Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Machafuko yaliyoshuhudiwa Tanzania yalichochewa kutoka nje- Waziri Mkuu

Serikali ya Tanzania, imedai kuwa maandamano yaliyosababisha maafa mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya taifa hilo, yalipangwa na kudhaminiwa na watu wenye nia mbaya na maslahi ya taifa hilo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Asha Juma & Rashid Abdallah

  1. Machafuko yaliyoshuhudiwa Tanzania yalichochewa kutoka nje- Waziri Mkuu

    Waziri mkuu wa Tanzania Dkt Mwigulu Nchemba amesema kuwa machafuko yaliyoshuhudiwa nchini humo wakati wa uchaguzi mkuu, yalichochewa kutoka nje.

    Akiongea jijini Dar es Salaam, Nchemba alisema kuwa waliopanga machafuko hayo wanadhamira ya kupora rasilimali zake.

    Serikali ya Tanzania, imedai kuwa maandamano yaliyosababisha maafa mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya taifa hilo, yalipangwa na kudhaminiwa na watu wenye nia mbaya na maslahi ya taifa hilo.

    Akiongea wakati alipofanya ziara jijini Dar es Salaam kukagua uharibifu uliosababishwa na maandamano ya tarehe 29 mwezi uliopita Nchemba amedai kuwa wale waliofadhili ghasia na machafuko hayo wana njama ya kuvuruga amani na usalama wa taifa hilo ili wapore madini yake.

    Nchemba alisema kuwa maandamano hayo yalikuwa na athari kubwa sio tu kwa miundombinu bali hata kwa maisha ya watu ambao walikufa au kujeruhiwa.

    Alisema kuwa Tume iliyoundwa na rais Samia Hassan, itasaidia kubainisha chanzo cha maandamano hayo ili suluhu la kudumu lipatikane.

    Tanzania haijatoa takwimu kuhusu idadi ya watu waliouawa au kujeruhiwa. Wakati huohuo serikali ya Tanzania imetangaza kuwa hakutakuwa na sherehe yoyote tarehe 9 mwezi ujao, na badala yake fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya sherehe hizo zitatumika katika kurekebisha miundombinu iliyoharaibiwa wakati wa maandamano hayo.

    Wafuasi wa upinzani walikuwa wamedai kuwa watafanya maandamano makubwa zaidi tarehe 9 mwezi ujao, kuendeleza shinikizo dhidi ya utawala wa sasa, licha ya idara ya polisi kuonya kuwa maandamano yoyote hayataruhusiwa.

    Unaweza kusoma;

  2. Watumiaji wa X kujulikana walipo

    Mwishoni mwa wiki hii, mtandao wa kijamii wa X umezindua kipengele kipya ambacho kinawaruhusu watumiaji kuona nchi au eneo ambalo mtumiaji wa akaunti yupo.

    Kulingana na mkuu wa masoko wa X, Nikita Bier, akaunti rasmi za serikali hazitaonyesha maeneo zilipo "ili kuzuia vitendo vya kigaidi dhidi ya viongozi wa serikali.”

    Kipengele hiki, kinachoitwa "kuhusu akaunti hii," kinaweza kuonekana katika wasifu wa mtumiaji yeyote na kubainisha nchi au eneo ambalo mara nyingi hutumia akaunti yake.

    X imefafanua kuwa taarifa kuhusu mahali akaunti inapopatikana inaweza kuathiriwa na safari, kwa hivyo huenda maelezo yasiwe sahihi na yanaweza kubadilika mara kwa mara.

    Matumizi ya mitandao ya VPN ambayo huruhusu watumiaji kubadilisha eneo wanalotumia kunaweza pia kupotosha mtu alipo.

    X itaboresha kipengele hicho leo, ambapo Bier anasema X itakuwa na usahihi wa 99%.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Watuhumiwa 104 wafutiwa mashtaka ya uhaini Tanzania

    Mahakama ya Wilaya ya Ilemela katika mkoa wa Mwanza, imewaachia huru watuhumiwa 57 na Mahakama ya hakimu Mkazi kisutu Dar es Salaam, imewaachia huru watuhumiwa 47 wa kesi ya uhaini waliokamatwa baada ya uchaguzi wa Oktoba 29.

    Hatua ya kuwaachia watuhumiwa 57 kati yao imechukuliwa baada ya upande wa mashtaka, kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, kuwasilisha ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) la kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao 57 kati ya 61 waliokuwa wanakabiliwa na tuhuma mbalimbali jijini Mwanza

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya kupitia upya mashtaka dhidi ya vijana hao, hatua iliyosababisha kuachiwa kwao.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Mhalifu wa ngono za mtandaoni ahukumiwa kifungo cha maisha jela

    Kiongozi wa kikundi cha uhalifu wa ngono katika Telegram ambacho kilisambaza maelfu ya maudhui ya unyanyasaji wa kijinsia amehukumiwa kifungo cha maisha nchini Korea Kusini.

    Kim Nok-wan, 33, alikuwa mkuu wa kundi la Vigilantes, ambalo liliwahadaa waathiriwa ambao walituma picha za utupu na kundi hilo kuzituma katika makundi mengine ya mtandaoni.

    Kati ya Mei 2020 na Januari 2025, Vigilantes iliwarubuni watu 261 - idadi kubwa zaidi ya waathiriwa wa unyanyasaji wa ngono mtandaoni katika historia ya Korea Kusini.

    Chini ya jina la "mchungaji," Kim alipatikana na hati ya kutekeleza uhalifu huo ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto wadogo na usambazaji wa picha za watoto.

    Alihukumiwa Jumatatu baada ya kukutwa na hatia kwa kupanga na kuendesha shirika la uhalifu, kuzalisha na kusambaza maudhui ya kingono na yaliyorikodiwa kinyume cha sheria, matumizi ya maudhui yaliyorikodiwa kinyume cha sheria, na ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia.

    "[Kim Nok-wan] amesema mahakamani kwamba anajuta.

    Alifanya uhalifu huo katika kipindi cha miaka minne hadi mitano iliyopita," mahakama ilisema.

    "Kwa kuzingatia ukatili wa uhalifu ni muhimu kumtenga kabisa na jamii."

    Kim alitumia wanaume na wanawake kupitia mitandao ya kijamii, akiwavuta kupitia Telegram kabla ya kuwahadaa, kulingana na polisi.

    Aliwasiliana na wanaume ambao walionyesha nia ya kuunda au kusambaza picha za uongo, na wanawake ambao walionyesha udadisi kuhusu masuala ya ngono, kisha kutishia kufichua habari zao za kibinafsi au kuziripoti kwa serikali.

    Baadhi ya waathiriwa hawa baadaye waliwekwa katika kundi lake kama viongozi.

    Kama kiongozi, Kim pia aliwabaka wanawake kumi wenye umri mdogo, akawalazimisha wanawake kufanya ngono na wanaume wengine na kujirekodi akifanya vitendo vya kikatili vilivyosababisha majeraha, polisi waliongeza.

    Kesi hiyo ni mara ya kwanza Telegram kushirikiana na polisi wa Korea Kusini, kutoa data zinazohusiana na uhalifu ambazo ziliwezesha uchunguzi zaidi na kusababisha kukamatwa kwa Kim.

    Shirika la Polisi la Kitaifa la Korea lilianzisha mfumo rasmi wa ushirikiano na Telegram Oktoba 2024, kuwezesha jukwaa hilo kutoa taarifa muhimu kwa mamlaka.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Nyota wa Bollywood, Dharmendra afariki akiwa na umri wa miaka 89

    Nyota wa Bollywood, Dharmendra amefariki dunia katika mji wa Mumbai nchini India akiwa na umri wa miaka 89.

    Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ametoa salamu za rambirambi kwa mwigizaji huyo, akisema kufa kwake "kunaashiria mwisho wa enzi ya sinema za India."

    Akijulikana zaidi kama Veeru, alionekana katika zaidi ya filamu 300, nyimbo nyingi, zilizoovutia watazamaji kwa miongo kadhaa.

    Alizaliwa tarehe 8 Desemba 1935 katika kijiji cha Nasrali katika wilaya ya Ludhiana ya Punjab, alipewa jina la Dharam Singh Deol na baba yake ambaye alikuwa ni mwalimu.

    Katika mahojiano na BBC Hindi 2018, alisema babake alitaka asome, lakini alipenda filamu na alitaka kuwa shujaa.

    Dharmendra alipata umaarufu kwa mara ya kwanza na filamu ya Bimal Roy ya 1963, Bandini, alipata sifa kwa uigizaji wake kama daktari wa gereza ambaye alimpenda mfungwa.

  6. Kiongozi wa upinzani wa Cameroon yuko Gambia baada ya kukimbia nchi

    Kiongozi wa upinzani wa Cameroon Issa Tchiroma Bakary, ambaye anapinga matokeo ya uchaguzi wa rais, amekimbilia Gambia kwa usalama wake, Serikali ya Gambia imesema.

    Tchiroma Bakary amesisitiza kuwa yeye ndiye mshindi halali wa uchaguzi wa Oktoba 12, akidai kuwa matokeo yalichakachuliwa na kumpa Rais Paul Biya, 92, muhula wa nane.

    Wizara ya habari ya Gambia ilisema Jumapili kwamba Tchiroma Bakary aliwasili tarehe 7 Novemba na aliruhusiwa kukaa kwa misingi ya kibinadamu.

    Serikali ya Cameroon imetishia kumfungulia mashtaka kwa madai ya kuchochea maandamano yenye vurugu baada ya uchaguzi. Anakanusha madai hayo, na kuvilaumu vikosi vya usalama kwa kutumia nguvu kubwa dhidi ya waandamanaji.

    Serikali inasema idadi ya watu waliouawa katika ghasia za baada ya uchaguzi ni 16, lakini mashirika mengine yametaja idadi kubwa zaidi.

    Tchiroma Bakary ameahidi kupinga serikali ya Biya hadi "ushindi" wake katika uchaguzi utakapotambuliwa.

    Biya amekuwa rais kwa miaka 43, na alitangazwa mshindi kwa 53.7% ya kura huku kukiwa na madai ya udanganyifu.

    Tchiroma Bakary, ambaye aliwahi kuhudumu katika serikali ya Biya, aliibuka wa pili kwa 35.2%.

    "Anakaribishwa kwa muda nchini Gambia kwa misingi ya kibinadamu na kwa madhumuni ya kuhakikisha usalama wake wakati majadiliano yakiendelea kutafuta azimio la amani na la kidiplomasia la mvutano wa baada ya uchaguzi nchini Cameroon," imesema taarifa ya serikali ya Gambia.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Vipengele muhimu katika mpango wa amani wa Urusi na Ukraine

    Ikulu ya Marekani imesema mpango wenye vipengele 28 - uliojadiliwa na Marekani na Ukraine mjini Geneva mwishoni mwa juma - umeidhinishwa na Rais Donald Trump baada ya kutayarishwa na maafisa wake.

    BBC bado haijaona waraka huo kwa ukamilifu - lakini hapa kuna muhtasari wa mambo matano tunayojua yaliyokuwa kwenye mpango huo kabla ya masahihisho:

    • Tarehe ya mwisho: Trump awali aliipa Ukraine hadi Alhamisi 27 Novemba kukubali mpango huo, lakini akasema muda huo unaweza kuongezwa ikiwa mazungumzo "yatakwenda vizuri."
    • Makabidhiano ya maeneo: Wanajeshi wa Ukraine lazima waondoke eneo la Donetsk wanalolidhibiti kwa sasa, ili kuunda "eneo la amani,’’ na udhibiti wa Urusi katika eneo hilo utatambuliwa kimataifa, na vile vile udhibiti wa Moscow juu ya eneo jirani la Luhansk na peninsula ya kusini ya Crimea, ambayo ilitwaliwa na Urusi 2014 utatambuliwa.
    • Kupunguza vikosi vya jeshi: Ukraine yatakiwa kupunguza vikosi vyake vya jeshi hadi watu 600,000 - Januari iliyopita ilikadiriwa kuwa wana jeshi la watu 880,000.
    • Mustakabali wa Ukraine: Kyiv lazima ijitolee kutojiunga na Nato, ingawa ina haki ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.
    • Kuanzisha tena uhusiano na Urusi: Nchi ya Urusi itarudi tena katika uchumi wa kimataifa.

    Ni muhimu kukumbuka, mpango huo unajadiliwa, na unaweza kubadilika kwa kiasi kikubwa.

    Marekani inasema "kulingana na masahihisho na ufafanuzi uliowasilishwa" huko Geneva, Ukraine "inaamini rasimu ya sasa inaakisi maslahi yao ya kitaifa na inatoa njia za kuaminika na zinazoweza kutekelezeka ili kulinda usalama wa Ukraine.

    Bado BBC haijapata masahihisho na ufafanuzi huo.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Shambulio la kujitoa mhanga laua watano Pakistan

    Washambuliaji wawili wa kujitoa mhanga wameshambulia makao makuu ya jeshi la wanamgambo wa Pakistan siku ya Jumatatu na kuua maafisa watatu na kujeruhi takriban watu 12.

    Polisi wameiambia BBC Urdu kwamba washambuliaji waliingia katika makao makuu ya kikosi cha Federal Constabulary huko Peshawar kaskazini-magharibi mwa Pakistan.

    Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo.

    Makao hayo yako katika eneo lenye ulinzi mkali sana huko Peshawar.

    Walioshuhudia waliambia vyombo vya habari kuwa walisikia milipuko miwili mikubwa siku ya Jumatatu.

    Eneo hilo limezingirwa na timu za uokoaji kwa sasa.

    Afisa mmoja amesema maafisa watano na raia saba wamejeruhiwa.

    Pakistani imeelezea shambulio hilo kama "njama ya kigaidi iliyotimizwa," ikibainisha kuwa washambuliaji walishambuliwa wakiwa kwenye lango, kabla ya kufanikiwa kuingia ndani ya jengo hilo.

    "Wahusika wa tukio hili wanapaswa kutambuliwa haraka iwezekanavyo na kufikishwa mahakamani," amesema Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif.

    Kikosi cha Federal Constabulary, kina jukumu la kushughulikia matukio ambayo ni makubwa kwa jeshi la polisi, ikiwa ni pamoja na vurugu za kikabila na ghasia za magenge ya wahalifu.

    Peshawar ni sehemu ya mkoa wa Khyber Pakhtunkhwa, ambao upo kando ya mpaka wa Afghanistan na kwa muda mrefu imekuwa kitovu cha vurugu za wanamgambo.

    Kundi la Taliban la Pakistani, pia linajulikana kama Tehreek-i-Taliban Pakistan, liko katika jimbo hilo na hudai kuhusika na mashambulizi kama hayo nchini kote.

    Pia unaweza kusoma:

  9. Marekani na Ukraine zasema mazungumzo ya amani yalikuwa na tija

    Marekani na Ukraine zimetoa taarifa ya pamoja na kuelezea kuwa mazungumzo ya amani ya wikendi huko Geneva yalikuwa na "tija kubwa."

    Wajumbe wa pande zote mbili walikutana nchini Switzerland kujadili mpango wa amani wenye vipengele 28 - taarifa ya pamoja inasema kulikuwa na "maendeleo mazuri kuelekea kubainisha hatua zinazofuata."

    Hapo awali viongozi wa Ulaya walikosoa mpango huo, wakisema unaipendelea sana Urusi.

    Ripoti ya Ikulu ya White House ya mazungumzo ya Geneva inasema "kulingana na marekebisho na ufafanuzi uliowasilishwa leo," Ukraine "inaamini kuwa rasimu ya sasa inaonyesha maslahi yao ya kitaifa".

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio anasema "bado kuna kazi ya kufanywa," huku Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akisema kuna "ishara kwamba timu ya Rais [Donald] Trump inatusikiliza."

    Ingawa rasimu ya mpango huo unaoungwa mkono na Marekani haijachapishwa kwa ukamilifu, maelezo makuu yamevuja.

    Wakati mazungumzo ya amani yakiendelea mjini Geneva, mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine yaliendelea siku ya Jumapili.

    Ndege zisizo na rubani za Urusi zilishambulia mji wa mashariki wa Kharkiv, watu wanne walikufa na wengine 17 kujeruhiwa, kulingana na meya wa jiji Igor Terekhov.

  10. 'Salah hana msaada' – asema Rooney

    Meneja wa Liverpool Arne Slot anafaa kumwacha Mohamed Salah, amesema mshambuliaji wa zamani wa Manchester United Wayne Rooney.

    Kipigo cha Jumamosi cha mabao 3-0 kutoka kwa Nottingham Forest Jumamosi, ulikuwa ni mchezo mwingine ambapo Mmisri huyo, ambaye amefunga mabao matano msimu huu, alishindwa kufunga bao au kutoa pasi ya bao.

    "Kama ningekuwa Slot, ningefanya uamuzi mgumu ili kuwe na mabadiliko katika timu," amesema Rooney.

    "Salah hawasaidii katika kujilinda.''

    Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Ligi Kuu kumaliza msimu akiwa na mabao mengi na pasi nyingi za mabao na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa msimu uliopita.

    Kiwango chake kizuri kiliambatana na msimu wa kwanza wenye mafanikio wa Mholanzi Slot, alipoiongoza Liverpool kutwaa ubingwa baada ya kumrithi kocha Jurgen Klopp.

    Baada ya dirisha dogo la usajili la majira ya kiangazi - ikiwa ni pamoja na kuwasajili Florian Wirtz na Alexander Isak kwa dau la pauni milioni 241 - Reds bado iko matatani.

    Liverpool wanashika nafasi ya 11 kwenye jedwali la ligi kuu England, wakiwa na pointi 18 baada ya kucheza michezo 12.

    Nahodha wa Liverpool Virgil van Dijk alisema baada ya kupoteza Jumamosi kwamba "kila mtu katika timu lazima awajibike" huku timu hiyo ikipata ushindi mmoja pekee katika mechi saba zilizopita za ligi.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Rais aagiza kuhamishwa kwa polisi wanaolinda watu mashuhuri Nigeria

    Rais wa Nigeria ameagiza kuhamishwa kwa maafisa wa polisi wanaolinda watu mashuhuri hadi sehemu zingine kukabiliana na tatizo la usalama nchini humo.

    Rais Bola Ahmed Tinubu ameamuru kuhamishwa kwa maafisa hao baada ya wanafunzi 50 kati ya zaidi ya 300 waliotekwa nyara kutoka shule ya Katoliki huko Nigeria kufanikiwa kutoroka kutoka kwa watekaji wao.

    Tinubu alikaribisha habari hiyo, na kuongeza kwamba alikuwa akielezewa juu ya hali ya usalama kote nchini.

    Operesheni ya utafutaji na uokoaji inaendelea kwa wanafunzi na walimu ambao walitekwa nyara na watu wenye silaha siku ya Ijumaa.

    Shule katika eneo hilo la Nigeria zimeamriwa kufungwa.

    Kuongezeka kwa matukio ya utekaji nyara wa watu wengi hivi karibuni kunatokea wakati utawala wa Trump umekosoa viongozi wa Nigeria kwa kushindwa kuwalinda Wakristo kutokana na kuuawa na wanamgambo wa Kiisilamu, madai ambayo serikali imekanusha.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Tanzania inahitaji mwanzo mpya haraka – Taasisi ya Thabo Mbeki

    Taasisi ya Thabo Mbeki umetoa risala za rambirambi kwa familia ambazo zilipoteza wapendwa wao kutokana na vurugu zilizotolewa kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania mnamo 29 Oktoba 2025.

    Wakfu huo umesema kwa kuzingatia taarifa za uchaguzi wa Tanzania zilizotolewa na ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa eneo lao na mashirika, SADC na AU, umehitimisha kwamba uchaguzi wa Tanzania ulikuwa na mapungufu kwenye kanuni na miongozo inayosimamia uchaguzi wa kidemokrasia katika viwango vya kimataifa.

    Ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi ulisema "wapiga kura wa Tanzania hawakuweza kutumia uhuru na dhamira yao ya kidemokrasia", Taasisi ya Thabo Mbeki ilisema na kuongeza nchi hiyo inahitaji mwanzo mpya haraka.

    Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa waangalizi wa SADC na AU walitangaza kuwa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi Tanzania hayaakisi ukweli wa mapenzi ya watu wa Tanzania.

    "Hii imepelekea hitimisho kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa haina serikali halali, ikionyesha badala yake kwamba utawala wa sasa umelazimishwa kwa watu kupitia mchanganyiko wa nguvu na njia za ulaghai", Wakfu wa Thabo Mbeki umesema.

    Taasisi hiyo imesema kuwa msingi wao unashikilia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake kwa heshima kubwa, na kuwaheshimu kama marafiki wa kweli na washirika.

    Taarifa hiyo imerejelea wito wa maridhiano uliotolewa lakini ikasema kuwa matokeo chanya yanaweza tu kupatikana kupitia ukweli, ujumuishaji wa kila mmoja na uhuru wa mazungumzo ya kitaifa.

    Aidha imetaka nchi ya Tanzania kujibu maswali muhimu kama vile nini kilikoseka na kipi kinastahili kufanywa kurejesha hali kuwa ya kawaida na kufikia haki, maridhiano na umoja wa kitaifa.

    Soma zaidi:

  13. Watoto 50 waliotekwa nyara Nigeria wafanikiwa kutoroka watekaji

    Kundi la Kikristo limetangaza kwamba takriban watoto 50 kati ya zaidi ya 300 waliotekwa nyara na watu wenye silaha kutoka shule ya Katoliki nchini Nigeria walifanikiwa kutoroka watekaji wao na tayari wameungana na familia zao.

    Watoto hao wanaosemekana kuwa na umri wa kati ya 10 na 18, walitoroka mmoja mmoja kati ya Ijumaa na Jumamosi, kulingana na Mchungaji Bulus Dauwa Yohanna zaidi, mwenyekiti wa Chama cha Kikristo cha Nigeria katika Jimbo la Niger ambaye pia ni mwanzilishi wa shule hiyo.

    Jumla ya watoto 253 wa shule na walimu 12 bado wanashikiliwa na watekaji nyara, alisema katika taarifa.

    "Tuliweza tu kuthibitisha hili baada ya kuwasiliana na kutembelea baadhi ya familia," Yohanna alisema.

    Wanafunzi na walimu wao walikamatwa na watu wenye silaha walioshambulia Shule ya St. Mary's, taasisi ya Kikatoliki katika jamii ya Papiri ya jimbo la Niger, siku ya Ijumaa.

    Hakuna kundi ambalo limedai kuhusika na utekaji nyara huo na mamlaka imesema vikosi vya kimkakati vimetumwa pamoja na wawindaji wa eneo hilo ili kuwaokoa watoto hao.

    Haikubainika mara moja ni wapi watoto hao walikuwa wanashikiliwa au waliwezaje kurejea nyumbani.

    Jeshi na polisi wa Nigeria halikujibu mara moja ombi la Associated Press.

    Papa Leo XIV amezungumzia suala hilo akitoa wito kwa watu wenye silaha waliowateka nyara watoto na walimu wao kuwaachilia mara moja.

    Alisema alihisi "anaumia sana moyoni" juu ya vijana wengi wa kiume na wa kike ambao wametekwa nyara na kwa familia zao zenye huzuni."

    Pia unaweza kusoma:

  14. 'Mabosi' wa BBC kuhojiwa bungeni

    Viongozi wa ngazi ya juu wa BBC waliohusika katika kashfa ya uhariri ya hivi karibuni watahojiwa na Bunge siku ya Jumatatu.

    Michael Prescott - mshauri wa zamani wa uhariri ambaye aliibua wasiwasi kuhusu namna BBC inavyoandaa na kutoa taarifa zake, ikiwa ni pamoja na hariri ya Panorama ya hotuba ya Donald Trump - atazungumza juu ya suala hilo hadharani kwa mara ya kwanza atakapofika mbele ya kamati ya Bunge.

    Barua ya ndani ya shirika ilioandikwa na Prescott ilifichuliwa kwa vyombo vya habari, na kusababisha kujiuzulu kwa mkurugenzi mkuu wa BBC na mkuu wa habari mapema mwezi huu.

    Pia atakayetoa ushahidi atakuwa mwenyekiti wa BBC Samir Shah, ambaye yuko chini ya shinikizo kwa namna alivyoshughulikia suala hilo, na wajumbe wenzake wa bodi Sir Robbie Gibb na Caroline Thomson.

    Kamati ya bunge ilisema kikao cha Jumatatu kitaangazia "michakato ya kamati ya bodi ya BBC ya miongozo na viwango vya uhariri (EGSC) na jinsi inavyohakikisha matangazo yanazingatia miongozo ya uhariri ya BBC".

    Prescott, mhariri wa zamani wa kisiasa wa Sunday Times, na Daniel, mhariri msaidizi wa zamani wa FT, walishauri EGSC kuhusu "hatari na masuala ya uhariri" baada ya kuteuliwa kama "wataalamu wa uhariri wa nje" wa kwanza wa BBC mnamo 2022.

    Kikao hicho kinafanyika wakati BBC ikisubiri kubaini iwapo Trump atawasilisha hatua za kisheria baada ya kutishia kushtaki shirika hilo kwa fidia ya kati ya $1bn (£759.8m) na $5bn (£3.8bn) juu ya uhariri wa makala ya Panorama.

    Soma zaidi:

  15. Uingereza 'mahali kwa gharama kubwa zaidi duniani' kuendeleza nishati ya nyuklia

    Uingereza imekuwa "mahali penye gharama kubwa zaidi duniani" kujenga vinu vya nguvu za nyuklia, kulingana na hakiki ya serikali inayoelezea urasimu "mgumu" katika sekta hiyo.

    Ripoti hiyo, ambayo iliagizwa na Waziri Mkuu Keir Starmer, ilitaka "mabadiliko" katika mkakati wa nyuklia wa serikali ili kufanya miradi kuwa salama na yenye ufanisi zaidi.

    Kufanya hivyo kunaweza kuokoa Uingereza "makumi ya mabilioni" katika gharama na kubadilisha "mengi yaliyokataliwa" katika sekta hiyo katika miaka ya hivi karibuni, Kikosi Kazi cha Udhibiti wa Nyuklia kilisema.

    Hili linajitokeza wakati serikali ya Uingereza inatazamia kujenga kizazi kipya cha mipango ya nyuklia ili kukidhi mahitaji ya nishati ya siku zijazo ya nchi.

    Ripoti hiyo iligundua kuwa mfumo wa udhibiti "uliogawanyika" umesababisha ukosefu wa uangalizi wa usalama wa sekta nzima, ambao umesababisha "maamuzi ya kihafidhina na ya gharama kubwa ambayo hayalingani na hatari halisi inayodhibitiwa".

    Ilielezea tasnia yenyewe kama "inayokaribia ukiritimba", na ikasema mipango ya kiraia na ya ulinzi ina uwezekano wa "kuongeza gharama kubwa na ucheleweshaji wa ratiba".

    Soma zaidi:

  16. Israel yamuua mjumbe mwandamizi wa Hezbollah

    Jeshi la Israel limemuua mjumbe wa ngazi ya juu wa kundi la wanamgambo wa Hezbollah katika shambulio la anga kwenye viunga vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, licha ya kusitishwa kwa mapigano.

    Ilimuelezea Haitham Ali al-Tabtabai, mkuu wa wafanyakazi wa Hezbollah, kama mjumbe mkongwe katika kundi hilo ambaye alikuwa ameshikilia nyadhifa za juu.

    Wizara ya afya ya Lebanon ilisema takriban watu watano waliuawa na wengine 28 kujeruhiwa katika shambulizi hilo, ambalo lilishambulia jengo la ghorofa katika wilaya yenye watu wengi ya Dahieh.

    Hezbollah ilithibitisha kifo cha Tabtabai, na kuongeza kuwa Israel ilikuwa imevuka "mpaka" katika kutekeleza shambulizi hilo ambalo ni la kwanza kwa Israel kusini mwa Beirut katika kipindi cha miezi kadhaa.

    Haya yanajiri wakati Israel imezidi kulenga watu na maeneo lengwa ikisema yanahusishwa na Hezbollah - kundi la Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaoungwa mkono na Iran - licha ya usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani na Ufaransa ambao ulianza kutekelezwa mwezi uliopita wa Novemba.

    Soma zaidi:

  17. 'Heko kwa 'hatua kubwa' iliyopigwa katika mazungumzo ya amani ya Ukraine' - Marekani

    "Mafanikio makubwa" yamepatikana katika mazungumzo ya kukamilisha mpango wa amani uliopendekezwa na Marekani kumaliza vita vya Urusi na Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio amesema.

    Lakini "bado kuna mengi ya kufanywa", Rubio alisema baada ya kukutana na wapatanishi wa Ukraine na Ulaya huko Geneva, Uswizi.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kulikuwa na "ishara kwamba timu ya Rais [Donald] Trump inatusikia".

    Ukraine na washirika wake wa Ulaya walikuwa wameelezea wasiwasi wao juu ya mapendekezo yaliyovuja, yanayoonekana kuipendelea Urusi na kukaribishwa na Vladimir Putin kama "msingi" wa suluhu.

    Zelensky alikuwa amesema Ukraine "huenda ikakabiliwa na chaguo gumu sana: ama kupoteza utu wake, au mshirika mkuu".

    Soma zaidi:

  18. Hujambo msikilizaji. Ni Jumatatu ya tarehe 24/11/2025, karibu katika matangazo yetu mubashara.