Ubalozi wa Marekani umetangaza kuongezwa kwa kiwango cha tahadhari ya usafiri kwenda Tanzania kutoka Kiwango cha 2 hadi Kiwango cha 3, ikimaanisha kuwa ina shauriwa kuepuka safari zisizo za lazima kuelekea nchini humo.
Kiwango hiki kipya kimeongezwa kufuatia kuongezwa kwa kiashiria cha hatari ya “machafuko”, pamoja na sababu nyingine za kiusalama ikiwemo uhalifu, ugaidi, na unyanyasaji dhidi ya watu wa jinsi moja (LGBTQ+).
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imetoa wito kwa wasafiri kutembelea tovuti yao kwa taarifa zaidi kuhusu hatari ya ugaidi hasa katika mkoa wa Mtwara.
Pia tahadhari hiyo imetolewa kwa watu wanaojitambulisha kama jinsi moja walioko nchini humo wakisema wanakamatwa, kunyanyaswa, au wanalengwa na vyombo vya usalama.
Wasafiri wanaopanga kuelekea Tanzania wanahimizwa kuwa na mpango wa dharura wa kuondoka ambao hautegemei msaada wa serikali ya Marekani.
Taifa kuwekewa tahadhari ya usafiri inamaanisha nini?
Tahadhari ya usafiri mara nyingi hutolewa kwa mataifa ambayo yako katika ghasia, uhalifu na unyanyasaji wa kibinadamu wa hali ya juu.
Tahadhari hizi hutolewa kwa viwango, cha juu zaidi kikiwa ni cha nne.
Kiwango cha 1 - Chukua tahadhari za kawaida
Hiki ndicho kiwango cha chini kabisa cha tahadhari.
Inamaanisha kuwa hali ya usalama ni ya kawaida. Wasafiri wanashauriwa kuchukua tahadhari zile zile za kawaida wanazochukua popote, kama vile kuepuka maeneo yasiyojulikana usiku au kutokuwa na vitu vya thamani hadharani.
Kiwango cha 2 - Chukua tahadhari ya juu
Hiki ni kiwango cha tahadhari kinachoonyesha kuwa kuna hatari fulani, ingawa si kubwa sana. Wasafiri wanashauriwa kuwa makini zaidi kuliko kawaida, hasa katika maeneo yenye matukio ya uhalifu, migogoro ya kisiasa, au hatari za kiafya.
Kiwango cha 3 -“Epuka safari zisizo za lazima.”
Kiwango hiki kinaashiria hatari kubwa zaidi kwa usalama wa msafiri.
Kiwango cha 4 – Epuka safari zote
Hiki ndicho kiwango cha juu zaidi cha tahadhari. Kinaonyesha kuwa kuna hatari kubwa sana kwa maisha au usalama binafsi. Safari kuelekea eneo hilo hazipendekezwi kabisa, kwa kuwa mazingira yanaweza kuwa hatarishi.
Athari ya tahadhari ya usafiri kwa nchi
Baada ya Marekani kutoa tahadhari ya usafiri ya Kiwango cha 3 kuelekea Tanzania, wachambuzi wanaonya kuhusu athari za moja kwa moja na za muda mrefu kwa taifa.
Tahadhari hiyo inaweza kusababisha kupungua kwa idadi ya watalii, kwani wasafiri huchagua maeneo salama zaidi, hivyo kupunguza mapato ya sekta ya utalii.
Pia, inachafua taswira ya kimataifa ya Tanzania kwa kuashiria kutokuwa na usalama au uthabiti.
Onyo hilo pia linaweza kuwazuia wawekezaji, wataalamu na mashirika ya kimataifa kuingia nchini, pamoja na kuathiri mahusiano ya kidiplomasia.
Pia linaibua wasiwasi kuhusu hali ya usalama na haki za binadamu nchini.