Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump akanusha ripoti kwamba kamanda mkuu wa jeshi la Marekani anapinga shambulio dhidi ya Iran

Trump amesema kuwa Jenerali Kane anaifahamu vyema Iran kwa sababu aliamuru Operesheni ya Midnight Hammer, mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya Iran majira ya joto yaliyopita.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Marekani yawaondoa baadhi ya wafanyikazi wake kutoka Beirut huku mvutano ukiongezeka

    Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, wafanyakazi wasio wa lazima wameagizwa kuondoka katika ubalozi wa Marekani ulioko Beirut, mji mkuu wa Lebanon, kufuatia tathmini ya hali ya usalama.

    Uamuzi huo umechukuliwa wakati mvutano ukiendelea kuongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati, huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran iwapo hakutakuwa na makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia.

    Iran tayari imetangaza kuwa itajibu endapo Marekani itafanya shambulio, na inaaminika kuwa kambi na vituo vya kijeshi vya Marekani katika Mashariki ya Kati vinaweza kuwa malengo ya mashambulizi.

    Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ameahirisha ziara yake ya kwenda Israel bila kutoa sababu rasmi.

    Afisa huyo mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje amesema: “Tunaendelea kutathmini mazingira ya usalama na, kulingana na tathmini yetu ya karibuni, tumeona ni busara kupunguza idadi ya wafanyakazi hadi wale wa lazima pekee. Ubalozi utaendelea kufanya kazi kwa kutumia wafanyakazi muhimu. Hii ni hatua ya muda inayolenga kuhakikisha usalama wa watumishi wetu na kuendelea kuwahudumia raia wa Marekani.”

    Takribani wafanyakazi 50 wa ubalozi wa Marekani wameagizwa kuondoka Beirut.

    Afisa mmoja wa uwanja wa ndege ameiambia Reuters kuwa wafanyakazi 32 pamoja na familia zao waliondoka kupitia Uwanja wa Ndege wa Beirut siku ya Jumatatu.

    Alhamisi, Trump alisema dunia itafahamu “ndani ya siku kumi zijazo au zaidi” iwapo kutakuwa na makubaliano au kama Marekani itachukua hatua ya kijeshi dhidi ya Iran.

    Soma pia:

  2. Tehran yatoa masharti mapya ili kufikia makubaliano na Marekani

    Iran imetoa “mapendekezo mapya ya maridhiano” kuhusu mpango wake wa nyuklia kwa lengo la kufikia makubaliano na Marekani.

    Baadhi ya mapendekezo hayo ni kama vile kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi, na kutambuliwa kwa haki ya Tehran ya “kuendeleza nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani'’, haya ni kwa mujibu wa Shirika la habari la Reuters.

    Aidha, Reuters imeripoti kuwa afisa mmoja mwandamizi wa Iran amesema kuwa bado kuna tofauti kubwa kati ya pande hizo mbili, hata kuhusu wigo na utaratibu wa kupunguza au kuondoa vikwazo vikali vya Marekani.

    Taarifa hiyo inakuja wakati Oman, ambayo inachukua jukumu la upatanishi katika mazungumzo kati ya Iran na Marekani, imethibitisha kuwa duru mpya ya mazungumzo itafanyika Geneva Alhamisi ijayo.

    Afisa huyo pia amesema kuwa Iran “inazingatia kwa umakini” uwezekano wa kusafirisha nje nusu ya akiba yake ya urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu, kupunguza kiwango cha nusu iliyobaki, na kuunda muungano wa kikanda wa urutubishaji.

    Kwa mujibu wa Reuters, wazo hilo limekuwa likijitokeza mara kwa mara katika juhudi za kidiplomasia zilizohusisha Iran kwa miaka kadhaa.

    Aidha, afisa huyo alieleza kuwa hatua hiyo itakwenda sambamba na Marekani kuitambua rasmi haki ya Iran ya “kuendeleza nyuklia kwa matumizi ya amani,” huku makubaliano hayo yakijumuisha pia kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Iran.

    Soma zaidi:

  3. Lissu ashinda pingamizi dhidi ya ushahidi wa ziada katika kesi yake ya uhaini

    Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, limetupilia mbali ombi la Mawakili wa Serikali la kuwasilisha ushahidi wa ziada kutoka kwa shahidi wa mpelelezi, ACP Amini Mahamba, katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

    Uamuzi huo umefuatia pingamizi lililowasilishwa na Lissu, akipinga hatua ya upande wa mashtaka kuomba kuongezwa kwa ushahidi huo wa ziada. Majaji wameridhia pingamizi hilo na kuamua kuwa ombi la Serikali halina msingi wa kisheria.

    Kwa uamuzi huo, Lissu ameshinda pingamizi lake la msingi, akidai kuwa kuongezwa kwa ushahidi huo ni kinyume cha Kifungu cha 308 cha sheria, ambacho kinaelekeza utaratibu wa kuwasilisha ushahidi au kumwita shahidi mpya ambaye hakuwepo katika mwenendo wa awali wa Mahakama Kabidhi.

  4. Ushuru mpya wa Trump wa 10% waanza kutekelezwa

    Ushuru mpya wa kimataifa wa Rais wa Marekani Donald Trump umeanza kutekelezwa kwa 10% baada ya Mahakama ya Juu Zaidi nchini humo kuzuia ushuru mkubwa wa uagizaji bidhaa siku ya Ijumaa.

    Saa chache tu baada ya uamuzi wa wiki iliyopita, rais alisaini amri ya serikali ya kutoza ushuru mpya kuanzia tarehe 24 Februari.

    Baadaye alitishia kuongeza ushuru huo hadi 15% lakini bado hajatoa agizo rasmi la kuongeza kiwango hicho. BBC imewasiliana na Ikulu ya White House kwa maoni.

    Utawala unatekeleza hatu hii ya kuongeza ushuru chini ya Kifungu cha 122 cha Sheria ya Biashara ya 1974, ambayo inaruhusu rais kutoza ada hiyo kwa siku 150 bila idhini ya bunge.

    "Nadhani inaongeza tu msukosuko," alisema Carsten Brzeski, mchambuzi wa benki ya uwekezaji ING, akimaanisha ushuru unaobadilika haraka na athari zake kibiashara.

    "Kuhusu kutokuwa na uhakika tumerudi mahali tulipokuwa mwaka jana," aliambia kipindi cha BBC Today programme, akiongeza kuwa sasa kuna hatari kubwa zaidi kwamba washirika wa kibiashara wa Marekani watalipiza kisasi.

    "Hatari ya vita kamili vya ushuru - vita vya kibiashara – iko uko juu zaidi kuliko mwaka jana," Brzeski alisema.

    Soma zaidi:

  5. Putin hajafikia malengo yake, Zelensky asema miaka minne baada ya uvamizi wa Urusi

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema kwamba Vladimir Putin wa Urusi alishindwa kuwakatisha tamaa Waukraine alipoivamia nchi yake miaka minne iliyopita.

    "Leo inaadhimisha miaka minne tangu Putin aanze harakati zake za siku tatu za kuichukua Kyiv," ameandika katika ujumbe kwenye Telegram.

    "Na hii ina maana kubwa juu ya upinzani wetu, kuhusu jinsi Ukraine imekuwa ikipigana wakati huu wote."

    Zelensky amesema kwamba, nyuma ya maneno hayo, "kuna mamilioni ya watu wetu, ujasiri mkubwa, kazi nzuri ya kupigiwa mfano, uvumilivu, na mengi ambayo Ukraine imekuwa ikiifanya tangu Februari 24 [2022]."

    "Tukiangalia nyuma mwanzoni mwa uvamizi na kutafakari leo, tuna haki ya kusema: tumetetea uhuru wetu, hatujapoteza uraia wetu, Putin hajafikia malengo yake," anaendelea.

    "Hajawakatisha tamaa Waukraine, hajashinda vita hivi."

    "Tumeilinda Ukraine, na tutafanya kila kitu ili kufikia amani na haki. Utukufu kwa Ukraine!"

    Soma zaidi:

  6. BBC yaomba msamaha kwa kutangaza maneno ya ubaguzi wa rangi katika matangazo ya Tuzo za Bafta

    BBC imeomba radhi kwa kutohariri maneno ya ubaguzi wa rangi wakati wa matangazo yake ya Tuzo za Filamu za Bafta baada ya mgeni mwenye ugonjwa wa mfumo wa neva unaoainishwa kwa mitetemo ya ghafla ya kimisuli na sauti unaojulikana kama ‘Tourette’ kupiga kelele wakati waigizaji wawili wenye asili ya Kiafrika walipokuwa jukwaani.

    John Davidson, ambaye simulizi yake ya maisha ilihamasisha filamu ya I Swear, alipiga kelele akitaja neno N huku nyota wa Sinners Michael B Jordan na Delroy Lindo wakitoa zawadi ya kwanza ya sherehe ya Jumapili.

    Sehemu hiyo haikuhaririwa kutoka kwa matangazo ya BBC One, ambayo yalionyeshwa kwa kuchelewa kwa saa mbili, na yakasikika kwenye BBC iPlayer siku ya Jumatatu asubuhi kabla ya kuondolewa.

    Msemaji wa BBC alisema: "Tunaomba msamaha kwa kutohariri sehemu hii kabla ya matangazo haya kupeperushwa hewani na sasa itaondolewa kwenye toleo la BBC iPlayer."

    Kelele zilisikika katika matangazo, ingawa watazamaji wengi hawakuelewa kwa urahisi neno hilo.

    Kiongozi wa Chama cha Conservative Kemi Badenoch alisema BBC ilifanya "kosa baya mno" kwa kutohariri sehemu hiyo kwa wakati, na kuongeza: "Nafkiri kuomba msamaha ni muhimu, wanahitaji kuelezea kwa nini sehemu hiyo haikufutwa kabisa."

    Katika taarifa yake, BBC ilisema: "Baadhi ya watazamaji huenda walisikia maneno makali na ya kukera wakati wa Tuzo za Filamu za Bafta."

    "Hili lilitokana na mitetemo ya maneno yanayotoka yenyewe yenye kuhusishwa na ugonjwa wa ‘Tourette’, na kama ilivyoelezwa wakati wa sherehe haikuwa makusudi."

    Shirika hilo lilikataa kutoa maoni zaidi kuhusu kwa nini halikuhariri au kufutwa kabisa sehemu hiyo mwanzoni.

    Taarifa kutoka Bafta ilisema imetambua athari ya tukio hilo, "zungumzia kilichotokea na uombe msamaha kwa wote".

    Davidson, mwanaharakati wa ugonjwa wa Tourette kutoka Galashiels huko Scotland, ambaye aliteuliwa kuwa MBE mnamo 2019, alipiga kelele kwa sauti kubwa mara kadhaa kabla na wakati wa sherehe ya Bafta.

    Alisema Jumatatu kwamba "ninasikitika sana ikiwa mtu yeyote atachukulia mitetemo yangu isiyo ya hiari kuwa ya makusudi au yenye maana yoyote".

    "Nilichagua kuondoka ukumbini mapema kabla ya sherehe kwani nilikuwa najua kero ambayo mitetemo yangu ilikuwa ikisababisha."

    Pia unaweza usoma:

  7. Pacquiao na Mayweather wakubali kuzichapa katika mechi ya marudiano

    Wanandondi maarufu Manny Pacquiao na Floyd Mayweather wamekubaliana kuzichapa tena katika pambano la kitaalamu mnamo mwezi Septemba.

    Pacquiao, 47, na Mayweather, 48, watapigana Sphere huko Las Vegas Jumamosi, Septemba 19, huku pambano hilo likionyeshwa moja kwa moja kwenye Netflix.

    Itakuwa pambano la kwanza la kitaalamu kwa Mmarekani huyo tangu amshinde Conor McGregor raundi ya 10 ya pigano kwa ‘knockout’ tangu mwaka 2017.

    Pacquiao wa Ufilipino alistaafu kutoka kwenye mchezo huo ili kujikita zaidi kwenye taaluma yake ya kisiasa mwaka wa 2021 lakini alirudi ulingoni Julai iliyopita kupambana na bingwa wa WBC wa uzito wa welterweight Mario Barrios, ambaye alihifadhi taji lake baada ya kutoka sare.

    Mayweather na Pacquiao walikutana kwa mara ya kwanza mwaka wa 2015, katika kile kilichoitwa 'Pambano la Karne' na linasalia kuwa la kihistoria katika ndondi.

    Mayweather aliibuka na ushindi, akimshinda Pacquiao kupitia uamuzi mpana wa pamoja huko Las Vegas.

    Pacquiao, mshindi wa mataji 12 ya dunia katika madaraja manane ya uzito, alisema: "Mimi na Floyd tuliipa dunia pambano kubwa zaidi katika historia ya ndondi."

    "Mashabiki wamesubiri vya kutosha. Wanastahili mechi hii ya marudiano."

    "Nataka Floyd aishi na majuto ya pambano alilopoteza katika rekodi yake ya kitaaluma na akumbuke kila wakati ni nani aliyempa kipigo hicho."

    Mayweather, ambaye anatimiza miaka 49 siku ya Jumanne, alisema: "Tayari nimepigana na kumshinda Manny mara moja. Wakati huu matokeo yatakuwa sawa."

    Mayweather ameshinda mapambano yake yote ya kitaaluma kwa 50-0, huku 27 akishinda kwa ‘knockout’.

    Maelezo kamili kuhusu upatikanaji wa tikiti na mengineo yatatangazwa katika wiki zijazo.

  8. Sesko na Lammens waruhusu Man Utd kuwa na ndoto ya kuingia Ligi ya Mabingwa

    Benjamin Sesko alikuwa mchezaji wa akiba wa Manchester United kwa mechi ya pili mfululizo huku Mslovenia huyo akifunga bao pekee dhidi ya Everton na kuwaweka vijana wa Michael Carrick katika nafasi ya nne.

    Siku kumi na tatu baada ya mshambuliaji huyo wa pauni milioni 73.7 kufunga bao katika dakika za majeruhi na kuokoa pointi moja dhidi ya West.

    Sesko aliendelea kutamba baada ya kumpa pasi Matheus Cunha. Kufikia wakati Cunha alipompa pasi ndefu Bryan Mbeumo, Sesko mwenye hamu kubwa alikuwa amewazidi nguvu walinzi wa Everton na alikuwa tayari kufunga bao lake la nane msimu huu.

    Cha kushangaza, mabao mawili tu kati ya hayo yalifungwa na kocha wa zamani Ruben Amorim, huku matatu yakifungwa na Darren Fletcher katika michezo miwili akiwa kama kocha wa muda na matatu chini ya Carrick, ambaye sasa ameshinda michezo mitano kati ya sita aliyocheza akiwa kama meneja.

    Ilikuwa wakati wa kusisimua baada ya muda mrefu katika mechi ambayo ilikuwa na ubora wa chini katika Uwanja wa Hill Dickinson.

    Pande zote mbili zilipambana dhidi ya ulinzi mkali, baada ya kukaa kwa karibu wiki mbili bila mchezo baada ya kucheza mapema katika raundi ya mwisho ya mechi, mechi hii ikiwa mwishoni, na bila mechi yoyote katika Kombe la FA baada ya kutolewa mapema.

    Katika mchezo wenye fursa finyu, mlinzi James Tarkowski alifanikiwa kuzuia mpira kuvuka mstari wa lango katika kipindi cha kwanza baada ya juhudi za Amad kuokolewa kiasi na Jordan Pickford.

    Kipa Senne Lammens alimnyima kinda Harrison Armstrong, ambaye alikuwa na mchezo mzuri upande wa Everton kabla ya Michael Keane kuachia mpira kwa nguvu dakika nane kabla ya mpira kuisha.

    Mpira ulikuwa unaelekea kwenye kona ya juu kushoto lakini Lammens alikuwa macho tena, huku mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji akiokoa mpira kwa njia ya kipekee.

    Matokeo haya yanamaanisha kuwa sasa ni michezo saba ya nyumbani bila ushindi katika mashindano yote kwa Everton, ambao wako katika nafasi ya tisa.

    Soma zaidi:

  9. Trump akanusha ripoti kwamba kamanda mkuu wa jeshi la Marekani anapinga shambulio dhidi ya Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump, Jumatatu jioni - Februari 23 - alikanusha ripoti kwamba Jenerali Daniel Kane, anayejulikana kama "Razen", anapinga hatua za kijeshi dhidi ya Iran.

    Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii Jumatatu jioni, Bw. Trump aliandika kwamba alizingatia ripoti hizo kuwa za "uongo kabisa" na kufafanua kuwa hakuna chanzo maalum kilichotajwa kuhusu madai haya.

    Amesisitiza kuwa: Jenerali Kane, sawa na maafisa wengine, hana mwelekeo wa vita, lakini iwapo uamuzi utatolewa wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran, anaamini kwamba atashinda kwa urahisi mzozo huo.

    Bw. Trump aliongeza kuwa Jenerali Kane anaifahamu vyema Iran kwa sababu aliamuru Operesheni ya Midnight Hammer, mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya Irani majira ya joto yaliyopita.

    Kufuatia shambulio hilo, alisema, mpango wa nyuklia wa Iran "hautaendelea tena" kwani "umeharibiwa kabisa" kufuatia mashambulizi ya ndege za Marekani za B-2.

    Rais wa Marekani alimtaja Jenerali Kane kama "shujaa mkubwa" na kusema anawakilisha "jeshi lenye nguvu zaidi duniani."

    Bw.Trump aliongeza kuwa kamanda huyo wa kijeshi wa Marekani hajawahi kusema kuchukua hatua dhidi ya Iran au hata mashambulizi machache - aliyoyaita "ya uwongo" - na analenga tu "ushindi" na ataelekeza operesheni hiyo ikiwa shambulio litaamriwa.

    Pia alisema kwamba nyenzo zote zilizochapishwa kuhusu uwezekano wa vita na Iran hazikuwa sahihi na ni za makusudi.

    Alisisitiza kwamba uamuzi wa mwisho ni juu yake na kwamba angependelea kufikia makubaliano na Iran, lakini kwamba ikiwa hakuna makubaliano yatafikiwa, "siku hiyo itakuwa mbaya sana kwa nchi hiyo" na, alisema, "kwa bahati mbaya kwa watu wake," ambao aliwataja kuwa "wakubwa na wanaostahili."

    Vyombo kadhaa vya habari vya Marekani, kama vile Wall Street Journal, Washington Post, na New York Times, vimechapisha ripoti katika siku chache zilizopita, vikinukuu "vyanzo vya habari" visivyojulikana, vinavyoelezea chaguzi, sifa, na majadiliano ndani ya White House kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.

    Soma zaidi:

  10. Habari za hivi punde, Iran yaonya: Shambulio lolote dhidi ya nchi hiyo halitafanyika kati ya nchi mbili pekee

    Iran imeonya kwamba uwezekano wa mashambulizi ya Marekani dhidi ya nchi hiyo hautafanyika kwa nchi mbili pekee.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran anasema hakuna kitu kinachoitwa shambulio lenye mipaka na operesheni yoyote dhidi ya Iran itakabiliwa na jibu kali.

    Hapo awali, baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kwamba Donald Trump alikuwa akizingatia shambulio dogo dhidi ya Iran ili kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu kukubali mistari myekundu ya Marekani kwa kufikia makubaliano.

    Israel pia imeonya kuwa shambulio la kisasi la Iran dhidi ya nchi hiyo litakuwa kosa kubwa zaidi katika historia ya Jamhuri ya Kiislamu.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Watu 15 wafariki baada ya helikopta kuanguka wakati wa uokoaji wa mafuriko Peru

    Watu kumi na tano wamefariki baada ya helikopta ya kijeshi inayotoa huduma za uokoaji wakati wa mafuriko makubwa kusini mwa Peru kuanguka siku ya Jumapili.

    Jeshi la Anga la Peru lilisema helikopta ya Mi-17 ilipoteza mawasiliano wakati ikifanya kazi katika eneo la Arequipa, ambalo limekumbwa na mvua kubwa na mafuriko.

    Maafisa walisema timu za uokoaji zilipata mabaki ya helikopta hiyo katika wilaya ya Chala Jumatatu. Watoto saba walikuwa miongoni mwa abiria 11 na wafanyakazi wanne waliofariki.

    Helikopta hiyo ilikuwa imetumwa kusaidia juhudi za utafutaji na uokoaji katika eneo hilo huku maporomoko ya matope na mito iliyofurika ikisababisha uharibifu mkubwa.

    Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba baadhi ya wanajeshi waliokuwa ndani ya ndege hiyo walikuwa na jamaa walioandamana nao. Mmoja wa waathiriwa alikuwa na umri wa miaka mitatu.

    Jeshi la Anga la Peru lilisema: "Tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia, marafiki, na familia nzima ya FAP kwa msiba huu wa wafanyakazi wetu na abiria."

    Uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hilo, maafisa walisema.

    Mvua kubwa imesababisha mafuriko makubwa katika eneo la Arequipa nchini Peru na kusababisha maporomoko ya matope, mitaa iliyofurika maji, nyumba na miti kuanguka.

    Pia unaweza kusoma:

  12. 'Ole wenu mnaocheza michezo ya paka na panya' na mikataba ya kibiashara – Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump ameonya nchi dhidi ya kujiondoa katika mikataba ya kibiashara iliyojadiliwa hivi karibuni na Marekani baada ya Mahakama ya Juu Zaidi nchini humo kutoa uamuzi kuwa ushuru wake wa dharura siyo halali, akisema kwamba ikiwa watafanya hivyo, atawatoza ushuru mkubwa zaidi chini ya sheria tofauti za kibiashara.

    Trump, katika mfululizo wa machapisho ya mitandao ya kijamii, alisema pia anaweza kutoza ada za leseni kwa washirika wa kibiashara huku kutokuwa na uhakika kuhusu hatua zake zijazo za ushuru kukiathiri uchumi wa dunia.

    "Nchi yoyote inayotaka 'kucheza mchezo wa paka na panya' na uamuzi wa kipuuzi wa mahakama ya juu zaidi, hasa zile ambazo 'zimeiibia' Marekani kwa miaka mingi, na hata miongo kadhaa, zitakabiliwa na ushuru wa juu na mbaya zaidi, kuliko ule ambao wameukubali hivi karibuni. MNUNUZI TAHADHARI!!!" Trump aliandika kwenye mtandao wa Truth Social.

    Trump alisema kwamba licha ya uamuzi wa mahakama wa kubatilisha ushuru wake chini ya Sheria ya Dharura ya Kiuchumi Kimataifa, uamuzi wake umethibitisha uwezo wake wa kutumia ushuru chini ya mamlaka zingine za kisheria "kwa njia yenye nguvu zaidi na ya kuchukiza, kwa uhakika wa kisheria, kuliko ushuru kama ulivyotumika awali."

    Alipendekeza kwamba Marekani inaweza kutoza ada mpya za leseni kwa washirika wa kibiashara, lakini hakutoa maelezo yoyote.

    Msemaji wa ofisi ya Mwakilishi wa Biashara wa Marekani hakujibu mara moja ombi la kutoa maoni zaidi kuhusu mipango ya Trump.

    Pia unaweza kusoma:

  13. Hujambo msomaji wetu. Karibu katika matangazo yetu mubashara, tarehe ni 24/02/2026.