawa’

Trump amepuuza kusuasua huko kwa masoko ya hisa akisema saa nyingine lazima tu unywe dawa

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Abdalla Seif Dzungu

  1. Aliko Dangote arudi kileleni mwa mtu tajiri zaidi barani Afrika - Forbes

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Aliko Dangote

    Aliko Dangote wa Nigeria anaongoza orodha hiyo kwa mwaka wa 14 mfululizo akiwa na thamani ya dola bilioni 23.9, kutoka dola bilioni 13.9 mwaka mmoja uliopita.

    Ongezeko la utairi wake linatokana na Forbes kuongeza thamani ya kiwanda chake cha kusafisha mafuta, ambacho kilifunguliwa mwaka jana nje kidogo ya Lagos baada ya kuchelewa kwa muda mrefu.

    Kulingana na jarida la forbes kiwanda hicho cha kusafishia mafuta kilitatizika kwa miaka mingi kuanza kutokana na mizozo ya udhibiti na vikwazo vingine, lakini kilianza kusafisha kiasi kidogo cha mafuta mapema 2024 na kinatarajiwa kufikia uwezo wake kamili mwezi huu. Hiyo imeruhusu Nigeria–nchi kubwa inayozalisha mafuta–kuanza kuuza bidhaa za petroli iliyosafishwa.

    "Hii ni ahueni kubwa sana," Dangote, 67, aliiambia Forbes mwezi Februari. Dangote, ambaye sasa ni mmoja wa watu 100 tajiri zaidi duniani, anaamini kwamba mradi wake wa hivi karibuni ni “hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba Afrika ina uwezo wa kusafisha mafuta yake ghafi, na hivyo kutengeneza utajiri na ufanisi kwa wakazi wake wengi.”

    Mwafrika wa pili tajiri zaidi ni tajiri wa bidhaa za anasa wa Afrika Kusini Johann Rupert, ambaye utajiri wake ulipanda kwa 39% hadi $ 14 bilioni, faida ya pili kwa ukubwa kati ya mabilionea.

    Rupert ameshikilia nafasi ya 2 tangu 2022.

    Ifuatayo ni orodha ya watu 10 matajiri Afrika.

    10. Patrice Motsepe

  2. Machifu wa Kenya waliotekwa nyara waachiliwa baada ya miezi miwili

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maafisa watano wa Kenya wameachiliwa miezi miwili baada ya kutekwa nyara na watu wanaoshukukiwa kuwa na silaha kaskazini mashariki mwa Kenya kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen.

    Watu wenye silaha wanaoaminika kuwa wa kundi la al Shabaab lenye mafungamano na al Qaeda waliwateka nyara machifu wa vijiji, ambao walikuwa maafisa wa eneo walioteuliwa na serikali, katika kaunti ya Mandera mwezi Februari karibu na mpaka wa Somalia, ambako waasi hao wanakaa.

    "Tuliamua kufanya kazi pamoja na jamii, na kufanya kazi na serikali ya kaunti ya Mandera... na mchakato huu umezaa matunda," Murkomen aliwaambia wanahabari, kulingana na kanda ya televisheni ya NTV Kenya iliyoonekana kwenye X.

    Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba al Shabaab walikuwa wamewavusha machifu hao mpaka na kuingia Somalia.

    Murkomen alisema machifu hao walikuwa mikononi mwa maafisa wa Kenya na kwamba "wangewasili nyumbani hivi karibuni," ingawa hakusema iwapo alifikiri al Shabaab walihusika na utekaji nyara huo, kama wasimamizi wa eneo hilo walivyoshuku wakati huo.

    Al Shabaab imekuwa ikipigana kwa miaka mingi nchini Somalia kuiangusha serikali kuu na kuanzisha utawala wake kwa kuzingatia tafsiri yake kali ya sheria za Kiislamu za sharia, na mara nyingi hufanya mashambulizi ya mipakani nchini Kenya.

  3. Makumi ya watu wafariki baada ya mvua kubwa kunyesha katika mji mkuu wa Congo

    .

    Chanzo cha picha, AFP

    Mvua kubwa na mafuriko imesababisha vifo vya takriban watu 33 huko Kinshasa - mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - kulingana na maafisa.

    Wakazi waliokata tamaa wanajaribu kukimbia maji ya mafuriko kwa kuogelea, au kupiga kasia hadi mahali salama kwa mitumbwi iliyotengenezwa kienyeji.

    Mji huo una wakazi milioni 17, na upo kwenye mto Congo, ambao ni mojawapo ya mito mikubwa zaidi duniani na umeenea kote nchini.

    Mafuriko ni ya kawaida - hivi karibuni mto ulifikia kiwango chake cha juu zaidi katika miongo sita.

    Sehemu za mji mkuu zinakabiliwa na mmomonyoko wa udongo na katika miaka ya hivi karibuni rais wa Congo ameonya kuwa mzozo wa mabadiliko ya tabianchi unafanya mafuriko kuwa mabaya zaidi.

    Nyumba nyingi magharibi mwa Kinshasa zilisombwa na maji kufuatia mafuriko usiku kucha kuanzia Ijumaa hadi Jumamosi.

    Takriban nusu ya wilaya 26 za jiji zimeathirika kwa jumla, kulingana na meya wa mji mkuu, ambaye anasema timu za utafutaji na uokoaji zimetumwa.

    Walioathirika zaidi ni maeneo yaliopo viungani mwa jiji hilo pamoja na baadhi ya vitongoji maskini zaidi.

    "Maji yamefikia urefu wa mita 1.5. Tumefanikiwa kujiokoa, wengine wamenasa majumbani mwetu," Christophe Bola anayeishi eneo la Ndanu aliambia shirika la habari la AFP.

    Wakaazi wengine wa eneo hilo wamewaambia waandishi wa habari kuwa wamekasirishwa na mamlaka, wakiishutumu kwa kutokuwa wepesi wa kujibu na kutotuma msaada wa kutosha.

  4. Sensa za upelelezi za nyambizi ya nyuklia zapatikana katika pwani ya Uingereza

    .

    Chanzo cha picha, UK MOD

    Sensa zilizofichwa zimegunduliwa katika maji ya Uingereza, ambapo jeshi linashuku ziliwekwa na idara ya ujasusi ya Urusi kuzichunguza nyambizi za nyuklia za Uingereza zilizobeba silaha za nyuklia.

    Sensa hizo zilizogunduliwa na jeshi la Uingereza zilionekana kuwa tishio kwa usalama wa taifa

    Waandishi wa habari wa taarifa hiyo pia walipata fursa ya kuingia katika meli inayofanya upepelezi baharini ya Royal Navy kwa jina Proteus, ambayo inafanya kazi katika maji ya Uingereza.

    Hii ni mara ya kwanza kwa raia kuruhusiwa kuingia kwenye meli hiyo ya siri, ambayo ilizinduliwa 2023, iliongeza taarifa hiyo.

    Kama gazeti hilo linavyosema, Urusi ndiyo nchi pekee yenye kundi la nyambizi maalumu kwa ajili ya vita vya baharini na ujasusi.

    Kulingana na taarifa hiyo, baadhi ya uwezo wa nyambizi hizo unavuka uwezo wa Uingereza na washirika wake wa NATO.

    Takriban nyaya 11 za intaneti zimeharibiwa katika Bahari ya Baltic katika kipindi cha miezi 15 iliyopita, zingine zikiangusha nanga na kupelekea baadhi ya watu kuzishuku meli za Urusi.

  5. Vifaa vya upelelezi vya Urusi, vyatishia usalama wa Uingereza - Times

    .

    Vyanzo vitatu katika Wizara ya Ulinzi ya Uingereza vililiambia jarida Sunday Times kwamba kabla ya uvamizi kamili wa Ukraine, kulikuwa na habari za kuaminika kwamba maboti ya kifahari yanayomilikiwa na mabilionea wa Urusi oligarchs yanaweza kuwa yalitumika katika upelelezi chini ya maji kote nchini Uingereza.

    Baadhi ya vyombo hivi vina madimbwi ya maji ambayo yanaweza kutumika kwa siri kuweka na kupata vifaa vya upelelezi na kupiga mbizi kwenye kina kirefu cha bahari.

    Kulingana na gazeti hilo mlipuko wa Nord Stream umeonyesha kuathirika kwa mfumo wa usambazaji wa nishati ya Uingereza: nchi hiyo inapokea karibu theluthi moja ya umeme wake kutoka kwa mitambo ya upepo ya pwani kupitia nyaya za chini ya maji.

    Mabomba ya mafuta na gesi, ambayo yanaweza kuzimwa kwa malipo ya chini ya maji, yanaweza pia kuwa hatarini.

    Nyaya za mtandao, ambazo maeneo yao yanajulikana, pia zipo hatarini.

    Hatahivyo, vyanzo vya Jeshi la Wanamaji vinasema kampuni za kibinafsi zinazotunza nyaya hizi zimeweka hifadhi kubwa ya nyaya hizo hali ya kwamba mfumo umejengwa kwa ustahimilivu wa kutosha kuhakikisha kuwa unajinasua kwa haraka kutoka kwa shambulio.

    Lakini kinachosumbua zaidi jeshi ni uwezo wa Urusi wa kuchora ramani, kushambulia au kuharibu nyaya za kijeshi.

    Jeshi la Wanamaji la Uingereza sasa linapendekeza mpango mpya kwa jina "Atlantic Bastion" ili kuunda magari ya angani, ardhini na chini ya maji pamoja na sensa ili kulinda maji ya Uingereza na eneo lote la Atlantiki ya Kaskazini.

    Vilevile, baadhi ya maafisa wa jeshi la wanamaji wanaamini Uingereza inahitaji kupiga hatua zaidi na kurejesha uwezo wake wa kutega mabomu ya ardhini, jambo ambalo haijafanya tangu kumalizika kwa vita baridi.

  6. Waziri wa Ulinzi wa Uingereza akutana na familia ya Agnes Wanjiru aliyeuawa Kenya

    Agnes Wanjiru alikuwa na umri wa miaka 21 alipouawa na kumwacha mtoto wa miezi mitano

    Chanzo cha picha, Rose Wanyua

    Maelezo ya picha, Agnes Wanjiru alikuwa na umri wa miaka 21 alipouawa na kumwacha mtoto wa miezi mitano

    Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healey MP, leo amekutana na familia ya Agnes Wanjiru, ambaye aliuawa kikatili huko Nanyuki, Kenya, mwaka 2012, ili kutoa rambirambi zake na kutimiza ahadi aliyotoa aliposhika wadhifa huo.

    Huu ni mkutano wa kwanza kwa Waziri wa Serikali ya Uingereza na familia ya Agnes Wanjiru.

    Waziri Healey alisema: “Ilikuwa ni heshima kubwa kukutana na familia ya Agnes Wanjiru leo. Katika miaka 13 tangu kifo chake, familia imeonyesha nguvu na uvumilivu mkubwa katika vita yao ya kudai haki''.

    Aidha ameeleza dhmira yake ya kuhakikisha kesi hii imetatuliwa huku akikiri kukutana na Rais wa Kenya William Ruto.

    “Tutazidi kutoa msaada wetu kamili kwa mamlaka za uchunguzi za Kenya, ikiwa ni pamoja na ziara za wachunguzi wa Kenya nchini Uingereza kuhoji mashahidi, na pia ziara ya maafisa wa uhalifu mkubwa kwenda Kenya'', waziri huyo alisema.

    Familia ya Agnes Wanjiru pia ilitoa tamko baada ya mkutano na Waziri Healey.

    “Kifo cha mpendwa wetu Agnes kimeleta maumivu makubwa na athari za kudumu katika familia yetu. Haikuwa tu mshtuko wa kumpoteza Agnes akiwa na umri mdogo, bali pia hali ya kutisha ambayo mwili wake ulipatikana na machungu yote ambayo familia yetu imepitia katika kutafuta haki na uwajibikaji kwa kifo chake, yaliyosababisha mateso makubwa kwa kila mmoja wetu'', familia yasema.

    Mkutano huu unajiri baada ya miaka 13 tangu Agnes auawe, na karibu miaka 6 tangu uchunguzi wa Kenya kugundua kuwa aliuawa na wanajeshi wa Uingereza, lakini bado hakuna maendeleo makubwa yaliyopatikana tangu wakati huo.

    “Tunashukuru kwa Waziri wa Ulinzi kukubali kukutana nasi, lakini tumekaa kwa miaka mingi tukiahidiwa ahadi zisizotekelezwa. Tunatumai kwamba mkutano wetu na Waziri wa Ulinzi utakuwa mwanzo wa hatua madhubuti kutoka kwa Serikali ya Uingereza na Wizara ya Ulinzi kuhakikisha kuwa kilichotokea kwa Agnes kinachunguzwa kwa kina, si tu Kenya bali pia Uingereza, na kwamba hakutatokea tena''.

    Waliohudhuria mkutano ni pamoja na Kamishna Mkuu wa Uingereza nchini Kenya, Neil Wigan, ambaye ameendelea kuhusika kikamilifu na familia ya Bi. Wanjiru.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Mlipuko wa ugonjwa wa surua waua watoto wawili Marekani

    ggg

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mtoto wa pili amefariki kutokana na ugonjwa wa Surua ambao umeenea hasa magharibi mwa Texas nchini Marekani.

    Kulingana na Naibu rais wa mfumo wa afya wa UMC, Aaron Davis ameiambia BBC kuwa Mtoto huyo hakuwa amepata chanjo ya kumkinga na ugonjwa huu na alikuwa akipokea matibabu hospitalini.

    Waziri wa Afya nchini Marekani Robert F Kennedy Jr ambaye tayari amelaumiwa kwa jinsi anavyosimamia na kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo alizuru jimbo la Texas huku idadi ya vifo ikiongezeka.

    Serikali ya jimbo hilo imeripoti visa 480 vya ugonjwa wa surua mwaka huu na mkurupuko huo unaonekana kuenea hadi majimbo jirani.

    Mtoto wa kwanza wa umri wa miaka 6 ambaye hakuwa amechanjwa dhidi ya ugonjwa huo alifariki mwezi Februari huku mwanaume ambaye pia hakuwa amechanjwa akifariki katika eneo la New Mexico mwezi Machi mwaka huu.

    Raia wa Marekani wamesisitiziwa kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua ili kujiepusha na maambukizi yanayosababisha madhara mwilini.

    Virusi vya surua hujidhihirisha kwa dalili kama joto jingi mwilini, vipele vya rangi nyekundu, kikohozi na nyingine.

    Ugonjwa huo unahusishwa pia na homa ya mapafu, ubongo kufura na kifo.

    Mwaka 2000 Marekani ilitangaza kwamba imetokomeza kabisa ugonjwa wa surua lakini visa vimeripotiwa tangu wakati huo huku wengi walioambukiza hawajapata chanjo.

  8. Kobe wa miaka 100 awashangaza wanaikolojia akijifungua watoto wanne

    Kobe mkongwe

    Chanzo cha picha, Philadelphia Zoo

    Maelezo ya picha, Kobe mkongwe

    Jozi ya kobe wakubwa wa Galapagos kutoka Santa Cruz magharibi, ambao wako hatarini kutoweka wamepata heshima ya kipekee baada yakuwa wazazi kwa mara ya kwanza katika mbuga ya Philadelphia, wakiwa na umri wa karibu miaka 100.

    Vifaranga vinne viliaguliwa kutoka kwa kobe wanaoitwa Abrazzo na Mommy, kobe wa Galapagos wa Santa Cruz Magharibi, na mbuga hiyo ilitangaza furaha isiyo na kifani kuhusu tukio hilo.

    Mommy, ambaye aliletwa kwa mbuga hiyo mwaka 1932, anashikilia rekodi ya kuwa mama mzee zaidi wa aina hii kutaga na kuagua mayai kwa mara ya kwanza.

    Hili ni tukio la kipekee katika historia ya zaidi ya miaka 150 ya mbuga hiyo.

    Vifaranga vya kobe hawa, kila kimoja kilichozaliwa na uzito wa kati ya gramu 70 na 80, sasa viko kwenye sehemu za nyuma za Nyumba ya Reptilia na Amfibia ya mbuga hiyo, ambapo wanakula na kukua kama ilivyotarajiwa.

    Tukio hili linatoa mwanga mpya katika juhudi za uhifadhi wa wanyama, hususan kwa kobe wa Galapagos wa Santa Cruz Magharibi, ambao idadi yao katika mbuga za Marekani inakadiriwa kuwa chini ya 50.

    Vifaranga hawa ni sehemu ya mpango wa uzalishaji wa Umoja wa mbuga na Akvaryum, ambao unalenga kuhakikisha uwepo wa kobe hawa kwa ajili ya uhifadhi wa kijenetiki na utofauti wa spishi katika siku zijazo.

    Katika taarifa yake, Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa mbuga, Jo-Elle Mogerman, alielezea furaha yao kwa kusherehekea hatua hii muhimu, akisema, “Hii ni hatua muhimu katika historia ya mbuga ya Philadelphia, na tunasherehekea kwa furaha kubwa kushiriki habari hii na jiji letu, eneo letu, na dunia nzima.”

    Maono ya mbuga hii ni kuona idadi ya kobe hawa ikistawi na kuwa na afya kwa miaka 100 ijayo, na kwamba vifaranga hawa watakuwa sehemu ya uhifadhi endelevu wa spishi hii ya kipekee.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Netanyahu atishia kulipiza kisasi huku Hamas ikilaumu Israel 'kuwalenga watoto katika kijiji cha Tufah'

    Afisa wa zima moto amesimama katika eneo lililoshambuliwa kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea Israel huko Ashkelon.

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Afisa wa zima moto amesimama katika eneo lililoshambuliwa kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea Israel huko Ashkelon.

    Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameagiza ‘’kulipiza kisasi’’ baada ya shambulizi la maroketi kutoka ukanda wa Gaza Jumapili.

    Taarifa hiyo ilibainisha kuwa Netanyahu alizungumza na Waziri wa Ulinzi Israel Katz kutoka kwenye ndege hiyo kuelekea Washington.

    Jeshi la Israel limesema liligundua roketi 10 zilizorushwa kutoka Ukanda wa Gaza kuelekea kusini mwa Israel, ambazo nyingi zilinaswa, huku ving'ora vya mashambulizi ya anga vikisikika huko Ashkelon na Ashdodi.

    Tishio la Netanyahu linajiri baada ya wanamgambo wa Hamas kutangaza kuwaa wamerusha makombora kutoka Gaza kuelekea Israel.

    Mtu mmoja amejeruhiwa katika mji wa Ashkelon.

    Jeshi la Israel nalo limesema limemuua mpalestina mmoja na kuwajeruhi wawili katika mji wa Turmus Ayya katika ukingo wa magharibi.

    Hayo yanajiri huku kukiwa na juhudi za kufufua mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza.

    Pia unaweza kusoma;

  10. Kuondolewa kwa misaada ya USAID kwawaweka wanawake wajawazito hatarini- UN

    Nigeria imeorodheshwa ya nne kwa kiwango cha juu zaidi cha vifo vya uzazi duniani

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Nigeria imeorodheshwa ya nne kwa kiwango cha juu zaidi cha vifo vya uzazi duniani

    Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kupunguzwa kwa bajeti za misaada kutahujumu hatua zilizokuwa zimefanikishwa za kupunguza vifo vya kina mama wakati wa kujifungua.

    Ripoti iliyotolewa na shirika la afya duniani WHO inasema vifo vitokanavyo na uja uzito na kujifungua vilikuwa vimeshuka kwa asilimia arobaini katika karne hii lakini wataalam wanahofu kuwa huenda vifo hivyo vikaongezeka tena kutokana na kusitishwa kwa misaada ya kigeni.

    Wanawake walio na uja uzito hukumbwa na changamoto nyingi hasa katika mataifa yanayokumbwa na mizozo kama Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Nigeria na Somalia.

    Mnamo mwaka 2020,WHO ilirekodi vifo elfu mia mbili sitini ikiwa ni sawa na mwanamke mmoja kufariki dunia kila baada ya dakika mbili kutokana na changamoto wakati wa kujifungua.

    Kifo cha uzazi ni kile kinachosababishwa na matatizo wakati wa ujauzito au ndani ya wiki sita baada ya mwisho wake.

    Sababu zinazoongoza ni pamoja na kutokwa na damu nyingi, maambukizi kama vile malaria, matatizo wakati wa kujifungua, na utoaji mimba usio salama.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Watu 30 wafariki kutokana na mafuriko DRC

    gg

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Watu thelathini wamefariki dunia katika mafuriko yaliyokumba Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

    Mvua kubwa iliyonyesha mwishoni mwa juma imeharibu makazi na miundo mbinu za mitaa ya mji huo.

    Mto Ndijili unaopita katika mji huo wenye wakazi karibu milioni kumi na saba, ulivunja kingo zake Ijumaa usiku na kuathiri usafiri wa magari.

    Mitaa kadhaa ya Kinshasa pia haina umeme na maji safi ya kutumia.

    zaidi ya nyumba 600 zilizozama ziko karibu na mji wa Masina, wilaya ya Abattoir, na Petro Kongo.

    Mitumbwi na boti za mwendo kasi zinatumika kuokoa watu walioathirika na kuwahamisha waathiriwa hadi eneo salama.

    "Kikao cha dharura kitafanyika ili kuamua jinsi ya kusaidia idadi ya watu," alisema Naibu Mkuu wa Polisi Blaise Kilimbalimba, kamanda wa polisi wa Kinshasa.

    Msimu wa mvua wa DRC kwa kawaida huanza Mwezi Novemba hadi Mei.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Trump alinganisha ushuru wa kimataifa na athari za soko kama ‘kula dawa’

    Trump

    Chanzo cha picha, Reuters

    Saa chache kabla ya kile ambacho wengine wanatabiri inaweza kuwa soko la kihistoria linalouzwa Jumatatu asubuhi juu ya ushuru wa Marekani, Rais Donald Trump alilinganisha sera zake - na athari – na kula dawa.

    "Sitaki chochote kishuke, lakini wakati mwingine lazima ule dawa kurekebisha kitu," Trump alisema kwa waandishi wa habari kwenye ndege ya Rais Air Force one jumapili.

    Akiendelea kugusia matozo ya ushuru ambayo amewekea mataifa mbalimbali ulimwenguni Trump ameendelea kusisitiza ajira na uwekezaji utarejea Marekani.

    "Ni nini kitatokea kwa soko, siwezi kukuambia.Lakini nchi yetu ina nguvu zaidi."Trump asema.

    Wakati huo huo, Waziri mkuu wa Japan, Shigeru Ishiba amesema serikali yake itazisaidia kampuni zilizoathirika na nyongeza mpya ya ushuru iliyotangazwa na Marekani wiki iliyopita.

    Japan ambayo ni msafirishaji mkubwa wa bidhaa zake kuelekea Marekani imesema itachukua pia hatua za kulinda ajira lakini pia itaendelea kutafuta kulegezewa masharti na Marekani.

    Hayo yakijiri, Rais Trump anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Jumatatu na wawili hao wana uwezekano wa kujadili asilimia 17 ya ushuru wa Israel waliotozwa na Trump Kwa mujibu wa gazeti la Marekani la Politico.

    Netanyahu alisema Jumapili anatarajia kutafuta afueni kutoka kwa Trump juu ya ushuru waliowekewa.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Hujambo, natumai umzima wa afya karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja.